Tuesday, May 12, 2009

MKRISTO NA MAVAZI: Mavazi yasiyofaa ni yepi?

Labda kabla hatujaendelea sana, nafikiri ipo haja ya kuyaangalia japo kwa kifupi, aina ya mavazi ninayotaka kuzungumzia katika makala haya. Ni vizuri tuwekane sawa kungali mapema, ili huko mbeleni nitakapoanza kuchambua kila aina ya vazi lisilofaa, tuelewane vizuri. Kwahiyo nitakutajia aina ya nguo zilizozoeleka sana siku za leo, lakini kusema kweli mavazi hayo hayafai mbele za macho ya Mungu.

Badhi ya mavazi yaliyotapakaa mitaani na yanayopendwa na wanawake wengi wa kidunia ni haya yafuatavyo;
(i) Suruali za kubana.
(ii) Magauni ya kubana.
(iii) Vimini au magauni mafupi (mini or short dresses)
(iv) Blauzi zinazoacha matiti au mgongo wazi (low-neckline blouses)
(v) Blauzi zisizo na mikono (Sleeveless blouses)
(vi) Fulana (T-Shirts)
(vii) Nguo nyepesi zinazoonyesha maungo (shear or see-through or transparent clothing)
(viii) Kaptula au pensi nyanya.
(ix) Fulana (Singlets) zinazoshikilia matiti tu na kuacha migongo na vifua wazi.
(x) Sketi ndefu zilizopasuliwa.
(xi) Pedo (Pedal push).

Baadhi ya mavazi yasiyo ya heshima
Ukichunguza kwa makini utagundua kuwa lengo la mavazi haya ni kumwacha mwanamke uchi kwa kiwango kikubwa sana (expose a woman). Kama ni vazi la kubana, hata kama limeshuka hadi miguuni, bado litaonyesha maungo ya mwanamke yalivyo na katika hali ya kutamanisha mno. Hili ndio lengo kuu la wanawake wasio na hofu ya Mungu la kuvaa mavazi kama haya. Kwa bahati mbaya wapo walokole wanaochangamkia mavazi kama haya. Yaani wee acha tu.

Ni kosa na aibu kukaa uchi
Kitu cha kwanza ambacho yapasa kila mtu afahamu ni kwamba, ni kosa kukaa uchi. Ni kosa kubwa sana kwa mtu yeyote kuvaa mavazi yasiyosetiri mwili wake vizuri. Ni aibu kwa mwanamke au mwanamume yeyote kuanika maungo yake nje nje na hovyo hovyo tu. Tena ni dhambi mbele za Mungu. Hili nitalifafanua huko mbeleni.

Mwanzo kabisa baada ya uumbaji, pale Adamu na Hawa walipomkosea Mungu (kwa kushindwa kutii agizo lake lililohusu aina ya matunda waliyopaswa kula), walijiona wako uchi. Biblia inatuambia kuwa baada ya kula yale matunda, “Wakafumbuliwa macho wote wawili, wakajijua wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo” (Mwanzo 3:7). Yaani walipojiona wako uchi, waliona aibu, wakajifunika kwa majani.

Tangu wakati ule hadi sasa, ni aibu kwa mwanadamu kukaa uchi mbele ya mwanadamu mwenzake, hata kama wote wawili ni wa jinsia moja. Ni ajabu kuwa hata kwa baadhi ya wale walio katika ndoa, bado ni aibu kwa mwanamke kujiacha uchi uchi tu mbele ya mumewe. Hali kadhalika kwa mwanamume ndivyo hivyo ilivyo. Kila mmoja anaona aibu fulani kuangalia utupu wa mwenzake.

Kwa wanandoa wengine, hata tendo la ndoa hufanyika gizani kabisa. Ni lazima wazime taa. Kwanini? Kwa sababu wanaona aibu kuangaliana wakiwa uchi. Ni siku hizi tu, watu wanajifanya wameendelea. Lakini ukimwuliza babu yako, kama ni mkweli atakuambia kuwa wao tendo la ndoa lilikuwa linafanyika gizani, tena usiku. Walikuwa hawafanyi mchana kweupe kweupe. Kwanini? Kwa sababu walikuwa wanaoneana aibu.

Tukirudi kwa wazazi wetu wa mwanzo, yaani Adamu na Hawa, tunaona kuwa wao walikuwa wawili tu katika ile bustani ya Eden. Pamoja na uchache wao, bado waliona aibu kuangaliana wakiwa uchi. Walikuwa na kila sababu ya kusema ‘kwani kuna shida gani bwana? Si tuko wawili tu? Nani mwingine anayetuona?’ Lakini haikuwa hivyo. Bado walioneana aibu, wakajifunika kwa majani. Vile vile hata Mungu hakuwaacha wakae uchi. Aliwashonea nguo.

Kusisitiza jinsi ilivyo kosa na aibu kwa mwanadamu kukaa uchi, hebu tuangalie nini kilichotokea pale Nuhu alipolewa divai na kujikuta yu uchi. Biblia inatuambia kuwa, “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; akanywa divai akalewa; akawa uchi katika hema yake. Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao”. (Mwanzo 9:20-23).

Hapa tunaona kuwa baada ya Shemu na Yafethi kusikia kuwa baba yao yuko uchi ndani ya hema, hawakuenda kuangalia baba yao anafananaje. Wao walichukua nguo nyingine, wakaenda kinyumenyume, wakamfunika ili kuusetiri uchi wake. Kwanini walienda kinyumenyume?. Kwanza kabisa walijua ni kinyume na maumbile, mtu kukaa uchi. Walijua hilo ni kosa. Lakini vile vile waliona ni aibu kumwangalia baba yao akiwa uchi. Walijua kuwa wangejisikia vibaya sana iwapo wangeuona uchi wa baba yao.

Ikumbukwe kuwa Nuhu alikuwa ndani ya hema. Wale wanawe wangeweza kusema ‘si yuko ndani bwana? Kwani kuna shida gani” Si tumwamche tu aendelee kuuchapa usingizi? Atakapoamka si atajifunika?’ Lakini hawakufanya hivyo. Badala yake walimfunika kabla hajazinduka kwenye ulevi wake. Kwanini walifanya hivyo? Kwa sababu walijua si vema baba yao kukaa uchi, hata kama hakuna mtu aliyekuwa anamuona.

Ukitaka kujua ni aibu kukaa uchi, jichunguze wewe mwenyewe binafsi. Utagundua kuwa hata ukiwa peke yako katika chumba chako cha kulala (bedroom), bado hupendi kukaa uchi kabisa, japo hakuna anayekuona. Utajikuta unatamani kuvaa nguo inayokusetiri japo kidogo. Kama ni akina mama utawakuta angalao wamejifunga kanga moja. Akina baba wanapendelea zaidi kuvaa bukta na fulana. Hii ni kwa sababu hawajisikii vizuri kukaa uchi kabisa.

