Friday, June 5, 2009
URITHI: Kumnyima mtu haki ya urithi
Huko nyuma nilieleza kwa kirefu kuwa urithi ni haki au stahili ya mtu na sio kitu cha kupewa kama huruma au upendeleo fulani. Nilisema kwamba pamoja na swala la urithi kuwa ni haki ya mrithi, yapo masharti au mambo ambayo anapaswa kuyatimiza, ndipo haki hiyo iwe yake. Vinginevyo anaweza kuipoteza au kuikosa kabisa.
Katika jamii zetu, yawezekana kabisa mwenye kurithisha au mwenye kutoa wosia akamnyima mrithi wake halali haki hiyo. Kwa mfano anaweza asimjumuishe katika wosia wake kama mmoja wa warithi. Au anaweza kutoa tamko kwamba atakapokufa, mrithi huyo asipate chochote katika mali yake. Watu wengine wanaweza hata kumlaani mrithi halali.
Sababu za kumyima mtu haki yake ya kurithi
Nchini Tanzania zipo sababu nzito takribani tatu, ambazo zikithibitika, mrithi halali anaweza kukosa haki hiyo. Sababu zenyewe ni hizi zifuatazo;
(i) Ikiwa mrithi amezini na mke wa mwenye kutoa wosia.
(ii) Ikiwa mrithi amejaribu kumuua, kumshambulia au kumdhuru vibaya mwenye kutoa wosia. Au kama amemtendea mambo kama haya mama wa mwosia, yaani mke wa marehemu au mjane aliyeachwa.
(iii) Ikiwa mrithi, bila sababu yoyote ya msingi, hakumtunza mwenye kutoa wosia katika shida ya njaa au ya ugonjwa.
Jambo muhimu la kukumbuka ni kwamba, mtoa wosia anayetaka kumnyima mrithi wake haki hiyo, ni lazima aandike au aeleze hivyo katika wosia wake. Vile vile anatakiwa ataje sababu za kufanya hivyo. Vinginevyo uamuzi wake unaweza usitekelezwe, halafu mrithi huyo akapewa haki yake ya kurithi.
Biblia inasema nini kuhusu kumnyima mtu haki ya urithi?
Tunapoigeukia Biblia tunaweza kuona kwamba nayo ina mazingira ambayo mrithi halali alikosa haki yake ya kurithi. Tunao mfano wa Reubeni, ambaye alikosa haki hiyo kwa sababu alizini na mke wa baba yake. Tunaambiwa kuwa, “Ikawa Israeli alipokuwa akikaa katika nchi ile, Reuben akaenda akalala na Bilha, suria wa babaye; Israeli akasikia habari (Mwanzo 35:22).
Ulipokuja wakati wa kuwabariki au kuwarithisha wanawe, Yakobo au Israeli alimnyima Reuben haki yake ya uzaliwa wa kwanza, ambapo alipaswa kuwa kiongozi wa ndugu zake. Sikiliza maneno yaliyotamkwa dhidi yake. “Reuben, u mzaliwa wangu wa kwanza, nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu. Umeruka mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu, kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu” (Mwanzo 49:3-4).
Mfano mwingine wa kunyimwa haki ya urithi ni wa Esau. Nafikiri wasomaji wazuri wa Biblia mnakifahamu kisa cha Esau, jinsi kwa uzembe wake alivyokosa haki yake ya mzaliwa wa kwanza (Mwanzo 25:29-34). Yeye ndiye aliyepaswa kubarikiwa na kuwa mkuu kuliko Yakobo. Bahati mbaya hilo halikutokea, na mpaka leo hii kizazi cha Esau hakina ukuu kama kile cha Yakobo, ambacho ndio chimbuko la Waisraeli.
Msomaji unaposoma kitabu cha Mwanzo 27:37-40 unaweza kuona jinsi Esau alivyojuta baada ya kukosa mbaraka wa baba yake. Na katika waraka kwa Waebrania 12:16-17 tunaonywa kwamba,“tusiwe kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kurithi Baraka, alikataliwa, ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi”.
Utetezi wa mtu aliyenyimwa urithi
Kama nilivyoeleza, mtu anayekusudia kumnyima mrithi wake haki ya kurithi, anatakiwa amwite na kumweleza sababu za kufanya hivyo. Anaweza kufanya hivyo mbele ya baraza la ukoo. Lengo la kuweka wazi jambo hili mapema ni kumpa mrithi nafasi ya kujitetetea, na vile vile kuondoa migongano inayoweza kutokea baada ya kifo cha mwenye kutoa wosia.
Ikiwa mtu aliyenyimwa urithi hakuwa na habari kabla ya kifo cha mwenye kutoa wosia, atasikilizwa utetezi wake na baraza la ukoo. Kama baraza hili litaona kwamba amenyimwa urithi pasipo sababu za msingi, wosia uliokuwepo utavunjwa, halafu mali ya marehemu itagawanywa kwa kufuata mpango wa urithi usio na wosia.
Kama ikitokea kwamba mrithi aliyenyimwa haki yake haridhiki na uamuzi wa baraza la ukoo, anaweza kupeleka madai au shauri lake mahakamani. Lakini ikiwa huyo mrithi alijua kwamba amenyimwa urithi, halafu hakujishughulisha kupata nafasi ya kujitetea wakati wa uhai wa mwenye kutoa wosia, hawezi kupinga wosia huo baada ya kifo kutokea.
0 maoni:
Post a Comment
Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.