Friday, June 5, 2009
URITHI: Biblia inasema nini kuhusu watoto wa kambo?
Tunapoigeukia Biblia tunaona kwamba yenyewe inakataa kabisa mtoto wa kambo kurithi. Huko nyuma tuliona kwamba Sara alikataa Ishmaeli (mtoto wa kambo) asirithi pamoja na Isaka (mtoto wa ahadi au mtoto halali wa ndoa). Tuliona jinsi Mungu alivyokubaliana na msimamo wa Sara (Mwanzo 21:9-12). Vile vile tuliona jinsi ambavyo Yeftha alipokosa urithi kwa sababu alikuwa ni mtoto wa nje ya ndoa (Waamuzi 11:1-3).
Pengine msomaji unaweza kusema haya mambo ya mtoto wa kambo kunyimwa urithi ni ya Agano la Kale. Unaweza kudai kwamba katika Agano Jipya hayapo. Kwahiyo ukataka kuwarithisha hata watoto wa kambo. Sasa subiri kidogo. Ngoja kwanza tupitie maandiko.
Agano Jipya haliruhusu mtoto wa kambo kurithi
Ukweli ni kwamba hata Agano Jipya linaungana na Agano la Kale katika kukataa mtoto au watoto wa kambo kurithi. Katika Wagalatia 4:28-31 imeandikwa hivi, “Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi. Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa. Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana. Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali sisi tu watoto wa huyo aliye mwungwana”.
Mistari hii inaendelea kupigilia msumari msimamo wa Agano la Kale kwamba watoto wa kambo hawana haki ya kurithi mali ya baba zao. Maneno ‘Lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana’ yanaendelea kukukumbushia na kusisitiza kile kilichotajwa katika Agano la Kale.
Vile vile maneno ‘Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali sisi tu watoto wa huyo aliye mwungwana’ yanaendelea kuweka tofauti kati ya mtoto wa ndoa na yule aliyezaliwa nje ya ndoa. Kwamba walio watoto wa mwungwana au wa ndoa, ndio pekee wenye haki ya kurithi. Huu ndio msimamo wa Biblia.
Wapalestina hawawezi kukalia nchi ya Israeli
Ili kuonyesha kuwa kufuatana na Biblia, mtoto wa kambo hawezi kurithi, nitazungumzia taifa la Israeli lilivyo kwa sasa. Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba Wapalestina, ambao kimsingi ni Waarabu, wanatokana na uzao wa Ishmaeli. Tayari nimeshaonyesha kwamba Ishmaeli ni mtoto wa kambo, na hakuruhusiwa kurithi pamoja na Isaka, mwana wa ahadi.
Kinachoendelea sasa ni watoto wa kambo (Wapalestina) wanadai kwamba nao wapewe ardhi au nchi yao ndani ya mipaka ya Israeli. Kwa maneno mengine wanadai haki ya kurithi pamoja na watoto halali wa ndoa (Waisraeli). Hili haliwezekani kamwe. Wala mikakati yote ya kuigawa nchi ya Israeli kati ya Waisraeli na Wapalestina haitafanikiwa kamwe.
Ardhi ya Israeli ni urithi kutoka kwa Mungu
Ukweli ni kuwa ardhi au nchi ya Israeli ni urithi kutoka kwa Mungu kwenda kwa Waisraeli, ambao ni watoto halali wa ndoa kupitia Sara. Biblia inayo maandiko mengi sana yanayoonyesha kuwa Mungu aliahidi kumpa Ibrahimu nchi yote ya Israeli, ili iwe urithi kwake na uzao wake. Lakini uzao huo ni kupitia kwa Isaka, Yakobo na hatimaye wanawe kumi na wawili. Sio nje ya mpangilio huu.
Ndio kusema kuwa Wapalestina hawatafanikiwa katika juhudi zao za kuimega Israeli katika mataifa mawili. Yaani kati ya Waisraeli na Wapalestina. Hata wakisaidiwa na ndugu zao Waarabu, au Waislamu wenzao, bado hawatafanikiwa. Hata Umoja wa Mataifa ukitaka kulazimisha mambo, ni kazi bure. Kwanini? Kwa sababu andiko la Biblia lasema ‘mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa Mwungwana’. Huu ndio msimamo wa Mungu; na kusudi lake ndilo litakalosimama.
Kibiblia watoto wa kambo wanakuwaje?
Pengine msomaji sasa unajiuliza kama mambo yako hivyo, hatima ya watoto wa kambo ni nini? Iwapo hawawezi kurithi mali za baba zao, sasa maisha yao yatakuwaje? Mbona wataharibikiwa? Nitajaribu kueleza kinachowasibu. Kwahiyo naomba tufuatane kwa makini.
