Tuesday, May 12, 2009
MKRISTO NA MAVAZI: Mavazi yatamanishayo ni tishio kwa kanisa
Ninaamini wengi wenu mtakubaliana nami kuwa, humu duniani yapo mavazi yanayotamanisha. Yapo mavazi yanayomfanya mvaaji avute hisia za jinsia iliyo tofauti na yake. Yaani yavute tamaa ya kujamiiana. Kama yamevaliwa na mwanamke, huwa yanawavuta wanaume. Kwa kiingereza mavazi haya yanaitwa ‘provocative’ au ‘sexy dresses’. Nitashangaa sana iwapo kuna anayebisha juu ya jambo hili.
Sasa kwa kuwa lengo la makala yangu ni kuzungumzia uvaaji usiofaa, nitalenga zaidi mavazi ya kike. Hii ni kwa sababu ukweli unadhihirisha kuwa wanawake ndio wanaoongoza katika swala hili la kuvaa mavazi yasiyokuwa ya heshima. Pili, ni kwa sababu ambayo nitaileza kwa kirefu huko mbeleni; kwamba madhara yanayoletwa na wanawake walio nusu uchi ni makubwa zaidi ukilinganishwa na yale yanayeletwa na wanaume walio katika hali kama hiyo.
Ukweli ni kuwa yapo mavazi ya kike, ambayo yameshonwa kwa minajili ya kuvuta macho na kuuteka moyo wa mwanamume. Kwa minajili ya kuamsha hisia zake za ngono. Katika hali ya kawaida, mavazi haya huvaliwa zaidi na wanawake wa kidunia; wale ambao bado hawajaokoka. Lakini kidogo kidogo tayari mavazi haya yamejipenyeza katika jamii ya watu waliookoka, kiasi ambacho huwezi kuona tofauti yoyote kati ya mtu wa Mungu na mtu wa kidunia.
Iwapo uvaaji usiofaa hautadhibitiwa mapema, unaweza kuwa ni sababisho la uzinzi wa kutisha ndani ya jamii ya wateule wa Mungu. Ndani ya makanisa yetu. Uvaaji huo unaweza kushusha kabisa heshima ya jamii ya watu waliookoka. Hiki ndicho kinachonisukuma kuandika makala haya na kuonya juu ya jambo hili.
Nia yangu sio kukulaumu wewe ambaye, aidha kwa kutokujua au kwa kutojali, umejikuta tayari umeshapitiliza mipaka kwa kuvaa mavazi yasiyofaa. Nia yangu ni kukumbusha kuwa ipo haja ya kuwa makini na uvaaji wako. Ni kukumbusha kuwa Mungu anajali sana jinsi tunavyovaa na kwamba ameeleza bayana kupitia neno lake ni jinsi gani wanadamu wanapaswa kuvaa. Kama utavuka mipaka ya aina ya uvaaji uliowekwa na Mungu, utahukumiwa naye. Hili halina ubishi.
Uvaaji usiozingatia maagizo ya Mungu ni hatari sana kwa kanisa. Ni kama kijinga cha moto ndani ya msitu mkubwa, ambacho kinaweza kuteketeza msitu wote, iwapo hakitazimwa mapema. Uvaaji wa aibu usipodhibitiwa, unaweza kuenea makanisani mwetu na kuyateketeza. Na ukweli ni kuwa hatari hii haipo mbali sana. Tayari imeshabisha hodi katika baadhi ya makanisa. Kwa makanisa mengine hatari hiyo imeshajikita kabisa na hali inatisha.
Chachu kidogo hulichachua donge lote
Biblia inatuonya katika 1Wakorintho 5:6 kwa kutuhoji iwapo hatujui kuwa ‘chachu kidogo hulichachua donge zima?’ Maneno haya yalizungumzwa na mtume Paulo baada ya wateule waliokuwa katika mji wa Korintho kujisahau mno mpaka zinaa ya kutisha ikaingia katikati yao. Yaani mpaka ikafikia hatua ya mshirika kumwoa mke wa baba yake mzazi.
Kanisa linapojisahau, matatizo kama haya yaliyojitokeza kati ya wateule waliokuwa Korintho yanaweza vile vile kujitokeza katika kanisa la leo. Ndio maana nikasema ipo haja ya kupambana na tatizo la mavazi yasiyofaa mapema kabla hali haijawa mbaya. Binafsi ninaamini hatujachelewa; bado hali inaweza kurekebishwa.
Nakumbuka tatizo la kuvaa mavazi yasiyo ya heshima lilianza kidogo kwa kuwahusisha washirika wachache tu, tena wakiwa wanavaa nguo ambazo hazikuwa mbaya sana. Lakini kidogo kidogo tatizo likakua kwa wavaaji wa aibu kuongezeka. Vile vile mavazi yenyewe yakaongezeka katika ubaya wake, yaani yakaongezeka katika ile hali ya kumwacha mvaaji uchi. Leo hii katika baadhi ya makanisa ya kilokole, ni jambo la kawaida kabisa kuwakuta wadada na wamama wakiwa wamevalia mavazi ya aibu yanayowaacha mapaja, matiti au migongo yao wazi kabisa.
Ninakumbuka miaka ya nyuma kidogo wakati mtindo wa vazi la mpasuo ulipoingia nchini mwetu. Mwanzoni wanawake wacha Mungu hawakuiga mtindo huu. Hata wahubiri na waimbaji wa nyimbo za Injili walionya sana juu ya mipasuo ya aibu. Lakini baada ya muda, wakaanza kujitokeza waumini wachache waliodiriki kupasua magauni au sketi zao. Tena walianza kwa kampasuo kadogo tu, ambako eti sio kakubwa sana na kwamba hakana neno.
Baada ya muda mfupi tu wavaaji wa mipasuo midogo wakaongezeka. Halafu punde tena, ukubwa wa mipasuo yenyewe ukaongezeka, sambamba na wavaaji wake. Leo hii ni jambo la kawaida kabisa kuwakuta mabinti pamoja na wamama wengi tu wakiwa wamevalia mipasuo ya aibu makanisani mwao; tena bila wasiwasi wowote. Yale yale ya chachu kidogo hulichachua donge zima.
Siku hizi uvaaji wa mipasuo ya aibu umezoeleka mno makanisani, kiasi ambacho nguo hizi zinaonekana kama vile ni vazi la kawaida kabisa lisilo na tatizo lolote. Ndio maana nikasema kuwa katika baadhi ya makanisa hali inatisha. Na ukweli ni kuwa hali hii imefikiwa kwa sababu tatizo halikudhibitiwa tangu mwanzo. Halikushughulikiwa kikamilifu pale lilipoanza kujitokeza. Kwa sasa tayari limeshajikita makanisani. Ndio maana watu wachache wanapojitokeza leo kukemea hali hii, wanaonekana kama wendawazimu. Wanaonekana kama waliopitwa na wakati au washamba wa kutupwa.
Dawa ya tatizo ni kulishughulikia kungali mapema. Ni kupambana nalo kabla halijakomaa na kuwa sugu. Sio kuliacha likue na kuzoeleka kama vile sio tatizo tena. Ndio maana Biblia inatuagiza kuwa, “Basi, jisafisheni mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu” (1Wakorintho 5:7). Kanisa linatakiwa lijisafishe. Lijirekebishe. Mavazi yote yasiyofaa yanatakiwa yaondoke katikati ya kusanyiko la watu wa Mungu.
0 maoni:
Post a Comment
Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.