Friday, June 5, 2009

Baraka ni urithi kutoka kwa Mungu
Jambo lingine ambalo mwanadamu anaweza kurithi kutoka kwa Muumba wake ni baraka za aina mbalimbali. Katika 1Petro 3:8-9 imeandikwa hivi, “Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitivu, wenyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka”.

Wanaoambiwa maneno haya ni watu wa Mungu. Ni wakristo waliookoka. Lakini jambo la kuzingatia hapa ni kuwa, watu hawa wameokolewa na wanatakiwa wawe na mwenendo mwema, ndipo wapate kurithi hizo baraka.

Aina za baraka
Nimesema kuwa mtu anaweza kurithi baraka za aina mbalimbali. Tunapolichunguza neno la Mungu kwa makini tunaweza kuona kwamba, baraka kutoka kwake zimegawanyika katika makundi makubwa mawili. Yaani baraka za mwilini na baraka za rohoni. Nitafafanua jambo hili baadaye kidogo, lakini kwa sasa hebu tuangalie maana ya baraka.

Maana ya baraka
Kamusi ya Kiswahili sanifu inaeleza kuwa baraka ni mambo mema kwa ujumla. Inatumia maneno kama mafanikio, fanaka, ustawi, neema, heri. Vile vile inaeleza kuwa baraka ni hali ya mtu kuwa na vitu vingi kama vile majumba, fedha, mifugo na kadhalika.

Swali ninalotaka tujiulize hapa ni je, hivi mtu akiwa na vitu vingi katika maisha yake, tunaweza kusema kuwa huyo amebarikiwa? Kwa haraka haraka jibu linaweza kuwa ni ndio. Lakini sivyo ilivyo katika maana ile ambayo binafsi ninamaanisha. Kwahiyo jibu sahihi ni ndiyo na hapana. Nitafafanua.

Unaweza kufanikiwa bila Mungu kuhusika
Baraka ninazotaka kuzungumzia katika makala haya ni zile ambazo Mungu amehusika kikamilifu. Ukweli ni kuwa duniani wapo watu wenye mali au mafanikio katika maisha yao, lakini Mungu hakuhusika katika upatikanaji wake. Pengine msomaji unajiuliza jambo hilo linawezekana vipi?

Hebu fikiria mtu ambaye amefanikisha mambo yake kwa kutimiza masharti aliyopewa na mganga wa kienyeji. Kwa akili ya kibinaadamu, ni rahisi kusema kuwa mtu kama huyo ana mafanikio. Lakini ukweli ni kuwa, nguvu iliyo nyuma ya mafanikio kama haya ni ya kishetani. Hiyo sio aina ya baraka ninayomaanisha katika makala haya.

Juhudi binafsi zinaweza kukufanikisha
Wakati mwingine mtu anaweza kufanikisha mambo yake kwa juhudi zake binafsi, bila kutafuta msaada wa Mungu au kwenda kwa waganga wa kienyeji. Unakuta mtu ni mchapakazi, wala huwa haendi kanisani. Mtu kama huyu anaweza kufanikiwa kimaisha, lakini nguvu ya Mungu inakuwa haipo kabisa katika mafanikio yake.

Ukweli ni kuwa kuna kanuni ambazo Mungu ameziweka kwa wanadamu wote, bila kujali ameokoka au la. Mtu akifuata kanuni hizo, anaweza kufanikiwa kimaisha. Mfano mzuri ni huu wa kufanya kazi kwa bidii.

Kanuni ya kufanya kazi kwa bidii itakufanikisha.
Mtu yeyote akifanya kazi kwa bidii anaweza kufanikiwa. Watu kama Wajapani au Wachina hawamwabudu Mungu muumba wa mbingu na nchi. Lakini watu hawa ni wachapakazi kweli kweli. Na kwa sababu hiyo nchi zao zimeendelea. Ni tajiri pengine kuliko nchi ambazo zina wakristo wengi.

Baraka ninayotaka kuizingumzia katika makala haya ni ile ambayo Mungu amehusika kikamikifu. Ni ile ambayo Yeye ndiye mwanzilishi na mshauri wake mkuu tangu mwanzo mpaka mtu anapojikuta tayari amefanikiwa. Hii ndiyo tutakayoizungumzia kwa kina.

