Friday, June 5, 2009

URITHI: Kwanini mzaliwa wa kwanza alipendelewa?

Pengine msomaji utakuwa unajiuliza ni kwanini mtoto wa kwanza alikuwa anapendelewa wakati wa kurithi? Moja ya sababu za kumrithisha mara mbili zaidi ya wadogo wake ni kutokana na majukumu yaliyokuwa yanamkabili. Kama baba yake hakuwepo, yeye ndiye alikuwa anachukua jukumu la ukuu wa nyumba au familia.

Endapo baba yake angefariki, mzaliwa wa kwanza alibaki na jukumu la kuilea familia iliyoachwa. Kwahiyo ilibidi awezeshwe kwa kuachiwa mali mengi zaidi. Vinginevyo angeweza kukwama katika majukumu aliyoachiwa.

Jambo hili la kuilea familia lilitokea hata kwa Bwana Yesu, ambapo historia inaonesha kuwa baba yake wa kimwili (Yusufu) alifariki mapema, akamwachia jukumu la kumlea mama yake pamoja na wadogo zake. Ndio maana alifanya kazi ya useremali kwa ajili ya kujipatia kipato.

Biblia inasema nini kuhusu haki ya mzaliwa wa kwanza?

Hebu tuangalie Biblia inasema nini kuhusu haki ya mzaliwa wa kwanza. Katika kitabu cha Mwanzo 25:29-34 tunakutana na kisa cha jinsi Yakobo alivyomlaghai kaka yake Esau, mpaka akamwuzia haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

Kwa kifupi Esau alitoka kuwinda wanyama na inaelekea siku hiyo hakupata kitu. Aliporudi nyumbani alimkuta mdogo wake (Yakobo) amepika chakula cha dengu, na kwa kuwa alikuwa na njaa sana, akamwomba amgawie hicho chakula.

Sasa sikiliza majibu ya mdogo wake “Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza” (Mwanzo 25:31-34).

Tunaweza kuona kuwa watoto wa Isaka (Esau na Yakobo) walijua swala la haki ya mzaliwa wa kwanza, na pia walikubaliana nalo. Yakobo alijua Esau alipaswa kubarikiwa zaidi yake. Ndio maana alitumia ujanja kununua haki ile. Swali la kujiuliza ni je, leo hii tuna haja ya kuendeleza swala la haki ya uzaliwa wa kwanza?

Haki ya mzaliwa wa kwanza iliheshimiwa sana

Mahali pengine ambapo Biblia inazungumzia haki ya mzaliwa wa kwanza ni katika amri, sheria na hukumu ambazo Mungu alizitoa kwa wana wa Israeli. Moja ya amri au sheria hizo inasema hivi, “Akiwa mtu yuna wake wawili, mmoja ampenda, mmoja hampendi, nao wamemzalia watoto, ampendaye na asiyempenda wote wawili; na yule mzaliwa wa kwanza akiwa ni wa mke asiyependwa; ndipo itakapokuwa ya kwamba siku atakayowarithisha wanawe alivyo navyo, asimweke mwana wa ampendaye kuwa mzaliwa wa kwanza mbele ya mwana wa asiyempenda, naye ndiye mzaliwa wa kwanza huyu; lakini amkubali mzaliwa wa kwanza mwana wa yule asiyempenda, kwa kumpa mafungu mawili katika vyote alivyo navyo; kwa maana ndiye mwanzo wa nguvu zake; haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake yeye” (Kumbukumbu la Torati 21:15-17).

Mistari hii inaonyesha jinsi haki ya mzaliwa wa kwanza ilivyokuwa inaheshimiwa. Mtu asingeweza kubadilisha haki hiyo kirahisi. Baadaye tutaona kuwa hata katika siku za leo, haki ya kurithi inaheshimiwa sana, na haiwezi kubadilishwa kienyeji. Ni lazima pawepo na sababu za msingi za kufanya hivyo.

Wana wa Israeli na kanisa ni wazaliwa wa kwanza
Hili swala la uzaliwa wa kwanza ni zito na lina maana kubwa sana, sio katika enzi za Agano la Kale tu, bali hata katika siku za leo. Mtu akiichunguza Biblia kwa makini atagundua kuwa Mungu alilichukulia taifa la Israeli kama mzaliwa wake wa kwanza.

