Friday, June 5, 2009

URITHI: Sheria za mirathi

Nchini Tanzania, maswala yote ya urithi au mirathi hutawaliwa na sheria za aina tatu, ambazo ni;

 1. Sheria za Kimila.
 2. Sheria ya Kiislamu.
 3. Sheria ya Kiserikali.
Kwahiyo, wakati wa kugawa mali za marehemu au kusimamia mirathi yake, mojawapo kati ya sheria hizi tatu itatumika. Sio zote kwa pamoja au kwa kuchanganya mbili. La hasha. Ni moja tu itakayotumika.

Kwamba ni sheria ipi itumike, vigezo vifuatavyo ndivyo vitakavyotumika kuamua;

 1. Aina ya maisha aliyoishi marehemu wakati wa uhai wake.
 2. Wosia alioacha marehemu.
 3. Makandokando au mambo mengine.
Hapa nataka ieleweke kuwa kila mojawapo ya sheria za mirathi hutoa haki tofauti za kurithi kwa walengwa. Jambo hili litaeleweka vizuri zaidi ninapoendelea kuchambua kila aina ya sheria. Kwahiyo msomaji tuzidi kufuatana kwa makini.

Sheria za Kimila

Kabla sijazungumzia sheria za kimila, naomba nieleze maana ya maneno ‘desturi’ na ‘mila’. Kwa kifupi neno desturi lina maana ya tabia ya kikundi au kabila fulani, inayotambulika, kukubalika na kufuatwa na jamii hiyo kwa muda mrefu, ambapo mtu akikiuka, anakuwa amekiuka mpangilio. Mila ni desturi zilizoshamiri au zilizotumika kwa muda mrefu na kukubalika katika jamii husika. Mila hizi zikipata nguvu ya sheria, yaani zikitungiwa sheria, huitwa sheria za kimila

Kwahiyo Sheria za Kimila za Mirathi tulizo nazo hapa nchini ni mila zilizokusanywa kutoka kwenye makabila mbalimbali yanayorithi kufuata ukoo wa upande wa baba (patrilineal). Sheria hizi zipo katika Tangazo la Serikali (Government Notice) namba 436 la mwaka 1963.

Hapa naomba nieleze kwamba nchini mwetu kuna baadhi ya makabila ambayo utaratibu wake wa kurithi hufuata mkondo wa mama (Matrilineal). Baadhi ya makabila hayo ni Wamakonde, Wayao, Wamakua, na kadhalika. Baadaye kidogo nitaeleza utaratibu huu unakuwaje wakati wa kurithisha.
Wanaotumia Sheria ya Kimila

Wanaotumia au wanaopaswa kutumia Sheria za Kimila ni Watanzania wote ambao ni wazawa (natives). Nchini mwetu wazawa ni Watanzania wasio na asili ya nchi nyingine kama za Kiasia, Kizungu, Kisomali, na kadhalika. Hapa naomba nitoe angalizo. Mtanzania mzawa anapofika mahakamani kufungua mirathi, inatarajiwa kwamba sheria itakayotumika kusimamia mirathi hiyo ni ya kimila, hata kama mtu huyo ni mkristo au mwislamu.

Lakini kama itadhihirika au itathibitika kuwa mzawa fulani aliachana kabisa na mila na desturi za kabila lake wakati wa uhai wake, mahakama inaweza kutumia sheria ya Kiislamu (kama marehemu alikuwa Mwislamu) au kutumia sheria ya Kiserikali kwa wengine. Uzoefu unaonyesha kwamba watu wengi huwa wanashindwa kuthibitisha jambo hili. Kwanini?
Watanzania wengi bado wanaendekeza mila

Ukweli ni kuwa, pamoja na Watanzania wengi kuwa na dini, wapo ambao hawafuati kile ambacho dini zao zinaelekeza. Unakuta mtu anajiita ni Mkristo au Mwislamu, lakini bado anafuata mila kama vile kutambika, kukeketa wanawake, kuweka na kuanua matanga, na kadhalika. Kama unaishi maisha ya namna hii, sheria itakayosimamia mirathi yako utakapofariki ni ya kimila, hata kama ulikuwa unajiita mkristo au mwislamu.

