Friday, June 5, 2009

URITHI: Wana wa Mungu na watoto wa Mungu

Tunapokuja katika maswala ya Kimungu tunakuta kuwa, napo kuna tofauti kati ya mwana na mtoto. Mwana wa Mungu ni mtu yeyote aliyezaliwa mara ya pili. Ni mkristo aliyeokoka. Huyu ndiye anayestahili kurithi baraka kutoka kwa Mungu. Ndiye anayestahili kubarikiwa.

Mtu ambaye hajaokoka ni mtoto wa Mungu. Huyu hana tofauti na mtoto wa kambo, ambaye tuliona kuwa hastahili kurithi chochote kutoka kwa baba au mama wa kambo, labda katika mazingira malumu. Ndio kusema kuwa, wewe ambaye hujaokoka, hustahili kurithi chochote kutoka kwa Mungu.

Wewe ambaye hujaokoka unaweza kuwa na mafanikio makubwa katika maisha yako, lakini hizo sio baraka za Mungu. Ukijichunguza kwa makini utagundua kuwa, hivyo vitu ulivyo navyo havina uhusianao wa moja kwa moja na Mungu. Havikupatikana kwa msaada wake.

Mafanikio uliyo nayo yanaweza kuwa yametokana na nguvu au jasho lako binafsi, lakini sio kwa kumwomba au kumtumainia Mungu. Na pengine ulienda kwa waganga wa kienyeji, wakakupa dawa ya kupata mali, au mtoto, au cheo kazini, na kadhalika. Huko sio kubarikiwa, hata kama jamii itakuona kuwa umefanikiwa kimaisha.

Unapookoka unabadilishwa kutoka ‘mtoto’ na kupewa cheo cha kuitwa ‘mwana’.
Ili swala la kuwa mwana lieleweke vizuri, hebu tusome maandiko machache. Katika Wagalatia 3:26 imeandikwa hivi, “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu”

Wanaozungumziwa hapa ni watu waliomwamimi Yesu. Ni watu waliookoka. Katika Warumi imeandikwa kuwa, “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba”.

Hawa wanaosemwa kwamba wanaongozwa na Roho wa Mungu ni wakristo waliookoka. Hao ndio waliopokea roho ya kufanywa wana na Mungu ni baba yao. Yaani wamebadiliswa kutoka katika hali ya kuitwa watoto na sasa wanapewa cheo cha kuitwa wana wa Mungu.

Katika Waefeso 1:5 imeandikwa kuwa, “Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake”. Hapa napo tunaona kuwa kuna watu ambao Mungu aliwachagua, ili awafanye wanawe. Hawa sio wengine bali ni watu waliomwamini Yesu. Ni watu waliookoka.

Tunaposoma 1Yohana 3:1 tunakutana na maneno haya, “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuiwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo.” Andiko hili linatuonyesha kuwa watu waliookoka wanaitwa wana wa Mungu. Hawaitwi watoto wa Mungu.


Tafsiri za Biblia zinatofautiana
Ninapojaribu kueleza tofauti ya mtoto na mwana, naomba nitoe tahadhari kidogo. Natambua kuwa Biblia inachanganya maneno haya mawili. Kwa mfano katika Yohana 1:12 imeandikwa kuwa, “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake”.

Ukweli ni ni kuwa, kama tungetumia Kiswahili fasaha, neno ambalo lingepaswa kutumiwa hapa ni ‘kufanyika wana wa Mungu’ na sio ‘kufanyika watoto wa Mungu’ Tatizo la kuchanganya mtoto na mwana lipo hata katika Biblia za Kiingereza.

Unakuta neno linalotumia zaidi ni ‘child’ au ‘children’ Lakini baadhi ya Biblia zinatumia neno ‘son’ au ‘sons and daughters of God’ Na ukweli ni kuwa hata katika lugha ya Kiingereza kuna tofauti kati ya ‘child’ na ‘son’ au ‘daughter’.