Mungu alipokuwa anataka kuwatoa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri, alimwambia Musa maneno yafuatayo, “Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu” (Kutoka 4:22).

Vile vile kanisa au watu waliookoka, nao ni wazaliwa wa kwanza. Hili lipo wazi tunaposoma Waebrania 12:22-23 ambapo tunakutana na maneno yafuatayo, “Bali ninyi (yaani kanisa) mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu wa kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika”.

Msomaji ninajaribu kueleza kwa kina umuhimu wa mzaliwa wa kwanza kwani katika sehemu ya pili ya makala haya, ambapo nitazungumzia urithi kutoka kwa Mungu, nitaonyesha kuwa kanisa ndio wanaopaswa kurithi baraka za Mungu. Kwahiyo nakuomba tufuatane kwa makini.

Yesu ni mzaliwa wa kwanza
Ukizidi kuichunguza Biblia unagundua kuwa Yesu ni mzaliwa wa kwanza kwa Baba yake, yaani Mungu Baba. Hii haimaanishi kuwa Yesu alianza kuwepo baada ya Baba yake. La hasha. Wote ni wamoja, ila katika ulimwengu wa roho, Yesu ni mwana pekee (yaani wa kwanza na wa mwisho) wa Mungu (Yohana 3:16).

Yesu anapata cheo cha kuwa mzaliwa wa kwanza kwa sababu yeye ndiye aliyetangulia kufufuka kutoka kwa wafu. Vile vile yeye ni kichwa au kiongozi wa kanisa, kama ambavyo mtoto wa kwanza wa kiume anavyokuwa kiongozi wa familia baba yake anapokuwa hayupo.

Katika Wakolosai 1:17-18 tunaambiwa kuwa, “Naye (Yesu) amekuwapo kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote”.

Yesu ni mkuu au kiongozi wa watu wote waliookoka. Ni kama kaka yetu na sisi ni wadogo au ndugu zake, yaani sisi tuliookoka. Hili lipo wazi tunaposoma Warumi 8:29 ambapo tunaambiwa, “Maana wale aliowajua (Mungu) tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake (Yesu), ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi”.

Nafikiri msomaji mpaka sasa umeshaelewa umuhimu wa uzaliwa wa kwanza. Katika sehemu ya pili ya makala haya nitaonyesha kuwa, Yesu kama mzaliwa wa kwanza na wa pekee, amekabidhiwa au amerithishwa vitu vyote na Baba yake (Mungu) kwa ajili ya kanisa au sisi wadogo zake tuliookoka.
Upendeleo wakati wa kurithisha

Sasa hebu tuachane na habari ya uzaliwa wa kwanza, tuendelee na somo letu. Katika baadhi ya makabila hapa nchini Tanzania, huwa kunakuwa na upendeleo kati ya watoto wa kiume wakati wa kuwarithisha mali za baba zao. Wachaga tuna mila na desturi hiyo.

Unakuta mtoto wa mwisho wa kiume ndiye anayerithi shamba na nyumba aliyojenga baba yao. Wengine wote inabidi watafute mashamba yao wenyewe au wanaweza kupewa shamba, lakini inawabidi waliendeleze kwa kujenga nyumba zao na kulistawisha.

Lakini huyu mtoto wa mwisho anapewa nyumba iliyo tayari na shamba ambalo tayari limestawishwa. Kwa namna fulani, huu ni upendeleo kwa huyo mtoto. Vile vile inaweza kuleta madhara kama wivu, uadui, kinyongo, chuki na kadhalika.

Watoto wengine kwa kufahamu kwamba wao ni wa mwisho kuzaliwa, na kwamba ni warithi wa sehemu kubwa ya mali ya baba yao, huwa hawajibidiishi katika maisha. Kama ni shuleni, huwa hawasomi kwa bidii. Wakati mwingine wala hawataki kufanya kazi yoyote. Wanachosubiri ni siku ya kupewa urithi tu. Hilo nalo ni tatizo.