Sasa kama uchi au utupu wa mwanadamu unaleta aibu, ni kwanini kizazi cha leo hakioni soni kujianika ovyo ovyo? Ni kwa nini kizazi cha leo kina tabia ya kuvaa mavazi yasiyosetiri miili yao vizuri? Ni kwanini wazazi wanakaa uchi mbele ya watoto wao na watoto wanakaa uchi mbele ya wazazi wao? Ni kwanini watu wanakwenda ‘beach’ kujianika uchi. Amini usiamini, sababu kubwa ni kuwa hiki ni kizazi cha zinaa. Ni kizazi cha watu waovu, watu wasiojali na wasiozingatia maagizo ya Mungu.

Kizazi cha leo kimetawaliwa na zinaa. Kimevamiwa na pepo la ngono. Shetani amefungulia mapepo ya uzinzi ambayo yanawafanya wanadamu wapende sana ngono. Moja ya njia ya kueneza uzinzi ni kuvaa mavazi yanayotamanisha. Mavazi yanayoamsha tamaa ya ngono. Na kwa bahati mbaya mapepo haya yameingia hadi katika makanisa ya wateule wa Bwana. Yameweza kuwavamia hata watu wa Mungu, tena maaskofu kabisa. Hii ndiyo hali halisi, tutake au tusitake. .......(itaendelea) Read More......

MKRISTO NA MAVAZI: Mavazi yatamanishayo ni tishio kwa kanisa

Ninaamini wengi wenu mtakubaliana nami kuwa, humu duniani yapo mavazi yanayotamanisha. Yapo mavazi yanayomfanya mvaaji avute hisia za jinsia iliyo tofauti na yake. Yaani yavute tamaa ya kujamiiana. Kama yamevaliwa na mwanamke, huwa yanawavuta wanaume. Kwa kiingereza mavazi haya yanaitwa ‘provocative’ au ‘sexy dresses’. Nitashangaa sana iwapo kuna anayebisha juu ya jambo hili.

Sasa kwa kuwa lengo la makala yangu ni kuzungumzia uvaaji usiofaa, nitalenga zaidi mavazi ya kike. Hii ni kwa sababu ukweli unadhihirisha kuwa wanawake ndio wanaoongoza katika swala hili la kuvaa mavazi yasiyokuwa ya heshima. Pili, ni kwa sababu ambayo nitaileza kwa kirefu huko mbeleni; kwamba madhara yanayoletwa na wanawake walio nusu uchi ni makubwa zaidi ukilinganishwa na yale yanayeletwa na wanaume walio katika hali kama hiyo.

Ukweli ni kuwa yapo mavazi ya kike, ambayo yameshonwa kwa minajili ya kuvuta macho na kuuteka moyo wa mwanamume. Kwa minajili ya kuamsha hisia zake za ngono. Katika hali ya kawaida, mavazi haya huvaliwa zaidi na wanawake wa kidunia; wale ambao bado hawajaokoka. Lakini kidogo kidogo tayari mavazi haya yamejipenyeza katika jamii ya watu waliookoka, kiasi ambacho huwezi kuona tofauti yoyote kati ya mtu wa Mungu na mtu wa kidunia.

Iwapo uvaaji usiofaa hautadhibitiwa mapema, unaweza kuwa ni sababisho la uzinzi wa kutisha ndani ya jamii ya wateule wa Mungu. Ndani ya makanisa yetu. Uvaaji huo unaweza kushusha kabisa heshima ya jamii ya watu waliookoka. Hiki ndicho kinachonisukuma kuandika makala haya na kuonya juu ya jambo hili.

Nia yangu sio kukulaumu wewe ambaye, aidha kwa kutokujua au kwa kutojali, umejikuta tayari umeshapitiliza mipaka kwa kuvaa mavazi yasiyofaa. Nia yangu ni kukumbusha kuwa ipo haja ya kuwa makini na uvaaji wako. Ni kukumbusha kuwa Mungu anajali sana jinsi tunavyovaa na kwamba ameeleza bayana kupitia neno lake ni jinsi gani wanadamu wanapaswa kuvaa. Kama utavuka mipaka ya aina ya uvaaji uliowekwa na Mungu, utahukumiwa naye. Hili halina ubishi.

Uvaaji usiozingatia maagizo ya Mungu ni hatari sana kwa kanisa. Ni kama kijinga cha moto ndani ya msitu mkubwa, ambacho kinaweza kuteketeza msitu wote, iwapo hakitazimwa mapema. Uvaaji wa aibu usipodhibitiwa, unaweza kuenea makanisani mwetu na kuyateketeza. Na ukweli ni kuwa hatari hii haipo mbali sana. Tayari imeshabisha hodi katika baadhi ya makanisa. Kwa makanisa mengine hatari hiyo imeshajikita kabisa na hali inatisha.


Chachu kidogo hulichachua donge lote
Biblia inatuonya katika 1Wakorintho 5:6 kwa kutuhoji iwapo hatujui kuwa ‘chachu kidogo hulichachua donge zima?’ Maneno haya yalizungumzwa na mtume Paulo baada ya wateule waliokuwa katika mji wa Korintho kujisahau mno mpaka zinaa ya kutisha ikaingia katikati yao. Yaani mpaka ikafikia hatua ya mshirika kumwoa mke wa baba yake mzazi.

Kanisa linapojisahau, matatizo kama haya yaliyojitokeza kati ya wateule waliokuwa Korintho yanaweza vile vile kujitokeza katika kanisa la leo. Ndio maana nikasema ipo haja ya kupambana na tatizo la mavazi yasiyofaa mapema kabla hali haijawa mbaya. Binafsi ninaamini hatujachelewa; bado hali inaweza kurekebishwa.

Nakumbuka tatizo la kuvaa mavazi yasiyo ya heshima lilianza kidogo kwa kuwahusisha washirika wachache tu, tena wakiwa wanavaa nguo ambazo hazikuwa mbaya sana. Lakini kidogo kidogo tatizo likakua kwa wavaaji wa aibu kuongezeka. Vile vile mavazi yenyewe yakaongezeka katika ubaya wake, yaani yakaongezeka katika ile hali ya kumwacha mvaaji uchi. Leo hii katika baadhi ya makanisa ya kilokole, ni jambo la kawaida kabisa kuwakuta wadada na wamama wakiwa wamevalia mavazi ya aibu yanayowaacha mapaja, matiti au migongo yao wazi kabisa.

Ninakumbuka miaka ya nyuma kidogo wakati mtindo wa vazi la mpasuo ulipoingia nchini mwetu. Mwanzoni wanawake wacha Mungu hawakuiga mtindo huu. Hata wahubiri na waimbaji wa nyimbo za Injili walionya sana juu ya mipasuo ya aibu. Lakini baada ya muda, wakaanza kujitokeza waumini wachache waliodiriki kupasua magauni au sketi zao. Tena walianza kwa kampasuo kadogo tu, ambako eti sio kakubwa sana na kwamba hakana neno.

