Friday, June 5, 2009

URITHI: Hitimisho



Kwa sasa nimefikia mwisho kabisa wa mada hii inayohusu urithi. Naomba nihitimishe kwa kusisitiza mambo yafuatayo.

Kwetu sisi wanadamu, Mungu ni kama walivyo baba zetu hapa duniani. Kama ambavyo wazazi wetu waliotuzaa huturithisha mali, vile vile Mungu naye huwarithisha wanadamu baraka za aina mabalimbali.

Wapo watu maalumu wataostahili kurithi. Sio kwamba kila mtu anaweza kupewa urithi. La hasha. Wana ndio warithi halali wa mali za wazazi wao.

Mungu naye ana wana. Watu waliozaliwa mara ya pili, au waliookoka, hao ndio wana wa Mungu. Hao ndio wanaostahili kurithi baraka kutoka kwake.

Urithi kutoka kwa mwanadamu mmoja kwenda kwa mwanadamu mwingine una sheria, kanuni au taratibu zinazosimamia jambo hili. Hali kadhalika, urithi au baraka kutoka kwa Mungu una kanuni au masharti au taratibu zake.

Ili mtu aweze kurithi mali au baraka, ni lazima atimize masharti yanayotakiwa. Ni lazima atimize wajibu wake. Hakuna haki isiyokuwa na wajibu.

Mali yote wanayochuma wazazi huwaachia au huwarithisha wana wao. Kadhalika, kila alichoumba Mungu, ni kwa ajili ya mwanadamu, hasa wale wanaolicha jina lake. Yaani wale waliookoka.

Kama ambavyo mzazi huona fahari kumrithisha mwanawe mali, vile vile Mungu hufurahi sana wana wake wanapofanikiwa au wanapobarikiwa. Kiu ya Mungu ni kuona wanadamu wote wanaishi maisha ya fanaka. Ndio maana huwarithisha mali (Mithali 8:17-21).

Watu wengi, au tuseme wana wa Mungu, wanashindwa kurithi baraka kutoka kwake kwa sababu ya kutotimiza masharti yanayoambatana na baraka hizo.Wapo wengine wanaozitaka, lakini hawamtaki mwenye kuzimiliki. Hawataki kufanyika wana wa Mungu au kuokoka.

Kundi kubwa la waumini wanaoshindwa kurithi baraka kutoka kwa Mungu ni wale wasiofuata kanuni au wasiotekeleza masharti yanayoambatana na baraka wanazozitaka. Wengi hawamtolei Mungu kiasi cha kutosha au hawamtumikii kabisa, lakini bado wanataka kubarikiwa.

Msomaji ni matumaini yangu kuwa mada hii imekufungua macho kiasi cha kutosha. Kama ni urithi kutoka kwa wanadamu, naaamini sasa unatambua haki zako, na vile vile wajibu wako. Kwahiyo unajua la kufanya ili usipoteze haki hiyo.

Kama ni baraka kutoka kwa Mungu, napo naamini kwa sasa unatambua mambo unayoweza kupokea kutoka kwake, na vile vile wajibu wako au mambo unayotakiwa kuyafanya ili ubarikiwe kwa vitu vya rohoni na vya mwilini.

Rai yangu ni hii. Kama kuna eneo ambalo umegundua kuwa ulikuwa na mapungufu, tafadhali lifanyie kazi. Lirekebishe.

Kumbuka kuwa kama baba yetu wa duniani anavyompenda mwanawe, Mungu wetu naye ni mwema sana na siku zote anatuwazia yaliyo mema sisi tulio wana wake. Ukiona hayo mema aliyoahidi hayakufikii, ujue tatizo sio Yeye, bali ni wewe. Jirekebishe.

Lishike sana neno hili, :”Mungu si mtu, aseme uongo; wala si mwanadamu ajute; Iwapo amesema hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? (Hesabu 23:19). Wewe timiza wajibu wako, halafu usubiri wakati wa Bwana. Uwe mvumilivu, nawe utarithi baraka. Asante sana na Mungu wa mbinguni akubariki. Amen. Read More......

URITHI: Ulimwengu uliumbwa kwa ajili ya mwanadamu


Mungu anapoturithisha baraka mbalimbali ni kwamba, anakuwa anaturudishia kile kilichokuwa stahili yetu tangu kuumbwa kwa ulimwengu huu. Ni kweli Biblia inasema kuwa Shetani ni mungu au mtawala wa dunia hii (2Wakorintho 4:4, Luka 4:6).

Shetani aliipata haki ya kuitawala dunia baada ya anguko la Adamu na Hawa, pale waliposhindwa kutii agizo la Mungu, wakala matunda ya mti waliokuwa wamekatazwa (Mwanzo 3:1-19). Lakini tangu mwanzo, mwanadamu ndiye aliyetawazwa juu ya uumbaji wa Mungu (Zaburi 8:3-8).

Mwanadamu ndiye mlengwa wa uumbaji wa Mungu
Ukweli ni kuwa mwanadamu ndiye mlengwa (focal point) wa kila alichoumba Mungu. Yeye ndiye aliyetawazwa juu ya vitu vyote (Mwanzo 1:26, Zaburi 8:4-8), ili avimiliki na kuvitumia kwa manufaa yake. Haya mahangaiko au uhitaji tulio nao hapa dunia haukuwa mpango wa Mungu hata kidogo.

Ni kweli kulitokea anguko la mwanadamu, akapoteza mamlaka aliyopewa na Mungu juuya ulimwengu huu.. Lakini baada ya Yesu kuja duniani, na hatimaye kufa pale msalabani, Mungu aliweka vitu vyote mikononi mwake (Waebrania 1:2-4). Biblia inatuambia kuwa Mungu, “akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa” (Waefeso 1:22).

Kifo cha Yesu pale msalabani kilirejeza kwa kiwango fulani mamlaka ambayo mwanadamu alikuwa nayo tangu mwanzo. Kwa njia ya Yesu, watu waliookoka wanaweza kumnyang’anya Shetani kile kitu au mamlaka aliyoyapata kwa ujanja (Mwanzo 3:1-7).

Sio mapenzi ya Mungu wanadamu waishi kwa taabu
Sababu ya pili inayomfanya Mungu aturithishe baraka ni ili tuishi kwa furaha na amani.. Ni kutokana na upendo alio nao kwetu sisi wanadamu. Katika Yohana 16:24 Yesu anatuambia kuwa, “Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu”. Unaweza kuona hapa kuwa Yesu anasema kuwa tukiomba tutapata ili tufurahi.

Ukweli ni kuwa sio mapenzi ya Mungu sisi wanadamu tuishi kwa taabu. Sio mpango wake tuugue, au tulale njaa, au tupungukiwe chochote, na kadhalika. La hasha. Hayo ni matokeo ya anguko la mwanadamu, au tuseme ni matokeo ya dhambi.

Mungu hufurahia mafanikio ya watu wake
Katika Zaburi 35:27 tunaambiwa kuwa, “Washangilie na kufurahi, wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe BWANA, apendezwaye na amani ya mtumishi wake”. Maneno haya katika Biblia ya Kiingereza yanasomeka hivi, “Let them shout for joy and be glad, who favour my righteous cause; and let them say continually, ‘Let the Lord be magnified, who has pleasure in the prosperity of his servant”.

Maneno ‘who has pleasure in the prosperity of his servant’ yana maana kuwa, Mungu hufurahi sisi wanadamu tunapofanikiwa au tunapobarikiwa. Na kama nilivyosema, hii ni moja ya sababu inayomfanya aturithishe baraka za namna mbalimbali.

Ni kwa jinsi gani tunaweza kurithi baraka kutoka kwa Mungu?
Nafikiri makala haya haya hatakamilika bila kueleza, ni kwa jinsi gani sisi wanadamu tunavyoweza kurithi baraka kutoka kwa Mungu. Msomaji utakumbuka kuwa huko nyuma niliainisha baadhi ya sababu au vikwazo vinavyoweza kuwazuia watu wa Mungu wasirithi baraka kutoka kwake.

Kwa kukumbushia nilisema kuwa vikwazo hivyo ni kama ifuatavyo;
  1. Mwamini kuendelea au kubaki kuwa mtoto mchanga.
  2. Kutokujua haki zetu au mambo tunayostahili kurithi.
  3. Kutotambua na kutekeleza masharti yaliyoambatana na kila aina ya baraka.
  4. Kutotembea au kutotumikia wito
Baada ya kuokoka, unatakiwa ukue
Nafikiri sasa tunaweza kukubaliana kuwa, ili mtu aweze kurithi baraka ni lazima aondoe vikwazo vilivyo mbele yake. Ni lazima atimize masharti yanayotakiwa. Kitu cha kwanza ni lazima afanyike mwana. Ni lazima azaliwe mara ya pili. Yaani ni lazima aokoke.

Kama tulivyoona huko nyuma, Mungu ni kama alivyo baba yetu wa hapa duniani. Kwa kawaida, baba huwa hamrithishi mali kila mtoto anayemwona. Hapana. Huwarithisha wanawe tu aliowazaa.

Vivyo hivyo Mungu naye huwarithisha wanawe. Na kama tulivyoona, wana wa Mungu ni wale waliookoka. Hao ndio wanaoweza kurithi baraka kutoka kwake.

Baada ya kufanyika mwana, ni lazima mwamini akue. Hatakiwi kuendelea kuwa mtoto mchanga kiroho. Ni lazima amjue sana Mungu (Ayubu 22:21), ajue neno lake kwa wingi (Wakolosai 3:16), awe imara katika imani (2Petro 1:10) na kadhalika. Sio mtu anasema ameokoka, lakini ni mbumbumbu katika katika maswala yanayohusu ufalme wa Mungu.

Ukikua utatambua haki na wajibu wako
Mwamini akikua, ndipo anaweza kutambua haki zake. Ndipo anaweza kutambua mambo ambayo anastahili kupokea au kurithi kutoka kwa Mungu. Akiisha kuyatambua, ndipo anaweza kuyadai au kuyaomba.

Biblia inatuambia kuwa tusisumbuke, “Bali utafuteni kwanza ufalme wake (yaani wa Mungu), na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa” (Mathayo 6:33). Kuutafuta ufalme wa Mungu ni kukubali kuokoka na vile kujifunza kwanza yale mambo yanayohusu ufalme huu. Baada ya hapo ndio unaweza kubarikiwa.

Mwamini anapokua, ndipo anaweza kutambua kanuni za kubarikiwa. Ndipo atatambua masharti yaliyoambatana na kila aina ya baraka. Ndipo atatambua wajibu wake au mambo anayotakiwa ayakamilishe, kabla hajabarikiwa. Vinginevyo atabaki anashangaa tu ni kwanini haoni baraka za Mungu katika maisha yake?

Tambua wito wako
Tumeona kuwa baraka nyingi za mwamini zimefungamanishwa ndani ya wito wake. Kwahiyo ni muhimu kila mtu aliyeokoka atambue wito au ile kazi maalumu ambayo Mungu anamtarajia aifanye hapa duniani. Na kusema kweli jambo hili sio rahisi hata kidogo.

Kazi ya kutambua wito sio nyepesi. Inahitaji mafunzo maalumu. Vile vile mwamini anatakiwa autafute uso wa Bwana kwa bidii, hadi hapo atakapopata jibu la uhakika kwamba anatakiwa afanye nini (Zaburi 32;8, Zaburi 143:8). Yawezekana jambo hili likachukua hata miaka zaidi ya kumi kabla jibu halijapatikana.

Uwe mvumilivu
Mwisho kabisa, pamoja na kutekeleza masharti yote yanayotakiwa, ni lazima mwamini awe mvumilivu. Ukweli ni kuwa baraka za Mungu huwa haziji kirahisi au kiulaini, kama watu wengi wanavyodhani. Kuna kuvumulia. Na hapa ndipo wengi wetu tunapokwama.

Siku hizi waumini wengi hawana uvumilivu. Hawataki kusubiri. Wanataka baraka za chapu chapu tu. Wakitoa sadaka leo, au wakimtumikia Mungu kidogo tu, au wakiombewa leo, wanataka kesho yake waone baraka. Mambo hayako hivyo ndugu zanguni.


Ibrahimu alivumilia
Ili jambo hili lieleweke vema, hebu tuangalie mifano michache ya watu waliovumilia kwa muda mrefu hadi wakabarikiwa au wakapokea ahadi walizoahidiwa na Mungu. Tuanze na Ibrahimu, baba yetu wa imani.

Wasomaji wazuri wa Biblia wanafahamu kuwa Mungu alianza kuongea na Ibrahimu wakati alipokuwa na umri wa miaka sabini na tano (Mwanzo 12:4). Lakini ilipita miaka ishirini na mitano, ndipo ahadi ya kupata mtoto ilipotimia, yaani wakati Ibrahimu akiwa mzee wa miaka mia moja (Mwanzo 17:17).

Sasa ndugu yangu, kusubiri ahadi ya BWANA kwa muda wa miaka ishirini na mitano sio jambo dogo. Yahitaji moyo mkuu. Yahitaji uvumilivu wa hali ya juu. Huo ndio ukweli wenyewe.

Kwa bahati nzuri baba yetu wa imani alishinda mtihani huu wa uvumilivu. Biblia inatuambia kuwa, “Kwa maana Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake. Akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki. Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi (Waebrania 6:13-15).

Yusufu alivumilia
Mfano mwingine wa uvumilivu ni wa Yusufu. Nafikiri wengi wetu tunafahamu historia ya ndugu huyu, jinsi alivyoota ndoto kwamba ipo siku baba yake, mama yake na ndugu zake watakuja kumsujudia (Mwanzo 37:5-11). Jambo hili halikutimia haraka, wala kirahisi.

Biblia inatuonyesha kuwa Yusufu alikuwa na umri wa miaka kumi na saba wakati alipoota ndoto zile (Mwanzo 37:2). Ilimchukua miaka kumi na mitatu hadi alipokuwa Waziri Mkuu wa Misri, wakati huo akiwa na umri wa miaka thelathini (Mwanzo 41:46).

Baada ya kuwa Waziri Mkuu, ilipita miaka mingine zaidi ya saba, ndipo ahadi ya BWANA ilipotimia. Ndipo baba yake na ndugu zake walipokuja kukaa chini ya himaya yake, wakati walipohamia Misri njaa ilipopamba moto katika nchi ya Kanaani (Mwanzo 46:1-26).

Daudi alivumilia
Mfano wa mwisho ni wa mfalme Daudi. Msomaji ukifuatilia maisha ya Daudi utagundua kuwa alipakwa mafuta (ili awe mtawala badala ya Sauli) wakati akingali kijana mdogo tu, mchunga kondoo (1Samweli 16:1-13).

Ilipita miaka mingi sana kabla hajawa mfalme wa Israeli. Biblia inatuambia kuwa, “Daudi alikuwa amepata miaka thelethini alipoanza kutawala, akatawala miaka arobaini” (2 Samweli 5:4). Hapa katikati Daudi alivumilia misukosuko au mapito mengi kabla hajapata fursa ya kutawala.

Usichoke; usikate tamaa
Ninachotaka kusema ni hiki msomaji wangu. Ijapokuwa Mungu amekuahidi jambo fulani, inaweza kupita miaka mingi sana kabla jambo hilo halijatimia. Unaweza kuahidiwa baraka kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu, lakini vile vile unaweza kupita muda mrefu sana kabla baraka hizo hazijatimia katika maisha yako.