Je, tuendelee kuwa na upendeleo au ubaguzi wakati wa kurithisha?
Pengine msomaji unajiuliza mbona ninatoa mifano ya kurithi kutoka katika Agano la Kale? Au mbona ninataja urithi kufuatana na mila au desturi za makabila yetu? Je, ndivyo tunavyopaswa kurithisha?

Nisikilize kwa makini. Sina maana hiyo hata kidogo. Ninaitoa hii mifano kwa sababu ninajua kuwa Wakristo wengi hufuata, aidha maelekezo ya Biblia, au mila na desturi za makabila yao. Kwahiyo wapo ambao watataka kuangalia neno la Mungu au mila zao zinasema nini kuhusu swala la urithi.

Vile vile hata sheria za nchi yetu zinazohusu maswala ya mirathi zimezingatia imani za kidini, pamoja na mila au desturi za makabila mbalimbali yaliyopo nchini Tanzania. Ndio maana nimetangulia kusema kwamba huu upendeleo upo hata katika sheria za mirathi zinazotumika hapa nchini.

Mwisho, katika jamii zetu kuna wazazi ambao wasingependa kugawa urithi katika hali ya usawa kabisa. Wangependa kuwe na tofauti kati ya watoto wa kike na wa kiume, au hata kati ya watoto wa kiume. Tutakapoanza kuangalia sheria za mirathi, jambo hili litakuwa dhahiri zaidi.
Watoto wa kambo

Mtoto wa kambo ni yule asiyekuwa na uhusiano wa damu na mwingine katika familia. Mume anaweza kuwa na mtoto ambaye hakuzaliwa na mke wake wa ndoa. Mifano mizuri katika Biblia ni Ishmaeli, ambaye Ibrahimu alimzaa kupitia binti wa kazi (Mwanzo 16:1-4) au Yeftha, ambaye Gileadi alimzaa na kahaba mmoja kabla hajaoa (Waamuzi 11:1-3).

Swala la kuwa na mtoto wa kambo haliwahusu wanaume peke yao. Hapana. Hata wanawake wanaweza kuwa na mtoto au watoto wa kambo. Kinachotokea ni kwamba mwanamke anaweza kuolewa akiwa tayari ana mtoto au watoto aliowazaa na mwanamume au wanaume wengine. Au anaweza kuzaa na mwanamume asiye mumewe wakati akiwa ndani ya ndoa.

Aina za watoto wa kambo
Sasa msomaji tayari tunapata picha kuwa kuna aina mbili za watoto wa kambo. Aina ya kwanza ni wale waliozaliwa na mwanamume au mwanamke mwingine kabla ya kuingia katika ndoa ya sasa. Aina ya pili ni wale waliozaliwa na mwanamume au mwanamke mwingine wakati wa uhai wa ndoa yake. Yaani watoto waliotokana na uzinzi.

Swali tunalotaka kujibu ni je, watoto wa kambo wana haki yeyote ya kurithi? Tunataka kuangalia sheria zinazosimamia maswala ya urithi hapa Tanzania zinasema nini kuhusu jambo hili. Vile vile tutaendelea kuangalia neno la Mungu linasema nini kuhusu tatizo hili.

Hapa naomba nitoe angalizo. Swala la watoto wa kambo linawakumba watu wengi katika jamii yetu. Jambo hili linaweza kuwakumba hata watu wa Mungu. Lisiposhughulikiwa vema, na kwa kufuata sheria zilizopo, linaweza kuleta matatizo katika familia na jamii kwa ujumla. Kwahiyo ni vema kuwa makini sana katika swala hili, wakati wa kurithisha.

Wanayotendewa watoto wa kambo
Kabla hatujaanza kuangalia sheria za nchi au Biblia inasema nini kuhusu watoto wa kambo, hebu nieleze uzoefu nilio nao kuhusu yale wanayotendewa na jamii. Yaani kile ambacho baadhi ya watu hukifanya, pale wanapojikuta wanakabiliana na swala la mtoto wa kambo. Na kusema kweli mambo mengine sio mazuri hata kidogo.