Baada ya muda mfupi tu wavaaji wa mipasuo midogo wakaongezeka. Halafu punde tena, ukubwa wa mipasuo yenyewe ukaongezeka, sambamba na wavaaji wake. Leo hii ni jambo la kawaida kabisa kuwakuta mabinti pamoja na wamama wengi tu wakiwa wamevalia mipasuo ya aibu makanisani mwao; tena bila wasiwasi wowote. Yale yale ya chachu kidogo hulichachua donge zima.

Siku hizi uvaaji wa mipasuo ya aibu umezoeleka mno makanisani, kiasi ambacho nguo hizi zinaonekana kama vile ni vazi la kawaida kabisa lisilo na tatizo lolote. Ndio maana nikasema kuwa katika baadhi ya makanisa hali inatisha. Na ukweli ni kuwa hali hii imefikiwa kwa sababu tatizo halikudhibitiwa tangu mwanzo. Halikushughulikiwa kikamilifu pale lilipoanza kujitokeza. Kwa sasa tayari limeshajikita makanisani. Ndio maana watu wachache wanapojitokeza leo kukemea hali hii, wanaonekana kama wendawazimu. Wanaonekana kama waliopitwa na wakati au washamba wa kutupwa.

Dawa ya tatizo ni kulishughulikia kungali mapema. Ni kupambana nalo kabla halijakomaa na kuwa sugu. Sio kuliacha likue na kuzoeleka kama vile sio tatizo tena. Ndio maana Biblia inatuagiza kuwa, “Basi, jisafisheni mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu” (1Wakorintho 5:7). Kanisa linatakiwa lijisafishe. Lijirekebishe. Mavazi yote yasiyofaa yanatakiwa yaondoke katikati ya kusanyiko la watu wa Mungu. Read More......

MKRISTO NA MAVAZI: Dhambi ya Bath-sheba

Katika kuelimishana juu ya jambo hili la mavazi, nitatoa maelezo marefu kidogo. Lakini kimsingi nitatumia kisa kimoja maarufu sana kilicho ndani ya Biblia. Hiki kinamhusu mfalme Daudi na mwanamke mmoja aliyeitwa Bath-sheba. Na kwa mantiki ya lengo la makala haya, nimekipa kisa hicho kichwa cha habari kinachosema ‘Dhambi ya Bath-sheba’.

Kisa chote kinachohusu mkasa wa Daudi na mwanamama Bath-sheba kinapatikana katika 2Samweli sura ya 11 na ile ya 12. Hebu tujikumbushe maneno machache ya kisa hiki. Biblia inatuambia kuwa, “Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleleza, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; kisha akarudi nyumbani kwake” (2Samweli 11:2-4).

Hapa tunamwona mfalme wa Israeli akivutwa na uzuri wa sura na umbile la mwanamke aliyekuwa akioga. Mwanamke yule alikuwa uchi. Baada ya kumwona tu, Daudi aliwaka tamaa kiasi ambacho alishindwa kabisa kujizuia. Matokeo yake alimchukua yule mwanamama aliyeitwa Bath-sheba, ambaye pia alikuwa ni mke wa mwanajeshi mmoja aliyeitwa Uria, kisha akazini naye.

Watu wengi wanapoelezea kisa hiki huwa wanapenda sana kuonesha kosa au dhambi ya Daudi ya kuzini na mke wa mtu. Huwa hawaoni kabisa kosa la Bath-sheba. Yeye anaonekana kuwa hakuwa na hatia yoyote. Hata mimi kwa kiwango fulani sipingani na wazo kama hilo, kwamba kweli mfalme Daudi alitenda dhambi. Lakini hebu leo tutazame kwa sura nyingine kabisa mazingira ya kisa hiki, ambacho kilimsababisha mfalme na heshima zake zote, aanguke katika dhambi ya uzinzi.

Ni kweli kabisa kuwa mfalme Daudi alitenda dhambi, tena ya kukusudia. Hakujali utu wa mtu mwingine. Hakuonyesha ubinadamu, hata baada ya kuambiwa kuwa yule alikuwa ni mke wa mtu. Ni kweli kabisa alifanya ukatili wa hali ya juu wa kulala na huyo mwanamke na kisha baadaye akamwua mumewe. Hilo silikatai; maana hata Mungu mwenyewe aliuelezea ukatili huo kwa kutumia kinywa cha nabii Nathani. Vile vile alimpatiliza Daudi kwa kosa hilo (2Samweli 12:1-23).

Lakini papo hapo kuna kosa alilolifanya Bath-sheba, hata kama hakufanya kosa hilo kwa kukusudia, kama ilivyokuwa kwa mfalme Daudi. Ukweli ni kuwa, bila kukusudia wala kuwa na nia yoyote mbaya, Bath-sheba alijiacha uchi mbele ya mwanamume aliyeitwa Daudi. Huyu mwanamume alipomwona, alishindwa kabisa kujizuia. Matokeo yake akajikuta tayari ameshamtenda Mungu wake dhambi (2Samweli 12:13).

Ni vigumu sana kuliona kosa la Bath-sheba. Kama nilivyosema ni kwamba, mwanamke huyu, kwa mtizamo wa nje, hakuwa na nia yeyote mbaya. Hakuwa na mpango wa kujionyesha mbele ya Daudi, wala kumvuta kwa uzuri wa maumbile yake. Lakini bado kitendo chake cha kukaa uchi kilimwangusha mwanamume wa watu katika dhambi ya uzinzi, hata kama kosa hilo lilitendeka pasipo kukusudia (unintentional).

Laiti mwanamama yule angekuwa makini kidogo tu; laiti angechunguza mazingira yaliyokuwa yanamzunguka kabla hajavua nguo zake. Laiti angeinua macho yake na kuangalia juu, pengine angemwona mfalme Daudi na kwa sababu hiyo asingevua nguo. Kwa bahati mbaya hilo halikutokea kwa siku ile. Na hilo ndio kosa au dhambi ya Bath-sheba. Kutokuwa mwangalifu. Ndipo madhara yakatokea. Tena madhara makubwa mno.

 
Dhambi ya Bath-sheba ilileta madhara makubwa sana
Dhambi au kosa la Bath-sheba ni dogo sana ukilinganisha na lile la Daudi. Lakini pamoja na hayo, dhambi ile ilileta madhara makubwa sana. Ukiendelea kuchunguza kisa chote kwa makini utagundua kuwa licha ya kusababisha uzinzi, pia yapo madhara mengine yaliyojitokeza. Kulitokea mauaji ya mtu asiyekuwa na hatia (Uria). Jina la Bwana lilitukanwa kutokana na mpakwa mafuta wa Bwana (Daudi) kuanguka katika dhambi.