Ukweli ni kuwa Mungu hawachukii watoto wa kambo. Bado anawapenda, hata kama hawapi haki ya kurithi. Kama anawachukia, angekuwa ni Mungu dhalimu kweli kweli; Mungu asiye na upendo, kitu ambacho sio kweli hata kidogo. Sivyo alivyo.
Hilo swala la watoto wa kambo kutokuwa na haki ya kurithi ni utaratibu aliojiwekea, ili kuilinda taasisi ya ndoa. Ukweli ni kwamba sio mapenzi ya Mungu wanadamu wazae ovyo ovyo. Hapana. Mpango wake mkamilifu (Gods perfect will) ni mume mmoja na mke mmoja tu katika maisha ya mwanadamu. Sio mtu anazaa kwanza na mwanamke au mwanamume huyu, halafu baadaye anaoa mke au anaolewa na mume mwingine.
Ishi sawasawa na mpango wa Mungu
Sio mpango wa Mungu mtu awe ndani ya ndoa, halafu atembee huko nje. Haya ni mambo yetu sisi wanadamu. Ni ujinga, uzembe, upumbavu na udhaifu wetu. Kwahiyo kimsingi watoto wa kambo ni matokeo ya mwanadamu kushindwa kuishi sawasawa na mapenzi makamilifu ya Mungu.
Iwapo Mungu ataruhusu hata watoto wa kambo warithi sawasawa na watoto halali wa ndoa, ina maana atakuwa anajipinga. Atakuwa anakwenda kinyume na mpango wake wa ndoa. Atakuwa kama vile ameruhusu watu wajizalie vyovyote vile watakavyo, halafu naye anabariki kitendo hicho kwa kuruhusu watoto waliozaliwa nje ya ndoa nao warithi. Hiyo sio haki hata kidogo; na Mungu hawezi kufanya kosa kama hili.
Hebu jiulize msomaji. Fikiria binti ambaye amejitunza na ni mwaminifu. Bahati mbaya anaolewa na mume ambaye baadaye anaanza kutembea nje ya ndoa, na huko anamletea watoto wengine.Je, huyu mwanamke ambaye amekuwa mwaminifu katika ndoa yake atakuwa ametendewa haki gani iwapo mali aliyochuma kwa taabu na mumewe, itarithishwa hadi kwa watoto waliozaliwa nje ya ndoa? Je ni haki kuulipa (reward) uaminifu wake kwa kumletea watoto wa kambo?
Mungu hajawatupa watoto wa kambo
Sasa hebu tuangalie ndani ya Biblia tuone maisha ya watoto wa kambo yanakuwaje. Kama nilivyotangulia kusema ni kwamba Mungu anawapenda na hawatupi. Kinyume chake ni kwamba hata wao anaweza kuwabariki, ila kwa njia nyingine.
Tunapoangalia maisha ya Ishmaeli tunaweza kuona kwamba, ingawa Mungu alikataa asirithi katika nyumba ya baba yake, lakini bado alimbariki. Ni kweli Ibrahimu alisikitika sana kwa mwanawe huyo kukosa urithi. Lakini jibu la Mungu lilikuwa ni hili, “Na kwa habari ya Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu (Mwanzo 17:20).
Kama kweli Waarabu ni uzao wa Ishmaeli, watu hawa wamebarikiwa kwa utajiri mkubwa. Kwanini ninasema hivyo? Ukiangalia hapo Mashariki ya Kati, utaona kuwa nchi za Kiarabu zina utajiri mkubwa wa mafuta. Yaani hata Waisraeli hawana mafuta mengi kama Waarabu.
Nani asiyejua kuwa mafuta ni utajiri? Kwa upande wa Waarabu, utajiri huu umetoka kwa Mungu. Ndio ile ahadi ambayo Mungu aliitoa kwa Ibrahimu, kwamba atambariki na kumzidisha Ishmaeli, ikiwa ni pamoja na uzao wake.
Yeftha alibarikiwa na Mungu
Tunapomgeukia Yeftha tunaona kwamba hata yeye alibarikiwa na Mungu. Ingawa ndugu zake walimfukuza ili asirithi pamoja nao mali ya baba yao, Mungu alifungua mlango mwingine wa baraka. Yeftha aliweza kuwa mtu mashuhuri na mkuu kuliko hata nduguze. Huu ndio uzuri wa mbaraka utokao kwa Mungu.