Tukianza na watoto wa kambo waliozaliwa kabla ya ndoa, unakuta baadhi ya wanandoa wanaficha jambo hili. Yaani wakati wa kuchumbiana, mwanamume au mwanamke hasemi kwamba tayari ana mtoto au watoto aliozaa na mtu mwingine. Unakuta huyo mtoto au watoto wapo kwa ndugu kama bibi, au shangazi, au kaka, au dada, na kadhalika.

Baada ya kuingia kwenye ndoa, wapo wanandoa ambao hufichua siri kwamba tayari walishazaa. Lakini wengine huendelea kujikausha. Wapo wanaoweza kufanya jambo hili kuwa ni siri katika muda wote wa uhai wa ndoa, ingawa ni wachache sana wanaofanikiwa kufanya hivyo. Wengi siri hufichuka mapema tu, mara baada ya kuanza maisha ya ndoa. Hapo ndipo ‘kasheshe’ au ‘sokomoko’ ndani ya nyumba inapozuka.

Wanaoficha ukweli ni pamoja na watu wa Mungu
Inasikitisha kuona kuwa wanaodanganya wakati wa uchumba kwamba hawajazaa ni pamoja na wakristo wanaokiri wokovu. Bila shaka wanaogopa kwamba wakijulikana tayari wamezaa, uchumba utavunjika. Kwahiyo mlokole wa watu anajifanya yeye ni ‘fresh’ kabisa; eti hana mtoto yeyote.

Sikiliza wewe dada au baba unayesoma makala haya. Kudanganya kwamba hujawahi kuzaa ni dhambi mbele za Mungu. Siri ikifichuka baadaye, ndoa yako itakuwa na matatizo. Lakini kibaya zaidi ni kwamba, kwa sababu ambazo baadaye nitazieleza, unamnyima huyo mtoto wa kambo fursa ya kupata urithi. Kwahiyo ni bora kuwa muwazi na mkweli tangu mwanzo wa uchumba wenu.

Tukija kwa watoto wa kambo wanaozaliwa ndani ya ndoa, tunakuta kwamba nalo ni tatizo kubwa katika jamii nyingi hapa nchini. Unakuta mmoja wa wanandoa, au wote wawili, kila mmoja ana mpenzi wa nje. Nafikiri wengi tunafahamu visa vya wanaume na nyumba ndogo, au wanawake wasio waaminifu katika ndoa zao.

Watu wa Mungu nao hukumbana na matatizo ya watoto wa kambo
Tunapowageukia walokole tunaona kuwa nao kuna wakati huwa wanakumbana na tatizo la watoto wa kambo waliozaliwa baada ya kufunga ndoa. Ukweli ni kuwa tatizo la kutembea nje ya ndoa au uzinzi, linawakumba hata watu wa Mungu. Tena utashangaa kuona kuwa watu walioathirika na tatizo hili ni watu wazito kama Maaskofu, Wachungaji, Wainjilisti, Mitume na Manabii.

Msomaji kama uko makini utakubaliana nami kuwa siku hizi visa vya walokole au watumishi wa Mungu kukumbwa na kashfa za uzinzi ni vingi mno. Ninao ushuhuda wa ndugu mmoja ambaye Mungu alimwonyesha jinsi baadhi ya watumishi wake wanavyozini bila hofu yoyote. Kwa kweli Mungu alisaidie na kuliponya kanisa lake. Hali sio nzuri hata kidogo.

Sasa bila kujali kwamba hao watoto wa kambo wamezaliwa kabla au baada ya ndoa, swali la kujiuliza ni je, sheria iliyopo inasema nini kuhusu haki yao ya kurithi? Je, nao wanaweza kugawiwa urithi? Na je, Biblia inasema nini kuhusu jambo hili? Kama mtoto wa kambo amezaliwa kutokana na uzinzi, je, ndoa inavunjika? Au watoto wa kambo wanafukuzwa kama ilivyokuwa kwa Ishmaeli? Haya yote tutayajadili katika makala haya.

