Friday, June 5, 2009

URITHI: Ni wakati gani wa kurithisha au kurithi?

Jambo lingine ambalo nafikiri ipo haja ya kuliongelea ni wakati wa kurithi. Swali la kujiuliza ni je, upi ndio muda sahihi wa kurithisha au kurithi? Jibu sahihi la swali hili ni njia mojawapo ya kuepukana na matatizo kama vile kutapanya au kudhulumiwa mali ya urithi, na kadhalika.

Kutokana na ile tafsiri ya urithi niliyoitoa mwanzoni mwa makala haya, na vile kama ilivyo katika jamii nyingi duniani, wakati wa kurithi ni baada ya kifo cha mmiliki wa mali hiyo. Sio jambo la kawaida kwa mtoto kudai urithi wake baba yake akingali hai, ingawa baadaye tutaona kuwa jambo hili linawezekana.

Biblia inataja muda wa kurithi
Kibiblia tunaweza kuona hivyo tunaposoma waraka kwa Waebrania 9:16-17 ambapo tunaambiwa kuwa, “Maana agano la urithi lilipo, lazima iwepo mauti ya aliyelifanya. Kwa maana agano la urithi lina nguvu palipotukia kufa kwa mtu; kwa kuwa halina nguvu kabisa, akiwa yu hai yeye aliyelifanya”.

Kinachozungumzwa hapa ni hiki. Tuseme baba ameandika wosia unaoonyesha jinsi mali yake itakavyorithiwa baada ya yeye kufariki. Wosia huo utakuwa na nguvu ya kisheria au utaanza kutekelezwa baada ya kifo cha huyo aliyeuandika; sio wakati wa uhai wake .

Unaweza kurithi wakati wa uhai wa mwenye mali
Ukweli ni kuwa sio lazima mtu arithi baada ya kifo cha mmiliki wa mali hiyo. Yanaweza kutokea mazingira ambapo mtu anaona ni vema arithishe mali yake kwa walengwa wakati akingali hai. Kwa mfano kama anahisi kwamba kunaweza kutokea ugomvi au dhuluma baada ya kifo chake, anaweza kugawa mali yake mapema akiwa bado yu hai. Au kama amezeeka sana, na anaona kwamba hana tena nguvu za kutunza mali aliyo nayo, hapo napo anaweza kuwagawia warithi wake.

Tunapoangalia Biblia tunaweza kuona kuwa Ibrahimu aligawa mali zake akingali hai. Tunaambiwa kuwa, “Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu? (Mwanzo 25:5-6).

Suria ni mke mdogo katika ndoa ya wake wengi. Vile vile neno hili lina maana ya hawara au kimada. Biblia inaonyesha kuwa Ibrahimu alioa wake wengine baada ya kifo cha Sara (Mwanzo 25:1-6). Wana wa masuria hawakurithishwa mali, bali waliambulia vitu vidogo vidogo tu. Na jambo hili lilifanyika wakati wa uhai wa Ibrahimu, ambaye ndiye aliyekua mrithshaji.
Mfano wa Ibrahimu ni wa kuigwa

Ibrahimu aliona ni vema agawe mali zake mapema kwani alikuwa na mtoto halali na pia watoto wa kambo. Aliona kungeweza kutokea ugomvi kati ya wanawe hawa, iwapo angesubiri mpaka kifo chake kitokee, ndipo tendo la kurithi lifanyike. Kwahiyo akaona ni bora kuepusha matatizo kungali mapema.

Hata wewe msomaji unaweza kuiga mfano wa Ibrahimu. Kama unahisi ndugu zako watamnyang’anya mkeo haki yake ya urithi, au wanao wanaweza kugombana na kudhulumiana wakati wewe haupo tena duniani, ni ruksa kugawa mali zako ukiwa bado u hai. Hiyo haikatazwi, nami ningekushauri ufanye hivyo.
Watoto wadogo huwa hawarithishwi

Muda mwingine muafaka wa kugawa urithi ni baada ya watoto kuwa watu wazima. Nafikiri msomaji utakubaliana nami kwamba ni upumbavu mtupu kumkabidhi mtoto mdogo urithi. Kwanza akili yake inakuwa bado haijakomaa. Kwa hiyo hawezi kufahamu aufanyie nini huo urithi.

Lakini vile vile mtoto anaweza kudhulumiwa mali aliyorithi kutokana na yeye kutokuwa na nguvu au uwezo wa kukabiliana na watu wenye nia mbaya. Yaani watu wenye nia ya kumnyang’anya au kumlaghai, ili wachukue kile alichoachiwa.

Iwapo baba atafariki watoto wake wakiwa bado wadogo, haki yao ya kurithi huwa haipotei. Badala yake, urithi wao huwekwa chini ya uangalizi au usimamizi wa mtu mwingine. Baadaye watoto hao wakikua, hukabidhiwa kilicho chao. Mwangalizi huyo anaweza kuwa ni mke wa marehemu, au ndugu wa karibu, au msimamizi wa mirathi, au wakili, na kadhalika.

Biblia inakataza watoto wadogo kurithi
Tunapoigeukia Biblia tunaweza kuona kwamba nayo inazungumzia wakati wa kurithi kwa ufasaha sana. Katika Wagalatia 4:1-2 imeandikwa hivi, “Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba”.

Kinachozungumziwa hapa ni kuwa, mtu anapokuwa bado yu mtoto mdogo, hawezi kukabidhiwa mali yake ya urithi. Kwahiyo hawezi kufaidi mali hiyo wakati wa utotoni. Badala yake anakuwa kama mtumwa, ambaye kama tujuavyo, hawezi kufaidi mali ya bwana wake.

Urithi wa mtoto huwekwa chini ya usimamizi au uangalizi wa mtu mkubwa na aliye mwaminifu. Baada ya huyo mtoto kuwa mtu mzima, ndipo sasa hukabidhiwa mali yake. Kama akiichezea au akitapanya baada ya kukabidhiwa (kama ilivyokuwa kwa yule mwana mpotevu), hiyo ni shauri yake. Lakini kamwe hanyimwi haki yake ya kurithi, eti kwa kuwa hawezi kuitumia vema au kuitunza. Cha mno anaweza kushauriwa namna nzuri ya kumiliki mali aliyorithi.

0 maoni:

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).