Friday, June 5, 2009

URITHI: Je, urithi ni haki au ni fadhila?

Baada ya kuangalia kwa kina maana ya urithi, matatizo yanayohusiana na jambo hili, pamoja na sheria za mirathi, sasa linakuja swali moja ambalo ni muhimu sana. Nalo ni je, hivi urithi ni haki ya mtu au ni fadhila tu anayopata kutoka kwa yule mwenye kurithisha? Jibu la swali hili ni muhimu sana, hasa kunapotokea tatizo la mtu kunyimwa urithi.

Msomaji utakumbuka kwamba mwanzo kabisa wa makala haya, nilitoa tafsiri ya neno urithi. Kwa kukumbushia nilisema kuwa urithi ni mali au vitu ambavyo mtu hupokea na kuvimiliki baada ya mmiliki wa mali hiyo kufariki. Tuliona kuwa mrithi ni lazima awe na uhusiano wa kindugu au wa kindoa kati yake na marehemu.

Kutokana na tafsiri ya urithi, tunaweza kuona kuwa mmiliki wa mali hana uhuru kamili wa kurithisha mali yake kwa mtu yeyote anayemtaka. Wapo watu maalumu wanaotambulika na jamii pamoja na sheria za nchi kwamba wao ndio wanaostahili kurithi. Kama hivyo ndivyo, ndio kusema kuwa urithi ni haki au stahili ya mtu fulani na sio fadhila au huruma kwake.

Hapa naomba nitoe angalizo kuwa urithi unaweza kuwa ni fadhila pale ambapo unarithishwa kwa mtu asiye na undugu wa uzawa au ndoa na mwenye kumiliki mali hiyo. Msomaji utakumbuka kuwa huko nyuma nilisema kwamba mmiliki wa mali anaweza kuwarithisha watu wasio na undugu naye, au mifuko ya maendeleo, taasisi mbalimbali, na kadhalika. Urithi wa namna hii ni fadhila na sio haki unayoweza kuidai.Yapo mambo ya kuthibitisha

Pamoja na urithi kuwa ni haki ya mtu, huyo mwenye stahili hiyo ana wajibu wa kutimiza masharti fulani au kuthibitisha mambo kadhaa. Kama ni mke, ni lazima jambo hili lithibitike kulingana na sheria za nchi au taratibu za jamii.

Kwa mfano, ni lazima awe na cheti cha ndoa, au ndugu pamoja na jamii wawe wanamtambua kwamba alikuwa mke wa marehemu. Sio mtu anazuka tu baada ya kifo, na kudai kwamba yeye ni mke wa marehemu, wakati hana uthibitisho wowote.

Kama ni watoto, ni lazima wawe wanatambulika hivyo tangu uhai wa marehemu baba yao. Sio mtoto anaibuka baada ya kifo, halafu analeta utata juu ya uhalali wake wa kurithi mali ya marehemu. Kwanini ninayasema haya?
Unaweza kuthibitisha uhalali wa mtoto

Ukweli ni kuwa katika jamii yetu, wapo watu ambao huzaa nje ya ndoa na kuficha jambo hilo. Watu hao wanaweza kuwa aidha wanaume, au wanawake. Kifo kinapotokea, mtoto au watoto wa nje huweza kujitokeza wakati wa msiba, na kudai haki ya kurithi.

Wakati mwingine kuna kusingiziwa. Nafikiri wengi wetu tumewahi kusikia visa vya wanaume waliosingiziwa watoto na wanawake ambao pengine waliwahi kutembea nao. Jambo kama hili lisiposhughulikiwa vema, linaweza kuleta utata au mtafaruku wakati wa kurithi.

Kwa bahati nzuri kutokana na maendeleo ya sayansi na tekinolojia, siku hizi kuna vipimo vya nasaba (DNA Test), ambavyo vinaweza kubainisha baba wa mtoto ni nani. Ili kukata maneno na kuepusha shari, kama ukijikuta katika utata kuhusu uhalali wa mtoto, unaweza kufanya kipimo hiki.
Usiishi kienyeji, weka mambo yako hadharani

Watu wengine huoa au huishi na mwanamke (au mwanaume) kwa siri. Unakuta ndugu na jamaa hawana habari kabisa juu ya jambo hili. Kwa mfano unakuta mwanamume alitoka kwao kijijini miaka mingi iliyopita, akaja mjini kutafuta maisha. Huku akakutana na mwanamke, halafu wakaishi kinyumba na kujaliwa watoto bila kuwa na ndoa rasmi, wakati ndugu kule alikotoka hawana habari.

Ingawa ni kweli mwanamume anaweza kuwa na mke pamoja na watoto kwa siri, jambo hili lisipowekwa sawa sawa kulingana na sheria za nchi, hao warithi wanaweza kupoteza haki ya kurithi. Ndio maana huko nyuma nilisema kuwa ni muhimu sana maswala ya ndoa yaendeshwe kulingana na sheria za nchi. Ni vema mume na mke wawe na cheti cha ndoa; sio wanaishi kienyeji.
Biblia inasema nini kuhusu haki ya kurithi.

Hebu sasa tuigeukie Biblia tuone jinsi nayo inavyoonyesha kwamba urithi ni haki ya mtu, na sio fadhila au huruma. Tuanze kwa kuangalia kile kisa cha mwana mpotevu. Huyu kijana alipokuwa mtu mzima, alimwendea baba yake na kudai apewe sehemu yake ya urithi. Biblia inatuambuia kuwa, “yule mdogo akamwambia babaye, ‘Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia” (Luka 1512)

Maneno ‘Baba nipe’ hayaonyeshi mtu anayeomba fadhila. Hapana. Yanaonyesha mtu anayedai kilicho chake. Yule mwana mdogo alitambua haki yake ya kurithi. Ndio maana alidai haki hiyo kutoka kwa baba yake, na sio kuiomba. Na ukweli ni kwamba katika maisha ya kawaida, huwa tunadai haki zetu. Huwa hatuziombi.

Tambua haki zako

Sehemu nyingine inayoonyesha kwamba urithi ni haki ni katika kile kisa cha mtu aliyemtaka Bwana Yesu aingilie kati ugomvi wa urithi ulikuwapo kati yake na nduguye. Biblia inatuambia kuwa, “Mtu mmoja katika makutano akamwambia, ‘Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu” (Luka 12:13).

Yule mtu alitambua haki yake ya kurithi. Alitambua kuwa ule urithi ni halali yake yeye pamoja na ndugu yake. Kwahiyo alikuwa haombi kuhurumiwa. Alikuwa anadai kilicho chake kwa kumtaka Bwana Yesu amwagize nduguye ampe haki yake ya urithi.

Baadaye tutaona kuwa, mtu anayestahili kurithi anaponyimwa haki hiyo, anaweza kulalamika kwa mrithishaji, au mbele ya ukoo au hata mahakamani. Tutaona kuwa mahakama inaweza kumrejeshea au kumpa haki hiyo.

Vile vile katika sehemu ya pili ya makala haya tutaona kuwa mambo kama kubarikiwa na Mungu, au kurithi uzima wa milele, ni haki ya mwamini. Tutaona kuwa haki zinakuja au zinakuwa dhahiri baada ya mwamini kutimiza masharti kadhaa yanayoambatana na haki hizo.

0 maoni:

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

Recent Posts

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).