Tofauti kati ya kubarikiwa na kufanikiwa kusikokuwa na uhusiano na Mungu
Labda kwa manufaa ya wasomaji, nitoe tofauti chache kati ya kubarikiwa na mafanikio ambayo chanzo chake sio Mungu. Tuanze kwa kuangalia andiko la Mithali 10:2 linalosema, “Hazina za uovu hazifaidii kitu; bali haki huokoa na mauti”.

Tunaweza kuona katika andiko hili kwamba, mtu anaweza kupata mali kwa njia ya uovu. Biblia inatuambia kwamba utajiri kama huo hauna faida au manufaa kwa mtu huyo. Sana sana utakuwa umeambatana na matatizo kibao.

Mafanikio yanayotokana na Mungu yana manufaa mengi. Kwa mfano yanakuwa hayana majuto au mahangaiko. Hili lipo wazi tunaposoma Mithali 10:6 ambapo tunaambiwa kuwa, “Baraka ya Bwana hutajirisha, wala hachanganyi huzuni nayo".

Utajiri kutoka kwa Mungu hudumu
Utajiri unaotokana na Mungu hupatika kwa njia za haki, na vile vile hudumu kwa muda mrefu. Hiki ndicho Mungu anachotuambia katika Mithali 8:18 kwamba, “Utajiri na heshima ziko kwangu, naam, utajiri udumuo, na haki pia”.

Nafikiri wengi wetu tumewahi kukutana au kusikia visa vya watu ambao hapo zamani walikuwa ni matajiri sana, lakini sasa wamefilisika. Moja ya sababu ambayo iliwafanya wafilisike ni kwamba, walipata mali hiyo kwa njia za uovu. Kwa njia ya dhuluma, udanganyifu, wizi, ulaghai na kadhalika.

Katika Yeremia 17:11 tunaambiwa kuwa, “Kama kware akusanyaye makinda asiyoyazaa, ndivyo alivyo mtu ajipatiaye mali, wala si kwa haki, katikati ya siku zake zitaachana naye, na mwisho wake atakuwa mpumbavu”

Hapa Biblia inatuthibitishia kuwa, mali isiyopatikana kwa haki huwa haidumu. Yaani mtu anafilisika katikati ya maisha yake, na mwishowe anakuwa hana kitu kabisa. Anaonekana kama juha. Hili ndilo tatizo la mali iliyopatikana kwa njia za uovu.

Aliyebarikiwa ni mkarimu

Mara nyingi mtu aliyebarikiwa na Mungu ni mkarimu mno. Ni mtoaji kwa ajili ya kazi ya Mungu. Na hili ndio moja ya lengo kuu la Mungu la kuwabariki watu wake. Kwamba wautumie utajiri huo au mafanikio hayo kwa ajili ya kuueneza ufalme wake hapa duniani.

Katika 2Wakoritho 9:8 imeandikwa hivi, “Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika tendo jema; kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, haki yake yakaa milele”.

Katika Biblia tuna kisa cha tajiri mmoja ambaye alikuwa hana tone la ukarimu. Huyu sio mwingine bali ni Nabali. Unaweza kusoma kisa cha mtu huyu katika 1Samweli 25:2-42.

Kwa kifupi ni kuwa Daudi alituma vijana wake ili wakaombe msaada wa chakula kutoka kwa Nabali. Biblia inatuambia kuwa, “Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, ‘Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake. Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya ya kondoo zangu, na kuwapa watu ambao sijui wametoka wapi?.(1Samweli 25:10-11)

Msomaji nafikiri unaweza kuona jinsi Nabali alivyojibu kwa jeuri na dharau. Majibu kama haya mara nyingi ni ya watu waliofanikiwa, lakini Mungu hana nafasi katika mioyo yao. Ni kama yule waziri fulani aliyefanya ufisadi wa kuiba fedha za umma, halafu alipoulizwa akatamka kwa dharau kubwa, eti ni vijisenti tu.

Jeuri ya fedha isiyo na uhusiano na Mungu haimfikishi mtu mbali. Nabali hakufika mbali. Alikufa baada ya muda mfupi tu. Yule waziri hakufika mbali. Punde akapoteza kazi yake. Hayo ndio matokeo ya utajiri ambao Mungu hakuhusika. Msomaji nisingetaka wewe nawe uwe na utajiri wa namna hii.

