Friday, June 5, 2009

URITHI: Kiini cha makala

Sasa msomaji wangu, katika sehemu hii ya kwanza ya makala haya sitazungumzia urithi wa vitu kama uchawi, sura, tabia au maumbile. Hapana. Hayo nimeyataja tu, ili mada iweze kueleweka vema.

Ninachotaka kuzungumzia ni urithi wa mali au vitu vya kushikika. Vitu kama mashamba, mifugo, viwanja, magari, majumba, maduka, viwanda na fedha. Hivi ndivyo tutakavyovizungumzia kwa kina, ila kwa sasa hebu tuangalie matatizo yanayohusiana na urithi.

Matatizo ya urithi
Ukweli ni kuwa, kwa upande mmoja, urithi ni jambo zuri. Lakini kwa upande mwingine, sio jambo la kupendeza, hasa mtu anaporithi vitu kama madeni, matatizo, majukumu ya kutunza familia ya marehemu na kadhalika. Hapo ndipo mara nyingi furaha ya kurithi inapotoweka. Na kwa jinsi binadamu wengi wasivyo wema, hukimbilia kurithi yale mambo mazuri kama vile mali za marehemu, halafu wanakimbia majukumu yaliyoachwa nyuma.

Tatizo lingine linaloweza kujitokeza wakati wa kurithi au kurithisha ni swala la haki ya urithi; kwamba ni nani hasa anastahili kupata sehemu ya mali iliyoachwa? Tatizo hili lisiposhughulikiwa vema, kunaweza kutokea ugomvi wakati wa kugawa urithi. Hili nitalieleza kwa kina huko mbeleni. Matatizo mengine ni kama dhuluma, kutapanya, utunzaji au uendelezaji wa mali ya marehemu, na kadhalika.

Serikali nyingi duniani zinafahamu matatizo yanayohusiana na urithi. Ndio maana zinatungwa sheria za kusimamia jambo hili. Baadaye nitaeleza sheria hizo. Kwa sasa hebu tuigeukie Biblia, tuone jinsi matatizo ya urithi yalivyojitokeza, na namna yalivyoshughulikiwa.

Ibrahimu na Sara walitofautiana
Tuanze na tatizo lililojitokeza katika familia ya Ibrahimu, baba yetu wa imani. Hili linahusu haki ya kurithi. Msomaji utakumbuka kuwa, Ibrahimu alimzaa Ishmaeli kwanza, halafu baadaye ndipo akamzaa Isaka. Lilipokuja swala la nani hasa awe mrithi kati ya hawa watoto wawili, tunaona kuwa haki hiyo ilienda kwa Isaka, mwana wa Sara.

Biblia inatuambia kuwa, “Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwahiyo akamwambia Ibrahimu, ‘Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka” (Mwanzo 21:9-10).

Hapa tunaona Sara akikataa Ishmaeli, mwana wa mjakazi, asipate urithi. Msimamo wa Sara ulikuwa ni tatizo kubwa kwa Ibrahimu, ambaye ndiye alikuwa mrithishaji, na vile vile watoto wote ni wa kwake, bila kujali ni wa kambo au la.

Tunaambiwa kuwa, “Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe” (Mwanzo 21:11). Yaani msimamo wa Sara ulimsononesha sana Ibrahimu. Kwanini? Kwa sababu yeye kama baba au mzazi, alimpenda pia mwanawe Ishmaeli, na alitaka naye arithi sehemu ya mali yake.

Tunaona kuwa tayari kulikuwa na mitizamo tofauti kati ya Ibrahimu na mkewe. Tunaweza kusema kuwa kulikuwa na mvutano au ugomvi kati ya wanandoa hawa. Bahati nzuri Mungu aliingilia kati tatizo lao, akaweka mambo sawa.

Biblia inatuambia kuwa, “Mungu akamwambia Ibrahimu, ‘Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake” (Mwanzo 21:12).

Msimamo wa Mungu kuhusu tatizo la mtoto wa kambo

Katika tatizo la Ibrahimu na Sara tunaweza kuona kwamba Mungu alikubaliana na msimamo wa Sara. Kwamba Ishmaeli, mwana wa mjakazi, hana haki ya kurithi. Kwahiyo alifukuzwa yeye pamoja na mama yake.

Tunaambiwa katika Mwanzo 21:14 kuwa, “Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba”. Loo! Ilikuwa inasikitisha kweli.

Sikiliza msomaji. Kwa upande wa Sara, Ishmaeli ni mtoto wa kambo, hata kama yeye ndiye aliyetangulia kuzaliwa; hata kama Sara alimruhusu mumewe alale na yule mjakazi. Tatizo la urithi lilipojitokeza, msimamo wa Mungu ukawa kwamba mtoto wa kambo hana haki ya kurithi. Baadaye tutaona kuwa hata sheria zetu hapa Tanzania haziruhusu mtoto wa kambo kurithi, labda kuwe na makubaliano kati ya wanandoa.

Pengine msomaji sasa unajiuliza mbona Mungu aliruhusu jambo baya kama hilo litendeke? Mbona aliruhusu mama na mwanae, watu wasio na hatia, wasipate urithi; na pia wafukuzwe nyumbani? Je, Mungu ni katili? Maswali kama haya nitayatolea ufafanuzi huko mbeleni. Kwahiyo msomaji tuendelee kuwa pamoja.
Yeftha alikataliwa asirithi

Mfano mwingine unaoonyesha tatizo la urithi tunaupata katika kitabu cha Waamuzi 11:1-2. Huu unamhusu mtu mmoja aliyeitwa Yeftha. Tunaambiwa kuwa, “Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha. Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa, wakamtoa Yeftha, na kumwambia, ‘Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine”.