Hapa naomba niwaase wakristo wenzangu mliookoka. Acha kabisa kuishi maisha ya kujichanganya. Kwenye ulokole upo, lakini vile vile kwenye mila upo. Ukifiwa unaweka matanga siku tatu au tano, halafu unaanua. Wengine siku hizi mnakuwa na ‘arobaini’ ya marehemu. Hivi wewe mtu wa Mungu unatokana wapi na mambo kama haya? Achana na upumbavu huu. Wewe unatakiwa uongozwe na neno la Mungu, na wala sio mila za kwenu.

Urithi chini ya Sheria za Kimila

Sasa hebu tuangalie urithi chini ya Sheria za Kimila unakuwaje. Hapa nina maana ya urithi ambao unafuata mkondo wa ukoo wa baba. Kwa kifupi kanuni zinasema kwamba, iwapo marehemu aliacha watoto, basi hao ndio pekee watakaorithi au watakaorithishwa mali ya marehemu baba yao.

Mjane au mama wa hao watoto hana haki ya kurithi mali iliyoachwa na mumewe, ingawa yeye naye alihusika katika uzalishaji wake. Huu ndio udhaifu mkubwa wa sheria za kimila. Mjane hapati chochote na inabidi aishi kwa kutegemea kile watoto wake walichorithi kutoka kwa marehemu mumewe.

Endapo marehemu mume wake hakumwachia watoto, basi mjane atabaki katika nyumba aliyoiacha marehemu wakati wote wa uhai wake. Mjane akifariki au akiolewa na mtu mwingine, mali au nyumba ya marehemu hugawiwa kwa warithi wengine halali wa marehemu mumewe (kufuatana na mila na desturi).
Sheria za kimila hazina usawa

Tunapokuja upande wa watoto, sheria hii haitoi haki sawa ya kurithi. Badala yake kunakuwa na ubaguzi. Yaani chini ya Sheria za Kimila, kuna madaraja matatu ya urithi. Madaraja hayo ni kama ifuatavyo.

Daraja la Kwanza

Ilivyo ni kwamba mtoto wa kiume wa kwanza wa ndoa ndiye anayerithi sehemu kubwa kuliko wenzake wote. Kama ndoa ilikuwa ni ya mitala, yaani ya wake wengi, mtoto wa mke mkubwa wa ndoa ndiye anayeangukiwa na bahati ya kurithi sehemu kubwa ya mali ya marehemu baba yake.

Msomaji kama utakumbuka, huko nyuma nilionyesha kuwa katika Agano la kale kulikuwa na upendeleo kwa mtoto wa kwanza. Kwa kukumbushia , hebu tunukuu tena lile andiko la Kumbukumbu la Torati 21:15-17 linalosema, “Akiwa mtu yuna wake wawili, mmoja ampenda, mmoja hampendi, nao wamemzalia watoto, ampendaye na asiyempenda wote wawili; na yule mzaliwa wa kwanza akiwa ni wa mke asiyependwa; ndipo itakapokuwa ya kwamba siku atakayowarithisha wanawe alivyo navyo, asimweke mwana wa ampendaye kuwa mzaliwa wa kwanza mbele ya mwana wa asiyempenda, naye ndiye mzaliwa wa kwanza huyu; lakini amkubali mzaliwa wa kwanza mwana wa yule asiyempenda, kwa kumpa mafungu mawili katika vyote alivyo navyo; kwa maana ndiye mwanzo wa nguvu zake; haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake yeye”

Niliponukuu andiko hili, nilizungumzia kwa kirefu kitu ambacho kinaitwa haki ya mzaliwa wa kwanza. Sasa hebu tujiulize. Sisi tuliookoka tuendeleze ubaguzi au upendeleo kwa watoto wetu wakati wa kuwarithisha? Kwa vile tunaongozwa na neno la Mungu, je tunaweza kusimamia andiko hili na kumpendelea mtoto wa kwanza wa kiume?

Daraja la pili
Katika darala la pili, watoto wote wa kiume waliosalia hurithi sehemu kubwa kuliko wale wa kike. Hapa napo msomaji unaona upendeleo unaendelea. Yaani watoto wa kike hawarithi sawasawa na wale wa kiume. Je, tuendeleze utaratibu huu katika kipindi hiki cha sasa cha Agano Jipya?

Daraja la tatu
Hili ni daraja la mwisho ambapo watoto wote wa kike, bila kujali umri wao au nafasi zao za kuzaliwa, hurithi sehemu ndogo kuliko wenzao wa kiume. Kama marehemu hakujaliwa kupata watoto wa kiume, wale wa kike hupewa urithi mkubwa zaidi.