Baraka za rohoni
Baada ya kufafanua maana halisi ya baraka, hebu sasa tuendelee kuangalia aina za baraka. Tayari nimeshasema kwamba kuna baraka za rohoni na za mwilini. Tuanze na baraka za rohoni.

Kwanza kabisa tuanze kwa kujiuliza swali hili; je, ni kweli kuna baraka za rohoni? Ili kupata jibu sahihi, hebu tusome Waefeso 1:3 ambapo tunambiwa kuwa, “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo”.

Andiko hili linatuonyesha wazi kuwa Mungu huwabariki wanadamu kwa baraka za rohoni. Baraka hizi hupitia kwa mwanawe Yesu Kristo. Huyu ndiye ambaye huko nyuma tuliona kuwa amekabidhiwa vitu vyote na Mungu , kwa ajili ya kanisa (Waefeso 1:22).

Baraka za roho ni zipi?
Baraka za roho ni mambo ambayo hayaonekani kwa macho ya kawaida, lakini utendaji wake unaweza kudhihirika kwa matendo au matokeo katika ulimwengo wa mwili. Uridhihiko huu hutokea pale baraka hizo zinapotumika au zinapokuwa kazini. Ili jambo hili lielewewke vema, nitatoa mifano michache.

Tayari tumeshaona kuwa baraka za rohoni ni urithi kutoka kwa Mungu. Vitu vya rohoni ambavyo mwanadamu anaweza kuvipata kutoka kwa Mungu ni kama vile ujazo wa Roho Mtakatifu, karama au vipawa mbalimbali, na kadhalika.Vitu hivi havionekani kwa macho ya nyama, lakini vinapotumiwa ndipo matokeo yake yanaweza kudhihirika kwa watu.

Ujazo wa Roho Mtakatifu
Katika Matendo ya Mitume 1:8 imeandikwa hivi, “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi”.

Tunaweza kuona katika andiko hili kuwa, chanzo au anayewagawia watu Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe. Sio mwanadamu, ingawa mwanadamu anaweza kumwekea mtu mikono, halafu mtu huyo akapokea ujazo wa Roho Mtakatifu.

Hiki ndicho kilichotokea katika Matendo ya Mitume 19:5 ambapo tunaambiwa kuwa, “Na Paulo alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha , na kutabiri”.

Kinachoonekana ni matokeo
Sasa ukweli ni kuwa hakuna mtu anyeweza kumwona Roho Mtakatifu. Kinachoonekana ni matokeo ya Yeye kuingia ndani ya mwamini. Matokeo hayo ni pamoja na kunena kwa lugha mpya (Matendo 2:1-2) au kuwa na nguvu pamoja na ujasiri wa kuhubiri au kushuhudia habari za Bwana Yesu kama alivyofanya Stefano (Matendo 7:51-60).

Katika Yohana 14:16-17 Yesu alisema kuwa, “nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli,; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa ndani yenu”.

Maneno haya yanatuthibitishia kuwa Roho Mtakatifu huwa haonekani kwa macho ya kawaida, wala mtu ambaye hajaokoka hawezi kumtambua. Wanaomtambua ni wale tu waliookoka na kujazwa Roho Mtakatifu. Jambo hili nitalifafanua zaidi huko mbeleni, nitakapokuwa naeleza nani anastahili kurithi baraka za Mungu.

Karama za rohoni hutoka kwa Mungu

Mungu huwagawia au huwarithisha wanadamu karama za rohoni. Katika 1Wakorintho 12:4-11 zimeorodheshwa karama za namna mbalimbali, utendaji wake na chanzo chake. Mstari wa 11 unamalizia kwa kusema, “Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.

Sikiliza msomaji. Karama hutoka kwa Mungu; halafu Yeye huzigawa kwa waumini wake kama atakavyo na sio kama wao wanavyotaka. Ninayasema haya kwa sababu kuna wakristo ambao hulazimisha karama fulani. Wengine hujifanya kwamba wao wana kila aina ya karama au wanaweza kufanya kila kitu peke yao.

Hakuna muumini, kikundi au kanisa linaloweza kusimama peke yake
Kulingana na neno la Mungu, hakuna muumimi anayeweza kufanya kila kitu peke yake. Kwanza kabisa, sote tunafahamu mambo ya Mungu kwa kiasi au kiwango fulani tu (1Wakorinho 13:9). Hatufahamu kila kitu. Halafu kila mtu hupewa karama ya aina fulani. Anaweza kupewa karama mbili tatu, lakini hapewi zote.

