Tuesday, May 12, 2009
MKRISTO NA MAVAZI: Mavazi yasiyofaa ni yepi?
Labda kabla hatujaendelea sana, nafikiri ipo haja ya kuyaangalia japo kwa kifupi, aina ya mavazi ninayotaka kuzungumzia katika makala haya. Ni vizuri tuwekane sawa kungali mapema, ili huko mbeleni nitakapoanza kuchambua kila aina ya vazi lisilofaa, tuelewane vizuri. Kwahiyo nitakutajia aina ya nguo zilizozoeleka sana siku za leo, lakini kusema kweli mavazi hayo hayafai mbele za macho ya Mungu.
Badhi ya mavazi yaliyotapakaa mitaani na yanayopendwa na wanawake wengi wa kidunia ni haya yafuatavyo;
(i) Suruali za kubana.
(ii) Magauni ya kubana.
(iii) Vimini au magauni mafupi (mini or short dresses)
(iv) Blauzi zinazoacha matiti au mgongo wazi (low-neckline blouses)
(v) Blauzi zisizo na mikono (Sleeveless blouses)
(vi) Fulana (T-Shirts)
(vii) Nguo nyepesi zinazoonyesha maungo (shear or see-through or transparent clothing)
(viii) Kaptula au pensi nyanya.
(ix) Fulana (Singlets) zinazoshikilia matiti tu na kuacha migongo na vifua wazi.
(x) Sketi ndefu zilizopasuliwa.
(xi) Pedo (Pedal push).
Baadhi ya mavazi yasiyo ya heshima
Ukichunguza kwa makini utagundua kuwa lengo la mavazi haya ni kumwacha mwanamke uchi kwa kiwango kikubwa sana (expose a woman). Kama ni vazi la kubana, hata kama limeshuka hadi miguuni, bado litaonyesha maungo ya mwanamke yalivyo na katika hali ya kutamanisha mno. Hili ndio lengo kuu la wanawake wasio na hofu ya Mungu la kuvaa mavazi kama haya. Kwa bahati mbaya wapo walokole wanaochangamkia mavazi kama haya. Yaani wee acha tu.
Ni kosa na aibu kukaa uchi
Kitu cha kwanza ambacho yapasa kila mtu afahamu ni kwamba, ni kosa kukaa uchi. Ni kosa kubwa sana kwa mtu yeyote kuvaa mavazi yasiyosetiri mwili wake vizuri. Ni aibu kwa mwanamke au mwanamume yeyote kuanika maungo yake nje nje na hovyo hovyo tu. Tena ni dhambi mbele za Mungu. Hili nitalifafanua huko mbeleni.
Mwanzo kabisa baada ya uumbaji, pale Adamu na Hawa walipomkosea Mungu (kwa kushindwa kutii agizo lake lililohusu aina ya matunda waliyopaswa kula), walijiona wako uchi. Biblia inatuambia kuwa baada ya kula yale matunda, “Wakafumbuliwa macho wote wawili, wakajijua wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo” (Mwanzo 3:7). Yaani walipojiona wako uchi, waliona aibu, wakajifunika kwa majani.
Tangu wakati ule hadi sasa, ni aibu kwa mwanadamu kukaa uchi mbele ya mwanadamu mwenzake, hata kama wote wawili ni wa jinsia moja. Ni ajabu kuwa hata kwa baadhi ya wale walio katika ndoa, bado ni aibu kwa mwanamke kujiacha uchi uchi tu mbele ya mumewe. Hali kadhalika kwa mwanamume ndivyo hivyo ilivyo. Kila mmoja anaona aibu fulani kuangalia utupu wa mwenzake.
Kwa wanandoa wengine, hata tendo la ndoa hufanyika gizani kabisa. Ni lazima wazime taa. Kwanini? Kwa sababu wanaona aibu kuangaliana wakiwa uchi. Ni siku hizi tu, watu wanajifanya wameendelea. Lakini ukimwuliza babu yako, kama ni mkweli atakuambia kuwa wao tendo la ndoa lilikuwa linafanyika gizani, tena usiku. Walikuwa hawafanyi mchana kweupe kweupe. Kwanini? Kwa sababu walikuwa wanaoneana aibu.