Baada ya uzinzi ule, mtoto haramu alizaliwa na vile vile akafa. Uasi ulitokea nyumbani mwa Daudi na kusababisha aibu kubwa ya Absalomu (mwana wa mfalme) kulala na wake za babaye, tena mbele ya kadamnasi ya Waisraeli. Kulitokea laana ya upanga kutoondoka katika nyumba ya Daudi, ubakaji, mauaji na kadhalika. Yaani amani ilitoweka kabisa nyumbani mwa mfalme Daudi.

Upo msemo wa Kiingereza unaosema, “Behold how great a matter, a little fire kindleth”. Yaani ‘tazama ni jinsi gani moto unaoonekana kuwa mdogo tu na usio na dhara lolote, unavyoweza kusababisha jambo kubwa bila kutarajiwa’. Waswahili wanasema ‘mdharau mwiba humchoma’.

Biblia kwa kuungana na huo msemo wa Kiingereza una haya ya kutuonya, “Angalieni, twatia lijamu katika farasi, ili wamtii, hivi twageuza mwili wao wote. Tena angalieni merikebu; ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, kokote anakoazimia kwenda nahodha. Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa” (Yakobo 3:3-5).

Lijamu (kipande cha chuma kinachopitishwa katikati ya midomo ya farasi ili kufungia hatamu au kamba za kumwongozea) ni kitu kidogo sana ukilinganisha na ukubwa wa farasi mwenyewe. Lakini ni kupita hiyo lijamu, ambapo mwili mzima wa farasi hugeuzwa. Usukani wa merikebu ni mdogo sana ukilinganisha na ukubwa wa merikebu yenyewe. Lakini ni usukani huo huo unaogeuza chombo kizima pamoja na ukubwa wake wote.

Yanayoelezwa hapa ndiyo yaliyotokea kumhusu Bath-sheba. Kosa dogo tu (tena lisilo la kukusudia) la kukaa uchi mbele ya mwanamume, lilisababisha madhara makubwa mno. Jambo lililoonekana kuwa ni la kawaida tu, bado jambo hilo likaleta madhara makubwa mno. Hata leo hii swala la mavazi yasiyofaa linaweza kuonekana ni jambo dogo tu. Lakini je, ni madhara kiasi gani yanayoletwa na wanawake wanaotembea nusu uchi barabarani?

Matatizo yaliyompata Daudi, familia yake na taifa la Israeli yasingetokea iwapo Bath-sheba angekuwa makini kidogo. Laiti angekuwa makini na mahali au muda wa kuoga, pengine Daudi asingemwona akiwa uchi. Laiti asingeogea nje mahali pa wazi au kama angeenda kuoga usiku badala ya mchana, ni saa ngapi Daudi angemwona katika hali ile hata amtamani? Lakini maskini, tahadhari haikuwepo. Bila kutegemea, kosa dogo tu la kutokuwa makini, likasababisha adha kubwa.


Makanisani tunao akina Bathisheba wengi
Kinachonisukuma kuandika makala haya ni kuwa, ndani ya makanisa yetu, tunao akina Bathi-sheba. Tena siku hizi ni wengi mno. Katikati ya jamii ya wakristo, wapo wanawake wanaokiri wokovu, lakini kwa kutokujua au kwa uzembe, wanajiacha nusu uchi. Wanavaa mavazi yanayoianika miili yao nje nje; na kwa sababu hiyo wanakuwa kwazo kwa washirika wenzao, hasa wanaume.

Sisemi kuwa hawa wanawake wote wanaovaa mavazi yasiyofaa wanafanya hivyo kwa makusudi. La hasha. Ninajua kuwa wengine wao ni wacha Mungu wazuri mno. Wengine ni wa kiroho vizuri kabisa na sio wazinifu hata kidogo, wala hawawi na nia yoyote mbaya wakati wanapovaa hizo nguo za aibu. Tatizo lao ni ile kutotambua madhara yanayoletwa na huo uvaaji wao.

Ukweli ni kwamba, makanisani mwetu tunao wanawake wapendwa ambao hawako makini na aina ya mavazi wanayovaa. Wapo wanaovaa nusu uchi; na kwa sababu hiyo tayari wamekuwa kwazo kwa wanaume wengi. Tayari wamekuwa ni sababisho la madhara kama yale yaliyoletwa na Bath-sheba kwa mfalme Daudi.

Ninachomaanisha ni kuwa wapo wanaume walioanguka katika uzinzi kwa sababu ya tamaa zao kuamshwa na hao wanawake wasiovaa mavazi ya heshima. Unaweza kuwa ni uzinzi wa macho au ule wa kufanya tendo lenyewe kabisa. Vyovyote vile iwavyo, uzinzi unakuwa umetokea. Hili nitaeleza kwa kirefu zaidi huko mbeleni.

Leo hii ukichunguza makanisa mengi utagundua kuwa uvaaji wa baadhi ya wanawake umevuka mipaka. Wanawake hawa wanavamia kila ‘fasheni’ au mitindo ya mavazi bila kujali kuwa baadhi ya mitindo hiyo ipo kinyume na maagizo ya Mungu. Kwa sababu hiyo basi, ipo haja ya kupambana na tatizo hili kabla halijakomaa na kulimeza kanisa la Bwana. Read More......

Monday, May 11, 2009

MKRISTO NA MAVAZI: Makanisa ya kimadhehebu yamepotoka

MAKANISA YA KIMADHEHEBU YAMEPOTOKA (Nyakati Toleo namba 302 la tarehe 17-23 Septemba 2006)

Hebu tuendelee na mada yetu. Msomaji mwingine anayeitwa Denis Nitu naye alieleza yafuatayo katika gazeti hilo hilo la Nyakati katika barua yake kwa mhariri iliyokuwa na kichwa cha habari kama ilivyo hapo juu.

Ndugu Mhariri
Napenda kumpongeza Mchungaji Moses Magembe wa T.A.G majumbasita Dar kwa kusimama imara na kukemea uchafu unaoendelea makanisani ukifanywa na watu wanaokiri kwamba wameokoka, lakini wakidumu kufanya mambo ya ulimwengu. Wanavaa vimini, nguo za kubana, wanapasua sketi, wanavaa suruali, wanakwangua nyusi zao na kujipaka rangi za kila aina machoni, midomoni, kwenye kucha za miguuni na mikononi, ili mradi wahakikishe kuwa hawajabaki nyuma kwenye mambo ya fashion na mitindo ya kidunia. BWANA akubariki sana mchungaji kwa kuona hilo na kulikemea……………..…(Mwisho wa kunukuu).

Mambo ya msingi yanayojitokeza
Katika barua hii tunajifunza mambo yafuatayo;
  • Wapo wakristo wanaokiri wokovu, lakini wanavaa mavazi ya aibu kama vile vimini, nguo za kubana, suruali, mipasuo, na kadhalika.
  • Kanisa la leo limepoteza mwelekeo na halifuati mafundisho ya mitume wa mwanzo.
  • Pamoja na matatizo ya kanisa, bado wapo wachungaji au viongozi walio na msimamo imara wa kulisimamia neno la Mungu kwa gharama yoyote ile.