Chini ya sheria za kimila, watoto wa kike hawaruhusiwi kabisa kurithi ardhi ya ukoo. Wanaruhusiwa kuitumia mpaka watakapoolewa au kufa. Aidha hawana mamlaka ya kuuza ardhi ya ukoo. Hiyo ndiyo sheria yenyewe pamoja na ubaguzi wake.

Watoto wa kambo
Chini ya sheria ya kimila, watoto waolizaliwa nje ya ndoa hawaruhusiwi kurithi chochote kile kilichokuwa cha marehemu. Wanaweza kurithi tu iwapo baba yao aliacha wosia kuwa nao warithi, au kama walihalalishwa (wakati wa uhai wa marehemu) kufuatana na desturi au taratibu zinazojulikana katika jamii au kabila husika.

Urithi unaofuata mkondo wa mama
Wakati ninaanza kuelezea sheria za mirathi za kimila nilisema kwamba hapa nchini kuna baadhi ya makabila ambayo utaratibu wao wa kurithi hufuata mkondo wa mama (Matrilineal). Chini ya utaratibu huu mambo yako hivi;
Mume huishi kwa mke. Kwa makabila mengine kama Wachaga, hiki ni kioja. Yaani mume anakuwa kama vile yeye ndiye aliyeolewa. Hizi ndio mila na desturi za baadhi ya makabila.

Mume akifa, mke hurithi mali yote.

Endapo mke atatangulia kufariki, mume hawezi kurithi mali ya marehemu mkewe, labda kuwe na wosia wa mkewe unaomruhusu arithi.

(iv) Ikiwa mke marehemu ameacha watoto, hao ndio watakaorithi mali ya mama yao.
Kama mke marehemu hakuacha watoto, kaka yake (mjomba) ndiye atakayerithi mali yote, labda kuwe na wosia unaomruhusu mume wake arithi.

Endapo marehemu hakuwa na kaka, mtu mwingine wa ukoo wake atarithi mali yake.

(vi) Ikitokea marehemu hakuacha kabisa watoto na hakuacha kabisa mtu yeyote wa ukoo wake, hapo ndipo mumewe atarithi mali yake.

Msomaji unaweza kuona kwamba, chini ya utaratibu huu mume anakuwa hana haki kabisa ya kurithi, japo naye alihusika katika kuzalisha mali hiyo akishirikiana na marehemu mkewe. Kwahiyo tunaweza kusema kwamba sheria za kimila zina mapungufu mengi. Zinamnyima mwanamke (au mwanamume), haki ya kurithi. Zinabagua kati ya watoto wa kike na wa kiume na kadhalika. Kusema kweli sio nzuri sana, ijapokuwa ndizo zinazotumiwa na watu wengi hapa nchini.

Sheria ya Kiislamu
Ninatambua kwamba wasomaji wakubwa wa gazeti hili ni Wakristo. Kwa sababu hiyo kusingekuwa na haja ya kuzungumzia Sheria ya Kiislamu ya Mirathi. Pamoja na kuufahamu ukweli huo, nimeona ni vema niizungumzie angalao kwa kifupi. Hii ni kwa sababu sheria yenyewe ina mambo ambayo yanawagusa (affect) wakristo. Ili kuwasaidia, ni vema nikayaweka mambo hayo bayana.

Kwanza tuanze na watumiaji wa sheria ya kiislamu. Kama ilivyo kwa Wakristo, hata mtu ambaye ni Mwislamu anapofariki, mirathi yake inatarajiwa ishughulikiwe kwa kufuata Sheria ya Kimila. Lakini kama ikiweza kuthibitika kwamba marehemu aliachana kabisa na mila na desturi za kabila lake wakati wa uhai wake, halafu uislamu ukawa ndio mfumo wake wa maisha, hapo ndipo sheria ya kiislamu inaweza kutumika katika kusimamia mirathi yake. Vile vile sheria hii hutumiwa na watu wote ambao sio wazawa, lakini ni waislamu.

Hapa naomba niseme hivi. Kama ilivyo kwa Wakristo, vile vile wapo Waislamu ambao katika maisha yao hawafuati misingi ya uislamu. Kwanza hawaijui Korani, hawaendi msikitini, wala hawajui namna ya kusali. Halafu nao wanajishughulisha na mambo ya kimila ya makabila wanayotoka.

Watu kama hawa ni Waislamu wa jina tu. Kwahiyo watakapofariki, mirathi yao inapaswa ishughukikiwe kwa kufuata sheria ya kimila ya mahali wanapotoka; sio kulingana na sheria ya kiislamu.

