Friday, June 5, 2009

URITHI: Mahakama ya kufungulia mirathi

Mirathi huwa haifunguliwi katika mahakama yoyote ile. La hasha. Itategemea sheria ya mirathi inayokusudiwa kutumika. Kama sheria itakayotumika kugawa mali za marehemu ni ya Kimila au ya Kiislamu, mirathi inapaswa kufunguliwa katika mahakama ya Mwanzo (Primary Court).

Kama sheria itakayotumika ni ya Kiserikali, mirathi itafunguliwa kule alikokuwa akiishi marehemu katika Mahakama ya Wilaya (District Court), au ya Hakimu Mkazi (Resident Magistrate) au Mahakama Kuu (High Court). Sio mtu anakwenda kufungua mirathi kwenye mahakama mradi ni mahakama. Mambo hayafanyiki hivyo hata kidogo.

Taratibu za kufungua mirathi
Katika nchi yetu, wapo watu ambao tayari wameshaelimika kiasi cha kutosha, na sasa wanafahamu umuhimu wa kuandaa wosia. Lakini vile vile wapo ambao bado wapo gizani na hawajui umuhimu wa jambo hili. Kwahiyo mauti yanapowakuta, kunakuwa hakuna wosia ulioachwa.

Watu wengine wanatambua umuhimu wa wosia, lakini kwa sababu mbalimbali, wanakumbana na kifo kabla ya kuuandaa. Wakati mwingine ni kwa sababu ya uzembe tu, yaani mtu anaahirisha jambo hili kila kukicha, mpaka mauti inamkuta. Sababu nyingine ni imani potofu kuwa mtu akiandaa wosia atakuwa anatabiri au anakaribisha kifo chake. Eti anaweza kufa mapema kabla ya wakati wake.

Kwa bahati nzuri serikali ya nchi yetu inatambua matatizo au madhaifu kama haya ya kijamii. Kwa sababu hiyo imeandaa taratibu za kufungua mirathi katika mazingira ambayo wosia upo na vilevile wakati haupo. Nitaeleza taratibu hizo.

Wosia ukiwepo
Kama marehemu aliacha wosia, utaratibu wa kufungua mirathi uko hivi;

 1. Kifo kiandikishwe kwa Mkuu wa Wilaya katika muda usiozidi siku 30. Lengo ni kupata cheti cha kifo (Death Certificate). Cheti hiki ni tofauti kabisa na kile cha uthibitisho wa kifo, ambacho huandkwa na daktari mara tu baada ya kifo kutokea.
 2. Msimamizi aende mahakamani kufungua mirathi akiwa na wosia wa marehemu, pamoja na cheti cha kifo.
 3. Mahakama itatoa tangazo la mirathi litakalodumu kwa muda wa siku 90. Iwapo hakutatokea pingamizi lolote, mahakama itatoa barua ya usimamizi wa mirathi kwa mtu aliyeomba au aliyefungua mirathi. Barua hiyo itampa uhalali wa kugawa mali ya marehemu (urithi) baada ya kulipa madeni.
 4. Msimamizi wa mirathi ataorodhesha mali ya marehemu na kuigawa kama ilivyoainishwa kwenye wosia.
 5. Baada ya kugawa mali, msimamizi atarejesha taarifa mahakamani akieleza jinsi alivyotekeleza wosia wa marehemu.
 6. Hatimaye mahakama itafunga jalada la mirathi.
Wosia usipokuwepo
Kama marehemu hakuacha wosia, utaratibu unaofuatwa ni kama ule wa mazingira ambayo wosia upo, isipokuwa msimamizi wa mirathi huchaguliwa na baraza au mkutano wa ukoo. Mtu aliyechaguliwa huenda mahakamani akiwa na kumbukumbu au muhtasari wa kikao kilichomchagua.

Hapa naomba niseme kwamba ni Watanzania wachache sana wanaofahamu na wanaofuata taratibu za ufunguzi wa mirathi. Wengi wanapeleka mambo kienyeji tu. Hilo ni kosa kisheria na mtu anaweza kushitakiwa mahakamani. Kwahiyo ni wajibu wetu kufahamu taratibu za mirathi na kuzifuata kama zilivyo, na sio vinginevyo.

Jukumu la msimamizi wa mirathi
Sasa tunakuja katika eneo ambalo binafsi ninaamini kwamba watu wengi sana huwa wanalikosea na vile vile lina lawama nyingi mno. Hili linahusu majukumu ya msimamizi wa mirathi. Kama kuna eneo ambalo inabidi mtu awe makini ni hili la kusimamia ugawaji wa mali ya marehemu. Kwanini ninasema hivyo?

Wapo watu wanaobeba au wanaokubali jukumu hili bila kujua wajibu wao. Kwahiyo wanaharibu utaratibu mzima wa kugawa mali iliyoachwa na marehemu. Wengine kwa sababu ya tamaa, wanakimbilia jukumu la usimamizi wa mirathi kwa lengo la kudhulumu au kujigawia sehemu ya mali iliyoachwa.

Ni vizuri kuzingatia kuwa msimamizi wa mirathi ni mdhamini au wakili tu wa kuchunga mali iliyoachwa kwa lengo la kuwagawia warithi halali wa marehemu. Msimamizi sio lazima awe mrithi, ingawa kwa sababu ya kuogopa dhuluma, mmoja wa warithi anaweza kusimamia mirathi kwa niaba ya wenzake. Mahakama nyingi humpa mke wa marehemu au mtoto mkubwa wa marehemu jukumu hili.