Unaposoma kitabu cha Waamuzi 11:4 hadi 12:7 unaweza kupata picha kamili ya jinsi Mungu alivyomwinua Yeftha, mtu ambaye alikuwa hatakiwi na nduguze pamoja na jamii iliyomzunguka. Kwa kifupi ni kwamba Mungu alisimama naye vitani, akampa ushindi, na hatimaye akamfanya mwamuzi wa Israeli yote.
Mara baada ya kuingia katika nchi ya ahadi, mwamuzi katika nchi ya Israeli alikuwa ndiye mtawala au kiongozi mkuu. Alikuwa kama mfalme, lakini akitawala kwa kufuata maongozi ya Mungu. Ndio kusema Yeftha alitawala taifa la Israeli, ikiwa ni pamoja na nduguze waliomfukuza. Lakini ikumbukwe kuwa alikuwa mtoto wa kambo. Hayo ndio maajabu ya Mungu.
Msomaji naomba nisisitize tena kwamba, sio mapenzi ya Mungu tuwe tunazaa watoto nje ya ndoa. Hapana. Lakini wanapozaliwa, Mungu huwa hawatupi kabisa, kwani sio wao waliotaka kuzaliwa hivyo. Mwanzoni wanaweza kupata taabu kama ilivyotokea kwa Ishmaeli na Yeftha wakati walipofukuzwa nyumbani. Baadaye Mungu anaweza kuwakumbuka, akawainua na kuwabariki.
Watoto wa kufikia na watoto wa kupanga
Huko nyuma nilieleza kwa kina maana ya watoto wa kufikia. Kwa kukumbushia nilisema kwamba hawa ni watoto waliokutwa na mmoja ( au wote) wa wanandoa, lakini kunakuwa na makubaliano kwamba watoto hao wahesabike kwamba ni wa wanandoa hao. Nilitoa mfano wa mtu anayekubali kumwoa mjane pamoja na watoto aliowakuta naye; au mtu anayemwoa mwanamke ambaye tayari ana mtoto au watoto.
Kuhusu watoto wa kupanga nilisema kwamba hawa ni watoto waliochukuliwa na wanandoa kwa minajili ya kuwalea, japo wenyewe hawakuwazaa. Nilitoa mfano wa wanandoa ambao hawakujaliwa kuzaa, lakini wanatafuta watoto wa watu wengine na kuishi nao kama wana wao.
Vile vile nilieleza jinsi wanandoa wenye uwezo na wenye watoto wao, lakini wanaweza kuwachukua watoto wanaoishi katika mazingira magumu, na kuwafanya kama wa kwao kabisa. Nafikiri kwa wale mliokuwa mnafuatilia vyombo vya habari mtakumbuka kile kisa cha Madonna, mwanamuziki maarufu wa nchi ya Marekani, aliyechukua mtoto wa kupanga kutoka Msumbiji.
Watoto wa kambo wanaweza kurithi
Kimsingi ni kwamba watoto wa kufikia au wa kupanga nao pia ni watoto wa kambo. Kinachowatofautisha na watoto wengine wa kambo ni yale makubaliano yanayokuwapo kati ya wanandoa. Kwa sababu ya hayo makubaliano, sheria ya kiserikali inawapa haki ya kurithi mali ya baba yao aliyewakubali au aliyewachukua na kuwalea.
Ninao ushauri katika swala hili. Kutokana na jamii kutowakubali na kuwapa watoto wa kambo haki ya kurithi, ni vema mtu mwenye kusudio la kuwarithisha, aweke jambo hili bayana. Mahali sahihi na salama pa kufanya hivyo ni katika wosia. Wosia ni mwisho wa maneno; ni mwisho wa ubishi. Nitafafanua jambo hili huko mbeleni.
Mkeo au mumeo akizaa nje ya ndoa utafanyaje?
Mambo ya urithi sio mepesi hata kidogo. Pamoja na kutungiwa sheria, bado kuna wakati ambapo huzuka mambo magumu katika ndoa, ambayo yanaweza kuleta matatizo wakati wa kurithi au kurithisha. Kuna wakati baba au mama anakosa uaminifu na kutembea nje ya ndoa. Kitendo hiki kinaweza kuzalisha watoto wa kambo, pamoja na matatizo yanayoambatana nao.
Sasa hebu tujiulize swali. Fikiria mlifunga ndoa takatifu kanisani. Baadaye mumeo au mkeo akaanza kutembea nje ya ndoa, na huko akapata mtoto. Je, utafanya nini hilo likitokea? Kama wewe ni mwanamume, na mkeo ndiye kazaa nje, je, utamwacha? Na kama hutamwacha, je, utamrithisha huyo mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa?