Ndio kusema mwamini anatakiwa awe na uvumilivu. Hiki ndicho Kinachozungumzwa katika Waebrania 6:11-12 kwamba, “Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho; ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu”

Huko nyuma nilisema kuwa mwamini hawezi kuwa na uhakika ni lini atakapobarikwa na Mungu, hata baada ya yeye kutimiza masharti yote yanayotakiwa. Anatakiwa asubiri wakati wa Bwana. Hicho ndicho tunachoambiwa katika Wagalatia 6:9 kwamba, “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho”.

Hizi baraka za papo kwa papo zinazohubiriwa na mitume au manabii wengi wa siku za leo sio mpango kamili wa Mungu. Nyingi ni kiini macho. Ni usanii. Mwenye sikio la kusikia na asikie. Read More......

URITHI: Uchanga wa kiroho, wito na huduma katika baraka

Katika sehemu ya kwanza ya mada hii nilisema kuwa, mtoto mdogo hawezi kurithi mali kutoka kwa baba au mama yake, hata kama urithi huo ni haki yake. Nilianisha matatizo yanayoweza kujitokeza iwapo watoto watarithishwa mali.

Matatizo hayo ni pamoja na matumizi mabaya ya urithi uliopatikana, kama vile kutokujua nini cha kuufanyia, kutapanya, kudhulumiwa na kadhalika. Tunapogeukia urithi au baraka kutoka kwa Mungu tunakuta kuwa, hali inafanana sana na ile ya urithi kutoka kwa wanadamu.

Ukweli ni kuwa hata Mungu hawezi kuwarithisha watoto wadogo baraka, hata kama ni haki yao. Na watoto ninaozungumzia hapa ni waumini ambao tayari wameokoka, lakini bado ni wachanga kiroho au hawajakomaa katika mambo ya Mungu.
Mtoto mdogo haaminiki

Msomaji kama ukichunguza kwa makini utagundua kuwa, kuzaliwa kimwili kunafanana sana na kuzaliwa kiroho. Mtu anapozaliwa na wazazi wake, anaanzia utotoni na baadaye anakua (grow) mpaka anapofikia utu uzima. Baada ya kukua na kukomaa, ndipo anaweza kuaminiwa katika mambo makubwa, ikiwa ni pamoja na kukabidhiwa urithi wake.

Tunapozaliwa na Mungu au tunapookoka kwa mara ya kwanza, hiyo ni hatua ya mwanzo tu ya safari ndefu ya kuelekea mbinguni. Mkristo aliyeokoka, lakini hana siku nyingi katika wokovu, anakuwa hajui mambo mengi yanayohusu ufalme wa Mungu. Anakuwa hata tofauti na mtoto mdogo, ambaye bado hajaufahamu ulimwengu. Mkristo wa namna hiyo tunasema ni mchanga kiroho.

Mkristo ambaye bado ni mchanga, hawezi kuaminiwa katika maswala yanayohusu ufalme wa Mungu. Kwa mfano, hawezi kupewa nafasi ya uongozi (1Timotheo 3:6). Vile vile hawezi kurithishwa baraka mbalimbali zinazopatikana katika ufalme huu.

Biblia inasema nini kuhusu uchanga wa kiroho?

Hebu sasa tuigeukie Biblia tuone inasema nini kuhusu uchanga wa kiroho. Mtume Paulo anasema yafuatayo katika Wagalatia 4:19-20, “Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu; laiti ningekuwepo pamoja nanyi sasa, na kuigeuza sauti yangu! Maana naona shaka kwa ajili yenu”

Hawa watu ambao Paulo alisema nao maneno haya walikuwa ni watu wazima kimwili, lakini akawaita vitoto. Aliwapa jina hilo kwa sababu ingawa walikuwa wameokoka, bado walikuwa hawajakomaa katika maswala ya Mungu. Na kwa sababu hiyo alikuwa hawaamini.

Mstari wa 20 una maneno ‘maana naona shaka kwa ajili yenu’. Maneno haya yanaonesha kutoaminika. Kwahiyo Paulo alikuwa hawaamini wale waumini. Kisa? Bado walikuwa wachanga kiroho. Watu kama hawa huwezi kuwatweka majukumu mazito. Huwezi kuwarithisha baraka.

Watoto hawashirikishwi mambo mazito

Hebu tuangalie tena andiko lingine linalozungumzia uchanga wa kiroho na athari zake. Katika 1Wakorintho 3:1-2 mtume Paulo nasema kuwa, “Lakini, ndugu zangu, nami sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi”.

Msomaji unaweza kuona kuwa Paulo alishindwa kuongea na wale waumni mambo mazito ya kiroho kwa sababu walikuwa bado ni wachanga katika ufalme wa Mungu. Wasingemwelewa. Kwa sababu hiyo akaongea nao mambo mepesi mepesi tu. Yaani akawapa maziwa au uji au ‘mtori’, badala ya ugali.
Uchanga wa kiroho unatunyima uhondo

Ni ukweli ulio wazi kuwa, wakristo tunapoendelea kubaki watoto wachanga katika maswala yanayohusu ufalme wa Mungu, ndivyo tunavyoshindwa kufaidi uhondo ulio katika ufalme huu. Ndivyo tunavyoshindwa kurithi baraka mbalimbali.

Uchanga wa kiroho unatufanya tushindwe kufaidi mambo mazuri yaliyo ndani ya wokovu. Tunashindwa kula mema au manono ya nchi (Isaya 1:19). Tunashindwa kufanikiwa katika maisha ya kawaida hapa duniani.

Hili ndio moja ya matatizo makubwa yanayolikabili kanisa la Mungu sehemu nyingi duniani. Waumini hawakui na kukomaa katika mambo ya Mungu. Wanadumaa japo wameokoka. Na kwa sababu hiyo Mungu anashindwa kuwamwagia baraka kama alivyoahidi (Malaki 3:10).

Sikiliza ni kwambie kitu msomaji. Mungu wetu ana kiu kubwa sana ya kuturithisha baraka za rohoni na za mwilini. Kiu hiyo ni kubwa kuliko sisi wenyewe tunavyowaza au tunavyodhani (Waefeso 3:20). Tatizo letu ni kwamba bado hatujaweza kukaa mkao wa kubarikiwa. Bado tu watoto wadogo katika Kristo.
Mungu aweza kukunyima baraka kwa nia njema

Kama nilivyoainisha huko nyuma, zipo athari za kumrithisha mtoto mdogo baraka. Anaweza asimudu baraka atakazokabidhiwa. Kwa mfano anaweza kuzipoteza. Wengine zinawaleta kiburi na dharau. Na ukweli ni kuwa, Mungu akikuona huwezi kumudu au kukabiliana na baraka anazokusudia kukupa, hatakupatia.

Nia ya Mungu ya kukunyima hizo baraka ni ili usipotee. Ni ili usiwe mbali Naye. Wapo watu waliorithishwa baraka, lakini kwa sababu ya kiburi na dharau, wakashindwa kuendelea na wokovu. Wakamwasi Mungu halafu wakaipenda dunia. Matokeo yake wakafa katika dhambi.

Lengo kuu la Mungu katika maisha ya watu wake ni kuona kuwa wanarithi au wanaingia katika uzima wa milele. Baraka, aidha za rohoni au za mwilini, ni moja tu ya matunda ya wokovu. Lakini sio jambo ya msingi. Msingi ni kufika mbinguni.

Mungu yupo radhi kukuacha ukiwa maskini, iwapo anaona kwamba akikubariki, hutafika mbinguni. Na msomaji kama umewahi kuchunguza kwa makini, utagundua wapo watu waliobarikiwa, tena kidogo tu, lakini baada ya muda wakamwacha Mungu. Wakalewa mafanikio.


Kutotembea katika wito

Sababu ya nne na ya mwisho nitakayoizungumzia, ambayo inaweza kumnyima mwamini fursa ya kubarikiwa ni kutotembea katika wito alioitiwa na Mungu. Unakuta mtu huyo ameokoka, ni mwaminifu na hatendi dhambi yeyote. Hakosekani kanisani, lakini bado hali yake kimaisha au kiuchumi sio nzuri. Kwanini hali inakuwa hivyo?

Ukweli ni kuwa Mungu ametuokoa kwa makusudi maalumu. Kuna kitu au kazi au wajibu maalumu ambao kila mwamini amepangiwa na anatakiwa autimize kabla hajaondoka hapa duniani. Wajibu huo ndio unaitwa ‘wito wa Mungu’.

Hebu tuone Biblia inasema nini kwa habari ya wito. Katika 2Timotheo 1:9 tunaambiwa kuwa Mungu, “alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadri ya makusudi yake yeye na neema yake”.

Huu mwito mtakatifu, ambao tunaambiwa ni kwa makusudi ya Mungu, ndio wito wenyewe.. Ni yale mambo ambayo anataka tuyafanye au tuyatimize katika maisha yetu ya wokovu hapa duniani. Huu ndio mwito mtakatifu au wajibu wetu maalumu kwa Mungu, na ni moja ya sababu iliyomfanya atuokoe.
Ndani ya wokovu kuna wajibu


Ukweli ni kuwa sisi hatukuokolewa ili kukae vivi hivi tu. La hasha. Hatukuokolewa ili tuburudike au tuifaidi matunda ya wokovu tu. Hapana. Yapo mambo ya kufanya; yapo majukumu; upo wajibu wa kutimiza.

Katika 1Petro 2:9 Biblia inasema hivi kuhusu watu waliookoka. “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ua ajabu”.

Maneno ‘mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani’ yanaonyesha kuwajibika. Yanaonyesha kwamba kila mtu aliyeokolewa na Mungu anapaswa kueneza habari hizi njema za wokovu kwa watu wengine ambao bado hawajaokoka.
Kanisa ni wapatanishi

Kila mtu aliyeokoka ni kuhani. Ni mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ambao bado wapo dhambini. Anapaswa kuwahubiria au kuwashuhudia habari za Mwokozi Yesu (2Wakorintho 5:17-19) na za ufalme wa Mungu.

Mtume Paulo anasema yafuatayo kuhusu watu waliookoka kuwa wapatanishi. “Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu” (2Wakorintho 5:20).

Pamoja na kila aliyeokoka kuwa mpatanishi, bado upo wajibu maalumu anaopaswa kuutimiza hapa duniani. Lipo eneo maalumu analotaka tumtumikie na sio kufanya chochote kile tunachoamua kwa matakwa yetu binafsi, hata kama kitu hicho ni kizuri.

Mwili mmoja, lakini viungo tofauti

Hebu tuangalie maana ya wito kwa kuangalia maumbile ya miili yetu. Katika Warumi 12:4-5 imeandikwa kuwa, “Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.”.

Sasa msomaji naomba uzingatie maneno ‘katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja’. Kinachozungumziwa hapa ni kuwa, ingawa sisi sote tuliookoka ni wamoja katika mwili wa Kristo, lakini kila mmoja ni kiungo fulani katika mwili huo.

Nafikiri sote tunafahamu kuwa kila kiungo katika miili yetu kina kazi yake maalumu. Hakifanyi wala hakiwezi kufanya chochote kile kitakachopenda. La hasha. Kinaweza tu kufanya kazi moja kwa ufasaha.

Jicho haliwezi kusema; hiyo ni kazi ya mdomo. Mguu hauwezi kusikia, ingawa unaweza kutembea. Kazi ya kusikia ni ya sikio na ya kunusa ni ya pua, na kadhalika. Kila kiungo kina kazi yake maalumu na hakiwezi kufanya lolote lile linalohitajika kufanywa na mwili.

Hata swala la wito ndio lilivyo. Kwamba ingawa kila aliyeokoka ni kiungo katika mwili wa Kristo, lakini ipo kazi maalumu anayoweza na anayotakiwa aifanye. Akiifanya tunasema huyo anatumikia wito wake.
Wakristo wengi hawatambui wito wao

Kwa bahati mbaya wapo wakristo wengi sana ambao hawaelewi maana ya wito, wala hawajui wito wao ni upi. Kama nilivyosema, ni kweli wameokoka wala hawatendi dhambi (1Yohana 3:9). Lakini hawajui ni kazi ipi ambayo Mungu amewapangia na anatarajia waifanye.

Wapo waumini ambao wanafanya chochote kile ambacho nafsi zao zinawatuma kufanya. Hawamwulizi Mungu kama hicho wanachofanya ndicho anachotaka wakifanye au la. Yaani hawamwulizi wito wao ni upi? Hili ni tatizo kubwa kweli kweli katika kanisa la leo.

Sikiliza msomaji nikwambie kitu. Kila aliyeokoka anatakiwa atambue wito wake. Anatakiwa autafute uso wa Mungu mpaka amjulishe kile ambacho anamtaka akifanye. Halafu akiishatambua kitu hicho, au tuseme akishatambua wito wake, anatakiwa autumikie kwa bidii na kwa moyo mmoja. Hapo ndipo atakuwa ameyafanya mapenzi ya Mungu.

Kila mwamini ana kazi yake maalumu

Katika 1Wakorintho 12:28 tunaambiwa kuwa, “Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha”.

Sio kila mtu aliyeokoka anaweza kuwa mtume, au nabii, au mchungaji, na kadhalika. Hapana. Wapo waumini maalumu walioteuliwa au waliochaguliwa na Mungu kwa ajili ya kufanya kazi kama hizi. Wanapotambua na kusimama katika nafasi zao, tunasema kuwa hawa wanatumikia wito wao.
Wito wa Paulo

Ili swala la wito liweze kueleweka vizuri, hebu tuchunguze utumishi wa Paulo. Nafikiri wengi wetu tunafahamu kuwa mtumishi huyu wa Bwana aliteuliwa na Mungu ili awe mtume. Jambo hili lipo wazi tunaposoma mistari ya mwanzo ya sura ya kwanza katika nyingi ya nyaraka zake.

Kwa mfano waraka kwa Wagalatia unaanza hivi. “Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka wafu”. Hapa Paulo anatuonyesha kuwa yeye hakujichagua, wala hakuambiwa na wanadamu kwamba yeye ni mtume. Utume wake alipewa na Mungu kupitia kwa Yesu.

Paulo hakuwa mtume peke yake. La hasha. Vile vile alikuwa na karama au vipawa vya ualimu na uinjilisti. Jambo hili lipo wazi katika waraka au barua aliyomwandikia Timotheo, ambapo tunakutata na maneno ‘ambayo kwa ajili ya hiyo (yaani Injili) naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu (2Timotheo 1:11).

Sasa msomaji nafikiri utakubaliana nami kuwa mwamini anaweza kuwa na karama au kipawa zaidi ya kimoja. Kama Paulo alipewa, hata leo hii sisi tuliookoka tunaweza kuwa na vipawa vingi. Ndio maana unasikia mtu anajiita mtume na nabii. Au mwingine ni mchungaji, mwinjililisti na vile vile ni mwalimu.
Usitumike popote pale

Tunapozidi kumchunguza Paulo tunaweza kuona kuwa yeye hakuwa mtume wa jumla jumla tu. Hapana. Yeye alikuwa ni mtume kwa ajili ya mataifa au watu ambao hawakuwa Wayahudi. Ndio maana alisafiri nchi nyingi akihubiri, akifungua makanisa na kufundisha.