Warithi chini ya Sheria ya Kiislamu
Warithi wakuu chini ya sheria hii ni mke au wake za marehemu, baba na mama yake (kama watakuwa bado hai), na mwishowe watoto wake. Msomaji utaona kwamba, tofauti na sheria za kimila, sheria ya kiislamu inawajumuisha pia mke au wake za marehemu, pamoja na wazazi wake. Inataja wake za marehemu kwa sababu waislamu wanaweza kuoa mke zaidi ya mmoja. Sheria yenyewe imezingatia jambo hili.

Chini ya sheria ya kiislamu, warithi wa marehemu hugawiwa mali zake kama ifuatavyo;

 1. Wajane wasiozidi wanne hupata kitu kinachoitwa ‘kithumuni’ pale ambapo marehemu ameacha watoto. Kithumuni ni sehemu moja ya nane (1/8) ya mali ya marehemu.
 2. Endapo marehemu alifariki bila watoto, mke au wake zake hupata robo (1/4) ya mali iliyoachwa. Robo tatu (3/4) ya mali iliyobaki huenda kwa wazazi wa marehemu.
 3. Mwanamume anaweza kumwosia au kumpa urithi yeyote amtakaye (ikiwa ni pamoja na mke au wake zake), sehemu ya mali yake, mradi tu isizidi theluthi moja (1/3) ya mali hiyo.
 4. Baba na mama wa marehemu hupata moja ya sita (1/6) ya mali yake iwapo ameacha watoto.
 5. Mali inayobaki baada ya mgawo kwa mke au wake pamoja na wazazi, hugawiwa kwa wototo wote wa marehemu. Katika mgao huo, watoto wa kiume hupata kiasi kikubwa kuliko wale wa kike. Kwa mfano kama marehemu aliacha mtoto mmoja wa kiume na wawili wa kike, yule wa kiume atapata theluthi mbili (2/3) halafu wale wa kike kwa pamoja watapata theluthi moja (1/3) tu.

Sheria ya Kiislamu ina mapungufu yake

Msomaji unaweza kuona kwamba, kama ilivyo kwa sheria ya kimila, hata sheria ya kiislamu nayo hubagua kati ya watoto wa kiume na wa kike. Huu nao ni udhaifu kwa namna moja. Kinachofurahisha katika sheria hii ni kwamba mke na wazazi wa marehemu wana haki ya kurithi.

Ikumbukwe kwamba wazazi wanapozeeka, hutegemea kutunzwa na watoto wao. Hao watoto wanapofariki, wazazi walioachwa nyuma wanaweza kuteseka kwa kukosa msaada wa matunzo. Angalao sheria ya kiislamu inalitambua tatizo hili, na kwa sababu hiyo imetenga fungu kutoka katika mali ya marehemu, kwa ajili ya matunzo ya wazazi.Tatizo ni kuwa wazazi hupewa sehemu kubwa sana ukilinganisha na kile mke au watoto wa marehemu wanachoambulia kama urithi.Watoto wa kambo

Kama ilivyo kwa sheria ya kimila, sheria ya kiislamu ya mirathi nayo haitoi haki ya kurithi kwa mtoto au watoto waliozaliwa nje ya ndoa. Wanaweza kurithi iwapo tu marehemu ameacha wosia unaosema kwamba nao warithi. Vile vile kama marehemu aliwagawia sehemu ya mali yake wakati wa uhai wake, huo utahesabika kwamba ni urithi kwa hao watoto wa kambo. Vinginevyo hawaambulii chochote katika mali ya marehemu baba yao.

Msomaji nadhani mpaka sasa unaweza kuona kwamba watoto wa kambo wana taabu sana. Sio sheria ya kimila wala ya kiislamu inayowapa haki ya moja kwa moja (outright) ya kurithi mali ya baba au mama waliowazaa. Inabidi yaandaliwe mazingira maalumu ya kuwarithisha. Vinginevyo hawapati kitu.

Ninatamani sana iwapo sisi wanadamu tungeyachunga maisha yetu, ili tuepukane na kitendo cha kuzaa watoto wa kambo. Angalia jinsi wanavyonyanyasika unapofika muda wa kurithi, wakati sio wao waliojitakia jambo hilo. Tungezingatia maadili mema, kamwe ndoa zetu zisingekuwa na matatizo yanayohusiana na watoto wa kambo.


Asiye mwislamu hawezi kurithi mali ya mwislamu.