Kama aliyezaa nje ni mwanamume, je, wewe mama utafanya nini? Je, utaikimbia ndoa yako? Kama hutamkimbia mumeo, je, utakubali huyo mtoto wa nje aletwe nyumbani? Tuseme mumeo amekuangukia na kukuomba msamaha. Je, utamsamehe? Kama utamsamehe, je, wakati wa kurithisha utakubali huyo mtoto wa nje naye apate sehemu ya mali mliyochuma na mumeo?
Sio mambo ya kufikirika
Kwa watu waliookoka, maswali kama haya yanaonekana kama vile ni mambo ya kufikirika au ya kutunga tu. Kwamba hayawezi kutokea katika ndoa ya watu wa Mungu. Amini usiamini, siku hizi yanatokea. Kwa jinsi kanisa lilivyoshuka hadhi, wapo wanandoa wanaokiri wokovu, lakini ni wazinzi. Hawa ndio wanaozalisha watoto wa kambo, pamoja na matatizo yanayoambatana nao.
Binafsi ninamfahamu mwimbaji mmoja maarufu (mwanamume) aliyezaa nje ya ndoa. Sijafuatilia nikajua mkewe alichukua hatua gani, lakini kitendo cha huyo baba kililiabisha mno kanisa la Bwana Yesu. Alitengwa kanisani, na baadaye akaanzisha huduma ya Injili. Sijui anaendelea vipi na kwamba hatima ya yule mtoto wa nje ilikuwaje.
Ili tuweze kuelewa jinsi tatizo la watoto wa kambo linavyoweza kujitokeza katika jamii, hebu tusome kisa kimoja nilichonukuu kutoka katika gazeti la Nipashe la tarehe 8 Juni 2008 kama ifuatavyo;
Mke wa ndoa, lakini watoto wa ‘kuchomekewa’
Mpenzi msomaji, leo hebu tuwagusie watoto wetu na jinsi wanavyojikuta katika misukosuko wasiyotarajia. Na hakika yote hayo ni kutokana na matendo ya wazazi wao.Samehe, usonge mbele na wakovu wako
Hivi majuzi nikiwa katika msiba wa mdogo wangu, nilimsikia mama mmoja akieleza kisa cha ndugu yake aliyejikuta akilea watoto wasiokuwa wake, ndani ya ndoa takatifu.
Mwanamama huyu akasema hivi, “Yupo kaka yake kwa baba mkubwa, ambaye alikuwa mfanya biashara. Alifunga ndoa takatifu kanisani, na kuishi maisha mazuri sana mwanzoni mwa ndoa yake.
Bwana huyu akawa ni mtu wa kusafiri kwa ajili ya biashara zake. Wakati fulani mkewe akamjulisha anao ujauzito, taarifa ambayo ilimfurahisha sana. Mtoto akazaliwa, nyumba ikachangamka.
Mle ndani ya nyumba yao, bwana yule alikuwa akiishi na mdogo wake mvulana, ambaye alikuwa ana kazi yake. Miaka mitatu ikapita, mama akapata ujauzito mwingine. Sasa nyumba ikawa na watoto wawili.
Baba mwenye nyumba, safari za kibiashara haziishi. Watoto wakakua hata kufikia umri wa kwenda shule. Yule mkubwa akapelekwa shule ya bweni. Kivumbi kikaanza pale mtoto huyu wa bweni alipougua na kuhitaji kuongezewa damu.
Baba mzazi akaitwa ili apimwe damu, na hatimaye mtoto naye apimwe ili aongezewe damu. Damu ya baba ilipopimwa haikufanana na ya mtoto. Daktari akamwambia akamlete baba wa mtoto. Yeye akang’ang’ania ndiye baba mzazi.
Baba huyu akapatwa kizunguzungu. Akarudi nyumbani. Mkewe akampokea, lakini hakumchangamkia. Kila alipomuuliza ‘kulikoni mume wangu?’ mume alimtazama tu. Hatimaye bwana akavunja ukimya akamuuliza mkewe, ‘huyu mtoto wa kwanza ni wa nani?
Mke akajibu, “si ni wako mume wangu? Hana baba mwingine na hakika watoto wote ni damu yako”.
Kumbe mwanamke huyu hasidi mtoto wa kwanza amezaa na shemeji yake, yaani mdogo wa mumewe; na mtoto wa pili kazaa na rafiki wa mumewe.
Sasa katika kujikanganya, bwana yule akamshikia kisu mkewe kumlazimisha amtaje baba wa mtoto. Mama kuona kisu akakubali kutaja baba wa mtoto. Bwana akaweka kisu pembeni ili amtaje.
