Friday, June 5, 2009

URITHI: Nani anastahili kurithi?

Baada ya kifo, jambo au swali ambalo hujitokeza mara moja ni je, nani hasa anastahili kurithi mali ya marehemu? Swala la haki ya kurithi lisiposhughulikiwa vizuri na mapema, linaweza kuleta mafarakano kati ya ndugu, familia, marafiki na jamii kwa ujumla. Vipo visa vya watu waliouwa, au waliogombana, na wengine mpaka sasa hawaongei kutokana na kutoelewana wakati wa kugawana mali ya urithi.

Pamoja na mambo mengine, nia ya makala haya ni kufafanua haki ya urithi na kueleza nini kinatakiwa kifanyike, pindi marehemu anapofariki. Na kwa jinsi hiyo matatizo mbalimbali yanaweza kuepukwa. Kwahiyo msomaji naomba tufuatane kwa makini. Vinginevyo nawe unaweza kujikuta unakumbwa na mtafaruku wakati wa kurithi. Au kama yalishakukumba, ujue namna ya kujinasua.
Warithi ni wengi

Ukweli ni kuwa wapo watu wengi ambao wanaweza kuwa warithi wa mali ya marehemu. Katika kujibu swali la nani anastahili kurithi, nimewagawa watu hao katika makundi yafuatayo;

  1. Mke wa ndoa wa marehemu au mjane.
  2. Watoto wa ndoa wa marehemu au yatima
  3. Watoto wa kambo.
  4. Watoto kupanga (Adopted Children).
  5. Watoto wa kufikia.
  6. Watu wasiokuwa ndugu wa marehemu.
  7. Sasa hebu tuanze kuchambua kila kundi.
Mjane au mke wa ndoa wa marehemu
Kabla sijaanza kuwachambua wajane, naomba nitoe ufafanuzi. Ninapozungumzia mjane nina maana mke wa ndoa aliyeachwa na marehemu mumewe. Ninasema hivyo kwa sababu katika kizazi cha leo, kuna wanaume wanaokuwa na ‘vimada’. Wengine mnaziita ‘nyumba ndogo’.

Huyo mwanamume anapofariki, kuna baadhi ya hao wanawake wa nje ambao hujitokeza na kudai haki ya kurithi, sambamba na mke halali wa ndoa. Yaani kimada anajihesabu kuwa yeye naye ni mke wa marehemu, na kwamba anastahili kurithi sehemu ya mali iliyoachwa.

Hapa nataka niseme kungali mapema kwamba sheria za nchi yetu hazimtambui mke wa nje au mwanamke yeyote asiyekuwa na ndoa rasmi na marehemu. Wala Biblia nayo haiwatambui wala haisemi kwamba wana haki ya kurithi. Ninaamini hata mila na desturi za makabila yetu haziruhusu mke wa nje arithi mali ya mwanaume aliyezaa naye.

Sikiliza wewe dada au mama unayesoma makala haya. Kama unaishi kimada na mume wa mtu, tangu sasa ujue kwamba huna haki ya kurithi mali za huyo baba. Jambo hili nitalifafanua zaidi huko mbeleni, wakati nitakapokuwa ninazungumzia sheria za mirathi zinazotumika hapa nchini Tanzania.
Hakikisha una cheti cha ndoa

Jambo lingine ambalo naona ni bora nilizungumzie hapa ni ujinga au uzembe unaofanywa na baadhi ya wanawake. Tena wanaofanya makosa kama haya ni pamoja na walokole au watu wa Mungu. Yaani unakuta dada au mama fulani anaishi na mwanamume, lakini hana ndoa rasmi naye. Yeye anajihesabu kuwa ni mke, lakini hana cheti cha ndoa.

Nisikilize dada au mama. Kama huna cheti cha ndoa na huyo mwanamume unayeishi naye, mbele ya sheria itakuwia vigumu sana kuthibitisha kwamba wewe ni mkewe, na kwamba unastahili kurithi mali yake. Hata kama utakuwa umezaa naye watoto wengi kiasi gani, bado mbele ya sheria au mahakama, itakubidi uonyeshe cheti cha ndoa. Hapo ndipo wanawake wengi wanapokwamia na kupoteza haki yao ya kurithi, ijapokuwa walikuwa wanaishi na marehemu kama mume na mke.

