Monday, May 11, 2009
MKRISTO NA MAVAZI: Mavazi yasiyofaa
Mwendelezo wa sehemu ya kwanza MKRISTO NA MAVAZI: Utangulizi
Sasa msomaji wangu ninachotaka kuzungumzia katika makala haya sio swala la uumbaji au dhambi ya Adamu na Hawa ya kumwasi Mungu. Hapana. Hicho sio kiini cha makala haya. Nia yangu hasa ni kuzungumzia tatizo la wanadamu wa leo la kukiuka maagizo ya Mungu kuhusiana na aina ya mavazi tunayopaswa kuvaa.
Nia yangu ni kuwakumbusha wakristo wenzangu kuwa, yapo mavazi yaliyoenea duniani kwa sasa, lakini mavazi hayo yapo kinyume kabisa na maagizo ya Mungu. Kwamba wanaoyavaa, wanaasi agizo la Muumba wao na wasipobadilika, watahukumiwa.
Kimsingi ninataka kulitahadharisha kanisa la Mungu au watu waliookoka kuwa baadhi yao wamejisahau mno katika eneo la mavazi. Kwamba wapo wakristo waliookoka, lakini hawazingatii maagizo ya Mungu yanayohusu mavazi wanayopaswa kuvaa. Kwamba yapo madhara makubwa sana kwa kanisa kwa sababu ya kutozingatia agizo la Mungu kuhusu mavazi. Hiki hasa ndio kiini cha makala haya.
Moja ya madhara au hasara ambazo mwamini anaweza kupata kwa sababu ya kutotii maagizo ya Mungu yanayohusu mavazi ni pamoja na kuukosa uzima wa milele. Ninaamini mpaka nitakapofika mwisho wa makala hii, wapo watakaoelimika na kama walishavuka mpaka kwa kuvaa mavazi yasiyostahili, watajirekebisha na kuanza kuvaa sawasawa na maelekezo ya Mungu. Kwahiyo msomaji wangu naomba tufuatane kwa makini.
Je, tatizo la mavazi yasiyofaa lipo?
Kabla sijaendelea sana, naona ipo haja ya kujiuliza na kutafakari kama kweli tatizo la mavazi yasiyofaa lipo miongoni mwa makundi ya wale tunaojiita walokole (au watakatifu wa Bwana au wateule au wapendwa na kadhalika (kama wanavyojulikana kwa majina mbalimbali). Ipo haja ya kufanya hivyo ili tusije tukajikuta tunazungumzia kitu ambacho hakipo kabisa.
Tutakapokubaliana kuwa ni kweli kuna tatizo katika aina ya mavazi yanayovaliwa na watu wa Mungu siku hizi, bila shaka itakuwa rahisi kubadilisha misimamo kwa wale walio radhi kufanya hivyo. Na kwa sababu hiyo wapo watakaoepukana na dhambi ya kuyaasi maagizo au mipaka iliyowekwa na Mungu wetu.
Kabla sijaendelea sana naomba nitoe tahadhari kungali mapema kwamba, ninafahamu fika kuwa ninazungumzia jambo ambalo ni tata na lenye ubishi mwingi. Ninatambua wazi kuwa huenda tusikubaliane kabisa katika eneo hili la mavazi yasiyofaa. Pamoja na kutambua hilo, binafsi siwezi kuendelea kukaa kimya.
Katika kizazi cha sasa, ambacho binafsi nimekibatiza kizazi cha ukaidi, hilo la kutokubaliana haliepukiki. Na wakaidi ninaozungumzia hapa ni pamoja na watu wa Mungu au walokole. Hawa nao ni wabishi, wee acha tu. Wakati mwingine ni wabishi hata kuliko watu ambao hawamjui Mungu kabisa. Pamoja na hayo, nitasema yale yaliyo moyoni mwangu, halafu uamuzi wa mwisho ninakuachia wewe msomaji wangu.
Ili kujua kama tatizo la mavazi lipo au la, hebu tuangalie watu wengine wanasema nini kuhusu jambo hili. Tutafanya hivyo kwa kuangalia, pamoja na mambo mengine, taarifa au habari nilizozinikuu kutoka katika magazeti mbalimbali ya Kikristo yaliyopo hapa nchini. Ninakusihi msomaji wangu usome na kutafakari kwa makini taarifa hizi. Jitahidi kuelewa na kuona kama kuna kitu unachoweza kujifunza.
0 maoni:
Post a Comment
Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.