NGUO ZINAZOBANA ZAWACHEFUA WALIOHUDHURIA MKUTANO WA INJILI (Nyakati Toleo na. 303 la Tarehe 24-30 Septemba 2006).

Mwandishi mmoja wa habari anayeitwa Zablon Mlimbila wa Moshi mkoani Kilimanjaro aliandika taarifa iliyokuwa na kichwa hicho hapo juu katika Gazeti la Nyakati.

Tabia chafu inayoonyeshwa na baadhi ya wasichana wanaoenda kwenye mikutano ya Injili ya kuvaa nguo zinazobana kiasi cha kuonyesha maungo yao ya ndani ilikuwa kero kubwa kwa watu waliohudhuria mkutano wa Injili uliofanyika mjini Moshi wa makanisa ya kipentekoste Kilimanjaro na kuhubiriwa na mhubiri wa Kimataifa Peter Pretorius kutoka Africa ya Kusini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya waliohudhuria mkutano huo walionyesha kukasirishwa mno na tabia hiyo. Mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Faraja alisema inabidi waandaaji wa mikutano kama hiyo wawe na watu maalum wa kuzuia wanaoenda mkutanoni na nguo za ajabu kwani zinapunguza uchaji wa ibada na mafundisho. Mtu mwingine ambaye alijitambulsha kwa jina la Mama Hawa alisema kitendo cha mabinti kuingia uwanjani na nguo za kubana ni aibu na haimpendezi MUNGU.
Katibu wa maandalizi ya mkutano huo Bw: Unity R. Msami alisema wao kama viongozi wamepokea kauli hiyo kama changamoto kwani na kwamba katika mikutano ijayo wataangalia suala hilo kwa umakini sana. Alisema kama ilivyo makanisani wataangalia pia uwezekano wa kuzuia watu kuhudhuria mikutanoni wakiwa wamevaa kofia, pamoja na kufunga simu…….(Mwisho wa kunukuu).

Mambo muhimu yanayojitokeza

Mambo muhimu yanayojitokeza katika barua hii ni haya yafuatayo;
  • Wapo watu wanaokerwa au wanaokwazwa na tabia ya uvaaji usiofaa.
  • Wapo wakristo waliojisahau mno mpaka wanaona ni jambo la kawaida kwenda kwenye mikutano ya Injili huku wakiwa wamevalia mavazi ya aibu.
  • Uvaaji usiofaa unapunguza uchaji wa Mungu na usikivu wa mafundisho au mahubiri.
  • Wakristo wengine hawana hofu ya Mungu kiasi ambacho, licha ya kuvaa mavazi yasiyofaa, vile vile hawavui kofia, hawazimi simu na kadhalika, wakati wanapoingia katika nyumba za ibada.

UVAAJI NGUO HUU UNADHALILISHA KINA DADA (Msemakweli Toleo Na. 473 la Tarehe 24-30 Septemba 2006)

Mawazo mengine niliyoweza kukusanya kuhusiana na uvaaji usiofaa yaliandikwa na Marietta Julius, Jovita Marko na Husna Rashid katika Gazeti la Msemakweli. Hawa ni wanafunzi wa shule moja iliyoko mjini Arusha, na walikuwa na haya ya kusema;

Mhariri,
Tunapenda kutoa shukrani zetu kwa Gazeti lako kwa kutoa nafasi kwa wasomaji wake kutoa maoni yao na hivyo kudumisha dhana ya uhuru wa kutoa mawazo. Sisi wanafunzi wa kidato cha kwanza mjini Arusha, ambao kwa uchungu mkubwa tunaandika barua hii tukitarajia viongozi wanaohusika watachukua hatua ya kukabiliana na Suala hili.
Suala kubwa ambalo tunataka kuzungumzia hapa ni juu ya dada zetu ambao wameamua kutembea wakiwa nusu uchi, bila ya wasiwasi, kwa kisingizio cha kwenda na wakati. Hivi sasa baadhi ya watu wanaona aibu kutembea na wazazi wao barabarani kwa kuhofia kukutana na wanawake hawa kwani utakapokutana nao hutaweza kumwangalia mzazi usoni. Ni aibu na fedheha kubwa.
Hawa kinadada wamekuwa wakivaa nguo laini sana zinazobana mwili, kiasi cha kuona maumbile ya ndani, nyingine zikiwa fupi mno ambapo mhusika mwenyewe hawezi hata kuinama. Lakini jambo moja linalotushangaza ni kwamba pamoja na ukweli kwamba hiki ni kipindi cha utandawazi, lakini hakuna kongozi hata mmoja anayekemea uvaaji huu. Wote wanaonekana kufurahia hali hii, ambayo inaharibu jamii yetu. Mfano baadhi ya kinadada wamewahi kumtembelea nyumbani kiongozi mmoja wa kitaifa, huku wakiwa wamevaa nguo ambazo kwa kweli hazistahili hata kidogo.
Ningeomba serikali itoe tamko la kupiga marufuku nguo za namna hii, kwani siyo tu kwamba zinatia aibu lakini zimekuwa chimbuko la kumomonyoka kwa maadili ya taifa letu. Aidha sambamba na nguo hizi, pia ningependa kuomba serikali ikemee majarida yanayohusiana na masuala ya ngono kwani kinachoonekana zaidi ni kwamba wenye majarida hayo wanajali zaidi fedha na biashara kuliko staha ya Watanzania. Tunaomba viongozi wetu waelewe sisi wanafunzi hatutaki haya mambo. Ni aibu kubwa kwa taifa letu na wengine wanasababishwa kubakwa kwa wingi na kujiletea madhara. (Mwisho wa kunukuu)
Mambo muhimu ya kujifunza
  • Hawa wanafunzi walioandika barua hii wanatufundisha mambo yafuatayo;
  • Wapo wakina dada wanaotembea nusu uchi kwa kisingizio cha kwenda na wakati.
  • Hakuna viongozi wa Serikali wanaoonekana kukemea tabia ya kuvaa mavazi yasiyofaa. Wengi wanaonekana kufurahia hali hii.
  • Uvaaji usifaa ni aibu sio kwa huyo mvaaji tu, bali hata kwa jamii inayomzunguka.
  • Nguo zisizofaa ni chimbuko na matokeo ya mmomonyoko wa maadili.
  • Sambamba na mavazi yasiyofaa, majarida ya ngono nayo ni tatizo lingine linaloikabili jamii ya Watanzania.
  • Mvaaji wa nguo za aibu anaweza kujiletea madhara kama vile kubakwa.

WATUMISHI WA MUNGU MNALIJUA HILI? (Nyakati Toleo Na. 315-Desemba 24-30, 2006)

Na mwisho kabisa yafuatayo ni mawazo ya ndugu Ibrahim Xavery kama yalivyotokea katika Gazeti la Nyakati.