Mama kwa ujasiri akataja kwamba mtoto yule wa kwanza amezaa na shemeji yake, na yule wa pili ni wa rafiki wa mumewe. Jamaa alibaki mdomo wazi, asijue la kufanya kwa wakati ule.
Huku nyuma mdogo wake alipobaini siri imefichuka kwa kutajwa ni mzazi wa mtoto mmojawapo, fumba na kufumbua akatoweka kama mvuke. Bwana yule akamwamuru mkewe afungashe virago kwani kuanzia wakati ule hakuwa tena mkewe. Pia alimwamuru aondoke na watoto wale, akawakabidhi kwa baba zao halisi. Ama kweli maisha ndivyo yalivyo.
Kusema kweli hakuna kitu kinachoudhi katika ndoa kama unakumbana na mwanamume au mwanamke ambaye ni mzinzi. Jambo hili linamwudhi sio mwananadamu peke yake, bali hata Mungu analichukia mno. Ndio maana imeandikwa katika Waebrania 13:4 kwamba, “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu”.
Ndoa inatakiwa iheshimiwe na watu wote, ikiwa ni pamoja na wanandoa wenyewe. Sio mtu unatoka nje ya ndoa, na kumwudhi mwenzio. Hapana. Ukifanya hivyo utamletea mwenzi wako majonzi. Na kibaya zaidi ni pale utakapomletea watoto wa nje.
Dhambi ya uzinzi inasameheka
Sasa ni vema kutambua kuwa uzinzi ni dhambi kama zilivyo dhambi nyingine. Swali la kujiuliza ni je, dawa ya dhambi ni nini? Ukweli ni kuwa dawa ya dhambi na kutubu na kuacha kabisa. Kama mumeo au mke amekuwa akizini, au kuna wakati alianguka katika dhambi hii, kama akija kwako na kutubu, tafadhali msamehe.
Usikatae kumsamehe mumeo au mkeo; usiwe na kinyongo; usiwe na uchungu moyoni. Usiseme hii dhambi ya uzinzi ni kubwa mno na kwamba haisameheki. Wewe samehe tu ili yaishe; ili uwe na amani moyoni mwako. Vinginevyo nawe utakuwa na hatia. Kumbuka maneno ya Bwana Yesu kwamba, ikiwa ninyi hamtasamehe wale wanaowakoseeni, hata Baba yenu wa mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu (Mathayo 6:12, 14-15, Marko 11:25-26).
9 maoni:
mi naomba Mungu akubariki, S.Tarimo na akupe fikra za kuendelea kutulisha habari nzuri kwani zintuerimisha mno, especially unaponukuu bible ukitudhihirishia ukweli kupitia neno la Mungu juu ya maisha yetu hapa duniani
God Kalisa( London)
Nashukuru sana kwa maelezo yako marefu na ya kina. Nilipenda sana kujua saha habari ya watoto wa kambo. Mimi nimeolewa na mume wangu alikuwa na mtoto wa nje. Alinipa taarifa hiyo tukiwa wachumba na kwa vile mimi ni mtu wa mungu sikuona haja ya kuachana naye kwa sababu ya mtoto huyo kwani alinieleza kuwa hata yeye hakuwa na uhakika kuwa yule alikuwa mwanawe ila kwa sababu tu hakupenda maneno ya watu alitaka akishakuwa na uwezo amchukue mtoto yule na kisha kumpima kama kweli ni mwanawe. na angekuta sio mwanae angemrudisha kwa mamaye na kumuonyesha majibu. Nilimsaidia sana katika kumleta mtoto huyo na tumemlea hadi sasa ana miaka zaidi ya 7 ila sijaona kama ana hatua yoyote ya kumpima mtoto huyu. Na cha ajabu ni kwamba baba huyu ana upendeleo fulani kwa mtoto huyu zaidi hata ya watoto wa ndoa yetu Ila mimi hilo sijari sana kwani nafanya kazi kwa kujituma na kumuwekea akiba mwanangu kwani baba yao ameajiriwa mimi nimejiajiri mwenyewe, ila nimeona kuwa mtoto huyu ameanza kupoteza amani katika ndoa yangu. Najiuliza nifanye nini kwani sijui hatma ya mtoto huyu itakuwaje.
Kielemu hana tatizo kwani tunamsomesha shule za English medium ingawa uwezo wake kwa kweli sio mzuri sana na ninapojaribu kumuelewesha babake anakuwa kama haelewi nimeamua nimuache tu sijui itakuwaje.
