Friday, June 5, 2009

Hata baraka za mwilini zina mashartiHata baraka za mwilini zina masharti yake. Kwanza kabisa, kama zilivyo za rohoni, nazo zina kusubiri kwa muda mrefu. Haziji chapuchapu. La hasha. Vile vile kiwango cha baraka hizi kinategemea aina na uzito wa masharti. Masharti magumu ni kiashiria kuwa baraka zitakazopatikana ni za hali ya juu.

Tuseme mwamini anataka awe na mali mengi. Moja ya masharti au wajibu atakaopaswa kutimiza ni kutoa sadaka. Lakini sio utoaji wa kawaida tu. La hasha. Ni lazima awe mtoaji mzuri. Mtoaji wa kilicho chema na kwa wingi pia.

Katika 2Wakorintho 9:6 mtume Paulo anaandika hivi, “Lakini nasema neno hili, Apandaye hapa atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu’. Hapa tunaona kuwa mtu akitaka kuvuna, kwanza ni lazima apande mbegu. Hilo ndio sharti la kwanza. Lakini kama anataka mavuno mengi, ni lazima vile vile apande mbegu kwa wingi. Vinginevyo atavuna kidogo.

Kwa kumalizia kipengele hiki cha wakati wa kurithi baraka, naomba nisisitize tena kwamba, mwamini hawezi kujua kwa hakika ni lini atabarikiwa na Mungu. Hata baada ya kutimiza masharti au wajibu wake, bado anatakiwa asubiri wakati uliopangwa na Mungu. Anatakiwa awe na subira au uvumilivu, hadi hapo BWANA atakapomkumbuka.

Kwanini wakristo wengi tunashindwa kurithi baraka kutoka kwa Mungu?
Msomaji haya ninayotaka kuzungumzia sasa ni mawazo au mtazamo wangu. Yanaweza yasiwe sahihi, na kama nitakuwa nimekosea, naomba nisamehewe. Lakini nitasema kile ninachokiona katika makanisa, huduma, vikundi mbalimbali vya kilokole na waumini binafsi.

Ninaposoma Biblia kuhusu baraka zilizoahidiwa kwa watu wa Mungu, halafu nikilinganisha na maisha ya walokole wengi ninaokutana nao, naona kama vile bado kabisa sisi tuliookoka hatujabarikiwa au hatujarithi baraka za Mungu.

Kunaweza kukawa na mafanikio kidogo katika eneo la baraka za rohoni, lakini bado sidhani kama ni katika vile viwango vilivyoahidiwa na Mungu. Nakubali kuwa wapo waumini wengi tu waliopokea ahadi ya kujazwa Roho Mtakatifu. Vile vile karama na vipawa mbalimbali vinaonekana katikati ya jamii ya watu waliookoka. Lakini udhihiriko wa baraka hizi haupo katika viwango vilivyokusudiwa na Mungu.

Tunapogeukia baraka za mwilini, napo hali ni ile ile ya wasiwasi. Tena naona kama vile huku ndio kwenye matatizo zaidi, ukilinganisha na baraka za rohoni. Yaani unapowatazama watu wengi waliookoka, hawafanani kabisa na watu waliobarikiwa. Wengi bado ni jua kali au walala hoi. Swali la kujiuliza ni kwanini hali iko hivi?

Watu waliookoka wameahidiwa baraka tele

Msomaji hebu tutafakari kidogo. Mungu anasema katika Mithali 8:18 kwamba, “Utajiri na heshima ziko kwangu, naam utajiri udumuo, na haki pia”. Halafu katika Mithali 8:20-21 anasema kwa uhakika kabisa kwamba, “Natembea katika njia ya haki, katikati ya mapito ya hukumu, niwarithishe mali wale wanipendao, tena nipate kuzijaza hazina zao?”

Tunapoliangalia Agano Jipya napo tunakuta kuwa ahadi za kubarikiwa ni nyingi mno. Kwa mfano katika 2Wakorintho 9:10-11 imeandikwa kuwa, “Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu; mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukurani kwa kazi yetu”.

Mistari niliyonukuu inaonyesha ahadi ya utajiri kwa watu wa Mungu. Lakini hebu tujiulize, je, hali halisi ndivyo ilivyo? Je utajiri wa dunia hii upo mikononi mwa nani kwa sasa? Mimi naona kama vile upo kwa watu ambao hawajaokoka; watu ambao hawamjui Mungu kabisa.

0 maoni:

Post a Comment

Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.

Recent Posts

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).