Katika Warumi 11:13 Paulo aliandika maneno yafuatayo, “Lakini nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa, naitukuza huduma iliyo yangu”. Waweza pia kusoma Warumi 15:15-16 ambapo napo tunaona kuwa huduma au utume wa Paulo ulikuwa ni kwa ajili ya watu wasiokuwa Wayahudi.

Mtume Paulo alipojaribu kuwahubiria Wayahudi, walimkatalia au hawakumkubali (Matendo 13:46-48). Moja ya sababu iliyowafanya wasiikubali Injili yake ni kwa sababu alikuwa anatumika mahali ambapo hakupangiwa na Mungu. Alikuwa anahudumu nje ya wito wake, japo lilikuwa ni neno sahihi la Mungu.

Siku za leo kuna watumishi ambao huduma zao hazisongi mbele. Zimedumaa na hali za hao watumishi ni mbaya mno. Moja ya sababu inayoweza kuwafanya watumishi kama hao wawe na hali duni ni kwa sababu wanatumika nje ya wito wao.

Paulo alikuwa mwalimu wa somo la imani

Hebu tumrudie tena Paulo. Tumeona kuwa alikuwa na karama au kipawa cha ualimu. Lakini hakuwa mwalimu wa jumla jumla au wa kila somo. Hapana. Yeye alikuwa ni mwalimu wa imani. Ushahidi wa jambo hili ni waraka kwa Waebrania, ambao umesheheni maswala ya imani na inaaminika kuwa uliandikwa na mtume Paulo.

Vile vile Paulo mwenyewe anajishuhudia kama ifuatavyo katika Tito 1:1, “Paulo, mtumwa wa Mungu, na mtume wa Yesu Kristo; kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu, na ujuzi wa kweli ile iletayo utauwa. Kwahiyo Paulo alitambua nafasi yake. Alijitambua kuwa yeye ni mwalimu wa maswala ya imani.

Paulo hakuwa mwalimu wa imani tu. Hapana. Alifundisha masomo mengine pia. Alifundisha somo la ndoa, somo la karama, upendo, utoaji na kadhalika. Ninachotaka ujue msomaji wangu ni kuwa alijua kwa uhakika wito wake. Alijua kile ambacho Mungu alimtaka akifanye au afundishe.
Wapo watumishi ambao hawakuteuliwa na Mungu

Sasa hebu liangalie kanisa la leo. Unakuta wapo watu wanaojiingiza katika uchungaji, lakini hawakuteuliwa na Mungu kwa ajili ya kazi hii. Unakuta washirika au wanakijiji wanamshauri au wanamshinikiza mtu akawe mchungaji, naye anakubali bila hata ya kumwuliza Mungu ili apate kibali chake.

Wapo wachungaji wanaojiingiza katika huduma ya ualimu, kumbe hawana karama au kipawa hicho. Wengine wanajitia eti wanaweza kufundisha kila somo. Kwenye somo la imani wapo, kwenye somo la ndoa napo wapo, kwenye utoaji napo wapo na kadhalika.

Matokeo ya mtumishi kujitia gwiji wa kila kitu ni ubabaishaji makanisani. Waumini hawabarikiwi kwa sababu ya mafundisho dhaifu. Kanisa linakuwa na matatizo mengi na washarika hawakui kiroho.

Usijipachike kweye huduma

Huko nyuma nilisema kuwa karama na vipawa mbalimbali hutolewa na Mungu kwa njia ya Roho wake Mtakatifu. Nilisema kuwa wapo waumini ambao hutamani sana iwapo wangekuwa na karama au kipawa fulani. Wengine wanajipachika vyeo vya kitume, kinabii, kichungaji na kadhalika.

Biblia inaonyesha jinsi ambavyo watu wanaojipachika vyeo, karama au wanaotumikia wito usiokuwa wa kwao watakavyopata hasara siku ya hukumu ya Mungu. Yesu alisema “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21).

Mapenzi ya Baba ni kile kitu ambacho Mungu anakutaka ukifanye. Ni wito wako. Sio unafanya chochote kile ambacho nafsi yako inatamani kukifanya. Ukienenda hivyo, unaweza kupata hasara ya milele.

Tahadhari usije ukakosa baraka ya uzima wa milele

Hawa watu ambao hawataingia katika ufalme wa mbiguni ni wale ambao walijiingiza katika kazi ambazo hawakupangiwa na Mungu. Wanaweza kuwa ni watumishi ‘feki’, au waumini waliotumika katika maeneo ambayo hayakuwa yao, japo walikuwa wameokoka.

Sikiliza Yesu anavyosema, “Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”. (Mathayo 7:22-23)

Sio kwamba watu kama hawa hawakumtumikia Mungu. La hasha. Walitumika, tena pengine vizuri tu. Ndio maana ishara na miujiza vilikuwa vinaonekana katika huduma zao. Lakini hawakuwasiliana na Mungu kuhusu aina ya utumishi aliowapangia. Hawakutumikia wito wao. Na kwa sababu hiyo watafukuzwa ili wasirithi uzima wa milele.

Ndani ya wito kuna baraka

Licha ya kutotambua wito ambao Mungu amewaitia, wapo waumini wengi sana wasiojua kuwa baraka zao zimeambatana au zimefungamanishwa na wito wao. Makanisani mwetu tunao waumini ambao ni waaminifu kwa Mungu na kwa viongozi wao, lakini bado hawaoni baraka zikiwajilia. Bado maisha yao ni duni. Moja ya sababu inayotufanya tusione mafanikio katika maisha ya wokovu ni kutotembea katika wito.

Ukweli ni kuwa, mwamini anapotembea katika wito au anapoyafanya mapenzi ya Mungu, ndipo anapoweza kuona baraka katika utimilifu wake. Ndipo anaweza kuwa karibu na Bwana, na kuuona uhalisi wake. Ndipo anapoweza kuufurahia wokovu wake. Vinginevyo ni mahangaiko matupu.

Ndani ya wito kuna mapito

Sina maana kuwa ukitumikia wito wako, hutakumbana na matatizo au majaribu. La hasha. Hayo yatakuwepo, maana ni sehemu ya kila aliyeokoka. Na ndio maana mtume Paulo anatuasa kuwa, “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake” (Wafilipi 1:19).

Unapotembea katika wito wako, Mungu atakuwa karibu sana na wewe. Ukipitia mambo magumu, msaada wake utapatika kirahisi zaidi kuliko mtu ambaye hatembei katika wito. Na mwisho wa yote utaona baraka tele katika maisha au utumishi wako.


Tafuta kuutambua wito wako

Nisikilize msomaji. Kama umeokoka, amani ya kweli haitakujia moyoni mwako mpaka pale utakaposimama katika wito wako. Wokovu nje ya wito ni mahangaiko mengi. Unaweza kupata mafanikio kiasi fulani, lakini hayatakuwa katika kile kiwango ambacho Mungu alikusudia. Huo ndio ukweli.

Ninayo changamoto kwako ndugu yangu unayesoma makala haya. Usikae kanisani mwako kijumla jumla tu baada ya kuokoka. Tafuta kuyajua mapenzi ya Mungu katika maisha yako ya wokovu. Tambua wewe ni kiungo gani katika mwili wa Kristo. Tambua kama wewe ni mkono, au mguu, au pua, au jicho, au sikio, na kadhalika. Huku ndio kutambua wito wako.

Baada ya kutambua wewe ni kiungo gani au wito wako, utumikie. Fanya kile ambacho Mungu anakutaka ukifanye, hata kama kiongozi wako au waumini wenzako watakuwa hawakuelewi. Kumbuka kuwa “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu” (Matendo 5:29, 4:19).Ukimtii Mungu kwa kuyafanya mapenzi yake, ndipo utakapobarikiwa mno.

Barnaba na Paulo walimtiii Mungu

Ninazungumzia swala la kumtii Mungu kwa habari ya wito kwa sababu yawezekana mwamini akafanya maamuzi mabaya katika eneo hili. Kwa mfano anaweza kufuata ushauri wa kiongozi wake wa kidini au waumini wenzake, ambapo sio lazima ushauri huo uwe katika mapenzi ya Mungu.

Kumtii Mungu kunaweza kukufanya utengane na waumini wenzako. Kunaweza kukufanya uhame kanisa au kikundi au huduma uliyopo kwa sasa, halafu uhamie sehemu nyingine. Mfano mzuri ni Paulo na Barnaba, ambao iliwabidi watengane na waumini wenzao katika mji fulani, halafu wakaenda kuhudumu sehemu nyingine kama Mungu alivyowaagiza.

Tunasoma katika Matendo 13;2 kuwa, “Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia”. Ujumbe huu ulitoka wakati Barnaba na Paulo wakiwa katika kanisa lililokuwa mji wa Antiokia. Ilibidi watengane na waumini wenzao, halafu waende kuhudumu katika miji ile ambayo walielekezwa na Bwana.

Wapo waumini waliopoteza mwelekeo

Leo hii wapo waumini walioacha kutumikia wito wao kwa sababu ya kuwasikiliza viongozi au ndugu na marafiki zao. Wapo wanaoona uzito wa kuhama sehemu fulani kwa sababu tu tayari wameshazoea sehemu hiyo na pengine tayari wana huduma fulani mahali hapo.

Linapokuja swala la wito, yawezekana mtu akaachana na wapendwa aliowazoea. au hali fulani ambayo inaonekana nzuri kwa wakati huo, ikabidi aende mahali pengine. Wakati mwingine hiyo sehemu nyingine inaonekana kama vile haina maslahi. Wito unahitaji kujikana nafsi na kuyafanya mapenzi ya Mungu kwa gharama yeyote ile (Marko 8:34).

Taji lako litategemea jinsi ulivyotumikia wito wako

Nafikiri kila mkristo mwenye matumaini ya kufika mbinguni anafahamu kuwa , baada ya kumaliza safari yake hapa duniani, atapewa taji ya uzima wa milele. Je, msomaji una habari kuwa uzuri wa taji yako itategemea jinsi ulivyotumikia wito wako hapa duniani?

Ukweli ni kuwa wakati wa kurithi uzima wa milele, sote hatutafanana. Wapo watakaong’ara kuliko wengine. Wapo watakaotukuzwa zaidi kuliko wenzao. Na kwa kiwango kikubwa, thawabu ya Mungu kwa wale watakaomaliza mwendo salama itategemea jinsi walivyotumika katika wito wao.

Je, haya ninayosema ni ya kweli? Je, yapo katika Biblia? Hebu tuangalie maandiko machache yanayoonesha jinsi tutakavyotofautiana wakati wa kurithi uzima wa milele. Kwahiyo msomaji naomba tufuatane kwa makini.
Tafuta dhahabu, usitafute manyasi

Tuanze na andiko la 1Wakorintho 3:11-15 linalosomeka hivi, “Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamanai, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto”.

Hapa mtume Paulo anatujulisha kuwa msingi wa ufalme wa Mungu ni Yesu Kristo na kwamba kila mwamini anatakiwa ajenge juu yake. Anazidi kutuasa kuwa, tuwe makini na kile kitu tunachojenga juu ya huo msingi.

Unaweza kujenga hapo dhahabu, fedha, miti, manyasi na kadhalika. Yaani unaweza kujenga kitu cha maana au kitu cha hovyo. Nafikiri sote tunakubaliana kuwa aliyejenga hapo dhahabu atakuwa amefanya jambo jema kuliko yule aliyejenga fedha au majani. Dhahabu ina thamani zaidi.

Siku ya hukumu tutatofautiana

Ujenzi unaojengwa na mwamini unamaanisha jinsi anavyomtumikia Mungu katika maisha yake ya hapa duniani. Ni jinsi anavyoutumikia wito wake baada ya kuokoka. Anaweza kuutumikia vizuri au vibaya; au asiutumikie kabisa.

Maneno ‘Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani’ yanazungumzia sikun yan hukumu. Yanaonesha kuwa siku ya hukumu kila mwamini atapimwa ni jinsi gani alivyomtumikia Mungu katika wito wake. Siku hiyo wengine watapata thawabu na wengine wataambulia hasara.

Katika 1Wakorintho 3:8 Paulo anazungumza maneno yafuatayo, “Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe”

Hapa mtume Paulo anazungumzia utumishi wake na ule wa Apolo. Kwamba ingawa wote wawili walikuwa ni ndugu katika Bwana, lakini kila mmoja alikuwa na majukumu yake au wito wake. Vile vile kila mmoja wao atapata thawabu kulingana na jinsi alivyotumika ndani ya wito huo. Yaani watatofautiana wakati wa kuvishwa taji ya uzima wa milele.

Usikae bure, mtumikie Mungu

Mfano mwingine unaoonyesha jinsi watu wa Mungu tutakavyotofautiana wakati wa hukumu ya mwisho ni ule unaohusu kabaila aliyewapa watumwa wake fedha, ili wakazifanyie biashara. Huu unapatika katika injili ya Luka 19:11-26.

Kwa kifupi ni kuwa tajiri mmoja alisafiri, akawaachia watumwa wake fedha, ili wakazifanyie biashara na vile vile wapate faida. Kila mmoja wao alipewa kiasi kile kile cha fedha, yaani fungu moja.

Kitendo cha kupewa fedha ili wakazifanyie biashara ni sawa na kukabidhiwa majukumu. Ni kama vile Mungu anavyotupatia vipawa au karama, ili tukavitumie katika wito wetu. Sio tuvikalie kama yule mtumwa mwovu, ambaye alikalia fungu lake, badala ya kulifanyia kazi ((Luka 19:20-23).

Katika mfano huu tunaweza kuona kuwa yule tajiri aliporudi safarini, aliwazawadia wale watumwa kulingana na jinsi walivyozalisha faida. Yupo aliyepewa mamlaka juu ya miji kumi na mwingine juu ya miji mitano. Yule ambaye hakuzalisha, aliambulia patupu.

Hata katika ufalme wa Mungu ndivyo itakavyokuwa. Sote hatutalingana. La hasha. Wapo watakaong’aa kuliko wengine, kulingana na jinsi walivyomtumikia Mungu. Kulingana na jinsi walivyotumikia wito wao.
Kwanini Mungu huturithisha baraka?

Hivi msomaji umewahi kujiuliza ni kwanini Mungu huwarithisha wanadamu baraka, ziwe za rohoni au za mwilini? Ninapokaribia mwisho wa makala haya, naona ni bora nitaje sababu angalao mbili zinazomfanya Mungu aturithishe baraka sisi watu wake.

Sababu ya kwanza ni kwamba, vyote alivyoumba Mungu ni kwa ajili ya mwanadamu. Dunia na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana (Zaburi 24:1). Lakini vitu hivyo vipo kwa ajili yako wewe na mimi msomaji wangu. Havipo kwa ajili ya Mungu. Read More......

Watu wa Mungu waliofanikiwa ni wachache

Ninakubali kunaweza kuwepo walokole wachache waliofanikiwa kimaisha, lakini si chochote wala si lolote, ukilinganisha na utajiri au mafanikio ya watu ambao hawajaokoka. Nataka tujiulize tena; kwanini hali iko hivi?

Naomba sote tutafakari. Kwanini watu wa Mungu wanaonekana kama vile hawana kitu wakati dunia na vyote viijazavyo ni mali ya Baba yao wa mbinguni? (Zaburi 24:1). Biblia inatuambia kuwa Mungu aliweka vitu vyote chini ya miguu ya mwanawe Yesu kwa ajili ya kanisa au watu waliookoka (Waefeso 1:22).