Kibaya zaidi ni kwamba upande wa mama wa mtoto huyu wanamsumbua sana mume wangu kuwa aliiba mtoto wao ingawa wakati anamchukua walifanya maandishi kabisa. Wanachotaka wao ni matunzo ya mama yule wa mtoto na wazazi wake kisa wamesikia kwa sasa mume wangu ana kauwezo kadogo wamekuwa wakiwasumbua wakwe zangu kuhusu pesa ya matunzo sasa hapo inakuwaje?? Naona sihishi kwa amani kwa ajiri ya machafuko ya familia yangu. Naomba unipe ufafanuzi na ushauri nifanye nini?? Mtoto napenda aishi vizuri na apate elimu kama watoto wengine na nilimpenda sana kwani nilinza kumtunza kwa pesa yangu mwenyewe hata kabla sijaolewa na mume wangu. Baada ya kuolewa nami nilibahatika kupata mtoto na kwa sasa tunao hao wawili tu.
Natumaini nitajibiwa haraka iwezekanovyo.
Asante sana ndg. God Kalisa kwa kunitia moyo.Nitajitahidi kuelimisha jamii katia maswala mbalimbali kadri nitakavyojaliwa na Mungu. Ubarikiwe.
Sabato Tarimo
Pole sana dada unayesumbuliwa na tatizo la mtoto wa kambo. Samahani sikuweza kujibu swali lako kwa haraka kama ulivyotarajia. Nilibanwa na shughuli nyingine.
Sasa kama sijakupa jibu la kina ningetaka kujua kuwa huyo mtoto wa kambo na vile vile huyo mliyezaa na mumeo ni wa jinsia gani? Halafu hebu niambie iwapo huyo mama wa mtoto wa kambo ameolewa au bado. Baada ya kunipa majibu ndipo nitakupa jibu la kina. Ila kwa sasa ninachoweza kusema ni kwamba kwa vyovyote vile hao wazazi wa huyo mama wa mtoto wa kambo (wakwe)hawastahili kabisa kutunzwa na mume wako. Hao ni wataabishaji wanaojipendekeza kwenu na kulazimisha mambo baada ya kuona mna uwezo. Kwahiyo wewe na mumeo muwe na msimamo. Maelezo mengine nitakupa baada ya wewe kujibu maswali yangu.
Pole sana na Mungu akutie nguvu katika kipindi hiki cha majaribu makubwa.
Sabato Tarimo.
Nashukuru sana ndugu Sabato Tarimo kwa ushauri wako mzuri sana na wa kina. samahani pia kwa kuchelewa kuandika matatizo yangu kwani kwa sasa nasumbuliwa sana na ugonjwa wa moyo hivyo nilikuwa kwenye matibabu,sasa nimepata nafuu na kuzidi kufuatilia tatizo langu kwa kina.
Mtoto huyu ni wa kiume na wa kwangu ni wa kike, mama wa mtoto huyu hajaolewa bado na yuko kijijini, hata mimi kusema ukweli simjui kwa sura ingawa namjua kwa jina tu.
Pia kingine ni kwamba kabla ya kunioa mimi mume wangu huyo alikuwa na ugomvi na wazazi wake uliotokana na mtoto huyo wa kambo kwani wazazi wa mume wangu hawakutaka kabisa uhusiano ule ambao mume wangu alisema matokeo ya mtoto huyo ni bahati mbaya. Hadi leo babamkwe wangu hataki hata kusikia habari za huyu mtoto.
Kabla ya ndoa nilifanya chini juu kujua ni kwa nini mume wangu hayuko karibu sana na wazazi wake nilipogundua hilo nilimshauri kuomba msamaha na walikubaliana naye na ndipo alipowaeleza kuwa anapenda kuwa na mwenza ukweli walifurahi sana na wananipenda sana kwa hilo namshukuru mungu sana napendwa na wakwe zangu na wanapendana na wazazi wenzao kwani wako maeneo ya karibu kijijini huko na wanatembeleana sana.
Nitashukuru sana sana nikipata majibu ya tatizo langu haraka ili niweze kupunguza mawazo.
Nakutakia kila la kheli katika kuelimisha jamii na Mungu akutie nguvu.