Kwanza napenda kutoa shukrani kwa MUNGU kwa ajili ya Gazeti letu la Nyakati ambalo limekuwa mstari wa mbele kuutetea mwili wa Kristo, ambao ulikwisha jengwa na Kristo mwenyewe (Mathayo 16:18). Baada ya kulipongeza gazeti hili, niingie kwenye kiini chenyewe.
Ninajisikia furaha sana, tena sana, hasa ninapoona mwili wa Kristo ukiongezeka kwa ukubwa na kuimarika kiimani. Lakini kuna tatizo ambalo linatia dosari, kama siyo kuleta kichefuchefu ndani ya kanisa. Watumishi wa MUNGU wenye waumini wengi, hili limeingia kwenye mikusanyiko yenu. Nasema hivyo ni kwanini? Ni kwa sababu imekuwa ni desturi kwa wakristo wa sasa, ambao hawana hofu ya MUNGU, kuwa wanafanya vituko huko mitaani. Sisi ndio tunaowaona, utadhani hawajaokoka.
Ukimshuhudia kwa habari ya kuokoka anakwambia nimeokoka naabudu (utakuta anataja makanisa yenye waumini wengi) mimi nasali pale. Unauliza umeokoka? Anakujibu ndiyo! Unauliza, hivi MUNGU anapenda kuona wewe dada umevaa suruali na hivyo vitop ulivyovaa? Au je, utaweza kwenda kanisani umevaa hivyo?
Majibu yanakuwa siyo mazuri, siyo ya kuridhisha. Atakuambia MUNGU haangalii mavazi. Hivi ni kweli MUNGU wetu haangalii mavazi? Utaweza kwenda kanisani uchi, eti kwa kigezo kwamba MUNGU haangalii mavazi? Soma 1Petro 1:14-15, 3:2-3. Akina dada jirekebisheni; mnaongoza kuvaa ovyo makanisani…. (Mwisho wa kunukuu).

Mambo ya kujifunza
  • Katika barua hii tunajifunza mambo yafuatayo;
  • Wapo wakristo wanaokiri wokovu, lakini mitaani wanaonekana wakiwa wamevaa mavazi ya aibu.
  • Wanaovaa mavazi ya aibu wanajitetea kuwa Mungu hajishughulishi na mavazi bali anaangalia moyo tu.
  • Wakina dada wanaongoza kwa kuvaa ovyo makanisani mwao.
  • Watumishi au viongozi wa makanisa wanapaswa kukemea kwa nguvu zao zote tabia ya kuvaa mavazi yasiyofaa.
  • Makanisa makubwa yanaweza kuwa ni vichaka vizuri sana vya kuwaficha wanawake wanaovaa mavazi ya aibu.

Tatizo lipo
Ninaamini mpaka sasa msomaji wangu utakubaliana nami kuwa tatizo lipo. Mimi sijui wewe una msimamo upi, lakini ninachoweza kusema kwa yakini ni kuwa lipo tatizo katika aina ya uvaaji wetu sisi tunaojiita wateule wa Bwana. Wapo waliopitiliza mipaka; wanaokaidi maagizo ya Mungu yanayohusu jinsi anavyotutaka tuvae. Na hiki ndicho kinachonisukuma kuandika makala haya.

Kama nilivyotangulia kutoa tahadhari mwanzoni kabisa mwa makala haya, ni kwamba ninatambua wazi kuwa mjadala wa mavazi, hasa siku za leo, ni mgumu na mara nyingi huwa hauna mshindi. Watu wengi, ikiwa ni pamoja na wakristo waliookoka, wanataka uhuru usio na mipaka katika maswala mbalimbali yanayohusu maisha yao. Hii ni pamoja na swala la mavazi.

Kwa sababu hiyo mimi na wewe msomaji tunaweza tusikubaliane ni aina gani ya mavazi tuvae na yepi tusiyavae. Katika jambo hili la mavazi, wengine huwa wanafikia hatua ya kuwa na misimamo yao, hata kama misimamo hiyo ipo kinyume kabisa na maagizo ya Mungu. Anayejua ni nani aliye sahihi ni Mungu mwenyewe. Na hilo hata mimi namwachia Yeye.

Lakini pamoja na sisi wanadamu kutofautiana, kuna jambo moja ambalo binafsi nina uhakika nalo. Nalo ni kwamba, hata kama tuna uhuru wa kuvaa tutakavyo, bado Mungu ametuwekea mipaka. Hakutuacha tuvae vyovyote vile tupendavyo. Hapana. Hakukaa kimya kuhusu eneo la mavazi. Ukweli ni kwamba, ametoa maagizo ni kwa namna gani wanadamu wavae. Ndio kusema ametuwekea mipaka katika jambo hili.

Hiki ndicho ninachotaka kuwakumbusha wakristo wenzangu. Na kama nilivyosema katika utangulizi wa makala haya, ninaamini wapo watakaonielewa. Kama tayari walikuwa wamepitiliza mipaka katika uvaaji wao, bila shaka watajirekebisha. Watapona sio wao tu, bali pamoja na watu wengine ambao tayari walishaanza kuathirika kutokana na kukithiri kwa tabia ya kuvaa mavazi yasiyofaa. Read More......

MKRISTO NA MAVAZI: Eti Mungu anaangalia moyo tu?

JAMANI ETI MUNGU ANAANGALIA MOYO TU?