Sasa tunakuja katika jambo linalonifanya nizungumzie sheria ya kiislamu ya mirathi. Ni ajabu kwamba sheria hii haimruhusu mtu asiye mwislamu arithi mali ya mtu ambaye ni mwislamu, hata kama kuna uhusiano kati wa watu hao. Hapa ndipo nilisema kwamba kanuni hii inawagusa au inawaathiri watu kama wakristo. Kwanini ninasema hivyo?

Ukweli ni kuwa katika jamii ya watanzania, kuna wakati unakuta mkristo na mwislamu wamependana mpaka wakaoana. Katika ndoa ya namna hii, ambayo nitaiita ya mseto (cross marriage), unaweza kukuta wanandoa wamekubaliana kwamba kila mmoja wao aendelee kufuata dini yake. Tuseme mwanamke ni mkristo. Katika hali hii, iwapo huyo mume ambaye alikuwa akiishi kwa kufuata desturi na taratibu za kiislamu atafariki, mkewe hataruhusiwa kurithi mali yake.

Kwahiyo wewe dada au mama ambaye ni mkristo na umeolewa na mwislamu, ujue kwamba mumeo atakapofariki, hutakuwa na haki ya kurithi chochote kilicho chake. Tuseme mlifunga ndoa yenu msikitini, au bomani, au kijijini. Tangu leo ujue kuwa sheria ya kiislamu ya mirathi haikuruhusu wewe urithi mali ya mumeo, hata kama mliichuma kwa pamoja. Hiyo ndiyo hali halisi.

Namna nyingine ambavyo mwanamke mkristo anaweza kukosa haki ya kurithi mali ya mumewe ambaye ni muislamu ni pale anapobadili dini. Tuseme wanandoa wote walikuwa waislamu na walifunga ndoa yao msikitini. Baadaye mwanamke akahubiriwa Injili na kuokoka, lakini mumewe akaendelea kuwa muislamu. Katika hali hii, huyo mwanamke ambaye sasa ni mkristo, hataweza kurithi mali ya mumewe.

Watoto au wazazi ambao sio waislamu hawawezi kurithi mali ya mwislamu
Watoto ambao ni wakristo, nao hawaruhusiwi kurithi mali ya baba yao, ambaye ni muislamu. Jambo hili linawezekana vipi? Hebu fikiria mtoto ambaye wazazi wake wote ni waislamu, lakini yeye akakubali kuokoka. Ni wazi kuwa kwa kitendo chake cha kuokoka, tayari atakuwa ameuasi uislamu na kujiunga na ukristo. Kutokana na sheria ya kiislamu ya mirathi, mtoto kama huyu hataweza kurithi mali ya baba yake.

Vile vile mzazi au wazazi ambao wataukana uislamu na kujiunga na ukristo, watapoteza haki ya kurithi mali ya mtoto wao, ambaye ni muislamu. Jambo hili linaweza kutokea kama inavyokuwa pale mke au watoto wanapobadili dini na kujiunga na ukristo. Kwahiyo baba au mama ambaye alikuwa muislamu halafu akawa mkristo, atakuwa amepoteza ile stahili yake ya 1/6 ya mali ya mwanawe.

Msomaji nafikiri utakubaliana nami kwamba katika jamii yetu au makanisani mwetu, wapo watu ambao hapo mwanzo walikuwa ni waislamu, lakini sasa ni wakristo. Hebu angalia jinsi watu hawa wanavyopoteza haki yao ya kurithi. Kusema kweli wanahitaji kupongezwa na kutiwa moyo kwa ujasiri wao wa kuwa tayari kupoteza haki zao za msingi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Ikiwezekana wasaidiwe na makanisa waliyojiunga nayo, ili wasijione kama vile wamepata hasara kwa kuukubali wokovu.

Mume anaweza kurithi mali ya marehemu mkewe au wake zake

Sheria ya Kiislamu inamruhusu mwanamume kurithi nusu (1/2) ya mali iliyoachwa na mke au wake zake, iwapo walitangulia kufa bila kumwachia watoto. Kama wapo watoto walioachwa, huyo mume atapata robo (1/4) ya mali iliyoachwa na huyo mkewe au wakeze, lakini baada ya kulipa madeni (kama yapo) na gharama za mazishi.