Sasa kama sisi tuliookoka tumeahidiwa baraka nyingi namna hiyo, inakuwaje hatuonekani kama watu waliobarikiwa? Tatizo liko wapi? Je, Mungu ni mwongo anapoahidi kuturithisha baraka au kuna mahali ambapo sisi watu wake tumekosea?

Katika makala haya nitajaribu kueleza sababu takribani nne, ambazo binafsi ninaamini ndizo zinazowafanya waumini wengi washindwe kurithi baraka kutoka kwa Mungu wao. Kwahiyo msomaji naomba tufuatane kwa makini katika eneo hili.

Kutokujua haki zetu
Moja ya mambo ambayo yanawafanya watu wa Mungu wasiweze kurithi baraka ni kutotambua haki zao. Ni ujinga wa kutotambua ni vitu gani na kwa kiwango gani wanaweza kurithi au kupokea kutoka kwa Mungu. Na kwa sababu hiyo wanashindwa kuomba au kudai haki hizo.

Katika Isaya 43:26 Mungu anatuambia sisi watu wake hivi, “Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako”. Hapa tunahimizwa tudai haki zetu kutoka kwa Mungu. Sasa utawezaje kudai haki ambayo huifahamu? Haiwezekani kabisa. Na hili ndio tatizo linalowakumba baadhi ya watu waliookoka. Hawajui haki yao ya kubarikiwa.

Katika sehemu ya kwanza ya makala haya, iliyohusu urithi kutoka kwa mwanadamu mmoja kwenda kwa mawanadamu mwingine, nilisema kuwa moja ya mambo yanayowafanya warithi halali wa marehemu wasipate mali iliyoachwa ni kutotambua haki yao na taratibu za kupata haki hiyo.

Ni ajabu kuwa hata tunapoangalia urithi kutoka kwa Mungu, hali ni hiyo hiyo. Wapo waumni wasiojua haki zao za kurithi baraka na mambo ya kufanya au wajibu wao, ili waweze kupewa haki hizo. Na kwa sababu hiyo wanaendelea kuwa maskini wa vitu vya rohoni na vya mwilini.

Tambua haki zako
Hebu tuanze kwa kuangalia baraka za rohoni. Tayari tumeshaona kuwa ujazo wa Roho Mtakatifu ni ahadi au haki ya kila mtu aliyeokoka. Cha ajabu makanisani mwetu wapo wakristo waliookoka, lakini bado hawajapokea ahadi ya kujazwa Roho Mtakatifu.

Tatizo la wakristo kama hawa sio kwamba hawataki kujazwa. La hasha. Wapo wanaodhani kuwa jambo hili halipo kabisa kwa kanisa la leo. Wanadhani hayo ni mambo yaliyolihusu kanisa la mwanzo tu, lile kanisa la enzi za Matendo ya Mitume.

Wapo wakristo wanaodhani kuwa ujazo wa Roho Mtakatifu upo, ila ni kwa ajili ya watu maalumu tu. Wao wanafikiri kwamba hawahusiki kabisa na jambo hili. Maskini watu hawa, yaani wamekosea kweli. Kujazwa ni haki ya kila mwamini (Mdo 2:17-18). Huo ndio ukweli.

Kwa sababu ya kutatambua haki ya kila mwamini kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu, yapo makanisa yasiyozungumzia au kufundisha jambo hili katikati ya makusanyiko yao. Unaweza kukutana na waumini wanaodai kuwa wameokoka, lakini ukizungumzia habari ya ujazo wa Roho Mtakatifu au kunena kwa lugha, hawakuelewi kabisa.

Tatizo la ujinga ni la miaka mingi
Hebu tugeukie Biblia tuone jinsi tatizo hili lilivyojitokeza katika kanisa la mwanzo. Tunasoma katika Matendo ya Mitume 19-1-2 kuwa, “Ikawa, Apollo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia”.

Msomaji unaweza kuona jinsi hawa waumini walivyokuwa wameokoka, lakini hawakujua kama kuna kitu kama kujazwa Roho Mtakatifu? Vile vile hawakujua ubatizo sahihi wa Kibiblia (Matendo 19:3-5). Tatizo kama hili laweza kuwepo katika makanisa ya leo. Usitegemee waumini walio chini ya kanisa au huduma ya namna hii waweze kupokea ahadi ya Roho Mtakatifu.

Kinachofurahisha katika lile kanisa alilokutana nalo Paulo ni kwamba, aliwafundisha ubatizo sahihi na habari ya ujazo wa Roho Mtakatifu. Biblia inatuambia kuwa, “Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri” (Matendo 19:6).

Ni haki yako kumpokea Roho Mtakatifu
Yawezekana wewe unayesoma makala haya umeokoka, lakini hujajazwa Roho Mtakatifu. Yawezekana jambo hili halitajwi wala halifundishwi hapo mahali unaposali. Pengine utendaji wa huyu Roho wa Mungu au miujiza haionekani kabisa hapo kanisani mwako.

Sikiliza nikwambie kitu ndugu yangu. Ni haki yako kupokea ahadi au baraka ya Roho Mtakatifu. Ni haki yako kujazwa. Hili lipo wazi kabisa, “Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie” (Matendo 2:39).

Karama na vipawa ni sehemu ya kanisa
Tunapokuja katika karama na vipawa mbalilmbali tunakuta kuwa hali ndiyo ili ile ya ujinga wa kutofahamu. Wapo waumini wasiojua kuwa mambo haya yapo na kwamba hata wao wanaweza kupokea baraka hizi. Kwamba wanaweza kuwa na karama au kipawa fulani.

Yapo makanisa au waumini wasiojua kuwa karama na vipawa ni nyenzo muhimu sana katika kuifanya kazi ya Bwana, na kwamba vitu hivi vinatakiwa vionekane katika makusanyiko ya watu wa Mungu. Kwa sababu ya kutofahamu, makanisa yao na wao binafsi wanadumaa kiroho. Hawaoni ishara na maajabu katika yao Marko 16:17, Matendo 14:3).

Usiringe na karama au kipawa ulicho nacho
Baadhi ya waumini au watumishi waliojaliwa kuwa na karama au kipawa fulani, wamevitaifisha. Kwanza kabisa wapo wanaoringa navyo. Wanajikweza. Halafu wapo wengine ambao hawawaambii wenzao jambo hili. Hawawafundishi wala hawatumii baraka hizi kwa manufaa ya waumini wenzao.

Kuhusu utendaji wa karama tunaambiwa hivi katika 1Wakorintho 12:4-11, “Basi pana tofauti ya karama, bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti ya huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye”.

Karama hutoka kwa Mungu
Msomaji nnachotaka uzingatie katika mistari hii niliyonukuu ni kuwa, chanzo cha karama ni Mungu mwenyewe. Mstari wa 7 unasema ‘lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana’. Lengo la karama ni kushirikishana na kusaidiana. Sio kuringiana au kunyanyasana nazo, kama baadhi ya watumishi wa Mungu wanavyofanya katika siku za leo.

Mstari wa 11 unamalizia kwa kusema ‘lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye”. Yaani Roho Mtakatifu ndiye mmiliki na msimamizi wa matumizi ya karama, na kwamba huzigawa kama apendavyo na sio kama mwamini anavyotaka.

Hali ilivyo katika makanisa mengi duniani ni kwamba, kuna waumini au watumishi ambao wanatamani sana kama wangekuwa na karama au kipawa fulani. Wengine wakivikosa, hulazimisha mambo. Unakuta mtu anajiita mtume na nabii, au anaingia katika huduma ya uchungaji au uinjilisti, wakati hana kibali cha Roho Mtakatifu. Hili ni kosa kubwa mno.

Kutokujua wajibu au masharti au taratibu au kanuni za kubarikiwa
Tatizo la pili linalolikabili kanisa la leo, na kwa sababu hiyo wanashindwa kubarikiwa, ni kutokujua kwamba kila haki imeambatana na masharti au wajibu. Hali ilivyo sasa hivi ni kuwa, walokole wengi wanakimbilia kudai haki ya kubarikiwa kabla ya kutimiza masharti, taratibu na kanuni zilizowekwa na Mungu kabla hajatoa (release) baraka hizo.

Sasa hivi tunashuhudia wimbi la waumini ambao nitawaita wakimbizi au wahamiaji. Hawa ni watu waliookoka vizuri kabisa, lakini wanahama kutoka kanisa moja la kilokole na kuhamia kwenye kanisa lingine la kilokole.

Ni waumini wanaohama kutoka kwa mchungaji huyu, au mtume huyu, au nabii huyu, au huduma hii, na kuhamia kwenye kikundi kingine cha kilokole. Swali la kujiuliza ni kwanini tuna wakimbizi au wahamiaji wa kikristo? Ni kwanini tuna walokole wanaohamahama ovyo?

Kuna uhamaji unaokubalika
Ninatambua kuwa kuna uhamaji ambao una sababu za msingi zinazokubalika. Uhamaji huu ni pamoja na waumini wanaotoka katika makanisa yasiyohubiri au yanayopinga dhana ya kuokoka. Ni pamoja na waumini wanaohamishwa kikazi au wanaohamia kwenye makazi mapya, na kwa sababu hiyo wanalazimika kutafuta kanisa la kilokole lililo karibu na mahali walipohamia.

Sasa wakimbizi ninaotaka kuzungumzia sio waumini wanaohama kwa sababu zinazokubalika. Hapana. Ni walokole wanaohama kwa sababu ya kutodhirika na mahali walipokuwa. Unakuta wala hawajafukuzwa, wala hakuna aliyewaudhi, lakini wanahama.

Hakuna kubarikiwa kabla ya kutimiza wajibu
Sikiliza msomaji. Moja ya sababu kubwa inayowafanya walokole wahame ovyo ovyo ni kiu ya kutafuta baraka za Mungu. Wanakaa katika kanisa moja au huduma fulani kwa muda, halafu wanaona kama vile hawabarikiwi. Na hapa nina maana kuwa hawaoni baraka za mwilini.

Ukizidi kuchunguza kiini cha uhamaji ninaozungumzia utakuta kuwa, tatizo kubwa ni waumini hao kushindwa kutimiza wajibu wao au masharti yanayoambatana na baraka wanazohitaji au walizoahidiwa na Mungu kupitia neno lake..

Hali ilivyo kwa sasa ni kwamba, walokole wengi wanataka au wanadai haki ya kubarikiwa, lakini hawataki kutimiza wajibu wao. Hawataki kumtumikia Mungu; hawataki kutoa sadaka au wanatoa kidogo sana; hawafanyi kazi, na kadhalika. Hili ndio tatizo kubwa la kanisa la leo.

Nimeshasema huko nyuma, na sasa narudia tena. Hakuna baraka au ahadi ya Mungu isiyo na masharti. Yapo mambo ambayo mwamini anatakiwa ayatimize, ndipo aweze kubarikiwa. Vinginevyo atabaki kuwa mkimbizi wa baraka katika maisha yake yote ya wokovu.

Mwamini mkimbizi asipokuwa makini, Yesu atakaporudi mara ya pili anaweza kumkuta barabarani akiwa bado anahama kutoka sehemu moja ya kilokole, akielekea sehemu nyingine. Mtu kama huyu asidhani kuwa anaweza kuziona baraka za Mungu. Ni mahangaiko matupu.

Baraka zinakuja; hazifuatwi
Ngoja nimalizie kipengele hiki kwa kusema hivi. Baraka hazifuatwi; hazitafutwi makanisani au kwenye huduma. Baraka hazitoki kwa mchungaji, mtume au nabii fulani. Hapana. Baraka zitakufuata mahali popote pale utakapokuwa, ali mradi umetimiza mashari au wajibu wako unaohusiana na baraka hizo.

Ninakubali kuwa makanisani au kwenye huduma tunaweza kufundishwa na wachungaji wetu, au hao mitume na manabii, namna ya kubarikiwa. Lakini wao sio wanaozigawa. Wao wanapaswa kutuelezea baraka hizo na masharti yake. Baada ya kuyatimiza, ndipo tunaweza kubarikiwa mahali popote pale tutakapokuwa.
Utabarikiwa popote pale utakapokuwa

Msomaji nakuomba usome tena kwa makini Kumbukumbu la Torati 28:1-14, ambapo zimeorodheshwa baraka tele, pamoja na masharti yake. Mstari wa 2 unasema kuwa, “na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako”

Unaweza kuona kuwa baraka zitakujilia, au zitakufuta (shall come upon you). Sio wewe unakimbizana nazo kutoka kanisa hili hadi jingine, au mtume huyu hadi yule, na kadhalika. Ndio maana Biblia inasema kuwa ‘utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani’ (mstari wa 3).Vile vile ‘utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo” (mstari wa 6).

Kinachotakiwa kwako ni kuisikia sauti ya Mungu. Sio unahama bila hata kuwasiliana Naye, ili akuruhusu. Matokeo yake unabaki kuwa mkimbizi. Na sote nadhani tunafahamu hali za wakimbizi popote pale walipo. Kwa kweli sio nzuri. Hali zao ni mbaya. Nami nisingetaka hali yako iwe mbaya. Read More......

Hata baraka za mwilini zina masharti



Hata baraka za mwilini zina masharti yake. Kwanza kabisa, kama zilivyo za rohoni, nazo zina kusubiri kwa muda mrefu. Haziji chapuchapu. La hasha. Vile vile kiwango cha baraka hizi kinategemea aina na uzito wa masharti. Masharti magumu ni kiashiria kuwa baraka zitakazopatikana ni za hali ya juu.

Tuseme mwamini anataka awe na mali mengi. Moja ya masharti au wajibu atakaopaswa kutimiza ni kutoa sadaka. Lakini sio utoaji wa kawaida tu. La hasha. Ni lazima awe mtoaji mzuri. Mtoaji wa kilicho chema na kwa wingi pia.

Katika 2Wakorintho 9:6 mtume Paulo anaandika hivi, “Lakini nasema neno hili, Apandaye hapa atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu’. Hapa tunaona kuwa mtu akitaka kuvuna, kwanza ni lazima apande mbegu. Hilo ndio sharti la kwanza. Lakini kama anataka mavuno mengi, ni lazima vile vile apande mbegu kwa wingi. Vinginevyo atavuna kidogo.

Kwa kumalizia kipengele hiki cha wakati wa kurithi baraka, naomba nisisitize tena kwamba, mwamini hawezi kujua kwa hakika ni lini atabarikiwa na Mungu. Hata baada ya kutimiza masharti au wajibu wake, bado anatakiwa asubiri wakati uliopangwa na Mungu. Anatakiwa awe na subira au uvumilivu, hadi hapo BWANA atakapomkumbuka.

Kwanini wakristo wengi tunashindwa kurithi baraka kutoka kwa Mungu?
Msomaji haya ninayotaka kuzungumzia sasa ni mawazo au mtazamo wangu. Yanaweza yasiwe sahihi, na kama nitakuwa nimekosea, naomba nisamehewe. Lakini nitasema kile ninachokiona katika makanisa, huduma, vikundi mbalimbali vya kilokole na waumini binafsi.

Ninaposoma Biblia kuhusu baraka zilizoahidiwa kwa watu wa Mungu, halafu nikilinganisha na maisha ya walokole wengi ninaokutana nao, naona kama vile bado kabisa sisi tuliookoka hatujabarikiwa au hatujarithi baraka za Mungu.