Ushauri wangu ni huu. Hakikisha kuwa una ndoa rasmi na huyo mwanamume unayeishi naye. Kama mlianza kuishi kabla ya kufunga ndoa, nendeni kwa Mkuu wa Wilaya. Kama mmeokoka nendeni kanisani. Huko mtahalalisha ndoa yenu, na vilevile mtapewa cheti cha ndoa.

Hicho cheti ndio uthibitisho unaotambuliwa mbele ya sheria kwamba wewe ni mke wa marehemu na kwamba unastahili kurithi sehemu ya mali yake. Vinginevyo utalia kilio cha mbwa huyo baba atakapofariki. Unaweza usiambulie au usirithi chochote.

Matatizo ya wajane
Sasa hebu tuangalie haki ya mjane ya kurithi mali ya marehemu mumewe. Nianze kwa kusema kuwa, wapo akina mama wengi sana wanaopata taabu baada ya waume zao kufariki. Nafikiri msomaji wangu kama ningekuwa na uwezo wa kukuuliza, hutakosa kuwa na kisa unachokifahamu cha mjane aliyedhulumiwa mali aliyochuma na marehemu mumewe.

Katika baadhi ya makabila hapa nchini, mwanamke haruhusiwi kurithi chochote kilichoachwa na marehemu mumewe. Wengine hufukuzwa mara tu waume zao wanapofariki. Na wengine hurithi kupitia watoto waliowazaa na marehemu. Hiyo ndiyo hali halisi ya jamii yetu; jamii ambayo haki ni kitu adimu sana, na hata ikipatikana, inakuwa imepinda (Habakuki 1:2-4, 12-14).

Tunapoigeukia Biblia tunakuta nayo inazungumzia matatizo ya wajane. Wakati ninaandaa makala haya nilijaribu kupitia maandiko yanayozungumzia wajane. Kusema kweli nilishangaa kugundua jinsi ambavyo kuanzia wakati wa Agano la Kale hadi kipindi hiki cha Agano Jipya, Biblia ilivyosheheni maandiko tele yanayozungumzia matatizo ya wajane na namna ya kukaa nao vizuri. Hebu tuangalie maandiko machache.

Yatupasayo kuwafanyia wajane

Katika kitabu cha Kutoka 22:22 hatutakiwi kuwatesa wajane. Katika Kumb.16:11,14 tunatakiwa tuwapende na kuwalisha. Katika Kumb. 24:19-21 tunaambiwa kwamba tunapovuna mazao shambani, tusimalize kila kitu, bali tubakize sehemu kwa ajili ya wajane na yatima. Katika Kumb.24:17 na Ayubu 24:3 hatutakiwi kuchukua mali za wajane kama rehani. Katika Isaya 1:17, Yeremia 7:6, 22:3, Ezekieli 22:7 na Zekaria 7:10 hatutakiwi kuwaonea au kuwadhulumu wajane kwa namna yoyote ile.

Tunapokuja katika Agano Jipya tunaona kuwa bado Mungu anaendelea kutuhimiza tukae vizuri na wajane. Tunatakiwa tuwaheshimu (1Timotheo 5:3), tuwasaidie (1Timotheo 5:16), tuwatembelee (Yakobo 1:27) na kadhalika.

Swali la kujiuliza ni je, tunawatendea wajane kama ambavyo Biblia inatuagiza? Je, tuna mkakati wowote wa kuhakikisha kuwa hawateseki kwa upweke, kwa njaa, kwa huzuni, kwa manyanyaso, na kadhalika? Je, makanisani mwetu tunayo mikakati ya kuwasaidia wajane katika dhiki zao? Jibu unalo wewe msomaji.

Je, wajane wanatambua haki zao?

Kwa kuwa lengo la sehemu hii ya makala ni kuzungumzia haki ya mjane ya kurithi mali ya marehemu mumewe, hebu sasa tuyaache hayo mengine, turudi kwenye kiini cha mada yetu. Swali tunalotaka kujibu ni je, mjane ana haki gani ya kurithi hapa nchini Tanzania? Je, sheria inasema nini kuhusu jambo hili? Kabla hatujafanya hivyo, hebu tuangalie kisa kimoja kilicho ndani ya Biblia.