Pole sana dada unayesumbuliwa na tatizo la mtoto wa kambo na vile vile ugonjwa wa moyo. Mungu wa mbinguni akuponye kabisa maradhi hayo (Zab.103:3). Sasa tukija katika tatizo lako, ninachokiona mimi ni baba (au mume) ambaye anathamini watoto wa kiume kuliko wa kike. Amepiga mahesabu akaona kuwa asipokuwa makini, mali yake itarithiwa na watoto wa kike, kitu ambacho asingekipenda. Inaelekea mumeo ni mtu anayezingatia mila, ndio maana ameanza kumpendelea huyo mtoto wa kiume, hata kama hana uhakika ni wake. Na pengine bila hata kupima DNA, tayari ameshaona ishara fulani kwamba mtoto huyo ana sura yake. Kwahiyo kimya kimya amenza kumkubali kwa sababu hana mtoto mwingine wa kiume, ambaye angeweza kuwa mrithi wake. Hili ni tatizo la waafrika wengi, kwamba hatuthamini watoto wa kike kama tunavyothamini wa kiume. Wazungu wameshajikomboa katika eneo hili na hawabagui kati ya mtoto wa kiume na wa kike. Sisi waafrika, mtu haridhiki mpaka amepata mtoto wa kiume, ambaye anachukuliwa kuwa ndiye mrithi.
Tunapoangalia huyo mwanamke aliyezaa na mumeo na sasa yuko kijijini, ni wazi kuwa maisha yake yameharibiwa. Pengine hataolewa tena kwa sababu alishazaa, jambo ambalo limesababishwa na mumeo. Kusema kweli kibinaadamu (morally) mumeo anatakiwa amfidie uharibifu huo (recompesate). Sasa kwamba amfidie kwa namna gani, huo ni uamuzi wake.
Tunapomgeukia mtoto wa kambo tunaona kuwa tayari wewe ulishamkubali na kumchukua kama mwanao. Sidhani kwa sasa wewe kama mtu wa Mungu unataka kubadili mawazo na kumchukia au kumfukuza huyo mtoto. Vile vile hata mumeo ameshamkubali na ndio maana anaanza kumuonyesha upendo, ambao wewe unauita upendeleo. Je, huoni kama vile roho ya chuki imeanza kukuingia?
Sasa kisheria kama nyie wawili (mume na mke) mlishamkubali huyo mtoto wa kambo, basi atakuwa na haki ya kurithi mali zenu. Kwamba arithi kiasi gani, itategemea ni sheria gani ya mirathi mtakayotumia. Mkitumia ya kimila, jambo ambalo naona kama lina uwezekano mkubwa wa kutokea, wewe hutakuwa na haki ya kurithi, lakini watoto wako wa kike watarithi sehemu kidogo ukilinganisha na huyo mtoto wa kiume wa kambo. Iwapo mtatumia sheria ya Kiserikali ya mirathi (jambo ambalo naona kama vile kweni ni gumu), hapo nyote, yaani wewe, wanao wa kike na huyo mtoto wa kiume wa kambo, mtakuwa na haki ya kurithi. Mwisho ninalo swali kwako. Je, mumeo ameshafikiria kuandika wosia? Naamini nitakuwa nimejibu swali lako kwa kiwango kikubwa. Kama bado una dukuduku usisite kuuliza. Mungu awe nawe.
Sabato Tarimo.
Nashukuru sana ndugu Sabato Tarimo kwa ukarimu na upendo wako mkubwa na kipaji ulichopewa na mwenyezi mungu kuwa mpenda watu.
Naamini kabisa kuwa unanipenda na unapenda maisha yangu yawe mazuri na unapenda ndoa yangu. Nashukuru pia kwa kunisaidia katika dukuduku langu kwani nimekuelewa kabisa. Ila sina wasiwasi sana na mambo ya urithi kwani nadhani kwa wakati tuliomo ni wajibu wa wazazi wote wawili kuandaa maisha ya watoto wao. Mtoto bado nampenda kwani sio kosa lake kuzaliwa, kama babake atapenda kumrithisha sio vibaya kwani hata mimi naweza penda kumfanyia kitu ambacho kitamsaidia katika maisha yake bila kujari kuwa ni mtoto wa kambo. Huo ugomvi wa ndugu zake upande wa mamake mimi haunihusu kabisa na wala sitopenda kujiingiza huko ninachojari ni kumrudia mungu wangu na kutenda mapenzi yake thats all.
Sitokata tamaa kwani wote wawili mimi mwenyewe kwa pesa yangu niliwafungulia junior account CRDB na huwa najitahidi kuwawekea visent kidogo kila mwezi hivyo siwezi kukata tamaa ya kumsaidia mtoto huyu.
Mume wangu hajaandika wosia na sidhani kama anaweza kuandika kwa wakati huu kwani elimu ya vijana wengi kuandika wosia haijasambaa sana ingawa mimi niliwahi kufanya kazi katika vitengo hivyo najua nini maana ya kuandika wosia na sio wazee tu.
