Friday, June 5, 2009

URITHI: Urithi kwa watu wasio na undugu na marehemu

Huko nyuma nilieleza kuwa, wakati mwingine mwenye kumiliki mali anaweza kuwarithisha watu baki kabisa, yaani watu wasio na undugu wa damu naye. Nilitoa mfano wa watu wanaoacha sehemu ya mali yao kwa wajane, yatima, maskini, wagonjwa wasaratani na kadhalika.

Vile vile nilisema kuwa, watu ambao hawakujaliwa kupata watoto, wanaweza kuacha mali zao zote kwenye mifuko au taasisi za maendeleo, au kwa marafiki zao. Mfano mzuri ni Mtanzania mmoja maarufu anayeitwa Kajumulo, ambaye alirithishwa mali na mjane mmoja, mzungu wa Marekani ambaye hakuwa na watoto.

Hapa swali la kujiuliza ni je, jambo hili linawezekana vipi? Linaweza kuwa rahisi kwa wale ambao hawakujaliwa kupata watoto. Lakini je, kwa marehemu aliyeacha mke na watoto, jambo hili linawezekana? Je, hao ndugu waliobaki wanaweza kupinga urithi uliolekezwa kwa watu wengine zaidi ya wao? Nitajaribu kueleza.

Yawezekana lakini kuna taratibu zake
Msomaji kama unakumbuka, huko nyuma nilieleza kwa kina ni watu wa namna gani wanaostahili kurithi mali ya marehemu. Nilisema kuna watu maalumu ambao jamii na Serikali vinawatambua kuwa hao ndio warithi halali. Watu hao ni mke na watoto. Unaweza kuona kuwa watu hawa wana uhusiano na marehemu, aidha wa ndoa au wa damu.

Iwapo marehemu anataka kuwarithisha watu wengine nje ya wale wanaotambulika kisheria, jambo hili linawezekana. Lakini lina taratibu zake. Yapo mambo mawili ambayo ni lazima mwenye kurithisha mali ayatimize au ayatekeleze. Vinginevyo kusudio au mpangilio wake wa urithi unaweza kutenguliwa na mahakama.

Mambo ya kufanya
Jambo la kwanza ni lazima ahakikishe kuwa amewarithisha warithi halali sehemu kubwa ya mali yake. Iwapo atawaritisha sehemu ndogo tu, warithi hao wanaweza kupinga jambo hilo mahakamani. Na kuna uwezekano mkubwa pingamizi lao kushinda.

Pili, ni lazima urithi ulioelekezwa kwa watu baki uwe kwenye wosia wa marehemu. Msomaji utakumbuka nilisema kuwa, wosia ni maandishi au kauli anayotoa marehemu, akieleza jinsi mali yake itakavyogawanywa kwa warithi wake halali., baada ya kifo chake. Nilisema kuwa wosia unatambuliwa na jamii, na vile vile una nguvu ya kisheria.

Usimamizi wa mirathi
Huko nyuma nilieleza maana ya mirathi na sheria zinazotumika hapa Tanzania kusimamia jambo hili. Kwa kifupi nilisema kwamba mirathi ni namna ambavyo mali iliyoachwa na marehemu hushughulikiwa na waliobaki, kwa lengo la kuwagawia warithi wake. Nilitaja sheria tatu za mirathi, ambazo ni sheria za kimila, ya kiislamu na ya kiserikali.

Kabla sijaanza kueleza taratibu za usimamizi wa mirathi, naomba nieleze mambo muhimu yanayohusiana na jambo hili. Mambo yenyewe ni haya yafuatayo;
Marehemu anaweza kuchagua au kupendekeza katika wosia wake mtu anayemtaka awe msimamizi wa mirathi yake.

Mahakama ndio chombo pekee kinachohusika na uteuzi wa msimamizi wa mirathi, kuwe na wosia au usiwepo.

Mahakama inaweza kukubaliana na pendekezo la mwenye kutoa wosia la msimamizi wa mirathi, lakini hailazimiki kulikubali, hasa kunapokuwepo na pingamizi.

Kama hakuna yeyote aliyechaguliwa au aliyejitokeza kuwa msimamizi wa mirathi, mahakama inaweza kumteua karani wake au mtu mwingine asimamie mirathi ya marehemu.

Marehemu au msimamizi wa mirathi hana uhuru wa kuamua sheria itakayotumika kugawa mali iliyoachwa. Mahakama ndiyo chombo pekee kinachoamua ni sheria ipi itumike kati ya zile sheria tatu za mirathi. Wajibu wa msimamizi ni kuishawishi mahakama ili ifanye maamuzi sahihi.

0 maoni:

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).