Katika kuhubiri kwake, kuna siku Bwana Yesu alitoa mfano ufuatao kwa kusema, “Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, ‘Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima” (Luka 18:2-5).

Mfano huu unatabainisha mambo yafuatayo;
Katika enzi za Bwana Yesu kulikuwa na makadhi au mahakimu.
Kama kulikuwa na hakimu, ina maana kulikuwa na mahakama pamoja na sheria zinazotawala maswala ya urithi.
Kazi ya hakimu ilikuwa ni kuhakikisha kwamba sheria hizo zinafuatwa na haki inatolewa. Ndio maana yule mjane alienda mahakamani.
Mahakimu walikuwa na tabia ya kukalia hukumu au kuchelewesha haki, kama ilivyotokea kwa yule mjane.

Zipo sheria zinazowalinda na kuwatetea wajane
Sikiliza msomaji. Kama ambavyo wakati wa Bwana Yesu kulikuwa na sheria zinazosimamia maswala ya urithi, mahakama na mahakimu wa kutekeleza hizo sheria, hata hapa Tanzania zipo sheria za namna hiyo. Hizi ndizo tutaziangalia katika makala haya, ili uzifahamu na pia ujue namna ya kuzitumia pale inapobidi.

Hebu turudi tena katika ule mfano uliosimuliwa na Bwana Yesu. Tunaona kwamba yule mjane alienda mahakamani kudai haki yake. Alienda mahakamani kwa sababu alijua nini anachopaswa kupewa katika mali za marehemu mumewe. Japokuwa alikuwa amedhulumiwa na adui yake, lakini alijua mahali pa kupeleka kilio chake. Hicho ndicho kilichomfikisha mahakamani.
Tambua haki zako

Katika kisa hiki cha mjane, tunaweza kuona kuwa swala la wajibu linajitokeza. Kwamba huyu mjane alikuwa na wajibu wa kujua haki yake. Baada ya kuijua, vile vile alipaswa kuifuatilia kule inapotolewa. Tena afanye hivyo bila kuchoka au kukata tamaa. Ndio maana daima alikuwa akienda au akishinda mahakamani. Yaani mpaka yule hakimu akamchoka; akaona ni bora tu ampe haki yake ili mambo yaishe.

Sasa hebu niulize swali. Je, ni wajane wangapi hapa nchini wanaotambua haki zao za kurithi? Je, ni wajane wangapi wanaojua sheria zinazotawala maswala ya urithi? Je, ni wangapi wanaojua mahali na namna ya kufuatilia hizo haki?

Ingawa sijawahi kufanya utafiki, lakini nina imani kuwa wapo wajane wengi sana wanaoteseka kwa kutojua wafanye nini kuhusiana na haki zao za kurithi mali za marehemu waume zao. Wengine wamedhulumiwa haki hizo na hawajui waende wapi. Wengine wamekufa na haki zao zimepotea kabisa.
Watoto wa marehemu

Kundi jingine la watu ambao wana haki ya kurithi ni watoto wa marehemu au yatima. Kamusi ya kiswahili sanifu inaeleza kuwa yatima ni mtoto aliyefiwa na wazazi wake wote wawili, au mmoja wapo wa wazazi hao. Yatima anaweza kuwa mtoto wa kike au wa kiume.

Kama ambavyo Biblia imezungumzia kwa kirefu maswala ya wajane, vile vile imezungumzia habari za yatima. Ukichunguza maandiko mengi yanayotaja habari za wajane, utakuta yatima nao wameunganishwa papo hapo. Utaona kuwa wajane, yatima, wageni (au wakimbizi) na maskini wametajwa kwa pamoja au tuseme wapo katika kundi moja.

Yatima nao wanapaswa kujua haki zao za kurithi, na vile vile kuwajibika katika kuzifuatilia. Vinginevyo haki hizo zinaweza kupotea au kudhulumiwa. Hapa napo yatupasa tujiulize, hivi haki za yatima ni zipi? Je, wenyewe wanazifahamu? Je, wanajua mahali na namna ya kuzifuatilia? Je, wanajua sheria za nchi zinasema nini kuhusu haki yao ya kurithi mali ya baba au mama yao?