Kunaweza kukawa na mafanikio kidogo katika eneo la baraka za rohoni, lakini bado sidhani kama ni katika vile viwango vilivyoahidiwa na Mungu. Nakubali kuwa wapo waumini wengi tu waliopokea ahadi ya kujazwa Roho Mtakatifu. Vile vile karama na vipawa mbalimbali vinaonekana katikati ya jamii ya watu waliookoka. Lakini udhihiriko wa baraka hizi haupo katika viwango vilivyokusudiwa na Mungu.

Tunapogeukia baraka za mwilini, napo hali ni ile ile ya wasiwasi. Tena naona kama vile huku ndio kwenye matatizo zaidi, ukilinganisha na baraka za rohoni. Yaani unapowatazama watu wengi waliookoka, hawafanani kabisa na watu waliobarikiwa. Wengi bado ni jua kali au walala hoi. Swali la kujiuliza ni kwanini hali iko hivi?

Watu waliookoka wameahidiwa baraka tele

Msomaji hebu tutafakari kidogo. Mungu anasema katika Mithali 8:18 kwamba, “Utajiri na heshima ziko kwangu, naam utajiri udumuo, na haki pia”. Halafu katika Mithali 8:20-21 anasema kwa uhakika kabisa kwamba, “Natembea katika njia ya haki, katikati ya mapito ya hukumu, niwarithishe mali wale wanipendao, tena nipate kuzijaza hazina zao?”

Tunapoliangalia Agano Jipya napo tunakuta kuwa ahadi za kubarikiwa ni nyingi mno. Kwa mfano katika 2Wakorintho 9:10-11 imeandikwa kuwa, “Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu; mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukurani kwa kazi yetu”.

Mistari niliyonukuu inaonyesha ahadi ya utajiri kwa watu wa Mungu. Lakini hebu tujiulize, je, hali halisi ndivyo ilivyo? Je utajiri wa dunia hii upo mikononi mwa nani kwa sasa? Mimi naona kama vile upo kwa watu ambao hawajaokoka; watu ambao hawamjui Mungu kabisa. Read More......

Ni wakati gani wa kurithi baraka au ahadi za Mungu?

Katika sehemu ya kwanza ya mada hii nilisema kuwa, mara nyingi urithi kutoka kwa mwanadamu mmoja kwenda kwa mwanadamu mwingine unahusisha kifo. Kwamba ni lazima mmiliki wa kwanza wa mali inayokusudiwa kurithiwa afe, ndipo kitendo cha kurithi kifanyike.

Tunapogeukia urithi kutoka kwa Mungu kwenda kwa wanadamu tunakuta mambo ni tofauti kabisa. Sote tunafahamu kuwa Mungu hafi. Yeye alikuwepo tangu milele, na atadumu milele. Sasa kama hivyo ndivyo, swali la kujiuliza ni je, upi ndio wakati sahihi wa kurithi au kupokea ahadi kutoka kwa BWANA?

Mungu huwa hasemi siku kamili ya kukubariki

Ukweli ni kuwa, ukiichunguza Biblia kwa makini, utagundua kwamba Mungu huwa hasemi kwa yakini ni wakati gani atakapombariki au kumtimizia mtu ahadi aliyomwahidi. Hata kama mwamini ameiskikia sauti ya Mungu wazi wazi, ni mara chache sana ataambiwa muda kamili (exact time) wa kutimiziwa kile alichoahidiwa.

Tuseme umemtolea Mungu sadaka. Ni kweli Biblia inasema ukitoa utabarikiwa. Lakini huwezi kujua kama utabarikiwa baada ya mwezi mmoja, au mwaka mmoja, au miaka mitano au kumi. La hasha. Itakubidi usubiri hadi hapo majira au wakati wa BWANA utakapotimia, ndipo upokee mbaraka wako. Hii ndiyo hali halisi.

Jambo hili la kusuburi linahusu aina zote za baraka, yaani za rohoni na za mwilini. Tuchukulie mfano wa ujazo wa Roho Mtakatifu, ambao Biblia inaonyesha kuwa ni ahadi ya Mungu kwa watu waliookoka (Mdo 1:4, Mdo 2:14-18).

Baada ya kuokoka, mwamini hawezi kujua ni lini atajazwa Roho Mtakatifu. Wapo wanaojazwa siku hiyo hiyo waliyookoka. Wengine ni baada ya miezi au miaka kadhaa. Halafu wapo waliosubiri kwa muda mrefu mpaka wakakata tamaa kabisa. Wajibu wa mwamini ni kusubiri hadi hapo Mungu atakapoona vema kumjaza. Sio kukata tamaa.

Karama na vipawa hujitokeza baada ya muda mrefu

Linapokuja swala la karama, huwa hazijidhihirishi mara moja. Karama za neno la hekima, au maarifa, au uponyaji, au miujiza na kadhalika, huwa havionekani mara tu baada ya kuokoka. Mwamini anatakiwa adumu katika wokovu, ndipo baada ya muda vitu hivi vitaanza kujitokeza katika maisha yake.

Vipawa navyo huwa havijitokezi mara tu mtu anapookoka. Hapana. Mwamini hawezi kuokoka leo na kesho akaanza kusema yeye ni mtume au nabii au mchungaji na kadhalika. Ukiona hivyo ujue kuna walakini. Haya mambo huanza kujitokeza baada ya kudumu katika wokovu kwa muda wa kutosha.

Mitume, manabii, wachungaji, au wainjilisti tunaowaona leo hii wakinguruma katika madhabahu mbalimbali, hawakuanza huduma zao mara tu baada ya kuokoka. La hasha. Wengi walianza kama washirika wa kawaida tu makanisani mwao. Baadaye kabisa ndipo vipawa vyao vikaanza kuibuka.

Kwanini wakati wa kurithi baraka haujulikani?

Pengine msomaji unaanza kujiuliza ‘mbona wakati wa kurithi baraka kutoka kwa Mungu hauko wazi?’ Mbona Mungu huwa hasemi waziwazi wakati au siku atakayotubariki? Mbona mara nyingi baraka zenyewe zinakuja kama kwa kushitukiza? Nitajaribu kuleza baadhi ya sababu.

Ukweli ni kuwa mambo ya Mungu yana kanuni au taratibu zake. Hayajitokezi kienyeji au shaghalabaghala. La hasha. Yana mkondo wake. Na moja ya mkondo huo ni kanuni ya imani. Lakini kwa vipi haswa?

Ili tupate kuielewa kanuni ya imani, hebu tusome maana yake kama inavyojitokeza ndani ya Biblia. Katika Waebrania 11:1 tunaambiwa kuwa, “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”.

Haya mambo yanayotarajiwa, lakini bado hayajaonekana ni nini haswa? Ukweli ni kuwa, hizi ni baraka au ahadi mbalimbali, ambazo Mungu amewaahidi wanawe, yaani wakristo waliookoka. Ni ule urithi ambao Biblia inatamka wazi wazi kuwa Mungu atawapa wale wote watakaomwamini mwanawe Yesu Kristo. Haya ndiyo mambo ambayo yanatakiwa yakitokeze katika maisha ya mwamini.

Mungu hawezi kutoa ahadi ya uongo

Wajibu wa mwamini ili baraka za Mungu zijitokeze kwake ni kuamini kuwa ahadi zenyewe ni za kweli. Ni kuamini kuwa, “Mungu si mtu, aseme uongo; wala si mwanadamu, ajute; iwapo amesema hatalitenda? Iwapo amenena hatalifikiliza?’ (Hesabu 23:19).

Baada ya kuamini kuwa ahadi za Mungu ni za kweli, mwamini anatakiwa awe mvumilivu. Anatakiwa awe na subira, akitumaini kuwa kuna siku ahadi ya BWANA itatimia katika maisha yake, japo haijui siku hiyo. Huku ndiko kuiweka kanuni ya imani katika matendo.

Kwa kumalizia maelezo ya utendaji wa kanuni ya imani katika maisha ya mwamini naomba tusome Waebrania 6:17-18 ambapo tunaambiwa, “Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati; ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu.”

Kinachozungumzwa katika andiko hili ni kuwa Mungu akikuahidi kitu hawezi kubadilisha mawazo kirahisi. Hii ndiyo faraja yetu sisi tuliookoka. Kwamba tukiamini kile ambacho Mungu ametamka juu ya maisha yetu, basi tuishi kwa matumainin kwamba ipo siku kitu hicho kitajitokeza maishani mwetu, hata kama hatuijui siku hiyo.

Walio wachanga hawawezi kurithi

Pamoja na kutakiwa kuenenda kwa imani, vile vile yapo masharti au mambo mengine ambayo mwamini anatakiwa ayatimize, ndipo baadaye aweze kurithi baraka kutoka kwa Mungu. Tayari tumeshaona kuwa moja ya masharti hayo ni kukubali kuokoka. Sharti lingine ni kukua na kukomaa katika wokovu. Nitaeleza kwa kifupi.

Katika sehemu ya kwanza ya mada hii tuliona kuwa, mzazi hawezi kumpa mtoto mdogo urithi, hata kama ni stahili yake. Tulisoma andiko la Wagalatia 4:1 linalosema, “lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wowote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote”.

Kinachozungumzwa hapa ni kuwa, mrithi hawezi kukabidhiwa mali yake wakati akiwa bado ni mtoto. Kwanza anatakiwa akue mpaka awe mtu mzima, ndipo aweze kukabidhiwa kilicho chake. Kwahiyo wakati akisubiri akue, anakuwa mtu asiye na kitu, japo ni tajiri.

Tunarithi baraka baada ya kukua kiroho

Nafikiri msomaji utakubaliana nami kuwa hakuna mzazi mwenye akili timamu atakayekubali kijana wake aoe, au atakayemwoza binti yake wakati bado ni mdogo. Nadhani wengi wetu tutakuwa tunafahamu jinsi serikali yetu inavyopiga vita tabia ya kuwaoza mabinti wenye umri mdogo. Wanatakiwa kwanza wakue na kukomaa miili na akili zao, ndipo waolewe.

Ni ajabu kwamba hata tunapogeukia urithi kutoka kwa Mungu, tunaweza kuona kuwa kuna kufanana na jinsi sisi wanadamu tunavyorithisha. Watoto wachanga kiroho hawawezi kurithishwa baraka kama vile karama au vipawa. Ni lazima kwanza wakue na kukomaa katika maswala ya ufalme wa Mungu, ndipo wanaweza kupokea baraka kama hizi.

Moja ya sababu inayomfanya Mungu asigawe baraka zake mapema ni kumpa mwamini nafasi ya kukua. Ni kumpa nafasi ya kulielewa vema neno la Mungu, kanuni na utendaji wake. Baada ya hapo ndipo anaweza kupewa baraka mbalimbali. Vinginevyo mwamini mchanga kiroho ni sawa na mtoto mdogo kimwili. Hawezi kurithishwa baraka kwa sababu zinaweza kumletea matatizo.

Tunarithi uzima wa milele baada ya kufa

Baraka kama ya uzima wa milele inarithiwa baada ya mwamini kufariki. Ni kweli kabisa baada ya kuokoka tunaamini kwamba tutafika mbinguni. Lakini jambo hili litakuwa kweli au dhahari baada ya kuondoka duniani kwa njia ya kifo. Kabla ya hapo, mtu aliyekiri wokovu anaweza kukwama njiani. Anaweza kushindwa kuvumilia hadi mwisho wa safari. Na kwa sababu hiyo asiweze kurithi uzima wa milele.

Mtume Paulo anaandika katika Wafilipi 3:12-14 kuwa, “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamililifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yalio nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu”.

Tukaze mwendo
Paulo alipoandika maneno haya alikuwa tayari ameokoka. Lakini vile vile alitambua kuwa bado hajaingia katika uzima wa milele. Alitambua kwamba bado yupo safarini na kwamba anapaswa kujitahidi. Vinginevyo anaweza asimalize mwendo. Anaweza asifike hatua ya kurithi uzima wa milele.

Yesu alisema katika Mathayo 24:13 kuwa,”Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka”. Mwisho unaozungumziwa hapa unaweza kuwa ni mwisho wa maisha ya mwamini hapa duniani, yaani kifo. Au ni wakati wa kunyakuliwa kwa kanisa wakati Yesu atakaporudi duniani mara ya pili.

Mwamini atakapofikia mwisho wake salama, ndipo atakuwa na uhakika wa kurithi uzima wa milele. Kwahiyo tunatakiwa tukaze mwendo kama Paulo. Vingine safari ya mbinguni inaweza kuwa ni ndoto za alinacha. Tunaweza tusifike huko, japo tuanasema tumeokoka. Read More......

URITHI: Wana wa Mungu na watoto wa Mungu

Tunapokuja katika maswala ya Kimungu tunakuta kuwa, napo kuna tofauti kati ya mwana na mtoto. Mwana wa Mungu ni mtu yeyote aliyezaliwa mara ya pili. Ni mkristo aliyeokoka. Huyu ndiye anayestahili kurithi baraka kutoka kwa Mungu. Ndiye anayestahili kubarikiwa.

Mtu ambaye hajaokoka ni mtoto wa Mungu. Huyu hana tofauti na mtoto wa kambo, ambaye tuliona kuwa hastahili kurithi chochote kutoka kwa baba au mama wa kambo, labda katika mazingira malumu. Ndio kusema kuwa, wewe ambaye hujaokoka, hustahili kurithi chochote kutoka kwa Mungu.

Wewe ambaye hujaokoka unaweza kuwa na mafanikio makubwa katika maisha yako, lakini hizo sio baraka za Mungu. Ukijichunguza kwa makini utagundua kuwa, hivyo vitu ulivyo navyo havina uhusianao wa moja kwa moja na Mungu. Havikupatikana kwa msaada wake.

Mafanikio uliyo nayo yanaweza kuwa yametokana na nguvu au jasho lako binafsi, lakini sio kwa kumwomba au kumtumainia Mungu. Na pengine ulienda kwa waganga wa kienyeji, wakakupa dawa ya kupata mali, au mtoto, au cheo kazini, na kadhalika. Huko sio kubarikiwa, hata kama jamii itakuona kuwa umefanikiwa kimaisha.

Unapookoka unabadilishwa kutoka ‘mtoto’ na kupewa cheo cha kuitwa ‘mwana’.
Ili swala la kuwa mwana lieleweke vizuri, hebu tusome maandiko machache. Katika Wagalatia 3:26 imeandikwa hivi, “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu”

Wanaozungumziwa hapa ni watu waliomwamimi Yesu. Ni watu waliookoka. Katika Warumi imeandikwa kuwa, “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba”.

Hawa wanaosemwa kwamba wanaongozwa na Roho wa Mungu ni wakristo waliookoka. Hao ndio waliopokea roho ya kufanywa wana na Mungu ni baba yao. Yaani wamebadiliswa kutoka katika hali ya kuitwa watoto na sasa wanapewa cheo cha kuitwa wana wa Mungu.

Katika Waefeso 1:5 imeandikwa kuwa, “Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake”. Hapa napo tunaona kuwa kuna watu ambao Mungu aliwachagua, ili awafanye wanawe. Hawa sio wengine bali ni watu waliomwamini Yesu. Ni watu waliookoka.

Tunaposoma 1Yohana 3:1 tunakutana na maneno haya, “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuiwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo.” Andiko hili linatuonyesha kuwa watu waliookoka wanaitwa wana wa Mungu. Hawaitwi watoto wa Mungu.