Watoto wa kupanga
Kundi lingine la watu ambao wanaweza kuwa na stahili ya kurithi mali ya marehemu ni watoto wa kupanga (adopted children). Kwa wale msiofahamu Kiswahili vizuri, watoto wa kupanga ni wale waliochukuliwa na wanandoa, kisha wakawalea kama watoto wao wa kuwazaa. Kwa mfano, unakuta wanandoa wamekubaliana kuchukua mtoto au watoto ambao ni yatima, au wakimbizi, au wanaoishi katika mazingira magumu au waliotelekezwa na mama zao.

Baadhi ya wanandoa ambao hawakujaliwa kuzaa, hupenda sana kuwa na watoto wa kupanga. Au unakuta wanandoa wengine wana watoto wao wa kuwazaa wenyewe, lakini kutokana na uwezo au moyo wa huruma, wanachukua watoto wa watu wengine na kuwalea kama wa kwao kabisa.

Swali la kujiuliza ni je, watoto wa kupanga wana haki ya kurithi mali ya huyo mlezi wao? Je, wanachukuliwa kama watoto wa ndoa, au watoto wa kambo, au vipi hasa? Mila na desturi zetu, au sheria za nchi zinasema nini kuhusu watoto wa kupanga? Msomaji tuzidi kufuatana, baadaye tutapata majibu ya maswali yote haya.

Watoto wa kufikia
Kundi lingine ambalo nataka nilizungumzie ni watoto wa kufikia. Hawa ni watoto ambao mmoja wa wanandoa anakuwa nao kabla ya kuolewa, lakini kabla ya kufunga ndoa wanakubaliana kuwa watawachukua na kuwalea kama watoto wao. Wakati mwingine unakuta kila mwanandoa alishazaa kabla ya kuoana, lakini wanakubaliana kwamba kila mmoja wao aje na mtoto au watoto alio nao, halafu wanawaunganisha na kuwalea kwa pamoja kama familia yao.

Binafsi ninamfahamu mtumishi mmoja wa Bwana, tena mtu maarufu sana, ambaye ndoa yake ina watoto wa kufikia. Kilichotokea ni kwamba kabla ya kuokoka, huyo mtumishi alishakuwa na watoto. Baada ya kuokoka, akampata mwanamke ambaye naye alikuwa amezaa na mwanamume mwingine. Wao walikubaliana waanze maisha na hao watoto wote ambao kila mmoja alishazaa, halafu wakaendelea kuzaa wengine. Mpaka leo wanaishi kwa furaha na amani tele.

Biblia inatambua kuwepo kwa watoto wa kufikia
Kibiblia jambo hili la watoto wa kufikia linaweza kutokea hivi. Katika 1Wakorintho imeandikwa kuwa, “Mwanamke hufungwa maadamu mumewe yu hai, lakini ikiwa mumewe amefariki, yu huru kuolewa na mtu yeyote amtakaye; katika Bwana tu.”.

Kinachozungumziwa hapa ni kwamba mjane yu huru kuolewa na mwanamume yeyote ampendaye. Kama mjane huyu ameokoka, ni lazima aolewe na mtu ambaye naye ameokoka. Sio anaolewa na mtu ambaye hajaokoka. Hii hairuhusiwi kwani Biblia inatuagiza kuwa, tusifungwe nira pamoja na watu wasioamini (2Wakorintho 6:14). Yaani tusioane na watu ambao bado hawajaokoka.

Sasa kuna wakati hutokea kwamba mjane alikuwa amezaa watoto na marehemu mumewe wa kwanza, na watoto hao bado anakaa nao. Kama atababahatika kumpata mtu anayempenda na anayetaka kumwoa, ni wazi kuwa huyo baba atakuwa amemkuta na watoto wa mwanamume mwingine. Kama atawachukua, hao kwake watakuwa ni watoto wa kufikia.


Watoto wa kufikia ni watoto wa kambo
Kimsingi watoto wa kufikia ni kama watoto wa kambo. Tofauti iliyopo ni kwamba, kwa upande wa watoto wa kufikia, kunakuwa na maelewano kabla ya kufunga ndoa. Lakini watoto wa kambo, kunakuwa hakuna maelewano yeyote. Jambo lenyewe linakuja kwa kushtukiza. Yaani tangu mwanzo linakuwa halijulikani au linajitokeza katikati ya uhai wa ndoa.