Matatizo yanayowakabili yatima
Kinachotokea katika familia nyingi ni kwamba, kwanza yatima hukosa malezi kutokana na mzazi au wazazi wao kutokuwepo tena duniani. Kama yatima waliachwa wakiwa wadogo, tatizo linakuwa ni kubwa zaidi maana ukweli ni kuwa hakuna mtu anayeweza kuwaangalia watoto vizuri kama mzazi wao. Hata ukijitahidi kiasi gani, huwezi kuwaridhisha kama ambavyo wangelelewa na baba au mama yao.

Vile vile yatima wanapoachwa wakiwa wadogo, wanakabiliwa na hatari ya kudhulumiwa urithi wao, hasa wanapokuwa wamefiwa na wazazi wote wawili. Wale waliokabidhiwa jukumu la kuwalea, wanaweza kuwadhulumu sehemu au mali yote iliyoachwa na marehemu. Ukweli ni kuwa mambo hayo hutokea katika baadhi ya familia au jamii.

Hata kama yatima wameachwa wakiwa watu wazima, wanaweza wasifahamu kwamba wanapaswa kurithi kiasi gani cha mali ya marehemu baba yao. Tatizo kama hili linaweza kujitokeza iwapo marehemu alikuwa hajagawa urithi kwa wanawe, au hakuacha wosia.

Vile vile kama mama mzazi wa watoto bado yupo hai, kunaweza kutokea mgongano kati ya watoto na mama yao, wakati wa kugawana mali iliyoachwa na marehemu. Lengo la kutunga sheria inayosimamia maswala ya urithi ni kuepusha migongano kwa kuhakikisha kuwa haki ya kila anayestahili kurithi inalindwa.
Watoto wa kiume dhidi ya watoto wa kike

Kwa haraka haraka unaweza kudhani kuwa yatima wote, yaani mtoto wa kiume na wa kike, wana haki sawa linapokuja swala la kurithi. Lakini ukweli ni kuwa mambo hayako hivyo mara zote. Mila na desturi za makabila mengi hapa nchini zinabagua kati ya watoto wa kike na wale wa kiume. Hata sheria za nchi zilizopo hapa Tanzania, kwa kiasi fulani zinabagua katika jambo hili la kurithi. Tutaziangalia kwa kina baadaye.

Katika jamii ya kibinaadamu (human society), ambayo kwa kiwango kikubwa sana ni ya mfumo dume (male dominated society), utakuta hakuna usawa kati ya watoto wa kiume na wa kike. Katika familia, jamii au makabila mengi hapa Tanzania, utakuta mtoto wa kiume anapendelewa kuliko wa kike wakati wa kurithisha mali za wazazi wao.

Kwa baadhi ya makabila, mtoto wa kike huwa harithi au harithishwi chochote kilichokuwa mali ya wazazi wake. Mimi ninayeandika makala haya ni Mchaga. Kwetu Uchagani, mtoto wa kike huwa harithishwi ‘kihamba’ au ardhi. Kwa sababu hiyo, marehemu baba yangu hakuwagawia dada zangu mashamba. Bila shaka yapo makabila mengine hapa nchini, ambayo nayo yana ubaguzi kama huu.

Wayahudi hawakurithisha watoto wa kike
Unapoiangalia Biblia wakati wa Agano la Kale utagundua kuwa katika mfumo wa Kiyahudi, watoto wa kike walikuwa hawarithi chochote kutoka kwa wazazi wao. Kusema kweli wanawake walikuwa wanadharauliwa sana. Myahudi asilia alikuwa anaona fahari sana anapozaliwa kama mwanamume, na nuksi kama ni mwanamke.

Urithi wote ulikuwa ni halali ya watoto wa kiume tu. Halafu kulikuwa na tofauti kati ya hao watoto wa kiume. Kulikuwa na kitu kilichokuwa kinaitwa ‘haki ya mzaliwa wa kwanza’. Mtoto wa kwanza wa kiume kuzaliwa kwa baba yake ndiye alikuwa anaitwa mzaliwa wa kwanza. Huyu alikuwa anarithishwa mara mbili zaidi ya ndugu zake (Kumbukumbu 21:17).

0 maoni:

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).