Tafsiri za Biblia zinatofautiana
Ninapojaribu kueleza tofauti ya mtoto na mwana, naomba nitoe tahadhari kidogo. Natambua kuwa Biblia inachanganya maneno haya mawili. Kwa mfano katika Yohana 1:12 imeandikwa kuwa, “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake”.

Ukweli ni ni kuwa, kama tungetumia Kiswahili fasaha, neno ambalo lingepaswa kutumiwa hapa ni ‘kufanyika wana wa Mungu’ na sio ‘kufanyika watoto wa Mungu’ Tatizo la kuchanganya mtoto na mwana lipo hata katika Biblia za Kiingereza.

Unakuta neno linalotumia zaidi ni ‘child’ au ‘children’ Lakini baadhi ya Biblia zinatumia neno ‘son’ au ‘sons and daughters of God’ Na ukweli ni kuwa hata katika lugha ya Kiingereza kuna tofauti kati ya ‘child’ na ‘son’ au ‘daughter’.

Neno ‘son’ au ‘daughter’ lina maana ya mtoto ambaye umemzaa. Yule ambaye hujamzaa anaitwa ‘a child’. Ndio maana utasikia Mwingereza mzuri akisema ‘my son or my daughter’. Hawasemi ‘my child’. Hicho sio Kiingereza safi. Ni sawa na kusema ‘mtoto wangu’ badala ya ‘mwanangu’.

Yesu ni ‘Mwana wa Mungu’, sio mtoto wa Mungu
Kwa kumalizia kipengele hiki cha tofauti kati ya mwana na mtoto, hebu tumwangalie Bwana wetu Yesu Kristo. Sote tunajua kuwa huyu anaitwa Mwana wa Mungu. Anaitwa hivyo kwa sababu amezaliwa na Mungu. Kuzaliwa huku kumefanyika kwa njia au kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Sio kwamba Maria alilala na Mungu (Mathayo 1:18-20).

Ukiisoma Biblia yote huwezi kukuta mahali wanamtaja Yesu kama mtoto wa Mungu. Kila mahali wanamwita Mwana wa Mungu. Hata katika Biblia za Kiingereza hawamwiti ‘child of God’. La hasha. Wanamtaja kuwa ni ‘Son of God’. Hii ndio lugha fasaha ya kumtaja Yesu.

Mwana ndiye mrithi
Baada ya kujadili kwa kina tofauti kati ya mwana na mtoto, hebu sasa tuendelee kuangalia jinsi ambavyo Biblia inaonyesha kwa mwana ndiye anayestahili kurithi. Tuanze na Bwana Yesu mwenyewe.

Tunaposoma Waefeso 1:20-22 tunaweza kuona uweza wa Mungu “aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa.”

Hili andiko linaonyesha jinsi ambayo Mungu alivyomtukuza sana mwanawe Yesu Kristo, baada ya kumfufua katika wafu, akaweka kila kitu chini ya miguu yake. Tunaposoma Waebrania 1:1-4 tunaweza kuona kuwa Yesu amefanywa kuwa mrithi wa vyote vilivyombwa na Mungu.

Yesu Kristo anakuwa mrithi wa vyote kwa sababu yeye ni mwana pekee wa Baba yake (Yohana 1:14). Pengine angekuwa na wadogo zake waliozaliwa na baba mmoja, wangegawana urithi. Lakini hivyo sivyo ilivyo.

Wale wadogo au ndugu zake wengine (Luka 8:19-21), baba yao ni Yusufu na sio Mungu. Yesu ni mzaliwa wa kwanza na wa mwisho kwa Baba yake (Waebrania 1:6-8). Wale wengine ni kama watoto wa kambo, ambao kama tulivyoona huko nyuma, hawawezi kurithi, labda katika mazingira maalumu.
Kanisa ndio wanaostahili kurithi baraka za Mungu

Baada ya kuonyesha kuwa kuna tofauti kati ya mtoto na mwana, na kwamba Yesu ndio aliyerithi, sasa naweza kusema kwa uhakika kabisa kuwa kanisa ndio wanaostahili kurithi baraka au ahadi za Mungu. Kanisa ni watu waliookoka. Hao tumeshaona kuwa ndio wanaoitwa wana. Na kwa sababu hiyo, wao ndio warithi.

Ukisoma Waefeso 1:15-23 unaweza kuona jinsi utaratibu mzima wa urithi kwa kanisa au watu waliookoka unavyokuwa. Mstari wa 22 na 23 unatuambia kuwa Mungu “akavitia vitu vyote chini ya miguu yake (Yesu), akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote”.

Tunaposoma Wagalatia 4:7 tunakutana na maneno haya, “Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu”.Yaani kama wewe umeokoka, unapata haki ya kuitwa mwana na vile vile kuwa mrithi wa baraka za Mungu. Saafi kweli kweli.
Watoto hawastahili kurithi baraka za Mungu

Mtu ambaye hajaokoka ni sawa na mtoto wa kambo. Ni sawa na Ishmaeli, ambaye alikuwa mwana wa mjakazi, lakini mtoto wa kambo kwa Sara, ingawa alikuwa mwana kwa Ibrahimu kama alivyokuwa Isaka. Ndio maana Biblia inatuambia kuwa, “Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe” Mwanzo 21:11).

Ishmaeli na Isaka walikuwa wana kwa Ibrahimu na baba yao alitaka wote warithi mali au baraka zake. Kikwazo kilikuwa ni Sara, ambaye kwake Ishmaeli alikuwa mtoto wa kambo, na kwa sababu hiyo hakustahili kurithi.

Kama ilivyokuwa kwa Isaka, kanisa au watu waliookoka ni wana wa ahadi; sio wana wa mjakazi au watoto wa kambo. Na kama tulivyoona huko nyuma, wana wa ahadi ndio warithi wa baraka za Mungu. Stahili hiyo ni yao.

Hebu tujikumbushe tena maneno ya Wagalatia 4:28-31 ambapo tunaambiwa, “Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi. Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa. Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana. Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana”.

Watu ambao hawajaokoka hawawezi kurithi baraka za rohoni.
Msomaji utakumbuka kuwa huko nyuma niligawa baraka zinazotoka kwa Mungu katika makundi mawili.. Nilisema kuna baraka za mwilini na baraka za rohoni. Niliainisha baraka za rohoni kama vile kujazwa au kupokea nguvu za Roho Mtakatifu, karama au vipawa mbalimbali na uzima wa milele.

Ukichunguza baraka au mambo haya utakubaliana nami kuwa huwa yanaonekana kwa watu waliookoka tu. Huwezi kukuta mtu ambaye hajaokoka akiwa naye kajazwa Roho Mtakatifu. Hawezi kunena kwa lugha. Kwanza haelewi ni kitu gani hiki.

Mtu ambaye hajaokoka hawezi kuwa na karama au vipawa kutoka kwa Mungu, kama vinavyotajwa katika Biblia. Aidha hawezi kurithi uzima wa milele. Haya ni mambo ya watu wa Mungu tu; ni ya wana wa Mungu peke yao. Huu ndio ukweli. Read More......
Baraka ni urithi kutoka kwa Mungu
Jambo lingine ambalo mwanadamu anaweza kurithi kutoka kwa Muumba wake ni baraka za aina mbalimbali. Katika 1Petro 3:8-9 imeandikwa hivi, “Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitivu, wenyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka”.

Wanaoambiwa maneno haya ni watu wa Mungu. Ni wakristo waliookoka. Lakini jambo la kuzingatia hapa ni kuwa, watu hawa wameokolewa na wanatakiwa wawe na mwenendo mwema, ndipo wapate kurithi hizo baraka.

Aina za baraka
Nimesema kuwa mtu anaweza kurithi baraka za aina mbalimbali. Tunapolichunguza neno la Mungu kwa makini tunaweza kuona kwamba, baraka kutoka kwake zimegawanyika katika makundi makubwa mawili. Yaani baraka za mwilini na baraka za rohoni. Nitafafanua jambo hili baadaye kidogo, lakini kwa sasa hebu tuangalie maana ya baraka.

Maana ya baraka
Kamusi ya Kiswahili sanifu inaeleza kuwa baraka ni mambo mema kwa ujumla. Inatumia maneno kama mafanikio, fanaka, ustawi, neema, heri. Vile vile inaeleza kuwa baraka ni hali ya mtu kuwa na vitu vingi kama vile majumba, fedha, mifugo na kadhalika.

Swali ninalotaka tujiulize hapa ni je, hivi mtu akiwa na vitu vingi katika maisha yake, tunaweza kusema kuwa huyo amebarikiwa? Kwa haraka haraka jibu linaweza kuwa ni ndio. Lakini sivyo ilivyo katika maana ile ambayo binafsi ninamaanisha. Kwahiyo jibu sahihi ni ndiyo na hapana. Nitafafanua.

Unaweza kufanikiwa bila Mungu kuhusika
Baraka ninazotaka kuzungumzia katika makala haya ni zile ambazo Mungu amehusika kikamilifu. Ukweli ni kuwa duniani wapo watu wenye mali au mafanikio katika maisha yao, lakini Mungu hakuhusika katika upatikanaji wake. Pengine msomaji unajiuliza jambo hilo linawezekana vipi?

Hebu fikiria mtu ambaye amefanikisha mambo yake kwa kutimiza masharti aliyopewa na mganga wa kienyeji. Kwa akili ya kibinaadamu, ni rahisi kusema kuwa mtu kama huyo ana mafanikio. Lakini ukweli ni kuwa, nguvu iliyo nyuma ya mafanikio kama haya ni ya kishetani. Hiyo sio aina ya baraka ninayomaanisha katika makala haya.

Juhudi binafsi zinaweza kukufanikisha
Wakati mwingine mtu anaweza kufanikisha mambo yake kwa juhudi zake binafsi, bila kutafuta msaada wa Mungu au kwenda kwa waganga wa kienyeji. Unakuta mtu ni mchapakazi, wala huwa haendi kanisani. Mtu kama huyu anaweza kufanikiwa kimaisha, lakini nguvu ya Mungu inakuwa haipo kabisa katika mafanikio yake.

Ukweli ni kuwa kuna kanuni ambazo Mungu ameziweka kwa wanadamu wote, bila kujali ameokoka au la. Mtu akifuata kanuni hizo, anaweza kufanikiwa kimaisha. Mfano mzuri ni huu wa kufanya kazi kwa bidii.

Kanuni ya kufanya kazi kwa bidii itakufanikisha.
Mtu yeyote akifanya kazi kwa bidii anaweza kufanikiwa. Watu kama Wajapani au Wachina hawamwabudu Mungu muumba wa mbingu na nchi. Lakini watu hawa ni wachapakazi kweli kweli. Na kwa sababu hiyo nchi zao zimeendelea. Ni tajiri pengine kuliko nchi ambazo zina wakristo wengi.

Baraka ninayotaka kuizingumzia katika makala haya ni ile ambayo Mungu amehusika kikamikifu. Ni ile ambayo Yeye ndiye mwanzilishi na mshauri wake mkuu tangu mwanzo mpaka mtu anapojikuta tayari amefanikiwa. Hii ndiyo tutakayoizungumzia kwa kina.

Tofauti kati ya kubarikiwa na kufanikiwa kusikokuwa na uhusiano na Mungu
Labda kwa manufaa ya wasomaji, nitoe tofauti chache kati ya kubarikiwa na mafanikio ambayo chanzo chake sio Mungu. Tuanze kwa kuangalia andiko la Mithali 10:2 linalosema, “Hazina za uovu hazifaidii kitu; bali haki huokoa na mauti”.

Tunaweza kuona katika andiko hili kwamba, mtu anaweza kupata mali kwa njia ya uovu. Biblia inatuambia kwamba utajiri kama huo hauna faida au manufaa kwa mtu huyo. Sana sana utakuwa umeambatana na matatizo kibao.

Mafanikio yanayotokana na Mungu yana manufaa mengi. Kwa mfano yanakuwa hayana majuto au mahangaiko. Hili lipo wazi tunaposoma Mithali 10:6 ambapo tunaambiwa kuwa, “Baraka ya Bwana hutajirisha, wala hachanganyi huzuni nayo".

Utajiri kutoka kwa Mungu hudumu
Utajiri unaotokana na Mungu hupatika kwa njia za haki, na vile vile hudumu kwa muda mrefu. Hiki ndicho Mungu anachotuambia katika Mithali 8:18 kwamba, “Utajiri na heshima ziko kwangu, naam, utajiri udumuo, na haki pia”.

Nafikiri wengi wetu tumewahi kukutana au kusikia visa vya watu ambao hapo zamani walikuwa ni matajiri sana, lakini sasa wamefilisika. Moja ya sababu ambayo iliwafanya wafilisike ni kwamba, walipata mali hiyo kwa njia za uovu. Kwa njia ya dhuluma, udanganyifu, wizi, ulaghai na kadhalika.

Katika Yeremia 17:11 tunaambiwa kuwa, “Kama kware akusanyaye makinda asiyoyazaa, ndivyo alivyo mtu ajipatiaye mali, wala si kwa haki, katikati ya siku zake zitaachana naye, na mwisho wake atakuwa mpumbavu”

Hapa Biblia inatuthibitishia kuwa, mali isiyopatikana kwa haki huwa haidumu. Yaani mtu anafilisika katikati ya maisha yake, na mwishowe anakuwa hana kitu kabisa. Anaonekana kama juha. Hili ndilo tatizo la mali iliyopatikana kwa njia za uovu.

Aliyebarikiwa ni mkarimu

Mara nyingi mtu aliyebarikiwa na Mungu ni mkarimu mno. Ni mtoaji kwa ajili ya kazi ya Mungu. Na hili ndio moja ya lengo kuu la Mungu la kuwabariki watu wake. Kwamba wautumie utajiri huo au mafanikio hayo kwa ajili ya kuueneza ufalme wake hapa duniani.

Katika 2Wakoritho 9:8 imeandikwa hivi, “Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika tendo jema; kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, haki yake yakaa milele”.

Katika Biblia tuna kisa cha tajiri mmoja ambaye alikuwa hana tone la ukarimu. Huyu sio mwingine bali ni Nabali. Unaweza kusoma kisa cha mtu huyu katika 1Samweli 25:2-42.

Kwa kifupi ni kuwa Daudi alituma vijana wake ili wakaombe msaada wa chakula kutoka kwa Nabali. Biblia inatuambia kuwa, “Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, ‘Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake. Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya ya kondoo zangu, na kuwapa watu ambao sijui wametoka wapi?.(1Samweli 25:10-11)

Msomaji nafikiri unaweza kuona jinsi Nabali alivyojibu kwa jeuri na dharau. Majibu kama haya mara nyingi ni ya watu waliofanikiwa, lakini Mungu hana nafasi katika mioyo yao. Ni kama yule waziri fulani aliyefanya ufisadi wa kuiba fedha za umma, halafu alipoulizwa akatamka kwa dharau kubwa, eti ni vijisenti tu.

Jeuri ya fedha isiyo na uhusiano na Mungu haimfikishi mtu mbali. Nabali hakufika mbali. Alikufa baada ya muda mfupi tu. Yule waziri hakufika mbali. Punde akapoteza kazi yake. Hayo ndio matokeo ya utajiri ambao Mungu hakuhusika. Msomaji nisingetaka wewe nawe uwe na utajiri wa namna hii.