Hapa tunaona kuwa Gileadi, baba yake Yeftha, alitangulia kuzaa na kahaba mmoja. Baadaye akaoa mke rasmi, ambaye alimzalia wana. Wale wana walipokua wakubwa, wakamfukuza Yeftha, ili asirithi nao mali za baba yao.

Yeftha alikuwa ni kaka wa wale watoto wengine, lakini mama zao walikuwa tofauti. Pamoja na hayo, hakuweza kurithi chochote kutoka kwa baba yake. Hili nalo lilikuwa ni tatizo kwa namna moja au nyingine.

Ukweli ni kuwa, kwa upande wa wale watoto wengine na mama yao, Yeftha ni mtoto wa kambo. Msimamo wao ni kwamba huyo hawezi kurithi pamoja nao. Na hicho ndicho kilichotokea. Biblia inatuambia kuwa, “Ndipo Yeftha akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu” (Waamuzi 11:3a).

Msomaji kama uko makini, utakubaliana nami kuwa matatizo kama haya ya akina Ishmaeli na Yeftha kukosa urithi yapo katika familia au jamii zetu. Unakuta watoto wa kambo nao wanataka kurithi, lakini wanakataliwa. Kama matatizo haya yasiposhughulikiwa vizuri, yanaweza kuleta uhasama mkubwa kati ya ndugu au familia.

Tatizo la dhuluma
Hebu tuangalie tatizo lingine la kurithi kama linavyojitokeza katika Biblia. Wakati wa huduma yake hapa duniani, kuna siku Yesu aliombwa aingilie kati ugomvi uliokuwepo kati ya ndugu wawili. Tunaambiwa kuwa, “Mtu mmoja katika mkutano akamwambia, ‘Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu” (Luka 12:13).

Hapa tunaona ndugu mmoja akiwa amekataa kumgawia mwenzake sehemu ya urithi ambao waliachiwa kwa pamoja. Huu ni uchoyo; ni tamaa; ni dhuluma. Na kusema kweli mambo kama haya yapo katika jamii yetu. Wengine hufikia hatua ya kutoana roho kwa sababu ya kugombea urithi.


Yakobo alimdhulumu Esau

Katika Biblia tunacho kile kisa cha Yakobo na Esau, ambacho naamini wengi wetu tunakifahamu. Ukweli ni kuwa kwa upande mmoja, Yakobo alimdhulumu kaka yake haki ya kubarikiwa. Matokeo yake ni kwamba, kidogo tu angetolewa roho. Tunaambiwa kuwa, “Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo” (Mwanzo 27:41).

Kilichomwokoa Yakobo ni kwamba, taarifa za mipango ya kumwua zilimfikia Rebeka mapema. Siri ilifichuka. Kwahiyo mama yake alimhamisha kutoka nyumbani, akamficha kwa mjomba wake (Mwanzo 27:42-45). Watu wengine katika jamii huwa hawana bahati kama ya Yakobo. Wanapodhulumu wanaweza kuuawa. Hiyo ndiyo hali halisi.

Wanaodhulumiwa ni wengi
Wanaodhulumiwa ni pamoja na wajane, yatima, au watu wasio na uwezo. Biblia inatambua tatizo hilo na ndio maana imelizungumzia sana katika sehemu mbalimbali. Kwa mfano katika Zekaria 7:9-10 imeandikwa hivi, “Bwana wa majeshi asema hivi, ya kwamba, fanyeni hukumu za kweli, kila mtu na amwonee ndugu yake rehema na huruma; tena msidhulumu mjane, wala yatima, wala mgeni, wala maskini; wala mtu awaye yote miongoni mwenu asiwaze mabaya juu ya ndugu yake moyoni mwake”.

Je, ni watu wangapi katika kizazi cha leo wanaozingatia haya maneno ya Mungu? Je, ni wangapi walio na huruma; wasiodhulumu? Je ni wangapi wanaowapa haki zao wajane, yatima na wahitaji wengine? Kusema kweli ni wachache sana. Hata pale sheria zinapotungwa, bado wapo wanaodhulumu. Hilo ndio tatizo la jamii yetu.

Tatizo la kutapanya
Hebu tuangalie tatizo la mwisho ambalo linaweza kujitokeza wakati wa kurithi. Hili linahusu kutapanya mali ya urithi. Wakati mwingine hutokea kwamba mtu ambaye amerithi mali, anaitumia ovyo ovyo mpaka inaisha kabisa. Unakuta mtu amerithishwa vitu kama nyumba, au fedha, au nyumba, au biashara fulani, na kadhalika. Akiisha kuvikamata tu, anaingia kwenye ‘matanuzi’ mpaka anajikuta ameshauza kila kitu alichorithi. Hili nalo ni tatizo kubwa katika jamii yetu.

Biblia nayo ina kisa cha mrithi aliyetapanya mali ya urithi, badala ya kuiendeleza. Hiki ni kisa cha yule mwana mpotevu, ambacho kipo katika Injili ya Luka 15:11-18. Nafikiri wengi wetu tunakifahamu, hivyo sina haja ya kukisimulia tena.

Swali la kujiuliza ni je, tunakabiliana vipi na tatizo la kutapanya? Je, tutafanya nini iwapo mrithi anaonekana kama vile akiisha kupokea sehemu yake ya urithi, ataitapanya? Je, tunaweza kumnyima haki ya kurithi? Nitajaribu kuyatolea majibu ya maswali yote haya kwa kuangalia sheria zinazotumika hapa nchini. Kwa sasa hebu tuangalie ni nani hasa mwenye haki ya kurithi mali za marehemu.

0 maoni:

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).