Hapa nataka tujiulize maswali yafuatayo. Hivi watoto wa kufikia wana haki gani wakati wa kurithi? Je, wanakuwa na haki sawa na hao watoto waliozaliwa ndani ya ndoa? Je, kama wewe unaishi na watoto wa kufikia, halafu baba zao wa kuwazaa (natural fathers) wakajitokeza baadaye na kudai wapewe watoto wao, utawaambia nini? Je, utawapa au utawakatalia?

Utakapofika wakati wa kurithisha, je, utawagawia mali watoto wa kufikia sawasawa na hao mliozaa ndani ya ndoa au utawabagua? Haya ndiyo mambo ambayo nataka tuyajadili katika makala haya. Tuendelee kuwa pamoja msomaji wangu.


Watu wasio na undugu na marehemu
Wakati mwingine marehemu anaweza kumrithisha mtu baki kabisa. Yaani marehemu anarithisha mali zake kwa mtu ambaye hana uhusiano wa damu naye. Kwa mfano wapo matajiri wanaoacha sehemu ya mali zao kwa ajili ya wajane, yatima, maskini, vilema, wagonjwa wa saratani na kadhalika. Pia watu ambao hawakujaliwa kupata watoto, wanaweza kuacha mali zao zote kwenye mifuko ya maendeleo au taasisi mbalimbali (Development Foundations or Institutions).

Maswali la kujiuliza ni je, jambo hili linafanyika vipi? Je, watu kama vile mjane au watoto wa marehemu wanaweza kupinga urithi ulioelekezwa kwa watu wengine zaidi ya wao? Je, sheria zinazosimamia maswala ya urithi zimeelekeza nini kuhusu marehemu ambaye amerithisha mali zake nje ya wale wanaodhaniwa kwamba ndio wenye haki ya kurithi? Baadaye tutapata majibu ya maswali magumu kama haya.

Sheria zinazotawala taratibu za urithi au mirathi
Baada ya kujadili matatizo ya urithi pamoja na watu ambao wanaweza kuwa warithi wa marehemu, sasa ni wakati wa kuangalia sheria zinazotawala maswala ya urithi hapa nchini Tanzania. Sheria hizi kwa pamoja zinaitwa sheria za mirathi na zimetungwa na Bunge letu tukufu. Hizi ndizo zinazotumika wakati wa kugawa mali ya marehemu, au kutatua matatizo yatokanayo na urithi.

Kabla hatujaanza kuchambua sheria za mirathi, nafikiri ipo haja ya kufahamishana maana ya mirathi. Ingawa neno hili limewahi kusikika na watu wengi, yumkini wapo wasiofahamu maana yake kikamilifu. Kwahiyo hapa ipo haja ya kuelimishana.

Kamusi ya Kiswahili Sanifu inaeleza kwamba mirathi ni vitu au mali yanayoachwa na mtu aliyekufa na kupewa watu wake kwa mujibu wa mipango maalumu. Vile vile inaeleza kuwa ni elimu maalumu inayohusika na ugawaji wa mali ya marehemu, hususan katika dini ya Kiislamu.

Kwa kifupi mirathi ni namna ambavyo mali iliyoachwa na marehemu hushughulikiwa na wale waliobaki, kwa lengo la kuwagawia warithi wake. Kwa kuwa mwenye kauli kamili juu ya mali yake anakuwa amefariki, kunaweza kutokea matatizo kwamba nani awe mrithi, na vile vile arithi kiasi gani cha mali iliyoachwa na marehemu.

Kama nilivyotangulia kusema, matatizo ya urithi huwagusa zaidi wajane na watoto wa marehemu. Hawa ndio huteseka, iwapo mambo hayakuwekwa sawa. Lengo kuu la sheria za mirathi ni kuwasaidia watu kama hawa, ili wapate haki zao. Ili wasidhulumiwe au wasidhulumiane.

1 maoni:

Gerald Malika said...

Nimefurahishwa na ufafanuzi juu ya maana ya mzaliwa wa kwanza na Baraka zinazotokana naye. Mungu akubariki sana kwa maarifa haya.

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

Recent Posts

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).