Baraka za rohoni
Baada ya kufafanua maana halisi ya baraka, hebu sasa tuendelee kuangalia aina za baraka. Tayari nimeshasema kwamba kuna baraka za rohoni na za mwilini. Tuanze na baraka za rohoni.

Kwanza kabisa tuanze kwa kujiuliza swali hili; je, ni kweli kuna baraka za rohoni? Ili kupata jibu sahihi, hebu tusome Waefeso 1:3 ambapo tunambiwa kuwa, “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo”.

Andiko hili linatuonyesha wazi kuwa Mungu huwabariki wanadamu kwa baraka za rohoni. Baraka hizi hupitia kwa mwanawe Yesu Kristo. Huyu ndiye ambaye huko nyuma tuliona kuwa amekabidhiwa vitu vyote na Mungu , kwa ajili ya kanisa (Waefeso 1:22).

Baraka za roho ni zipi?
Baraka za roho ni mambo ambayo hayaonekani kwa macho ya kawaida, lakini utendaji wake unaweza kudhihirika kwa matendo au matokeo katika ulimwengo wa mwili. Uridhihiko huu hutokea pale baraka hizo zinapotumika au zinapokuwa kazini. Ili jambo hili lielewewke vema, nitatoa mifano michache.

Tayari tumeshaona kuwa baraka za rohoni ni urithi kutoka kwa Mungu. Vitu vya rohoni ambavyo mwanadamu anaweza kuvipata kutoka kwa Mungu ni kama vile ujazo wa Roho Mtakatifu, karama au vipawa mbalimbali, na kadhalika.Vitu hivi havionekani kwa macho ya nyama, lakini vinapotumiwa ndipo matokeo yake yanaweza kudhihirika kwa watu.

Ujazo wa Roho Mtakatifu
Katika Matendo ya Mitume 1:8 imeandikwa hivi, “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi”.

Tunaweza kuona katika andiko hili kuwa, chanzo au anayewagawia watu Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe. Sio mwanadamu, ingawa mwanadamu anaweza kumwekea mtu mikono, halafu mtu huyo akapokea ujazo wa Roho Mtakatifu.

Hiki ndicho kilichotokea katika Matendo ya Mitume 19:5 ambapo tunaambiwa kuwa, “Na Paulo alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha , na kutabiri”.

Kinachoonekana ni matokeo
Sasa ukweli ni kuwa hakuna mtu anyeweza kumwona Roho Mtakatifu. Kinachoonekana ni matokeo ya Yeye kuingia ndani ya mwamini. Matokeo hayo ni pamoja na kunena kwa lugha mpya (Matendo 2:1-2) au kuwa na nguvu pamoja na ujasiri wa kuhubiri au kushuhudia habari za Bwana Yesu kama alivyofanya Stefano (Matendo 7:51-60).

Katika Yohana 14:16-17 Yesu alisema kuwa, “nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli,; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa ndani yenu”.

Maneno haya yanatuthibitishia kuwa Roho Mtakatifu huwa haonekani kwa macho ya kawaida, wala mtu ambaye hajaokoka hawezi kumtambua. Wanaomtambua ni wale tu waliookoka na kujazwa Roho Mtakatifu. Jambo hili nitalifafanua zaidi huko mbeleni, nitakapokuwa naeleza nani anastahili kurithi baraka za Mungu.

Karama za rohoni hutoka kwa Mungu

Mungu huwagawia au huwarithisha wanadamu karama za rohoni. Katika 1Wakorintho 12:4-11 zimeorodheshwa karama za namna mbalimbali, utendaji wake na chanzo chake. Mstari wa 11 unamalizia kwa kusema, “Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.

Sikiliza msomaji. Karama hutoka kwa Mungu; halafu Yeye huzigawa kwa waumini wake kama atakavyo na sio kama wao wanavyotaka. Ninayasema haya kwa sababu kuna wakristo ambao hulazimisha karama fulani. Wengine hujifanya kwamba wao wana kila aina ya karama au wanaweza kufanya kila kitu peke yao.

Hakuna muumini, kikundi au kanisa linaloweza kusimama peke yake
Kulingana na neno la Mungu, hakuna muumimi anayeweza kufanya kila kitu peke yake. Kwanza kabisa, sote tunafahamu mambo ya Mungu kwa kiasi au kiwango fulani tu (1Wakorinho 13:9). Hatufahamu kila kitu. Halafu kila mtu hupewa karama ya aina fulani. Anaweza kupewa karama mbili tatu, lakini hapewi zote.

Pamoja na mambo mengine, nia ya Mungu ya kutupatia karama chache ni ili tushirikiane. Ni ili tutambue kuwa kila mwenye karama fulani anamuhitaji muumini mwingine mwenye karama iliyo tofauti na ya kwake.

Lengo la Mungu ni kutuondolea kiburi na kudharauliana. Ni ili tutambue kwamba sote tu viungo vya Kristo (1Wakorintho 12:12-27) na kwamba kila kiungo, au kila muumini, au kila kikundi au kila kanisa linalihitaji kanisa lingine. Kwamba tunahitajiana. We need one another.

Kanisa linatakiwa likamilike katika umoja

Mambo yalivyo kwa sasa ni kwamba, ushirikiano kati ya wakristo haupo kabisa au hata kama upo, ni mdogo sana. Waumini hawashirikiani wao kwa wao katika mambo kama biashara, mali zao na kadhalika. Kila mtu yuko kivyake vyake tu.

Huduma moja haishirikiani na huduma nyingine. Kwanza wanapigana vita. Halafu kanisa moja la kiroho halishirikiani na kanisa jingine. Sana sana makanisa yanasemana ovyo. Manabii na mitume hawapatani; wanapingana madhabahuni.

Huu sio mpango wa Mungu hata kidogo. Mpango wake ni sisi tushirikiane ili tuwe na umoja wa Kristo. Ili tuwe na nguvu. Hiki ndicho ambacho Yesu aliliombea kanisa kabla hajaondoka duniani (Yohana 17:11, 17:20-23).

Mungu hugawa vipawa mbalimbali
Unaposoma Biblia unaweza kuona kuwa Mungu huwagawia wanadamu vipawa au vipaji mbalimbali. Katika Waefeso 4:7-8 imeandikwa kua, “Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipawa chake Kristo. Hivyo husema, ‘Alipopaa juu aliteka mateka, akawapa wanadamu vipawa”.

Vipawa hivi ni pamoja na uwezo wa kuwa mtume au nabii, au mwinjilislisti au mchungaji, na kadhalika. Hiki ndicho kinachozungumzwa katika Waefeso 3:11 ambapo tunaambiwa kuwa, “Naye (Yesu)alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu.”
Jambo la kuzingatia ni kwamba, vipawa hivi havipatikani kwa kulazimisha. La hasha. Havipatikani kwa kujipachika. Hapana. Huu ni urithi kutoka kwa Mungu, kama aonavyo Vema kuwagawia waumini, na sio kama wao watakavyo au wanavyotamani. Huu ndio ukweli.

Uzima wa miliele ni urithi kutoka kwa Mungu

Uzima wa milele ni moja ya baraka za rohoni. Ni kitu ambacho sisi tulio hai hatujawahi kukiona, labda wale ambao tayari wamekufa. Lakini kwa imani tunaamini kwamba uzima wa milele upo. Ndio maana tunakaza mwendo ili tuweze kuingia katika uzima huo.

Bwana Yesu anatutia moyo pale anapotuambia kuwa, “Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, au mama, au watoto, wa mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele” (Mathayo 19:29)

Ni tumaini langu msomaji kwamba utasimama imara katika wokovu wako, ili uweze kurithi huo ufalme wa Mungu. Baadaye nitaonyesha kuwa uzima huu ni stahili ya watu waliookoka tu.

Kwahiyo kama wewe hujaokoka, nakutia shime ufanye hivyo, maana mtu asipookoka au asipozaliwa mara ya pili, hataweza kuurithi ufalme wa Mungu. Hiki ndicho ambacho Nikodemo aliambiwa na Bwana Yesu, wakati mmoja alipokwenda kumtembelea (Yohana 3:1-7).

Baraka za mwilini.
Baraka za mwilini ni vitu vinavyoonekana kwa macho ya kawaida au vinavyoweza kushikika. Ni ile hali ya kuwa na vitu vingi kama vile magari mengi, nyumba nyingi, mashamba makubwa, fedha nyingi na kadhalika. Mtu anapokuwa na vitu kama hivi kwa wingi, tunasema huyo amebarikiwa au ni tajiri.

Afya ya mwilini nayo ni baraka. Tunaweza kuliona hili wakati Yohana alipomwombea mzee Gayo hivi, “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo” (3Yohana 1:2).

Uzazi au kuwa na watoto nayo ni baraka kutoka kwa Mungu. Hili lipo wazi kabisa tangu mwanadamu alipoumbwa ambapo Biblia inatuambia kuwa, “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha” (Mwanzo 1:28).

Vile vile tunaposoma Zaburi 127:3 tunakutana na maneno yafuatayo, “Tazama wana ndio urithi wa BWANA, uzao wa tumbo ni thawabu” Hapa napo tunaona kuwa watoto ni baraka au zawadi kutoka kwa Mungu.

Baraka au mafanikio halisi hutoka kwa Mungu

Kama zilivyo baraka za rohoni, ukweli ni kuwa hata chanzo cha baraka za mwilini ni Mungu. Lakini sio kila baraka ya mwilini imetokana na Mungu. Hapana. Jambo hili nililizungumzia kwa kina huko nyuma, wakati ninatoa tafsiri ya neno baraka.

Nilisema kwamba mtu anaweza kuwa na utajiri wa vitu vingi, au afya njema, au watoto wengi na kadhalika, lakini vitu hivi visitokane na Mungu. Binafsi siwezi kusema mtu kama huyu amebarikiwa. Sasa sana nitasema amejitahidi kimaisha. Kwanini ninasema hivyo?

Ukweli ni kuwa baraka halisi hutoka kwa Mungu. Kama nilivyoonesha huko nyuma, inawezekana kabisa mtu akafanikiwa maishani, lakini Mungu hana nafasi katika moyo wake. Unakuta mtu ni tajiri, lakini hana dini, au anaabudu miungu isiyo ya kweli. Utajiri kama huu una matatizo mengi; sio kama ule ambao chanzo chake ni Mungu.

Nani anastahili kurithi baraka za Mungu?
Katika sehemu ya kwanza ya makala haya, iliyohusu urithi kutoka kwa mwanadamu mmoja kwenda kwa mwanadamu mwingine, nilianisha watu wanaostahili kurithi vitu au mali ya mmiliki wa kwanza. Kwa kukumbushia nilisema kuwa, sio kila mtu anaweza kurithi mali ya marehemu.

Nilisema kwamba, wapo watu maalumu ambao jamii na sheria za nchi zinawatambua kuwa hao ndio warithi halali. Ndipo nikasema kuwa, watoto wa kambo hawastahili kurithi, labda katika mazingira maalumu..

Tunapokuja katika swala la urithi kutoka kwa Mungu, napo tunakuta kuwa kuna watu maalumu ambao ndio wanaostahili kurithi baraka, ziwe za rohoni au za mwilini. Hawa sio wengine bali ni wana wa Mungu. Sasa swali la kujiuliza ni je, hivi wana wa Mungu ni akina nani? Nitaeeleza.

Tofauti ya mwana na mtoto
Kwanza kabisa, ni vizuri tukatambua kuwa kuna tofauti kati ya mtoto na mwana. Ingawa watu wengi hutumia maneno haya mawili wakiwa wanamaanisha kitu kile kile, lakini ukweli ni kwamba kuna tofauti.

Mwana ni yule hasa aliyezaliwa na baba au mama yake. Kwa Kiswahili safi, mtu kama anamtaja mtoto wake, anatakiwa aseme ‘huyu ni mwanangu’. Mwana anaweza kuwa mtoto mdogo kiumri, lakini hata akikua akawa mtu mzima au mzee, bado ataendelea kuwa ni mwana mbele ya wazazi wake.

Nafikiri wengi tunafahamu ule msemo wa Kiswahili unaosema ‘mtoto hakui mbele ya wazazi wake’. Maana halisi ya msemo huu ni kwamba, wazazi wake wataendelea kumwita mwanetu, hata akiwa mzee mwenye mvi au akiwa na cheo kikubwa kazini. Kwa mfano Rais ataendelea kuwa ni mwana mbele ya wazazi wake, ingawa kiumri sio mtoto tena. Read More......

SEHEMU YA PILI: URITHI KUTOKA KWA MUNGU

Utangulizi
Katika sehemu ya kwanza ya makala haya, tuliangalia pamoja na mambo mengine, tafsiri ya urithi, vitu ambavyo mwanadamu mmoja anaweza kuvirithi kutoka kwa mwanadamu mwenzake, watu wanaostahili, muda au wakati wa kurithi, na kadhalika.

Tunapoingia katika sehemu ya pili, ambayo inayohusu urithi kutoka kwa Mungu, lipo swali moja muhimu sana, ambalo inabidi tupate jibu lake mapema kabisa. Swali lenyewe ni je, hivi ni kweli kwamba Mungu huwa anarithisha wanadamu?

Jibu la swali hili ni muhimu kwani litatoa mwelekeo wa kile ninacholenga kuzungumzia. Tayari tumeshaona kuwa wanadamu hurithishana vitu kama mali, sura, tabia, madeni, majukumu na kadhalika. Sasa kwa upande wa Mungu mambo yanakuwaje?

Mungu hurithisha
Ninatambua kuwa wasomaji wengi wa gazeti ilio ni wakristo. Kwa sababu hiyo basi, nitatumia maandiko kadhaa ya Biblia katika kuonyesha kwamba, hata Mungu muumba wa mbingu na nchi, huwa anarithisha wanadamu mambo mbalimbali. Kwahiyo msomaji wangu naomba tufuatane kwa makini.

Tuanze kwa kusoma andiko la Agano la Kale. Katika Mithali 8:20-21 Mungu wetu anatamka kuwa, “Natembea katika njia ya haki, katikati ya mapito ya hukumu. Niwarithishe mali wale wanipendao, tena nipate kuzijaza hazina zao”.

Hapa tunaona kuwa Mungu ni wa haki, na moja ya malengo yake ni kuwarithisha mali wale wanaompenda. Kwahiyo tunaanza kupata picha kuwa Mungu huwarithisha wanadamu mali au vitu vya kushikika.

Je, Agano Jipya lina ahadi ya urithi?
Sasa hebu tutafute andiko lingine katika Agano Jipya, linaloonyesha kuwa Mungu hurithisha. Inabidi tufanye hivyo kwa sababu, ukweli ni kuwa yapo mambo ambayo yametajwa katika Agano la Kale, lakini mambo hayo hayapo au yamebadilishwa katika Agano Jipya. Mfano mzuri ni swala la kutoa sadaka za kuteketezwa au kafara za mbuzi, kondoo, ng’ombe na kadhalika.

Mambo haya yaliagizwa na Mungu katika Torati ya Musa. Lakini katika kipindi hiki cha Agano Jipya, huwa wakristo hatutoi sadaka za kuteketezwa kama ilivyokuwa zamani. Yesu alitolewa kama sadaka ya ondoleo la dhambi wakati aliposulubishwa pale msalabani (Mathayo 26:27-28).