Hebu tuanze na sehemu ya barua ya msomaji anayeitwa Isope Mwakibasa iliyokuwa na kichwa cha habari kama ilivyo hapo juu, na ambayo iliyotokea katika Gazeti la Kikristo la Nyakati. Nanukuu kama ifuatavyo;
………………… Kuna mambo mengi sana ambayo yamekuwa yakihaririwa (kusahihishwa) sana kwenye Biblia na kuonekana kwamba wale walioandika ni watu wa zamani sana (wamepitwa na wakati) ambao mambo mengi waliyoyaandika yalifaa kwa kipindi kilichopita na sasa ni wakati wa Sayansi na Teknolojia. Walokole wengi wamekuwa wakisahihisha maneno ya MUNGU ili waweze kutimiza matakwa yao na wala si ya MUNGU.
Leo nitalitolea mfano jambo moja tu ambalo limekuwa ni tatizo kubwa sana kwa kanisa la leo. Jambo hili linatetewa sana na wakristo pamoja na makanisa na viongozi wa juu wa dini hii kwa kuwafundisha waumini wao ambao wako tayari kwenda Jehanamu na makundi yao kuliko kulikosa kwa kisingizio kuwa watachekwa na mataifa mengine, eti kwa kutokwenda na wakati.
Jambo lenyewe ni kuhusu mavazi ya kiume na ya kike. Mabinti, wamama na vijana wa kiume wa Kikristo (walokole) wa sasa ambao wanadai kuwa wako safarini kwenda mbinguni, leo hii kuvaa mavazi yasiyo ya jinsia yao ni jambo la kawaida. Ukisoma katika Kumbukumbu la Torati 22:5 neno la MUNGU linasema “Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanaume, wala mwanaume asivae mavazi yampasayo mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa BWANA, MUNGU wako”.
Sasa mimi nimekuwa nikijiuliza sana bila kupata majibu kuhusu hawa wamama. Je, andiko hili hawalioni? Na je, kama wanaliona, inakuwaje vijana wa kiume na mabinti wanavaa mavazi haya? Nimewahi kuwauliza baadhi ya mabinti na wamama kadhaa, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wajiitao kuwa ni watumishi wa MUNGU kuhusu uvaaji wa mavazi yasiyo yao, kama wamewahi kuliona andiko hilo ama la! Wengi wamekuwa wakiliona na kulisoma sana, ila ni ujeuri na kiburi cha uzima ndani ya mioyo yao. Majibu niliyokutana nayo hayamo kwenye Biblia bali ni historia na unafiki wa mtu ikiwa ni pamoja na ulimwengu unavyokwenda. Kati ya hao ambao nimekuwa nikizungumza nao kuhusu suala hilo wamekuwa wakijitetea kwa kusema kuwa, suruali si vazi la kiume bali ni la watu wote, Vilevile suruali ni vazi la heshima sana kwa mtu wa jinsia yoyote kuliko vazi lingine lolote kwa maana hata nikianguka sikai wazi.
Mwingine alijitetea kwa kueleza kuwa Taifa la Israeli, ambalo ni taifa la MUNGU, alisema kuwa askari wa Kiyahudi wa kiume wanavaa sketi na wale wa kike wanavaa kaptula. Sasa iweje kwa mataifa mengine iwe ni vibaya. Akasema huko si kumkosea MUNGU maana ameruhusu kwa taifa lake wavae kama mataifa mengine wavaavyo.
Wengine ukiwauliza kuhusu jambo hilo wanakuwa wakali na kusema kuwa mambo mengine yaliyoandikwa enzi zile si yote ya kutumika kwa nyakati hizi za sasa, bali yalikuwa ya wakati ule. Kwa sasa ni lazima wakristo tubadilike na kuenenda kama ulimwengu unavyokwenda na wala si kung’ang’ania mambo ya kishamba.
Jamani tangu lini mambo ya MUNGU yakaenda na wakati? Akina kaka nao hawako nyuma. Kukutana ama kuwaona vijana wa kiume wakiwa wamevaa hereni ama kusuka nywele nalo ni jambo la kawaida siku hizi. Wengine husema kuwa MUNGU anaangalia moyo haangalii mavazi ya mtu wala kitu kingine chochote. Jamani jamani! Kweli Mungu anaangalia moyo tu na wala si mwenendo au matendo ya mtu na mavazi kweli? MUNGU atusaidie sana katika hili. ……….(Mwisho wa kunukuu).

Mambo muhimu yanayojitokeza katika barua hii
Hebu tuangalie mambo muhimu yanayojitokeza katika barua hii. Nitajaribu kuyaandika kwa kifupi kama ifuatavyo;
  • Wapo wakristo waliookoka, lakini wanalihalifu neno la Mungu linaloweka mipaka kati ya mavazi ya kike na ya kiume.
  • Wapo wakristo waliotekwa na tamaa au nia ya kutaka kwenda na wakati katika mambo mengi, ikiwa ni pamoja na eneo la mavazi.
  • Wapo viongozi na waumini wanaotetea kwa nguvu zao zote uvaaji ulio kinyume na maagizo ya Mungu.
  • Kuna sababu za aina mbalimbali zinazowafanya wakristo wavae mavazi yaliyo kinyume na maagizo ya Mungu.
Read More......

MKRISTO NA MAVAZI: Mavazi yasiyofaa

Mwendelezo wa sehemu ya kwanza MKRISTO NA MAVAZI: Utangulizi

Sasa msomaji wangu ninachotaka kuzungumzia katika makala haya sio swala la uumbaji au dhambi ya Adamu na Hawa ya kumwasi Mungu. Hapana. Hicho sio kiini cha makala haya. Nia yangu hasa ni kuzungumzia tatizo la wanadamu wa leo la kukiuka maagizo ya Mungu kuhusiana na aina ya mavazi tunayopaswa kuvaa.

Nia yangu ni kuwakumbusha wakristo wenzangu kuwa, yapo mavazi yaliyoenea duniani kwa sasa, lakini mavazi hayo yapo kinyume kabisa na maagizo ya Mungu. Kwamba wanaoyavaa, wanaasi agizo la Muumba wao na wasipobadilika, watahukumiwa.

Kimsingi ninataka kulitahadharisha kanisa la Mungu au watu waliookoka kuwa baadhi yao wamejisahau mno katika eneo la mavazi. Kwamba wapo wakristo waliookoka, lakini hawazingatii maagizo ya Mungu yanayohusu mavazi wanayopaswa kuvaa. Kwamba yapo madhara makubwa sana kwa kanisa kwa sababu ya kutozingatia agizo la Mungu kuhusu mavazi. Hiki hasa ndio kiini cha makala haya.

Moja ya madhara au hasara ambazo mwamini anaweza kupata kwa sababu ya kutotii maagizo ya Mungu yanayohusu mavazi ni pamoja na kuukosa uzima wa milele. Ninaamini mpaka nitakapofika mwisho wa makala hii, wapo watakaoelimika na kama walishavuka mpaka kwa kuvaa mavazi yasiyostahili, watajirekebisha na kuanza kuvaa sawasawa na maelekezo ya Mungu. Kwahiyo msomaji wangu naomba tufuatane kwa makini.

Je, tatizo la mavazi yasiyofaa lipo?
Kabla sijaendelea sana, naona ipo haja ya kujiuliza na kutafakari kama kweli tatizo la mavazi yasiyofaa lipo miongoni mwa makundi ya wale tunaojiita walokole (au watakatifu wa Bwana au wateule au wapendwa na kadhalika (kama wanavyojulikana kwa majina mbalimbali). Ipo haja ya kufanya hivyo ili tusije tukajikuta tunazungumzia kitu ambacho hakipo kabisa.

Tutakapokubaliana kuwa ni kweli kuna tatizo katika aina ya mavazi yanayovaliwa na watu wa Mungu siku hizi, bila shaka itakuwa rahisi kubadilisha misimamo kwa wale walio radhi kufanya hivyo. Na kwa sababu hiyo wapo watakaoepukana na dhambi ya kuyaasi maagizo au mipaka iliyowekwa na Mungu wetu.

Kabla sijaendelea sana naomba nitoe tahadhari kungali mapema kwamba, ninafahamu fika kuwa ninazungumzia jambo ambalo ni tata na lenye ubishi mwingi. Ninatambua wazi kuwa huenda tusikubaliane kabisa katika eneo hili la mavazi yasiyofaa. Pamoja na kutambua hilo, binafsi siwezi kuendelea kukaa kimya.

