Friday, June 5, 2009

Ni vitu gani sisi wanadamu tunavyoweza kurithishana?

Baada ya kufahamishana maana ya urithi, hebu sasa tuangalie vitu ambavyo mtu anaweza kurithi au kumrithisha mtu mwingine. Katika jamii nyingi za Kiafrika, ambazo watu wengi huishi vijijini, mtu anaweza kumiliki na baadaye kurithisha vitu kama ardhi au mashamba, mifugo na pengine nyumba.

Kutokana na maendeleo pamoja na utajiri uliopo duniani siku hizi, sasa watu wanaweza kurithi au kurithisha vitu kama majumba makubwa ya kisasa, maduka na makampuni makubwa ya biashara, viwanja vilivyopimwa mijini, vito vya thamani kama dhahabu, akaunti zenye mamilioni ya fedha, na kadhalika.

Unaweza kurithi madeni au madai
Sio lazima mtu arithi mali peke yake. Hapana. Wakati mwingine hutokea kwamba wakati wa uhai wa marehemu, unakuta alikuwa na madeni au alikopesha watu vitu au fedha. Ndio kusema anaweza kufariki akiwa anadaiwa au anadai. Baada ya kifo chake, ni lazima madeni au madai yote yarithiwe, kwa maana ya kuyalipa au kulipwa.

Biblia inao mfano mzuri sana unaoonyesha ulazima wa kulipa deni la marehemu.Tunaposoma katika kitabu cha 2Wafalme 4:1 tunakutana na kisa kifuatacho; “Basi mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, ‘Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha BWANA; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa”.

Katika kisa hiki tunaona kuwa mtu mmoja aliyekuwa mcha Mungu alifariki na kuacha madeni. Leo hii tungeweza kusema kuwa mlokole fulani amefariki akiwa anadaiwa. Sasa yule mdai hakusema kwamba, ‘kwa kuwa marehemu amekufa, basi huo ndio mwisho wa deni langu’. Hapana. Aliendelea kudai kilicho chake. Alienda kwa mke wa marehemu, akataka kuchukua watoto walioachwa ili wakawe watumwa wake.

Ni wajibu kulipa madeni
Elisha alipoletewa kisa cha deni, hakuwa na jinsi ya kukwepa wajibu wa kulipa. Alijua ni lazima deni lilipwe. Alichofanya ni kutafuta namna ya kupata fedha za kulipa, na sio kujikausha. Kwa njia ya muujiza, mafuta yalipatikana. Baada ya kupatikana, Biblia inatuambia kuwa Elisha alimwambia yule mjane hivi, “Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako” (2Wafalme 4:7).

Naomba nisisitize kwamba madeni ya marehemu ni lazima yalipwe. Hiki hata Mungu anakifahamu. Ndio maana aliruhusu muujiza wa kupata mafuta utendeke. Alitaka fedha ya kulipa deni ipatikane. Kama wewe umeokoka na una tabia ya kukopa ovyo ovyo, kumbuka kuwa utakapoondoka duniani kabla ya kulipa madeni yako yote, utaiachia familia yako huo mzigo. Labda mdai asamehe hilo deni.

Unaweza kurithi mke na watoto wa marehemu
Kama marehemu alikuwa ameoa, anaweza kuacha mke na watoto. Hawa nao wanatakiwa warithiwe, kwa maana ya kuwatunza na kuwalea, hasa kama ni watoto wadogo. Hapa naomba nitoe angalizo. Sina maana ya kumrithi mke wa marehemu kwa kumwoa. Hapana. Nina maana ya kumsaidia kwa mfano kumiliki na kutunza mali za marehemu mumewe au kumtunza, kama atakuwa hajiwezi.

Ninasema hivyo kwa sababu ninatambua kuwa hapa nchini kuna makabila ambayo yana tabia ya kurithi mke wa marehemu. Hata katika Agano la Kale jambo hili lilikuwa linaruhusiwa, iwapo marehemu alikuwa ni mume aliyekufa kabla hajazaa mwana wa kiume.

Tunasoma hivi, “Watakapoketi pamoja mtu na nduguye, mmojawapo akafa, wala hana mwana wa kiume, mke wa yule aliyekufa asiolewe nje na mgeni; nduguye yule mumewe amwingilie amweke kwake awe mkewe, kumfanyia yampasayo nduguye mumewe” (Kumbukumbu la Torati 25:5). Haya ndiyo mazingira ambayo mke angeweza kurithiwa.