Neno ‘son’ au ‘daughter’ lina maana ya mtoto ambaye umemzaa. Yule ambaye hujamzaa anaitwa ‘a child’. Ndio maana utasikia Mwingereza mzuri akisema ‘my son or my daughter’. Hawasemi ‘my child’. Hicho sio Kiingereza safi. Ni sawa na kusema ‘mtoto wangu’ badala ya ‘mwanangu’.

Yesu ni ‘Mwana wa Mungu’, sio mtoto wa Mungu
Kwa kumalizia kipengele hiki cha tofauti kati ya mwana na mtoto, hebu tumwangalie Bwana wetu Yesu Kristo. Sote tunajua kuwa huyu anaitwa Mwana wa Mungu. Anaitwa hivyo kwa sababu amezaliwa na Mungu. Kuzaliwa huku kumefanyika kwa njia au kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Sio kwamba Maria alilala na Mungu (Mathayo 1:18-20).

Ukiisoma Biblia yote huwezi kukuta mahali wanamtaja Yesu kama mtoto wa Mungu. Kila mahali wanamwita Mwana wa Mungu. Hata katika Biblia za Kiingereza hawamwiti ‘child of God’. La hasha. Wanamtaja kuwa ni ‘Son of God’. Hii ndio lugha fasaha ya kumtaja Yesu.

Mwana ndiye mrithi
Baada ya kujadili kwa kina tofauti kati ya mwana na mtoto, hebu sasa tuendelee kuangalia jinsi ambavyo Biblia inaonyesha kwa mwana ndiye anayestahili kurithi. Tuanze na Bwana Yesu mwenyewe.

Tunaposoma Waefeso 1:20-22 tunaweza kuona uweza wa Mungu “aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa.”

Hili andiko linaonyesha jinsi ambayo Mungu alivyomtukuza sana mwanawe Yesu Kristo, baada ya kumfufua katika wafu, akaweka kila kitu chini ya miguu yake. Tunaposoma Waebrania 1:1-4 tunaweza kuona kuwa Yesu amefanywa kuwa mrithi wa vyote vilivyombwa na Mungu.

Yesu Kristo anakuwa mrithi wa vyote kwa sababu yeye ni mwana pekee wa Baba yake (Yohana 1:14). Pengine angekuwa na wadogo zake waliozaliwa na baba mmoja, wangegawana urithi. Lakini hivyo sivyo ilivyo.

Wale wadogo au ndugu zake wengine (Luka 8:19-21), baba yao ni Yusufu na sio Mungu. Yesu ni mzaliwa wa kwanza na wa mwisho kwa Baba yake (Waebrania 1:6-8). Wale wengine ni kama watoto wa kambo, ambao kama tulivyoona huko nyuma, hawawezi kurithi, labda katika mazingira maalumu.
Kanisa ndio wanaostahili kurithi baraka za Mungu

Baada ya kuonyesha kuwa kuna tofauti kati ya mtoto na mwana, na kwamba Yesu ndio aliyerithi, sasa naweza kusema kwa uhakika kabisa kuwa kanisa ndio wanaostahili kurithi baraka au ahadi za Mungu. Kanisa ni watu waliookoka. Hao tumeshaona kuwa ndio wanaoitwa wana. Na kwa sababu hiyo, wao ndio warithi.

Ukisoma Waefeso 1:15-23 unaweza kuona jinsi utaratibu mzima wa urithi kwa kanisa au watu waliookoka unavyokuwa. Mstari wa 22 na 23 unatuambia kuwa Mungu “akavitia vitu vyote chini ya miguu yake (Yesu), akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote”.