Katika kizazi cha sasa, ambacho binafsi nimekibatiza kizazi cha ukaidi, hilo la kutokubaliana haliepukiki. Na wakaidi ninaozungumzia hapa ni pamoja na watu wa Mungu au walokole. Hawa nao ni wabishi, wee acha tu. Wakati mwingine ni wabishi hata kuliko watu ambao hawamjui Mungu kabisa. Pamoja na hayo, nitasema yale yaliyo moyoni mwangu, halafu uamuzi wa mwisho ninakuachia wewe msomaji wangu.

Ili kujua kama tatizo la mavazi lipo au la, hebu tuangalie watu wengine wanasema nini kuhusu jambo hili. Tutafanya hivyo kwa kuangalia, pamoja na mambo mengine, taarifa au habari nilizozinikuu kutoka katika magazeti mbalimbali ya Kikristo yaliyopo hapa nchini. Ninakusihi msomaji wangu usome na kutafakari kwa makini taarifa hizi. Jitahidi kuelewa na kuona kama kuna kitu unachoweza kujifunza. Read More......

MKRISTO NA MAVAZI: Utangulizi

DHAMBI YA BATH-SHEBA: JE, MUNGU ANAJALI JINSI NINAVYOVAA?

Utangulizi
Mtu yeyote akichunguza Biblia kwa makini atagundua kuwa Mungu wetu ni wa utaratibu. Atagundua kuwa Mungu hafanyi mambo au mapenzi yake kienyeji tu. Hapana. Hafanyi jambo kwa kubahatisha. La hasha. Atagundua kuwa Mungu huwa anafuata utaratibu fulani aliojiwekea yeye mwenyewe.

Kwa mfano, tunapoangalia jinsi alivyoumba dunia na vyote viijazavyo, tunaona kuwa alifanya hivyo hatua kwa hatua. Alifuata utaratibu wa ni jambo lipi lifanyike siku ya kwanza na ni lipi lifanyike siku ya sita au siku ya mwisho. Hakuwa tu anaumba ali mradi vitu viwepo. Hapana hata kidogo.

Unapozidi kuichunguza Biblia utagundua kuwa Mungu amempa mwanadamu uhuru wa kumtosha kwa ajili ya kuendesha maisha yake hapa duniani. Lakini pamoja na kumpa uhuru wa kutosha, vile vile amemwekea mipaka fulani fulani ambayo hapaswi kuivuka. Kuna mambo ambayo amemkataza asiyafanye.

Mungu hakutuacha tujiendee tu kama tunavyotaka. La hasha. Hakutuacha tuogelee tu bila kizuizi chochote. Hii imekuwa ni tabia ya Mungu tangu alipoumba dunia na viumbe vyote viijazavo, ikiwa ni pamoja na wanadamu. Hakumpa mwanadamu uhuru wa kujifanyia mambo yake au kujiendea vyovyote vile anavyotaka bila mipaka yoyote.

Sio tu kwamba Mungu amemwekea mwanadamu mipaka, bali vile vile amemwagiza mambo fulani fulani. Yapo mambo ambayo Mungu ametuagiza sisi wanadamu tuyafanye na mengine ametukataza tusiyafanye. Yale mambo aliyotuagiza tufanye ni kwa ajili ya makusudi yake na wakati wote yanakuwa na faida kwetu sisi tunaoyafanya.

Mara nyingi yale aliyotukataza ni kwa ajili ya manufaa yetu. Mungu anajua kuwa yapo mambo ambayo tukiyafanya tutadhurika au tutapata hasara. Tutajikuta mahali pabaya. Kwahiyo anapotukataza anakuwa na lengo zuri la kutuepusha na matatizo, japo kwa akili zetu za kibinaadamu tunaweza tusitambue hayo makusudi mazuri ya Muumba wetu. Na wakati mwingine huwa haelezi bayana ni kwanini anatukataza jambo fulani.

Tunapoangalia kitabu cha Mwanzo 2:16 tunaona kuwa Mungu alipomwumba Adamu na kisha kumweka katika bustani ya Eden, alimpa uhuru wa kula matunda yote yaliyokuwa ndani ya ile bustani, isipokuwa matunda yaliyotokana na mti wa ufahamu wa mambo mazuri na mambo mabaya. Biblia inatuambia kuwa, “Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akisema, matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika”.

Katazo la kutokula matunda yaliyokuwa katika mti wa ujuzi wa mambo mema na mabaya ni mojawapo wa aina ya mipaka ninayozungumzia. Kwamba Adamu alikuwa na uhuru wa kumtosha kabisa wa kula matunda ya miti mingine yote iliyokuwa bustanini, isipokuwa matunda ya huo mti mmoja tu. Mungu alijua kwamba kutakuwa na madhara iwapo Adamu atakula matunda ya mti wa ujuzi wa mambo mema na mabaya. Ndio maana alimkataza asiyale.

Kwa bahati mbaya Adamu alishindwa kutii agizo la Muumba wake. Yeye alivuka mpaka aliokuwa amewekewa kwa kile kitendo chake cha kula matunda aliyokuwa amekatazwa. Hakujua ni madhara gani yatakayotokea iwapo atakula hayo matunda. Na kama sote tunavyojua ni kwamba, matokeo ya Adamu kushindwa kutii agizo la Mungu ni dhambi kuingia ulimwenguni.

Sina haja ya kuelezea madhara ya dhambi humu duniani, kwani naamini wengi wetu tunayafahamu. Lakini kwa kifupi tu ni kuwa madhara hayo ni laana kwa wanadamu, ardhi na viumbe alivyoumba Mwenyezi Mungu (Mwanzo 3:14-19). Ndio hizi taabu na mahangaiko tuliyo nayo ulimwenguni kwa sasa. Ni pamoja na mauti inayowapata wanadamu, jambo ambalo halikuwa limekusudiwa na Mungu wakati wa uumbaji wake. Hakika uasi wa Adamu uliiletea dunia hasara kubwa.

Hata sasa uasi wa mwanadamu unaendelea kuifanya dunia isiwe mahali salama pa kuishi. Wanadamu bado hawajaacha tabia ya kuyaasi maneno au maelekezo ya Mungu. Uasi umeendelea kudumu tangu mwanzo wa ulimwengu huu hadi sasa. Kwa bahati mbaya anayepata hasara kadri uasi unavyoendelea kudumu ni mwanadamu na wala sio Mungu.

Kama nilivyosema ni kuwa Mungu ni wa utaratibu. Kila agizo lake lina sababu zake. Sisi kama wanadamu tunaweza tusielewe ni kwanini anatuagiza jambo fulani. Lakini ukweli ni kuwa kila nyuma ya agizo litokalo kwa Mungu, ipo sababu ya msingi kabisa iliyomfanya atoe agizo hilo. Usipotii agizo lake, utajikuta matatani. Wewe ndiye utakayepata hasara. Read More......

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).