Friday, June 5, 2009

URITHI: Umuhimu wa wosia

Huko nyuma nilisema kwamba, ingawa urithi ni jambo zuri, yapo matatizo yanayoambatana na swala hili. Niliainisha baadhi ya matatizo hayo na nikasema kwamba waathirika wakubwa ni wajane pamoja na watoto walioachwa na marehemu. Baadhi ya matatizo hayo ni kunyimwa haki ya kurithi, kudhulumiwa au kudhulumiana kati ya warithi, na kadhalika.

Vile vile niliainisha watu wanaostahili kurithi na nikasema kwamba watu kama watoto wa kambo, watoto wa kufikia na watu baki (au wasio ndugu) wanaweza kuleta utata wakati wa kurithi. Ni vema kama kuna kusudio la kuwarithisha watu kama hawa, maswala yao yakawekwa sawa kulingana na taratibu za nchi na kijamii.

Ili kuepusha migongano wakati wa kurithi, mwenye kumiliki mali anaweza kuandaa kitu kinachoitwa wosia, au wasia au usia. Maneno yote haya yana maana ya kitu kile kile, ila katika makala haya nitatumia neno wosia. Nitaeleza maana ya wosia, namna ya kuuandika na pia utunzaji wake. Kwahiyo msomaji naomba tufuatane kwa makini.

Wosia ni nini?
Kwa kifupi wosia ni maandishi yanayoandikwa au kauli anayotamka mtu wakati wa uhai wake, akieleza jinsi mazishi yake yatakavyokuwa na mali yake itakavyogawanywa kwa warithi wake baada ya kifo chake. Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba , wosia huandaliwa na mwenye kumiliki mali wakati akiwa bado yu hai na vile vile akili zake zikiwa bado timamu.

Wosia ni kitu kinachotambulika katika jamii nyingi duniani, na pia kina nguvu za kisheria. Bahati nzuri hata hapa kwetu Tanzania, sheria za mirathi zinatambua kuwepo kwa kitu hiki na pia zipo taratibu au miongozo inayoelekeza namna ya kuandaa wosia. Baadaye tutaangalia taratibu hizo.

Aina za wosia
Kutokana na tafsiri ya neno wosia tunaweza kuona kwamba kuna aina mbili za wosia. Aina ya kwanza ni wosia wa maneno au wa kutamka. Yumkini katika jamii zetu hapa nchini, wapo watu ambao hawajui kusoma wala kuandika, au ambao ni vipofu. Wosia wa watu kama hawa unaweza katika matamshi ya vinywa vyao. Kwahiyo kutokuwa na elimu ya darasani au kuwa kipofu sio sababu ya mtu kuacha kuandaa wosia.

Tunapoigeukia Biblia tunaweza kuona kuwa Yakobo au Israeli alitoa wosia wa maneno , akieleza ni wapi atakapozikwa baada ya kifo chake. Tunaambiwa kuwa, “Siku za kufa kwake Israeli zikakaribia; akamwita mwanawe Yusufu, akamwambia, Kama nimeona kibali machoni pako, weka mkono wako juu ya paja langu, ukanifanyie rehema na kweli; nakusihi usinizike katika Misri. Lakini nitakapolala pamoja na baba zangu, unichukue toka Misri, unizike katika kaburi lao” (Mwanzo 47:29-30).

Yusufu alipokaribia kufa aliwaagiza wana wa Israeli kwamba watakapoondoka Misri, waondoke na mifupa ya mwili wake hadi katika nchi ya Kanaani (Mwanzo 50:24-26). Kauli iliyotamkwa na Yakobo au Yusufu ilikuwa ni wosia. Yumkini walitoa wosia wa maneno kwa sababu hawakujua kuandika.

Aina ya pili ya wosia ni ule unaofanywa kwa njia ya maandishi. Huu ni rahisi zaidi kuuandaa na mara nyingi hufanywa na watu wenye uwezo wa kusoma na kuandika. Hata kama huna uwezo wa kuandika, bado unaweza kumwambia mtu mwingine unayemwamini akuandikie wosia wako, halafu mwenyewe ukaweka sahihi ya dole gumba.

Kitu cha muhimu ni wewe mtoa wosia kuhakikisha kwamba hayo yaliyoandikwa ni sahihi. Unaweza kufanya hivyo kwa kumwomba mtu akusomee hicho kilichoandikwa. Ndio kusema hata vipofu wanaweza kuandaa wosia wa maandishi.