Kwahiyo ni vema mtu anaponukuu andiko la Agano la kale, vile vile atafute andiko lingine katika Agano Jipya, ambalo linalokubaliana na kile anachokizungumzia. Vinginevyo mtu anaweza kuleta utata au upotoshaji, wakati wa kufafanua maandiko ya Biblia.

Waliookoka ni warithi wa Mungu

Tunaporudi katika mada yetu tunaweza kuona imeandikwa katika Warumi 8:16-17 kwamba, “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo.”

Wanaozungumzia katika andiko hili ni watu waliookoka; kwamba wao ni warithi wa Mungu. Loo! Ama kweli hili ni jambo zuri mno. Kumbe mtu akiokoka anapata heshima ya kuweza kurithi kutoka kwa Mungu! Saaafi kweli kweli.

Tunarithi kupitia kwa Yesu
Tunapozidi kuchunguza andiko hili tunaweza kuona kuwa watu wa Mungu wanarithi pamoja na Kristo. Swali la kujiuliza hapa ni je, hivi Bwana Yesu alirithi kitu gani kutoka kwa Mungu?

Ili kupata jibu sahihi la swali hili, nakusihi msomaji wangu usome kwa makini waraka kwa Waefeso 1:2-22. Hapa utapata picha kamili ya kile ambacho Kristo Yesu alirithi, na vile vile kile ambacho sisi wakristo tuliookoka tunaweza kurithi kupitia kwake.

Katika mistari hii tunaweza kuona kuwa Paulo anaomba waamini wafunguke macho yao ya rohoni, ili watambue uzuri wa kuokoka “na utajiri wa utukufu wa urithi wake (yaani Mungu) katika watakatifu jinsi ulivyo (mstari wa 18).

Katika mstari wa 20-22 tuunaweza kuona jinsi Mungu alivyomtukuza Kristo baada ya kumfufua katika wafu, halafu akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa”. Yaani kila kitu alichokabidhiwa Bwana Yesu ni kwa ajili ya kanisa lake au wale waliomwamini kwa njia ya kuokoka.

Ni vitu gani tunavyoweza kurithi kutoka kwa Mungu?

Sasa baada ya kupata uthibitisho kuwa Mungu huwa anarithisha, hebu sasa tujiulize swali jingine. Je, ni vitu gani ambavyo sisi wanadamu tunaweza kuvirithi kutoka kwa Mungu wetu? Je, vitu hivyo vinafanana na vile ambavyo tunarithi kutoka kwa wanadamu au wazazi wetu?

Ukweli ni kuwa yapo mambo tunayorithishana sisi wanadamu, ambayo kwa namna fulani yanafanana na yale tunayoweza kurithi kutoka kwa Mungu. Lakini mengine ni tofauti kabisa, na wala hayawezi kupatikana kwa wanadamu. Nitafafanua jambo hili kadri tunavyosonga mbele na makala haya.

Tunarithi kufanana na Mungu.
Katika sehemu ya kwanza ya makala haya, nilieleza kuwa moja ya mambo ambayo mtu anaweza kurithi kutoka kwa mwenzake ni vitu kama sura, au tabia, au maumbile na kadhalika. Nilionyesha jinsi ambavyo baada ya anguko, Adamu alimzaa mwana aliyefanana naye (Mwanzo 5:3).

Moja ya mambo ambayo mwanadamu anaweza kuyarithi kutoka kwa Mungu ni kule kufanana na huyu Muumba wake. Katika Warumi 8:29 imeandikwa kuwa, “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye (Bwana Yesu) awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi”.

Wanaozungumziwa hapa ni watu waliookoka; kwamba baada ya kuokoka, wanabadilishwa na kuanza kufanana na Yesu. Sote tunafahamu kwamba Kristo ni mfano wa Mungu (Wakolosai 1:15). Ni chapa ya Mungu (Waebrania 1.3).

Yesu Kristo mwenyewe alisema kwamba yeye na Mungu ni kitu kimoja, na kwamba Mungu yu ndani yake na yeye ndani ya Mungu (Yohana 14:8-13, Yohana 17:20-23). Kwahiyo kufanana na Yesu ni sawa na kufanana na Mungu. Hiki ndicho kinachotokea mtu anapookoka..

Tunarithi tabia za Kiungu au nia ya Mungu
Msomaji utakumbuka kuwa katika sehemu ya kwanza ya makala haya nilisema kuwa moja ya vitu ambavyo mtu anaweza kurithi kutoka kwa wazazi wake ni tabia nzuri kama vile upole, ukarimu, huruma; au tabia mbaya kama uchoyo, usengenyaji, hasira, ugomvi na kadhalika.

Ni ajabu kuwa sisi wanadamu tunaweza kurithi tabia za Kiungu. Bahati nzuri tabia hizi ni njema tu siku zote. Hazikuchanganyika nzuri na mbaya, kama inavyotokea pale tunaporithi tabia za wazazi wetu .

Mwanadamu anapookoka, Roho wa Mungu huanza kukaa ndani yake. Huyo Roho ndiye anayemwezesha kuwa na tabia za Kiungu. Katika Wagalatia 5:22-23 tunaambiwa kuwa, “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi”

Hili tunda la Roho linalozungumziwa hapa ni matokeo ya kumkubali Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Ni mambo ambayo mtu huyapokea kutoka kwa Roho Mtakatifu. Huu ni urithi kutoka kwa Mungu, kwani Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe. Read More......

URITHI: Mahakama ya kufungulia mirathi

Mirathi huwa haifunguliwi katika mahakama yoyote ile. La hasha. Itategemea sheria ya mirathi inayokusudiwa kutumika. Kama sheria itakayotumika kugawa mali za marehemu ni ya Kimila au ya Kiislamu, mirathi inapaswa kufunguliwa katika mahakama ya Mwanzo (Primary Court).

Kama sheria itakayotumika ni ya Kiserikali, mirathi itafunguliwa kule alikokuwa akiishi marehemu katika Mahakama ya Wilaya (District Court), au ya Hakimu Mkazi (Resident Magistrate) au Mahakama Kuu (High Court). Sio mtu anakwenda kufungua mirathi kwenye mahakama mradi ni mahakama. Mambo hayafanyiki hivyo hata kidogo.

Taratibu za kufungua mirathi
Katika nchi yetu, wapo watu ambao tayari wameshaelimika kiasi cha kutosha, na sasa wanafahamu umuhimu wa kuandaa wosia. Lakini vile vile wapo ambao bado wapo gizani na hawajui umuhimu wa jambo hili. Kwahiyo mauti yanapowakuta, kunakuwa hakuna wosia ulioachwa.

Watu wengine wanatambua umuhimu wa wosia, lakini kwa sababu mbalimbali, wanakumbana na kifo kabla ya kuuandaa. Wakati mwingine ni kwa sababu ya uzembe tu, yaani mtu anaahirisha jambo hili kila kukicha, mpaka mauti inamkuta. Sababu nyingine ni imani potofu kuwa mtu akiandaa wosia atakuwa anatabiri au anakaribisha kifo chake. Eti anaweza kufa mapema kabla ya wakati wake.

Kwa bahati nzuri serikali ya nchi yetu inatambua matatizo au madhaifu kama haya ya kijamii. Kwa sababu hiyo imeandaa taratibu za kufungua mirathi katika mazingira ambayo wosia upo na vilevile wakati haupo. Nitaeleza taratibu hizo.

Wosia ukiwepo
Kama marehemu aliacha wosia, utaratibu wa kufungua mirathi uko hivi;
  1. Kifo kiandikishwe kwa Mkuu wa Wilaya katika muda usiozidi siku 30. Lengo ni kupata cheti cha kifo (Death Certificate). Cheti hiki ni tofauti kabisa na kile cha uthibitisho wa kifo, ambacho huandkwa na daktari mara tu baada ya kifo kutokea.
  2. Msimamizi aende mahakamani kufungua mirathi akiwa na wosia wa marehemu, pamoja na cheti cha kifo.
  3. Mahakama itatoa tangazo la mirathi litakalodumu kwa muda wa siku 90. Iwapo hakutatokea pingamizi lolote, mahakama itatoa barua ya usimamizi wa mirathi kwa mtu aliyeomba au aliyefungua mirathi. Barua hiyo itampa uhalali wa kugawa mali ya marehemu (urithi) baada ya kulipa madeni.
  4. Msimamizi wa mirathi ataorodhesha mali ya marehemu na kuigawa kama ilivyoainishwa kwenye wosia.
  5. Baada ya kugawa mali, msimamizi atarejesha taarifa mahakamani akieleza jinsi alivyotekeleza wosia wa marehemu.
  6. Hatimaye mahakama itafunga jalada la mirathi.
Wosia usipokuwepo
Kama marehemu hakuacha wosia, utaratibu unaofuatwa ni kama ule wa mazingira ambayo wosia upo, isipokuwa msimamizi wa mirathi huchaguliwa na baraza au mkutano wa ukoo. Mtu aliyechaguliwa huenda mahakamani akiwa na kumbukumbu au muhtasari wa kikao kilichomchagua.

Hapa naomba niseme kwamba ni Watanzania wachache sana wanaofahamu na wanaofuata taratibu za ufunguzi wa mirathi. Wengi wanapeleka mambo kienyeji tu. Hilo ni kosa kisheria na mtu anaweza kushitakiwa mahakamani. Kwahiyo ni wajibu wetu kufahamu taratibu za mirathi na kuzifuata kama zilivyo, na sio vinginevyo.

Jukumu la msimamizi wa mirathi
Sasa tunakuja katika eneo ambalo binafsi ninaamini kwamba watu wengi sana huwa wanalikosea na vile vile lina lawama nyingi mno. Hili linahusu majukumu ya msimamizi wa mirathi. Kama kuna eneo ambalo inabidi mtu awe makini ni hili la kusimamia ugawaji wa mali ya marehemu. Kwanini ninasema hivyo?

Wapo watu wanaobeba au wanaokubali jukumu hili bila kujua wajibu wao. Kwahiyo wanaharibu utaratibu mzima wa kugawa mali iliyoachwa na marehemu. Wengine kwa sababu ya tamaa, wanakimbilia jukumu la usimamizi wa mirathi kwa lengo la kudhulumu au kujigawia sehemu ya mali iliyoachwa.

Ni vizuri kuzingatia kuwa msimamizi wa mirathi ni mdhamini au wakili tu wa kuchunga mali iliyoachwa kwa lengo la kuwagawia warithi halali wa marehemu. Msimamizi sio lazima awe mrithi, ingawa kwa sababu ya kuogopa dhuluma, mmoja wa warithi anaweza kusimamia mirathi kwa niaba ya wenzake. Mahakama nyingi humpa mke wa marehemu au mtoto mkubwa wa marehemu jukumu hili.

Msimamizi wa mirathi awe ni mtu mwadilifu
Kinachotokea katika jamii nyingi za kiafrika ni kwamba, mtu aliyeteuliwa kugawa mali ya marehemu humega sehemu ya mali hiyo wakati yeye sio mrithi. Kama ni mmoja wa warithi, yeye hujipendelea. Hili ni kosa kisheria na mtu anaweza kushitakiwa mahakamani.

Jambo lingine ambalo huwa halieleweki na watu wengi, na kwa sababu hiyo huwa haliwekwi vizuri au halifafanuliwi na wanandugu, ni gharama za usimamizi wa mirathi. Ukweli ni kuwa jukumu la kusimamia mirathi hugharimu muda, nguvu za mtu pamoja na fedha.

Watu wengi huwa hawatambui kuwepo kwa gharama hizi, na msimamizi anapozidai au anapozikata katika mali ya marehemu (recover costs), anaonekana kama vile anawadhulumu warithi halali. Hata kama msimamizi huyo ni mmoja wa warithi, bado akizikata ataonekana kama vile anawadhulumu wenzake au anajipendelea. Swali la kujiuliza ni je, gharama za usimamizi wa mirathi zinalipwa na nani?

Wasimamizi wengine sio waaminifu. Wanaweza kumega sehemu kubwa ya mali ya marehemu, kwa kisingizio kwamba ni gharama za usimamizi. Ndio maana nilisema kwamba msimamizi wa mirathi ni vema awe mtu mwadilifu, na sio mbabaishaji. Vinginevyo warithi halali wanaweza kudhulumiwa kilicho haki yao.

Mambo ya kufanya
Baada ya maelezo ya jumla juu ya sifa, matatizo na jukumu la msimamizi wa mirathi, naomba sasa niainishe mambo ambayo mtu huyu anapaswa kuyafanya. Kwa kifupi msimamizi anapaswa kufanya mambo yafuatayo;
  1. Kukusanya madeni na kuorodhesha mali ya marehemu.
  2. Kulipa madeni yote halali yaliyoachwa.
  3. Kugawa mali iliyobaki (baada ya kulipa madeni) kwa warithi halali kwa kuzingatia wosia wa marehemu au katika msingi wa haki na usawa kulingana na sheria inayosimamia mirathi hiyo.
  4. Kutayarisha taarifa ya jinsi alivyosimamia na kugawa mali ya marehemu. Taarifa hiyo iwasilishwe katika mahakama ambayo mirathi ilifunguliwa, na iwe na vipengele vifuatavyo;
  • Aina na thamani ya mali za marehemu.
  • Madeni
  • Matumizi kama vile gharama za mazishi, gharama za usimamizi wa mirathi, na kadhalika.
  • Jinsi mali iliyobaki ilivyogawiwa kwa warithi halali.
Taarifa hii inatakiwa isainiwe na warithi wote wa marehemu.

Hitimisho sehemu ya kwanza
Msomaji wangu nafikiri mpaka sasa tumeelewana kuhusu maswala mbalimbali yanayohusu urithi kutoka kwa mwanadamu mmoja kwenda kwa mwanadamu mwingine. Ninaamini kwamba yapo mambo ambayo ulikuwa huyafahamu, lakini sasa umefunguka macho na umeelimika kiasi cha kutosha.

Ninapomaliza sehemu hii ya kwanza ya mada hii, naomba niwasisitizie wakristo wenzangu umuhimu wa kuelewa sheria za nchi na kuzifuata. Ikumbukwe kuwa Biblia inatuagiza hivyo kwa kutuambia kwamba, “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo imeamriwa na Mungu” (Warumi 12:1).

Mambo tunayopaswa kuyatii ni pamoja na sheria za nchi, zikiwemo sheria za mirathi. Ninatambua kuwa wapo waumini ambao wamekuwa wa kiroho sana, kiasi ambacho huwa hawakumbuki kuchunguza na kutambua sheria za nchi yetu zinasema nini. Kwa sababu hiyo wanajikuta katika matatizo mbalimbali ya kiutawala na kisheria wakati wanaposhughulikia .maswala yao.

Kwa vile wakristo ni sehemu ya jamii, na vile vile swala la urithi linawagusa kwa namna moja au nyingine, ni vema wakatambua wajibu wao na haki zao katika jambo hili. Vinginevyo wanaweza kujikuta hawajui la kufanya, au wanaweza kuingia matatani, au wakapoteza haki zao za kurithi. Baada ya hitimisho hili, sasa tunaweza kuingia katika sehemu ya pili ya mada hii. Karibu tuendelee kuwa pamoja msomaji wangu. Read More......

TaCHe & Subi.nukta77 chose to wear BlueWeed by BlogOh!Blog | to Blogger by Gre at Template-Godown | Entries (RSS) and Comments (RSS).