Friday, June 5, 2009
URITHI: HAKI NA WAJIBU WAKO
SEHEMU YA KWANZA: URITHI KUTOKA KWA WANADAMU
Utangulizi
Urithi au kitendo cha kurithi ni jambo ambalo lipo katika jamii yetu. Limekuwepo katika jamii ya wanadamu tangu kuumbwa kwa ulimwengu huu tulio nao. Ukichunguza kwa makini utagundua kuwa, hakuna mtu ambaye hajawahi kukutana na jambo hili, aidha akiwa ni mrithi au mrithishaji.
Kutokana na kuwepo kwa swala la kurithi, tangu zamani kulikuwa na taratibu zilizokuwa zinasimamia jambo hili. Mababu zetu walitambua uzito wake na katika makabila mbalimbali kulikuwa na kanuni zilizokuwa zinasimamia swala hili. Kulikuwa na mila na desturi zilizokuwa zinatawala maswala yote ya urithi, na watu walizitambua na kuziheshimu.
Katika miaka ya sasa, ambapo mfumo wa utawala upo katika sura ya serikali mbali mbali, utakuta nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, zina sheria zinazosimamia maswala ya urithi. Kutokana na unyeti wa jambo hili, watu hawakuachwa warithishe au warithi vyovyote vile wanavyotaka. Hapana. Zipo sheria zilizotungwa na Bunge, au mabaraza ya kutunga sheria, zinazoelekeza mambo ya kufanya wakati wa kurithisha au kurithi.
Swala la urithi linajitokeza katika Agano la kale
Tunapoichunguza Biblia kwa makini tunagundua kuwa hata yenyewe haikukaa kimya kuhusu swala la kurithi. Yapo maandiko mengi sana yanayozungumzia maswala ya urithi. Kwa mfano katika Agano la Kale, jambo hili lilijitokeza katika familia ya Ibrahimu, baba yetu wa imani.
Kwanza tunaona Sara akikataa Ishmaeli, mtoto ambaye Ibrahimu alimzaa na binti wa kazi, asirithi. Biblia inatuambia kuwa, “Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwahiyo akamwambia Ibrahimu, ‘Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka”. (Mwanzo 21:9-10).
Baadaye tunaona jinsi ambavyo Ibrahimu aligawa urithi kwa mwanawe Isaka, pamoja na watoto aliowazaa na wanawake wengine. Tunaambiwa kuwa, “Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu” (Mwanzo 25:5-6).
Katika Agano hilo hilo la kale tunaona swala la urithi likijitokeza katika kitabu cha Waamuzi, ambapo ndugu za mtu mmoja aliyeitwa Yeftha walimkatalia asirithi pamoja nao mali iliyokuwa ya baba yao. Tunasoma kwamba, “Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha. Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, ‘Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine” (Waamuzi 11:1-3).
Swala la urithi linajitokea katika Agano Jipya
Tunapokuja katika Agano Jipya napo tunaona swala la urithi likijitokeza kwa namna mbalimbali. Mfano mzuri ni kile kisa cha mwana mpotevu (Luka 15:11-32), ambacho nina imani wengi wetu tunakifahamu.
Katika kisa hiki, kijana mmoja alimdai baba yake ampe sehemu ya mali aliyostahili kupewa kama urithi wake. Baada ya kugawiwa sehemu yake, alisafiri kwenda nchi ya mbali, na huko akaponda maraha mpaka akaishiwa kabisa. Hatimaye akarudi nyumbani kwa baba yake.
Mahali pengine ambapo swala la urithi linajitokeza ni wakati mtu mmoja alipomwomba Bwana Yesu aingilie kati ugomvi wa urithi uliokuwepo kati ya mtu huyo na nduguye. Tunaambiwa kuwa, “Mtu mmoja katika mkutano akamwambia, ‘Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu”.
Nafikiri msomaji mpaka sasa utakubaliana nami kuwa swala la urithi limekuwa likijitokeza katika jamii tunayoishi kwa namna mbalimbali. Katika maandiko niliyonukuu utaona kuwa urithi umetajwa katika hali ya tatizo. Kwahiyo sio kitu cha kuchukulia kijuu juu. Hapana. Ni vizuri kuwa makini na jambo hili, vinginevyo linaweza kuleta mtafaruku kati ya wanandugu, familia na jamii kwa ujumla.
Lengo la makala
Katika makala haya, ambayo nimeyagawa katika sehemu mbili, ninalenga kuangalia swala la urithi kama lilivyo katika jamii ya Kitanzania. Sehemu ya kwanza, ambayo inahusu urithi kutoka kwa mwanadamu mmoja kwenda kwa mwanadamu mwingine, nitazungumzia mambo yafuatayo;
Maana au tafsiri ya urithi.
- Vitu ambavyo mtu anaweza kuvirithi kutoka kwa mwanadamu mwenzake.
- Matatizo yanayohusiana na urithi
- Watu wanaostahili kurithi
- Sheria zinazotumika kusimamia maswala ya urithi hapa Tanzania.
- Wakati wa kurithi au kurithisha.
- Umuhimu na namna ya kuandika wosia.
- Usimamizi wa mirathi.
Katika sehemu ya pili, ambayo inahusu urithi kutoka kwa Mungu kwenda kwa wanadamu, nitazungumzia mambo yafuatayo;
- Nitaonyesha kuwa hata Mungu huwa anarithisha.
- Nitaainisha vitu au mambo ambayo sisi wanadamu tunaweza kurithi kutoka kwa Mungu.
- Nitafafanua wanaostahili kurithi kutoka kwa Mungu.
- Nitaelezea wakati wa kurithi.
- Nitaonyesha ni kwanini Wakristo wengi wanashindwa kurithi kutoka kwa Mungu.
- Nitamalizia kwa kueleza jinsi sisi wanadamu tunavyoweza kurithi kutoka kwa Mungu.
0 maoni:
Post a Comment
Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.