Sifa za wosia halali

Tayari nimeshasema kwamba wosia unatambuliwa na sheria za nchi au tuseme sheria za mirathi. Lakini ili uweze kuwa na nguvu ya kisheria, zipo sifa kadhaa ambazo ni lazima zitimizwe, ndipo wosia huo uweze kutambuliwa na mahakama. Kwa kifupi sifa hizo ni kama ifuatavyo;

  1. Kama ni wosia wa mdomo, uwe umeshuhudiwa na mashahidi wasiopungua wanne, ikiwa ni pamoja na watu wa ukoo wasiopungua wawili.
  2. Kama ni wosia wa maandishi, ushuhudiwe na mashahidi wawili wenye kujua kusoma na kuandika, mmoja akiwa ni wa ukoo, ila wa pili anaweza kuwa mtu baki.
  3. Wosia uandikwe ama kwa kuchapa au kwa kalamu ya wino usiofutika na kuwekwa saini na wote, yaani mtoa wosia pamoja na mashahidi. Mashahidi washuhudie wosia huo kwa wakati mmoja na uwekwe tarehe ya kuandikwa kwake.
  4. Wosia ushuhudiwe pia na mke (au wake za marehemu), kama mwenye kutoa wosia ni mume aliyekuwa na ndoa.
  5. Warithi waliotajwa katika wosia, isipokuwa mke (au wake wa mwenye kutoa wosia) hawawezi kuwa mashahidi wa wosia huo.
  6. Mwenye kutoa wosia awe na akili timamu wakati wa kufanya hivyo. Asiwe mwenda wazimu, mgonjwa wa akili, asiwe katika hali ya ulevi au hasira ya ghafla, nk.
  7. Karatasi yenye wosia au wosia wenyewe usiwe na mabadiliko yoyote katika maandishi yake. Lengo ni kuepukana na wosia wa kughushi au uliobadilishwa na mtu mwingine zaidi ya yule aliyeutoa.
Ikumbukwe kuwa mtu aliye chini ya umri miaka 21 hawezi kutoa wosia, uwe wa mdomo au wa maandishi. Sheria za nchi zinakataza kabisa jambo hili.

Mabadiliko katika wosia
Wosia unaweza kuandaliwa na kutolewa wakati wowote baada ya mhusika kufikisha umri wa miaka 21. Lakini haina maana kwamba baada ya kuutoa, mhusika hawezi kufanya tena mabadiliko yotote. La hasha. Sheria inaruhusu marekebisho wakati wowote wa uhai wa mtoa wosia huo, lakini zipo taratibu za kufuata. Nitazitaja kwa kifupi.
  1. Mwenye kutoa wosia anaweza kufanya mabadiliko wakati wowote wa uhai wake, mradi mabadiliko hayo yashuhudiwe na mke au wake wa ndoa (kwa ndoa ya mke zaidi ya mmoja) pamoja na mashahidi wawili.
  2. Wosia wa maandishi hauwezi kubadilishwa au kufutwa kwa wosia wa mdomo.
  3. Wosia wa mdomo unaweza kubadilishwa au kufutwa kwa wosia wa maandishi, mradi wawepo mashahidi wote walio hai na wanaoweza kupatikana, ambao walishuhudia wakati wosia huo ulipotolewa kwa mdomo.
  4. Kwa upande wa utekelezaji wa wosia wa mdomo, endapo baadhi ya mashahidi wamekufa, lakini walio hai hawapungui wawili, wosia huo utafuatwa na kutekelezwa. Vinginevyo kunaweza kukawa na utata wa kisheria.
Mfano wa wosia
Baada ya kueleza maana ya wosia, umuhimu wa kuandaa wosia, aina za wosia na namna ya kuandaa wosia, nafikiri ipo haja ya kuangalia mfano wa wosia wa maandishi. Ikumbukwe kuwa wosia huandikwa kulingana na mazingira ya mtu anayeuandika na kwamba wosia mmoja sio lazima ufanane na wosia mwingine, ingawa yapo mambo ya msingi ambayo yanatakiwa yawepo katika kila wosia. Hebu tuangalie mfano ufuatao;