Pamoja na mambo mengine, nia ya Mungu ya kutupatia karama chache ni ili tushirikiane. Ni ili tutambue kuwa kila mwenye karama fulani anamuhitaji muumini mwingine mwenye karama iliyo tofauti na ya kwake.

Lengo la Mungu ni kutuondolea kiburi na kudharauliana. Ni ili tutambue kwamba sote tu viungo vya Kristo (1Wakorintho 12:12-27) na kwamba kila kiungo, au kila muumini, au kila kikundi au kila kanisa linalihitaji kanisa lingine. Kwamba tunahitajiana. We need one another.

Kanisa linatakiwa likamilike katika umoja

Mambo yalivyo kwa sasa ni kwamba, ushirikiano kati ya wakristo haupo kabisa au hata kama upo, ni mdogo sana. Waumini hawashirikiani wao kwa wao katika mambo kama biashara, mali zao na kadhalika. Kila mtu yuko kivyake vyake tu.

Huduma moja haishirikiani na huduma nyingine. Kwanza wanapigana vita. Halafu kanisa moja la kiroho halishirikiani na kanisa jingine. Sana sana makanisa yanasemana ovyo. Manabii na mitume hawapatani; wanapingana madhabahuni.

Huu sio mpango wa Mungu hata kidogo. Mpango wake ni sisi tushirikiane ili tuwe na umoja wa Kristo. Ili tuwe na nguvu. Hiki ndicho ambacho Yesu aliliombea kanisa kabla hajaondoka duniani (Yohana 17:11, 17:20-23).

Mungu hugawa vipawa mbalimbali
Unaposoma Biblia unaweza kuona kuwa Mungu huwagawia wanadamu vipawa au vipaji mbalimbali. Katika Waefeso 4:7-8 imeandikwa kua, “Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipawa chake Kristo. Hivyo husema, ‘Alipopaa juu aliteka mateka, akawapa wanadamu vipawa”.

Vipawa hivi ni pamoja na uwezo wa kuwa mtume au nabii, au mwinjilislisti au mchungaji, na kadhalika. Hiki ndicho kinachozungumzwa katika Waefeso 3:11 ambapo tunaambiwa kuwa, “Naye (Yesu)alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu.”
Jambo la kuzingatia ni kwamba, vipawa hivi havipatikani kwa kulazimisha. La hasha. Havipatikani kwa kujipachika. Hapana. Huu ni urithi kutoka kwa Mungu, kama aonavyo Vema kuwagawia waumini, na sio kama wao watakavyo au wanavyotamani. Huu ndio ukweli.

Uzima wa miliele ni urithi kutoka kwa Mungu

Uzima wa milele ni moja ya baraka za rohoni. Ni kitu ambacho sisi tulio hai hatujawahi kukiona, labda wale ambao tayari wamekufa. Lakini kwa imani tunaamini kwamba uzima wa milele upo. Ndio maana tunakaza mwendo ili tuweze kuingia katika uzima huo.

Bwana Yesu anatutia moyo pale anapotuambia kuwa, “Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, au mama, au watoto, wa mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele” (Mathayo 19:29)

Ni tumaini langu msomaji kwamba utasimama imara katika wokovu wako, ili uweze kurithi huo ufalme wa Mungu. Baadaye nitaonyesha kuwa uzima huu ni stahili ya watu waliookoka tu.

Kwahiyo kama wewe hujaokoka, nakutia shime ufanye hivyo, maana mtu asipookoka au asipozaliwa mara ya pili, hataweza kuurithi ufalme wa Mungu. Hiki ndicho ambacho Nikodemo aliambiwa na Bwana Yesu, wakati mmoja alipokwenda kumtembelea (Yohana 3:1-7).

Baraka za mwilini.
Baraka za mwilini ni vitu vinavyoonekana kwa macho ya kawaida au vinavyoweza kushikika. Ni ile hali ya kuwa na vitu vingi kama vile magari mengi, nyumba nyingi, mashamba makubwa, fedha nyingi na kadhalika. Mtu anapokuwa na vitu kama hivi kwa wingi, tunasema huyo amebarikiwa au ni tajiri.