Agano Jipya haliruhusu kurithi mke

Ninatambua kuna wakristo ambao hutumia maandiko ya Biblia vibaya, na wanaweza kunukuu andiko kama hili kuhalalisha kitendo cha wao kumwoa mke wa marehemu ndugu yao. Lakini ukweli ni kuwa tabia ya kurithi mke imefutwa kabisa wakati huu wa Agano Jipya. Tunaambiwa katika 1Wakorintho kwamba, “Mwanamke hufungwa maadamu mumewe yu hai, lakini ikiwa mumewe amefariki, yu huru kuolewa na mtu yeyote amtakaye; katika Bwana tu”.

Hapa ina maana kuwa mwanamke akifiwa na mumewe, ana uhuru wa kuolewa na mtu mwingine yeyote yule. Kama ameokoka ni lazima aolewe na mwanamume aliyeokoka. Sio anarithiwa na ndugu wa mumewe (shemeji yake), kama baadhi ya makabila wanavyofanya hapa nchini. Kibiblia hiyo hairuhusiwi.

Unaweza kurithi matatizo
Wakati mwingine hutokea kwamba marehemu ameacha mlolongo wa matatizo, aidha ya kifamilia, au kijamii, au ya kikazi, na kadhalika. Matatizo nayo hurithiwa, kwa maana ya kuyatatua kama ambavyo marehemu angefanya, iwapo angekuwa bado yu hai. Sio kuyaacha yakielea hewani.

Mfano mzuri wa kurithi matatizo ni pale Rais au kiongozi fulani anapoondoka madarakani, aidha kwa njia ya kifo au anapofikia mwisho wa muhula wake wa uongozi. Kama ameacha matatizo, yule atakayechukua nafasi yake atalazimika kuyashughulikia. Hapo tunasema fulani amerithi matatizo ya uongozi.

Katika hali ambayo haifurahishi sana, kuna watu wengine ambao hurithi uchawi. Unakuta baba yake, au mama yake, alikuwa mchawi. Huyo mzazi anapofariki, anaweza kumrithisha mwanawe huo uchawi. Tena wakati mwingine jambo hili hufanyika wakati wa uhai wa marehemu. Mambo kama haya hutokea katika baadhi ya watu na jamii tunayoishi hapa Tanzania.

Unaweza kurithi sura na tabia za wazazi wako
Kuna wakati ambapo mtu anaweza kurithi sura au tabia au maumbile ya wazazi wake. Unakuta mtoto anafanana na baba yake au mama yake. Wakati mwingine mtoto anarithi tabia ambazo wazazi wake wanazo au walikuwa nazo kama vile hasira, chuki, uchoyo, ukarimu, upole, na kadhalika. Wengine huchukua urefu, ufupi, unene, au wembamba wa wazazi wao. Huku nako ni kurithi.

Tunapoiangalia Biblia tunaona kuwa hii hali ya watoto kurithi sura, tabia au maumbile ya wazazi wao imekuwepo tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Mungu alipomwumba mwanadamu, alimfanya kwa mfano wake na kwa sura yake (Mwanzo 1:26).

Baada ya kutenda dhambi, Adamu alimzaa mtoto wa kufanana naye kwa sura na kwa tabia. Tunaambiwa kuwa, “Adamu akaishi miaka mia na thelathini, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi” (Mwa. 5:3).

Baada ya anguko mambo yalibadilika

Tunaweza kuona kuwa Sethi alikuwa anafanana na baba yake, yaani Adamu. Kufanana huku ni kwa sura ya nje, pamoja na ile hali ya ndani ya kutenda dhambi. Ikumbukwe kuwa Mungu alipomwumba Adamu, alimkusudia awe mkamilifu, asiyejua wala asiyetenda dhambi. Baada ya anguko, ndipo dhambi ilipoingia ndani yake.

Kwahiyo Adamu alipozaa wana, hawakuwa watakatifu tena kama yeye alivyokuwa kabla hajaangakuka katika dhambi ya kuasi agizo la Mungu. Hapana. Walizaliwa katika hali ya kutenda dhambi. Na hali hii waliipata wapi? Waliirithi kutoka kwa baba yao Adamu, na sio kwa Mungu.

Ndio maana mpaka leo wazazi wanazaa wototo ambao tayari wana tabia ya kutenda dhambi tangu utotoni. Watoto wanapozaliwa tayari wana hasira, chuki, uchoyo, wivu na kadhalika.

Watoto au hata watu wazima hugombana na kupigana. Tabia hizi hawakuzipata kutoka kwa Mungu. La hasha. Wamezirithi kutoka kwa wazazi wao waliowazaa. Katika sehemu ya pili ya makala haya nitaonyesha kuwa mtu anaweza kufanana au kurithi tabia za Mungu.

0 maoni:

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).