Msimamizi wa mirathi awe ni mtu mwadilifu
Kinachotokea katika jamii nyingi za kiafrika ni kwamba, mtu aliyeteuliwa kugawa mali ya marehemu humega sehemu ya mali hiyo wakati yeye sio mrithi. Kama ni mmoja wa warithi, yeye hujipendelea. Hili ni kosa kisheria na mtu anaweza kushitakiwa mahakamani.

Jambo lingine ambalo huwa halieleweki na watu wengi, na kwa sababu hiyo huwa haliwekwi vizuri au halifafanuliwi na wanandugu, ni gharama za usimamizi wa mirathi. Ukweli ni kuwa jukumu la kusimamia mirathi hugharimu muda, nguvu za mtu pamoja na fedha.

Watu wengi huwa hawatambui kuwepo kwa gharama hizi, na msimamizi anapozidai au anapozikata katika mali ya marehemu (recover costs), anaonekana kama vile anawadhulumu warithi halali. Hata kama msimamizi huyo ni mmoja wa warithi, bado akizikata ataonekana kama vile anawadhulumu wenzake au anajipendelea. Swali la kujiuliza ni je, gharama za usimamizi wa mirathi zinalipwa na nani?

Wasimamizi wengine sio waaminifu. Wanaweza kumega sehemu kubwa ya mali ya marehemu, kwa kisingizio kwamba ni gharama za usimamizi. Ndio maana nilisema kwamba msimamizi wa mirathi ni vema awe mtu mwadilifu, na sio mbabaishaji. Vinginevyo warithi halali wanaweza kudhulumiwa kilicho haki yao.

Mambo ya kufanya
Baada ya maelezo ya jumla juu ya sifa, matatizo na jukumu la msimamizi wa mirathi, naomba sasa niainishe mambo ambayo mtu huyu anapaswa kuyafanya. Kwa kifupi msimamizi anapaswa kufanya mambo yafuatayo;
 1. Kukusanya madeni na kuorodhesha mali ya marehemu.
 2. Kulipa madeni yote halali yaliyoachwa.
 3. Kugawa mali iliyobaki (baada ya kulipa madeni) kwa warithi halali kwa kuzingatia wosia wa marehemu au katika msingi wa haki na usawa kulingana na sheria inayosimamia mirathi hiyo.
 4. Kutayarisha taarifa ya jinsi alivyosimamia na kugawa mali ya marehemu. Taarifa hiyo iwasilishwe katika mahakama ambayo mirathi ilifunguliwa, na iwe na vipengele vifuatavyo;
 • Aina na thamani ya mali za marehemu.
 • Madeni
 • Matumizi kama vile gharama za mazishi, gharama za usimamizi wa mirathi, na kadhalika.
 • Jinsi mali iliyobaki ilivyogawiwa kwa warithi halali.
Taarifa hii inatakiwa isainiwe na warithi wote wa marehemu.

Hitimisho sehemu ya kwanza
Msomaji wangu nafikiri mpaka sasa tumeelewana kuhusu maswala mbalimbali yanayohusu urithi kutoka kwa mwanadamu mmoja kwenda kwa mwanadamu mwingine. Ninaamini kwamba yapo mambo ambayo ulikuwa huyafahamu, lakini sasa umefunguka macho na umeelimika kiasi cha kutosha.

Ninapomaliza sehemu hii ya kwanza ya mada hii, naomba niwasisitizie wakristo wenzangu umuhimu wa kuelewa sheria za nchi na kuzifuata. Ikumbukwe kuwa Biblia inatuagiza hivyo kwa kutuambia kwamba, “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo imeamriwa na Mungu” (Warumi 12:1).

Mambo tunayopaswa kuyatii ni pamoja na sheria za nchi, zikiwemo sheria za mirathi. Ninatambua kuwa wapo waumini ambao wamekuwa wa kiroho sana, kiasi ambacho huwa hawakumbuki kuchunguza na kutambua sheria za nchi yetu zinasema nini. Kwa sababu hiyo wanajikuta katika matatizo mbalimbali ya kiutawala na kisheria wakati wanaposhughulikia .maswala yao.

Kwa vile wakristo ni sehemu ya jamii, na vile vile swala la urithi linawagusa kwa namna moja au nyingine, ni vema wakatambua wajibu wao na haki zao katika jambo hili. Vinginevyo wanaweza kujikuta hawajui la kufanya, au wanaweza kuingia matatani, au wakapoteza haki zao za kurithi. Baada ya hitimisho hili, sasa tunaweza kuingia katika sehemu ya pili ya mada hii. Karibu tuendelee kuwa pamoja msomaji wangu.

3 maoni:

Anonymous said...

nashukuru kwa msaada wako wa tafsiri ya mambo....naomba kuuliza swali.....je wajukuu wanaweza kufungua mirathi baada ya kifo cha bibi yao au babu yao ambaye alikuwa na mali .....

protas valerian swagger said...

asante sana kwa msaada wako wa kisheria

Seudende Mngoma said...

jE UNAWEZA KURITHI HUKUMU YA KESI ILIYOKUWA TAYARI IMESHAHUKUMIWA ILA MARA TU BAADA YA HUKUMU MHUKUMIWA AKAFARIKI

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).