Kwa kumalizia kipengele hiki cha sheria ya kiislamu ya mirathi, naomba niseme tena kwamba sio nia yangu kuichambua sheria hii kwa kina. Nimechagua mambo machache tu, yale ninayoona kuwa yanawagusa wakristo, na kwamba wanapaswa kuyafahamu. Anayetaka kufahamu mengi zaidi anaweza kuipata kitabu chenye sheria yenyewe mahakamani au mahali pengine popote inapopatikana, akajisomee kwa wakati wake. Sheria yenyewe inatambulika kama Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.

Sheria ya Kiserikali
Sasa tunakuja katika sheria ya mwisho ya mirathi, ambayo binafsi ninaamimi kwamba ndiyo ambayo sisi wakristo tuliookoka, tunapaswa kuifuata wakati wa kurithisha mali zetu, au wakati wa kushughulikia mirathi za walokole wenzetu. Hii inaitwa Sheria ya Kiserikali ya Mirathi.

Tunaweza vile vile kutumia mwongozo wa Biblia, iwapo tutaona kwamba sheria ya kiserikali haikidhi matakwa yetu. Lakini bado nadhani ni vema tukatumia sheria hii kuliko kutumia ile ya kimila. Kwanini ninasema hivyo?

Kwanza kabisa ni kutokana na asili au msingi wa sheria yenyewe. Ukweli ni kuwa sheria ya kiserikali ya mirathi imetokana na sheria ya urithi ya nchini India ya mwaka 1865, ambayo kwa Kiingereza inatambulika kama “The Indian Succession Act, 1865. Bunge la Tanzania limeichukua sheria hii (adopt) na kuiidhinisha, ili itumike hapa nchini.

Sheria ya Kiserikali imewalenga Wakristo

India ni nchi ambayo wananchi wao wengi ni Wahindu. Lakini vile vile wapo watu wa makundi madogo madogo (minorities) kama vile Wakristo, Waislamu, Wasikh na kadhalika. Hawa nao wametungiwa sheria zao za mirathi. Kwahiyo sheria ya urithi ya India iliyotungwa mwaka 1865, inalenga kushughulikia mirathi za Wakristo.

Wanasheria na Wabunge wetu waliichambua sheria hiyo, wakaona kwamba inafaa katika mazingira ya Kitanzania. Ndipo ilipopitishwa na Bunge letu tukufu. Hii ndiyo sheria ambayo nimesema kwamba inafaa kutumiwa na watu waliookoka wakati wa kushughulikia maswala ya urithi.

Jambo lingine linalonifanya nione kwamba sheria ya kiserikali ndiyo inayowafaa watu wa Mungu ni kwa sababu imejitahidi kwa kiwango kikubwa kutenda haki kwa wajane na watoto wa kike. Ni kwamba, Sheria hii imempa mjane haki ya kurithi mali ya marehemu mumewe. Vile vile haibagui kati ya watoto wa kike na wale wa kiume.


Watumiaji wa Sheria ya Kiserikali

Hapa nchini mwetu, watu wanaopaswa kutumia Sheria ya Kiserikali ya Mirathi ni Watanzania wote walio wazawa, na ambao wameachana na desturi au mila za makabila yao, lakini sio waislamu. Vile vile watu wa jamii nyingine, ambao sio wazawa wala waislamu, nao wanaweza kutumia sheria hii.

Hapa naomba nitoe angalizo. Haiwezekani mirathi ya mkristo isimamiwe kwa sheria ya Kiislamu, au mirathi ya mwislamu isimamiwe kwa sheria ya Kiserikali. Hapana. Kama marehemu alikuwa muislamu, sheria inayotumika ni aidha ya kimila au ya kiislamu. Na kama marehemu alikuwa mkristo, sheria inayotumika ni aidha ya kimila au ya kiserikali.

Sasa msomaji unaweza kuona kwamba wanaopaswa kutumia sheria ya kiserikali ni wale tu ambao wameachana na mila na desturi za makabila yao au jamii wanayoishi. Huko nyuma nilidokeza kwamba ni Watanzania wachache sana wanaoweza kuthibitisha kwamba wamechana kabisa na tamaduni zao. Nilisema kwamba, pamoja na dini kuingia nchini miaka mingi iliyopita, bado watu wengi wanafuata mila za makabila au jamii zao.

Chunga mfumo wako wa maisha
Linapokuja swala la kuthibitisha kwamba mtu fulani ameachana kabisa na mila, wanasheria wengi hapa nchini hupenda kunukuu kesi ya marehemu Innocent Mbilinyi iliyoamuliwa na Mahakama Kuu jijini Dar-es-salaam mnamo mwaka 1969. Kwa kifupi ni kwamba, mjane mmoja Mchagga aliyeolewa na Mngoni, alifaulu kuithibitishia mahakama kuwa yeye na mumewe walishaachana kabisa na mila na desturi za makabila yao.

