Friday, June 5, 2009
Urithi ni nini?
Kabla hatujaendelea sana, nafikiri ipo haja ya kufahamishana maana ya urithi. Ninaamini tafsiri sahihi ya neno hili ni muhimu katika hatua hii ya mwanzo. Tukifahamu maana ya jambo hili mapema, huko mbeleni hakutakuwa na mkanganyiko katika kile ninacholenga kuzungumzia.
Kamusi ya Kiingereza inaeleza kuwa ‘to inherit is to receive property as a result of the death of the previous owner’. Kutokana na tafsiri hii, kwa Kiswahili tunaweza kusema kwamba, kurithi ni kupokea mali baada ya kifo cha mmiliki wa mali hiyo.
Baadaye tafsiri hii itabadilika kidogo kwani mtu anaweza kurithi hata mmiliki wa mali hiyo akingali hai. Vile vile sio lazima mtu arithi au arithishe mali (property). Wakati mwingine kunaweza kukawa hakuna kitu au mali ya kurithisha. Mfano mzuri katika Biblia ni Isaka, ambaye alimrithisha Yakobo maneno baraka, badala ya mali (Mwanzo 27:18-29).
Urithi unahusisha kifo pamoja na uhusiano kati ya mrithi na mrithishaji
Kamusi ya Kiswahili Sanifu inaeleza kuwa, kurithi ni kumiliki mali au kitu cha mtu aliyekufa na ambaye ana uhusiano wa uzawa au ndoa na mrithi. Inaendelea kueleza kwamba, urithi ni mali au vitu vinavyoachwa na marehemu na kupewa mtu fulani, aghalabu wa ukoo.
Tafsiri ya Kiswahili, kama ilivyo ya Kiingereza, nayo inahusisha urithi na kifo; kwamba ni lazima mmiliki wa mali hiyo afe, ndipo tendo la kurithi lifanyike. Vile vile inaonyesha kwamba, mrithi ni lazima awe na uhusiano wa kuzaliwa au wa ndoa na marehemu.
Swala la uhusiano ni muhimu sana katika hatua hii ya mwanzo, kwani huko mbeleni tutaona kwamba, mmiliki wa mali hawezi kurithisha mtu asiye na uhusiano naye, labda katika mazingira maalumu. Kwahiyo kimsingi wapo watu ambao jamii na sheria za nchi zinawatambua kuwa ndio wanaostahili kurithi. Baadaye nitafafanua jambo hili.
Mmiliki wa awali wa mali anaweza kuwa ni ndugu kama vile baba, au mama, au mjomba, au shangazi, au kaka, au dada. Kuna wakati babu naye anaweza kuwa na mali, halafu akawarithisha hadi wajukuu zake. Jambo hili ni la kibiblia kabisa kwani katika Mithali 13:22(a) tunaambiwa kuwa, “Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi”.
1 maoni:
Mm ni kijana mwenye umri 17.nakumbuka kuna siku nilifanya kosa mzazi wangu akanitamkia tukiwa kwenye gari letu pamoja na watu wengine kwamba sitakupa urithi.............sasa mm hapo nilibaki njia panda si kuelewa chochote ndio maana naomba ww unisaidie kwa mawazo hapo............
Post a Comment
Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.