Tunaposoma Wagalatia 4:7 tunakutana na maneno haya, “Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu”.Yaani kama wewe umeokoka, unapata haki ya kuitwa mwana na vile vile kuwa mrithi wa baraka za Mungu. Saafi kweli kweli.
Watoto hawastahili kurithi baraka za Mungu

Mtu ambaye hajaokoka ni sawa na mtoto wa kambo. Ni sawa na Ishmaeli, ambaye alikuwa mwana wa mjakazi, lakini mtoto wa kambo kwa Sara, ingawa alikuwa mwana kwa Ibrahimu kama alivyokuwa Isaka. Ndio maana Biblia inatuambia kuwa, “Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe” Mwanzo 21:11).

Ishmaeli na Isaka walikuwa wana kwa Ibrahimu na baba yao alitaka wote warithi mali au baraka zake. Kikwazo kilikuwa ni Sara, ambaye kwake Ishmaeli alikuwa mtoto wa kambo, na kwa sababu hiyo hakustahili kurithi.

Kama ilivyokuwa kwa Isaka, kanisa au watu waliookoka ni wana wa ahadi; sio wana wa mjakazi au watoto wa kambo. Na kama tulivyoona huko nyuma, wana wa ahadi ndio warithi wa baraka za Mungu. Stahili hiyo ni yao.

Hebu tujikumbushe tena maneno ya Wagalatia 4:28-31 ambapo tunaambiwa, “Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi. Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa. Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana. Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana”.

Watu ambao hawajaokoka hawawezi kurithi baraka za rohoni.
Msomaji utakumbuka kuwa huko nyuma niligawa baraka zinazotoka kwa Mungu katika makundi mawili.. Nilisema kuna baraka za mwilini na baraka za rohoni. Niliainisha baraka za rohoni kama vile kujazwa au kupokea nguvu za Roho Mtakatifu, karama au vipawa mbalimbali na uzima wa milele.

Ukichunguza baraka au mambo haya utakubaliana nami kuwa huwa yanaonekana kwa watu waliookoka tu. Huwezi kukuta mtu ambaye hajaokoka akiwa naye kajazwa Roho Mtakatifu. Hawezi kunena kwa lugha. Kwanza haelewi ni kitu gani hiki.

Mtu ambaye hajaokoka hawezi kuwa na karama au vipawa kutoka kwa Mungu, kama vinavyotajwa katika Biblia. Aidha hawezi kurithi uzima wa milele. Haya ni mambo ya watu wa Mungu tu; ni ya wana wa Mungu peke yao. Huu ndio ukweli.

2 maoni:

Esther said...

Nionavyo mimi neno mtoto wa Mungu ni bora zaidi kuliko mwana kwa lugha ya Biblia, Kwa maana kwa lugha ya Biblia neno Mwana linamaanisha mtoto wa kiume ndiyo maana wagalatia 3:26 kwa kiingereza "for in Christ Jesus you are all sons of God, through faith". Sons of God maana yake ni wana wa kiume wa Mungu ama watoto wa kiume wa Mungu. Katika 1Yohana 3:1 Kiingereza inasema "Behold what manner of love the Father has bestowed on us, that we should be called children of God" (NKJV) Neno Children kama lilivyotumika hapa naona ni sahihi kabisa kwa sababu hapo linajumuisha watoto wote wa kike na wa kiume. Kwani mara nyingi Biblia ya Kiingereza inapotaja sons of God huwa inaishia hapo haikumbuki kuwa kuna daughters of God, Na ukikuta imetaja sons and daughters ujue pia hata Biblia ya Kiswahili ina fafanua watoto ama wana wa kiume na wa kike. Kwa maoni yangu ni heri neno Child/Children of God lingetumika kuliko Son/Sons of God. Hata hivyo wapo wanaofundisha kuwa waliookoka huitwa wana ama watoto wa Mungu ila wasiookoka hawawezi kamwe kuitwa watoto wa Mungu ila huitwa watu wa Mungu Kwa sababu wameumbwa na Mungu.

pascal nyangi said...

somo lako zuri linabariki mtumishi Mungu akubariki

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

Recent Posts

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).