Huyu mjane aliieleza mahakama kwamba walifunga ndoa ya Kikristo na marehemu mumewe, na kwamba walikuwa wanaishi Dar-es-salaam. Marehemu aliondoka Songea akiwa na umri wa miaka saba, na alisoma mpaka akapata shahada ya kwanza. Mara chache sana wanandoa hawa walitembelea Songea au Moshi. Kwa sababu hiyo hawakuwa na fursa ya kushiriki katika mila na tamaduni za makabila yao.

Je, wewe umeachana na mila zenu?
Angalao huyu mjane alifanikiwa kuthibitisha kwamba yeye na mumewe walishaachana na mila. Je, ni Watanzania wangapi wanaoweza kama yeye? Pamoja na kusoma sana na kustaarabika kwa kiasi fulani, bado watu wanaendekeza mila na tamaduni za makabila yao.

Ikifika Desemba, pale Ubungo nauli za mabasi hazishikiki, hasa kwa watu wanaokwenda mikoa ya kaskazini. Nafikiri wengi tunafahamu ni kabila gani mashuhuri linaloishi kaskazini mwa Tanzania. Watu wanajitia wanakwenda likizo ya Krismasi au Pasaka, kumbe wapo wanaokwenda kushiriki mitambiko pamoja na mambo mengine ya kimila..

Wanaondekeza mila ni wengi

Ukweli ni kuwa wanaoshiriki mila sio watu wa Kaskazini tu. Hapana. Mikoa ya kati (Wagogo, Warangi, Wanyaturu) bado wanaendekeza utamaduni wa kukeketa. Mikoa ya Kusini (Lindi, Mtwara na Songea), kikifika kipindi cha unyago, hata watoto wa mawaziri wanaosoma Dar-es-salaam wanarudishwa vijijini. Kisa? Eti wakachezwe ngoma. Na wanaofanya hayo ni wasomi ambao wengine wao ni wakristo.

Ninaamini kwamba mtu aliyeokoka sawasawa hawezi kushiriki mambo ya kutambika, kukeketa wanawake, kucheza ngoma za kienyeji au za unyago, na kadhalika. Hawezi kurudi kijijini kwao kila mwisho wa mwaka, eti akatimize maswala ya mila na utamaduni wa kwao. Haya ni mambo ya watu ambao hawajaokoka.

Kwa kuwa watu waliookoka huongozwa na neno la Mungu, hawawezi kushiriki katika mambo ya kimila. Kwahiyo itawawia rahisi kuthibitisha kwamba wao wameachana kabisa na mila na desturi za makabila yao. Na kwa sababu hiyo, sheria itakayotumika kusimamia mirathi zao watakapofariki, ni ile ya Kiserikali.

Urithi chini ya Sheria ya Kiserikali
Utaratibu wa urithi chini ya sheria ya kiserikali uko hivi. Kama marehemu alipofariki aliacha mjane na watoto, huyo mjane hupata theluthi moja (1/3) na watoto wote kwa pamoja hupata theluthi mbili (2/3) ya mali iliyoachwa. Hao watoto hugawana hiyo sehemu yao sawasawa bila kujali kwamba ni wa kiume au wa kike, au nani mkubwa na nani ni mdogo.

Iwapo kwa bahati mbaya marehemu hakuacha watoto, mjane hupata nusu (1/2) ya mali iliyoachwa. Nusu nyingine hugawiwa kwa baba, mama, kaka na dada wa marehemu. Hapa msomaji unaweza kuona kwamba warithi wakuu chini ya sheria ya kiserikali ni mke wa marehemu na watoto wake. Wazazi hawana haki ya kurithi mali ya mtoto wao, labda katika mazingira niliyoyaeleza hapo juu.

Je, Biblia inaruhusu watoto wa kike warithi?
Tunapoangalia swala la watoto wa kike nao kupewa urithi, tunaweza kuona kuwa hata Biblia nayo kuna mahali imezungumzia jambo hili. Ingawa kwa desturi Wayahudi walikuwa hawarithishi wanawake, lakini tunaweza kuona Ayubu, ambaye hakuwa Myahudi, aliweza kurithisha hadi watoto wake wa kike.