WOSIA WA MWISHO WA SABATO TARIMO

  • Huu ni wosia wangu wa mwisho mimi Sabato Tarimo wa S.L.P. 9111, Dar-es salaam ambao nimeuandika nikiwa na akili zangu timamu na bila kushurutishwa na mtu yoyote.
  • Nitakapokufa mwili wangu ukazikwe Himo-Moshi katika shamba nililopewa na marehemu baba yangu.
  • Nitakapofariki dunia, mali yangu yote, inayohamishika na isiyohamishika, igawanywe kama ifuatavyo;. 
  1. Nyumba iliyopo Kiwanja Namba 285 Kitalu J Ipagala Dodoma itakuwa mali ya mwanangu Kevin S. Tarimo.
  2. Nyumba iliyopo Kiwanja Namba 995 Kitalu E Tegeta-Dar-es-salaam itakuwa mali ya mwanangu Pamela S. Tarimo.
  3. Shamba la ekari tatu lililopo Himo litakuwa mali ya wazazi wangu Elimeleki Tarimo na Elisia Tarimo, ambalo watalitumia kama kitega uchumi chao. Baada ya maisha yao hapa duniani, shamba hilo litakuwa ni mali ya mwanangu Kevin S. Tarimo.
  4. Shamba la ekari tano lililopo Boko Dar-es-salaam likabidhiwe kwa Kanisa la TAG kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
  5. Nyumba na shamba lilipo katika kiwanja namba 993 Kitalu E Mbezi Beach-Dar-es-salaam vitakuwa mali ya mke wangu na atakuwa huru kuvitumia na baadaye kuvirithisha jinsi anavyoona inafaa.
  6. Gari aina ya Toyota RAV4 yenye namba za usajili T622AFB litakuwa mali ya mwanangu wa kike Pamela S. Tarimo na Gari aina ya Toyota Landcruiser yenye namba za usajili T323AGV litakuwa mali ya mwanangu wa kiume Kevin S. Tarimo.
  7. Gari aina ya Nissan Patrol yenye namba za usajili T238ADX niliyoipata kwa mkopo kazini itakuwa mali ya mke wangu Rehema Tarimo baada ya kulipa deni ninalodaiwa na mwajiri wangu.
  8. Fedha zote zitakazokuwa katika akaunti zangu za benki zilizopo Benki ya NBC Akaunti Na 23600055 na Benki ya NMB Akaunti Na 40002685 zitakuwa mali ya mke wangu Rehema Tarimo kwa ajili ya kujitunza yeye na wanangu wawili.
  9. Biashara ya vifaa vya ujenzi iliyopo Mwenge Dar-es-salaam itamilikiwa na kuendeshwa na mke wangu. Faida itakayopatikana itagawanywa sawasawa kati ya mke wangu na watoto wangu wawili, ambapo kila mmoja atapata theluthi moja (1/3) ya faida hiyo.
  10. Mke wangu atapewa fedha yangu yote ya pensheni ambapo atatumia asiliamia hamsini (50%) kwa ajili ya kuitunza familia yangu na asilimia nyingine hamsini (50%) kwa ajili ya uwekezaji na shughuli nyingine kama atakavyoona inafaa. 
  • Kwa wosia huu namchagua Remin Tarimo wa S.L.P 1309 Moshi kuwa msimamizi wa mirathi yangu. Natumaini atafanya kazi hii kulingana na taratibu za sheria zilizopo na kwa uaminifu mkubwa.
Wosia huu wa mwisho unafuta wosia mwingine wowote uliotangulia na umetiwa sahihi hapa (sahihi ya mume)………………………………

Tarehe:…………………………………………………………

Sahihi ya mke:……………………………………......

Mbele ya mashahidi wafuatao;

Shahidi wa kwanza: Sahihi……………………………………

Jina………………………………………

Anwani…………………………………..

Shahidi wa pili: Sahihi…………………………………….

Jina……………………………………….

Anwani…………………………………..

Utunzaji wa wosia
Wosia ni kitu nyeti sana. Tayari tumeshaona kuwa ni kitu kinachotambulika kisheria. Kwa sababu hiyo basi, ni lazima wosia utunzwe vizuri, ili utakapohitajika uweze kupatikana. Vinginevyo kunaweza kuzuka matatizo kama hautaonekana.

Kutokana na tamaa mbaya za wanadamu, wapo watu ambao hupanga njama za kudhulumu mali ya marehemu. Kama hakuna wosia ulioachwa, watu wengine wapo tayari kughushi wosia na kudai kuwa uliandaliwa na marehemu wakati akiwa hai. Wengine wakipata nafasi, wanaweza kufanya mabadiliko katika wosia ulioachwa na marehemu. Ndio maana upo umuhimu wa kutunza wosia mahali palipo salama kabisa.

Utunzaji wa wosia wa mdomo
Kama wosia ni wa mdomo, huu unaweza kutunzwa na mtu aliyependekezwa na marehemu ili awe msimamizi wa mirathi yake. Vile vile unaweza kutunzwa na mashahidi wa wosia huo. Ndugu wa marehemu, ambao sio warithi, nao wanaweza kuhusishwa katika utunzaji wa aina hii ya wosia.