Tukirudi kwa wazazi wetu wa mwanzo, yaani Adamu na Hawa, tunaona kuwa wao walikuwa wawili tu katika ile bustani ya Eden. Pamoja na uchache wao, bado waliona aibu kuangaliana wakiwa uchi. Walikuwa na kila sababu ya kusema ‘kwani kuna shida gani bwana? Si tuko wawili tu? Nani mwingine anayetuona?’ Lakini haikuwa hivyo. Bado walioneana aibu, wakajifunika kwa majani. Vile vile hata Mungu hakuwaacha wakae uchi. Aliwashonea nguo.
Kusisitiza jinsi ilivyo kosa na aibu kwa mwanadamu kukaa uchi, hebu tuangalie nini kilichotokea pale Nuhu alipolewa divai na kujikuta yu uchi. Biblia inatuambia kuwa, “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; akanywa divai akalewa; akawa uchi katika hema yake. Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao”. (Mwanzo 9:20-23).
Hapa tunaona kuwa baada ya Shemu na Yafethi kusikia kuwa baba yao yuko uchi ndani ya hema, hawakuenda kuangalia baba yao anafananaje. Wao walichukua nguo nyingine, wakaenda kinyumenyume, wakamfunika ili kuusetiri uchi wake. Kwanini walienda kinyumenyume?. Kwanza kabisa walijua ni kinyume na maumbile, mtu kukaa uchi. Walijua hilo ni kosa. Lakini vile vile waliona ni aibu kumwangalia baba yao akiwa uchi. Walijua kuwa wangejisikia vibaya sana iwapo wangeuona uchi wa baba yao.
Ikumbukwe kuwa Nuhu alikuwa ndani ya hema. Wale wanawe wangeweza kusema ‘si yuko ndani bwana? Kwani kuna shida gani” Si tumwamche tu aendelee kuuchapa usingizi? Atakapoamka si atajifunika?’ Lakini hawakufanya hivyo. Badala yake walimfunika kabla hajazinduka kwenye ulevi wake. Kwanini walifanya hivyo? Kwa sababu walijua si vema baba yao kukaa uchi, hata kama hakuna mtu aliyekuwa anamuona.
Ukitaka kujua ni aibu kukaa uchi, jichunguze wewe mwenyewe binafsi. Utagundua kuwa hata ukiwa peke yako katika chumba chako cha kulala (bedroom), bado hupendi kukaa uchi kabisa, japo hakuna anayekuona. Utajikuta unatamani kuvaa nguo inayokusetiri japo kidogo. Kama ni akina mama utawakuta angalao wamejifunga kanga moja. Akina baba wanapendelea zaidi kuvaa bukta na fulana. Hii ni kwa sababu hawajisikii vizuri kukaa uchi kabisa.
Sasa kama uchi au utupu wa mwanadamu unaleta aibu, ni kwanini kizazi cha leo hakioni soni kujianika ovyo ovyo? Ni kwa nini kizazi cha leo kina tabia ya kuvaa mavazi yasiyosetiri miili yao vizuri? Ni kwanini wazazi wanakaa uchi mbele ya watoto wao na watoto wanakaa uchi mbele ya wazazi wao? Ni kwanini watu wanakwenda ‘beach’ kujianika uchi. Amini usiamini, sababu kubwa ni kuwa hiki ni kizazi cha zinaa. Ni kizazi cha watu waovu, watu wasiojali na wasiozingatia maagizo ya Mungu.
Kizazi cha leo kimetawaliwa na zinaa. Kimevamiwa na pepo la ngono. Shetani amefungulia mapepo ya uzinzi ambayo yanawafanya wanadamu wapende sana ngono. Moja ya njia ya kueneza uzinzi ni kuvaa mavazi yanayotamanisha. Mavazi yanayoamsha tamaa ya ngono. Na kwa bahati mbaya mapepo haya yameingia hadi katika makanisa ya wateule wa Bwana. Yameweza kuwavamia hata watu wa Mungu, tena maaskofu kabisa. Hii ndiyo hali halisi, tutake au tusitake. .......(itaendelea)
5 maoni:
Mbona umekita kwenye mavazi ya wanawake tu? je kikristu wanaume hata wavaaje wao hawawatamanishi wanawake kwa mavazi yao yasiyofaay ya kiume ambayo kwa bahati mbaya au nzuri hukuyataja?