Kuhusu mwanangu wa kike sina wasiwasi sana kuwa hatarithi kwani kwa sasa ana miaka miwili na nusu na nimemuandalia maisha mazuri nafanya kazi kwa ajiri ya kuandaa maisha yake na pia mume wangu naye anampenda tu kwani kwa sasa tunapojenga nyumba yetu ya kuishi kiwanja kile kimeandikwa jina la mtoto na hati miliki ipo ni ya jila la mtoto wangu huyu wa kike. Nina mtoto mmoja tu na ninafikiri kuwa na mtoto mwingine mmoja, sasa hayo yatakuwa mapenzi ya mungu atanipa mtoto gani wa kike au wa kiume ninachoamini mimi ni kwamba wote ni watoto yoyote atakayetokea nitamshukuru kwa uumbaji wake.
Ndugu Tarimo ubarikiwa sana na mungu azidi kukutangulia katika uelimishaji wa jamii na hasa pale nitakapokosea/ninapokosea nitaomba ushauri wako zaidi nami nitazidi kukueleza na kukuuliza mengi tu ambayo yatakuwa yananitatiza katika maisha yangu.
Mungu akubariki sana.
Hongera kwa kutuelemisha mtumishi.
Naomba msaada wa hili.
Bwana Yesu asifiwe mtumishi!!
Naomba ushauri juu ya familia yenye hali ifuatayo.
Baba alikuwa mzinzi. Mke alimvumilia sana huku akimwombea. Japo aliahidi kubadilika kila siku lakini mke alikuwa akimshika na wanawake wapya aliokuwa akizini nao mara kwa mara.
Japo mme alikuwa mzinzi lakini hakutaka watoto nje ya ndoa na alikuwa akiwaambia hao wanawake kuwa ana mke na hataki watoto. Ilitokea siku moja akakutana na mwanamke aliyekuwa ana uhitaji wa mtoto. Japo alimwambia hahitaji mtoto lakini alibeba mimba bila kukubaliana na huyu mume. Mwisho wa siku alipotoa taarifa kwa huyu mume kuwa ni mjamzito alimwambia atoe na akumtumia hela ya kutoa lakini huyu mama akakataa akasema atamlea mtoto wake mwenyewe.
Huu ukawa mtihani kwa mume. Alikataa kumhudumia huyu mama na wakakata mawasiliano. Ikumbukwe kwanza wakati wanakutana na kuamua kufanya uzinzi huyu mama alikuwa na mchumba wake na alimuweka wazi baba.
Mwisho wa Yote hili lilikuwa kama funzo kwa huyu mume. Alimshirikisha mke wake jambo hili. Na wakabahatika kufanyabmazungumzo na huyo mama mzinzi ili kuhakikisha maneno ya mumebwake. Ni kweli kabisa kuwa huyu mamma alijua kuwa huyu mume alikuwa mme wa mtu, ni kweli kabisa huyu mama alipewa hela ya kutoa mimba lakiniakairudisha na ni kweli kabisa huyu mama alibeba mimba bila makubaliano na mume huyo na ni kweli kabisa kuwa huyu mama alisema atamtunza mtoto wake peke yake.
Sasa mume huyu amefikia muda anataka amfuate Yesu. Atubu dhambi zake ila hataki kuhusika kabisa na huyu mtoto aliyezaliwa bila ridhaa yake.
Ushauri ninaoba ni
1. Je huyu mume ataziona mbingu kwa hali hii?
2. Sijawa msomaji mzuri wa biblia kwa hiyo sijawahi kukutana na andiko linalozungumzia haya. Unaweza kunisaidia?
Kwa upande wangu nimeonelea kuwa ikiwa atasimama na kuachana na huyu bado hana dhambi kwa kuwa huyu mama alitaka mwenyew hiyo hali.
Pia alikshasema atamlea mwanae mwenyewe hivyo sioni tatizo kwa huyu mume.
Je unamtazamo gani wewe?
Nitashukuru sana ukinisaidia na mimi nipate pia namna ya kushauri hapa.
Bwana Yesu asifiwe!!
Msimamo Wa biblia uko vizuri mno shida ni msimamo Wa kidunia,ukiangalia hukumu za mahakama kuu na mahakama za rufaa kabla sheria ya mtoto haijaanza ni wazi kabisa mahakama ilitambua mtoto wa ndoa na sio mtoto Wa nje ya ndoa na aliiytwa mtoto haram na hakuwa na cha kirithi kwa baba yake vilevile sheria za kimila. Baada ya kuja kwa sheria ya mtoto iliequalize na kusema hakuna mtoto haram so shida ndio iko hapo kati ya biblia na sheria za nchi
Post a Comment
Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.