Baada ya Ayubu kufiwa na wanawe wote wa mwanzo, Biblia inatuambia kuwa baadaye Mungu alimjalia kupata wana wengine wa kiume na wa kike. Tunasoma kwamba, “Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wanaume” (Ayubu 42:15).

Ikumbukwe kwamba Ayubu alikuwa mtu wa haki. Leo hii tungeweza kusema kuwa alikuwa ameokoka. Kama aliweza kuwarithisha hadi watoto wa kike, hata sisi tuliookoka tunaweza kuwarithisha mali wana wetu wa kike.

Watoto wa kike waliweza kurithi
Ingawa kwa desturi Wayahudi walikuwa hawarithishi watoto wa kike, katika mazingira maalumu, jambo hili liliwezekana. Kama wanandoa hawakujaliwa kupata mtoto wa kiume, wale wa kike waliweza kupewa haki hiyo. Tena ilikuwa ni amri kutoka kwa Mungu (Hesabu 27:1-8, 36:1-13)

Jambo la kuzingatia ni kwamba, ingawa watoto wa kike waliweza kurithi, walikuwa hawaruhusiwi kuolewa nje ya kabila lao. Lengo lilikuwa ni kuzuia urithi usitoke katika kabila moja kwenda kwenye kabila jingine kwa sabau taifa la Israeli liligawanywa kikabila.

Swali la kujiuliza ni hili. Katika siku za leo mtu akiwa na watoto wa kike tu, afanye nini? Je afuate mfumo wa Wayahudi, huu wa Agano la kale? Au je, afuate sheria ya kimila inayomnyima mwanamke haki ya kurithi? Ni kwanini asifuate sheria ya kiserikali inayompa hata mtoto wa kike haki hiyo?


Watoto wa kambo

Kama ilivyo katika sheria ya kimila na ya kiislamu, vile vile sheria ya kiserikali nayo haimpi mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa haki ya moja kwa moja (outright) ya kurithi, Watoto wa kambo wanaweza tu kurithi iwapo marehemu baba yao aliacha wosia unaoelekeza hivyo; au kama aliwahalalisha wakati wa uhai wake.

Watoto wa kambo wanaweza kuhalalishwa kwa kufuata desturi au taratibu zinazojulikana na kutambulika katika kabila au jamii husika. Kuhalalisha huku ni pamoja na kuwatambulisha hao watoto katika familia, au kuwachukua huko walipo, na kuishi nao katika nyumba ya ndoa.

Jambo la kuhalalisha litapendeza iwapo wanandoa watakubaliana kufanya hivyo. Sio baba mwenye nyumba analazimisha mambo. Akilazimisha anaweza kuleta mtafaruku katika familia yake. Na ukweli ni kuwa katika familia nyingi kumekuwa na mitafaruku pale ambapo jambo hili halikufanyika kwa busara na hekima..

3 maoni:

ginfizz said...

kaka napenda mada zako na nukuu zako lakini mbona hamna sheria ya kristo hata dhehebu moja roman,lutheran, anglican ina kabla serikali kutunga sheria za mirathi hakukuwa na mirathi upande wa wakrito.

tanzaniachristianheritage said...

Ndugu Ginfizz swali lako ni zuri sana. Kwa haraka haraka mtu anaweza kudhani kwamba hakuna Sheria ya Kikristo ya Mirathi. Lakini ukweli ni kuwa ile Sheria ya Kiserikali niliyoileza kwa kina ndiyo inayoshughulikia mirathi za wakristo. Hii ni kwa sababu sheria hiyo imetokana na sheria za India ambazo kwa huko ilikuwa inashughulikia mirathi za watu wasio Wahindu, hususan Wakristo. Tanzania tuliichukua sheria hiyo inayoitwa 'Indian Succession Act, tukaifanyia marekebisho kidogo na tukaanza kuitumia katika mazingira yetu. Hii ndiyo sheria inayotumika kushughulikia mirathi za Kikristo, ingawa haiitwi Sheria ya Kikristo ya Mirathi. Nadhani nitakuwa nimejibu swali lako. Karibu sana.
Sabato Tarimo.

hafidhu mdanku said...

assalam aleykum.naoma kuuliza iwapo marehemu atakuwa ameacha wosia kuwa hii mali ni ya Fulani na mke wangu hausiki na hii mali ,je hiyo mali inawezekana kuuzwa na kugawia mtu mwingine hata kama ni mke wa marehemu

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

Recent Posts

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).