Afya ya mwilini nayo ni baraka. Tunaweza kuliona hili wakati Yohana alipomwombea mzee Gayo hivi, “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo” (3Yohana 1:2).

Uzazi au kuwa na watoto nayo ni baraka kutoka kwa Mungu. Hili lipo wazi kabisa tangu mwanadamu alipoumbwa ambapo Biblia inatuambia kuwa, “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha” (Mwanzo 1:28).

Vile vile tunaposoma Zaburi 127:3 tunakutana na maneno yafuatayo, “Tazama wana ndio urithi wa BWANA, uzao wa tumbo ni thawabu” Hapa napo tunaona kuwa watoto ni baraka au zawadi kutoka kwa Mungu.

Baraka au mafanikio halisi hutoka kwa Mungu

Kama zilivyo baraka za rohoni, ukweli ni kuwa hata chanzo cha baraka za mwilini ni Mungu. Lakini sio kila baraka ya mwilini imetokana na Mungu. Hapana. Jambo hili nililizungumzia kwa kina huko nyuma, wakati ninatoa tafsiri ya neno baraka.

Nilisema kwamba mtu anaweza kuwa na utajiri wa vitu vingi, au afya njema, au watoto wengi na kadhalika, lakini vitu hivi visitokane na Mungu. Binafsi siwezi kusema mtu kama huyu amebarikiwa. Sasa sana nitasema amejitahidi kimaisha. Kwanini ninasema hivyo?

Ukweli ni kuwa baraka halisi hutoka kwa Mungu. Kama nilivyoonesha huko nyuma, inawezekana kabisa mtu akafanikiwa maishani, lakini Mungu hana nafasi katika moyo wake. Unakuta mtu ni tajiri, lakini hana dini, au anaabudu miungu isiyo ya kweli. Utajiri kama huu una matatizo mengi; sio kama ule ambao chanzo chake ni Mungu.

Nani anastahili kurithi baraka za Mungu?
Katika sehemu ya kwanza ya makala haya, iliyohusu urithi kutoka kwa mwanadamu mmoja kwenda kwa mwanadamu mwingine, nilianisha watu wanaostahili kurithi vitu au mali ya mmiliki wa kwanza. Kwa kukumbushia nilisema kuwa, sio kila mtu anaweza kurithi mali ya marehemu.

Nilisema kwamba, wapo watu maalumu ambao jamii na sheria za nchi zinawatambua kuwa hao ndio warithi halali. Ndipo nikasema kuwa, watoto wa kambo hawastahili kurithi, labda katika mazingira maalumu..

Tunapokuja katika swala la urithi kutoka kwa Mungu, napo tunakuta kuwa kuna watu maalumu ambao ndio wanaostahili kurithi baraka, ziwe za rohoni au za mwilini. Hawa sio wengine bali ni wana wa Mungu. Sasa swali la kujiuliza ni je, hivi wana wa Mungu ni akina nani? Nitaeeleza.

Tofauti ya mwana na mtoto
Kwanza kabisa, ni vizuri tukatambua kuwa kuna tofauti kati ya mtoto na mwana. Ingawa watu wengi hutumia maneno haya mawili wakiwa wanamaanisha kitu kile kile, lakini ukweli ni kwamba kuna tofauti.

Mwana ni yule hasa aliyezaliwa na baba au mama yake. Kwa Kiswahili safi, mtu kama anamtaja mtoto wake, anatakiwa aseme ‘huyu ni mwanangu’. Mwana anaweza kuwa mtoto mdogo kiumri, lakini hata akikua akawa mtu mzima au mzee, bado ataendelea kuwa ni mwana mbele ya wazazi wake.

Nafikiri wengi tunafahamu ule msemo wa Kiswahili unaosema ‘mtoto hakui mbele ya wazazi wake’. Maana halisi ya msemo huu ni kwamba, wazazi wake wataendelea kumwita mwanetu, hata akiwa mzee mwenye mvi au akiwa na cheo kikubwa kazini. Kwa mfano Rais ataendelea kuwa ni mwana mbele ya wazazi wake, ingawa kiumri sio mtoto tena.

1 maoni:

chaula salatiel said...

Asante kwa mafundisho yako,mazuri;umekatisha uhondo hapo na nini maana ya mtoto?

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

Recent Posts

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).