Yes, sasa mmeanza kuja kwa Allwa. Qurani ilishasema siku nyingii haya mambo
Hebu wewe padri soma vizuri Quran /Mashaf , uone waislam walivyo rich kwenye sheria / maamrisho yao. Nakukaribisha katika uislam
Kaka Trio asante kwa swali lako zuri. Ni kweli nimejikita zaidi katika mavazi ya kike kwa sababu hata Biblia nayo imejikita zaidi katika mavazi ya kike. Wanaume nao wanatakiwa wavae mavazi ya staha kwa sababu hata wao wakitembea nusu uchi wanatamanisha wanawake, lakini ukweli nikuwa madhara yanayoletwa na wanawake waliovaa nusu uchi ni makubwa sana ukilinganisha na yale yanayoletwa na wanaume. Hii inatokana na maumbile. Maumbile wa wanawake yanawavutia au yanawatamanisha sana wanaume. Halafu tangu zamani tatizo la kuvaa mavazi yasiyo ya staha ni la jinsia ya kike zaidi kuliko ya kiume. Ndio maana Biblia ina maandiko mengi zaidi kuhusu namna iwapasavyo wanawake kuvaa.
Sabato Tarimo.
Asante sana kwa huduma mtumishi. Tunashukuru kwa mawazo yako. Mimi nami ninamaswali kuhusu mavazi kidogo. Ninaomba utueleweshe kuwa mavazi gani ndio yanafaa wanawake wavae ikiwezekana utupatie picha japo za wapendwa hata bila kuonyesha uso wao ili tuelewe kwa vitendo maana tunachanganyikiwa sasa. Kila mtu anapopendeza haikosekani kasoro. Iwe amevaa gauni,Suti,Dira,na Suruali n.k.
Pili ninaomba unishauri kuhusu kukaa uchi, kwa jinsi nilivyoelewa mavazi ya kuacha mgongo na kifua wazi, kubana,nguo ndefu na mipasuo nayo inakuwa ni kukaa uchi, nimekengeuka kidogo hapo kuwa hata mgongoni ni uchi pia.
Mi ninaona hii topic ingekuwa katika moja ya sababu za tamaa ya mwanaume kwa mwanamke kama kichocheo hivyo tujihami. Ninajua mavazi mengine ya duniani ni mabaya kupindukia lakini tusaidie wapenda tuvaeje. Tuvae oversize tuu.
Mbona katika semina za ndoa tunafundishwa kuwa wazi na kufahamiana kila kitu, sasa hivi dunia sio ile ya zamani kila kitu kimebadilika. Ndoa za wakristo wengi zinavunjika kutokana na kutokufahamiana. Kama haumfahamu mwenzio vizuri akiingia majaribuni na kubahatika kuachiwa kila kitu wazi itakuwa ni shida. Sometimes tunahitaji kujiupdate. Hata blog zinakuwa updated la sihivyo we cant read same thing everyday. Kanisa / Wakristo wanatakiwa kujiupdate kimavazi. Wanamitindo wanatoa kila siku fashion mpya za duniani na sisi kanisa tutoe za kwetu alafu ziwe wazi na mifano maana za duniani pia zinamifano halisi hapa tutaondoa kigugumizi. Kama inakuwa Ngumu basi tuwe na vazi moja tuu linalokubalika kwa wapendwa kama ilivyokwa wenzetu, Sikuhizi hata kwenye misiba tuna ukengeufu hatujui tuvae kanga au suti nyeusi au nyeupe. Mapokeo ni mengi kwenye mavazi mi ninafikiri tunahitaji kuliombea hili swala sana. Maana hata hao wapendwa wanaovaa hivyo hawajui wavaeje ili iwe pleased in the sight of the Wapendwa wanaume. Siku hizi wanaobakwa ni wazee, watoto, wanafunzi n.k. Kwa kweli niko njia panda. Nisamehe sana kwa kukusumbua ila ni mtazamo tuu. Ni mawazo tuu. Sina nia ya kupinga kitu ambacho roho wa Mungu amekuvuvia. Forgive me.
Thanks.
Mjadala wa mavazi ni mabaki ya ukoloni. Ni vizuri tukajua katika asili yetu tulivaa nini. Lasivyo kukaa kuzungumzia mavazi wakati kuna mambo mengi ya kimaendeleo ambayo tupo nyuma, ni kufanikiwa kwa ukoloni kuturubuni ubongo wetu. Kweli waafrika tutabaki maskini kama tusipoangalia asili zetu. Katika jambo la mavazi, si ukristo wala uislamu utakaotoa jibu, bali ni mazingira yetu.
Post a Comment
Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.