Huko nyuma nilisema kuwa wosia wa mdomo ni lazima uwe umeshuhudiwa na mashahidi wasiopungua wanne, ikiwa ni pamoja na watu wa ukoo wasiopungua wawili. Hawa ndio wanaoweza kuandika tamko, au kauli, au maagizo ya marehemu, na baadaye wakayatoa wakati yatakapohitajika.

Utunzaji wa wosia wa maandishi
Wosia wa maandishi unaweza kutunzwa na msimamizi wa mirathi, au taasisi zinazoshughulika na utunzaji wa nyaraka mbalimbali. Baadhi ya taasisi hizo ni mahakama, mabenki, ofisi ya kabidhi wasii mkuu, vyombo vya kidini kama makanisa, ofisi za Mkuu wa Wilaya au Mkoa, na kadhalika.

Kutokana na mwamko na vile vile watu wengi kutambua umuhimu wa kuandaa wosia, siku hizi kumezuka mashirika, jumuia na taasisi mbalimbali za kijamii, ambazo zinatunza wosia. Wengine wanatoza ada kidogo. Ninakushauri msomaji utafute mahali vyombo hivi vilipo, ili upate maelezo ya kina kuhusu taratibu zao za utunzaji wa wosia, na vile vile namna ya kuuandika.

Ili kuelewa jinsi serikali ya nchi yetu inavyotilia maanani swala la wosia, hebu tusome ushauri uliotolewa na kiongozi mmoja mkubwa serikalini, kama ilivyotokea katika gazeti la Nipashe la tarehe 8 June 2008 chini ya kichwa cha habari kama ifuatavyo.

Wosia uandikwe na kuhifadhiwa maeneo salama-Wizara
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Bwana Sazi Salula ametoa wito kwa jamii kuandika na kuhifadhi wosia katika maeneo salama kama njia ya kuondokana na migogoro ya mirathi. Bwana Salula alisema hayo jana jijini Dar-es-salaam kwenye hafla ya uzinduzi wa huduma mpya ya kuhifadhi wosia iliyoanzishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Registration, Insolvency and Trusteeship Agency-RITA).

Alisema wanawake na watoto wamekuwa waathirika wakubwa ambao hudhulumiwa mali zao za urithi pindi wenzi ama wazazi wanapofariki bila kuacha wosia. Alisema wakati mwingine wosia umekuwa ukiandikwa bila kuhifadhiwa katika maeneo salama. “Watu wengi wamekuwa na mazoea ya kuhifadhi wosia kwenye uvungu wa vitanda, ambapo mara nyingi huangukia katika mikono ya watu wasiokuwa waaminifu”, alisema.

Aidha, Katibu Mkuu alisema watu wengi hudhani kwamba wasimamizi wa mirathi ndio warithi wa mali, hali ambayo husababisha malumbano yasiyokwisha katika familia nyingi. Alisema ili kuondoa tatizo la kudhulumiwa mirathi, ni vema watu wakawa na utamaduni wa kuandika na kuhifadhi wosia kupitia wakala.

“Kwa kiasi fulani elimu ya kuandika wosia katika jamii yetu ni nzuri, ila tatizo kubwa ilikuwa ni wapi pa kuhifadhi baada ya kuandika”, alisema. Aliongeza kuwa wakala umekuwa ukipokea maombi kutoka kwa watu kutaka huduma ya kuhifadhiwa wosia, ndio maana uamuzi wa kuanzishwa kwake ukafikiwa.

Alisema Watanzania wengi ni maskini, hivyo hawawezi kumudu gharama za kutunza wosia zao kwenye mabenki, ambayo yanafanya shughuli hiyo kibiashara. Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bwana Phillip Saliboko alisema kuwa, ingawa huduma hiyo imeanzia jijini Dar-es-salaaam, itaendelea kupanuka katika mikoa yote nchini.

Alisema huduma itaendelea kupanuka mikoani kwa kutumia mtandao wa ofisi za wakala ambazo ziko katika kila wilaya ya Tanzania Bara. Aliwataka wananchi kuondokana na dhana iliyojengeka kwamba kuacha wosia ni sawa na kujitabiria kifo au uchuro.

2 maoni:

Unknown said...

Mimi nahitwa Mr M.Mulokozi,
Mimi sina comment ila nina swali,kwamba wasimamizi wa mirathi wasio waaminifu ktk sheria ya Mirathi ya Tanzania wanachukuliwa hatua gani ili kudhibiti tabia hiyo,endapo wamebainika na kosa hilo?

Unknown said...

Barikiwa hadi ushangae kwa kutoa Elimu hii ,naitwa Mary Mwita ,Mwandishi wa habari na Mwanasheria umenibariki sana

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).