Monday, May 11, 2009
MKRISTO NA MAVAZI: Makanisa ya kimadhehebu yamepotoka
MAKANISA YA KIMADHEHEBU YAMEPOTOKA (Nyakati Toleo namba 302 la tarehe 17-23 Septemba 2006)
Hebu tuendelee na mada yetu. Msomaji mwingine anayeitwa Denis Nitu naye alieleza yafuatayo katika gazeti hilo hilo la Nyakati katika barua yake kwa mhariri iliyokuwa na kichwa cha habari kama ilivyo hapo juu.
Ndugu Mhariri
Napenda kumpongeza Mchungaji Moses Magembe wa T.A.G majumbasita Dar kwa kusimama imara na kukemea uchafu unaoendelea makanisani ukifanywa na watu wanaokiri kwamba wameokoka, lakini wakidumu kufanya mambo ya ulimwengu. Wanavaa vimini, nguo za kubana, wanapasua sketi, wanavaa suruali, wanakwangua nyusi zao na kujipaka rangi za kila aina machoni, midomoni, kwenye kucha za miguuni na mikononi, ili mradi wahakikishe kuwa hawajabaki nyuma kwenye mambo ya fashion na mitindo ya kidunia. BWANA akubariki sana mchungaji kwa kuona hilo na kulikemea……………..…(Mwisho wa kunukuu).
Mambo ya msingi yanayojitokeza
Katika barua hii tunajifunza mambo yafuatayo;
- Wapo wakristo wanaokiri wokovu, lakini wanavaa mavazi ya aibu kama vile vimini, nguo za kubana, suruali, mipasuo, na kadhalika.
- Kanisa la leo limepoteza mwelekeo na halifuati mafundisho ya mitume wa mwanzo.
- Pamoja na matatizo ya kanisa, bado wapo wachungaji au viongozi walio na msimamo imara wa kulisimamia neno la Mungu kwa gharama yoyote ile.
NGUO ZINAZOBANA ZAWACHEFUA WALIOHUDHURIA MKUTANO WA INJILI (Nyakati Toleo na. 303 la Tarehe 24-30 Septemba 2006).
Mwandishi mmoja wa habari anayeitwa Zablon Mlimbila wa Moshi mkoani Kilimanjaro aliandika taarifa iliyokuwa na kichwa hicho hapo juu katika Gazeti la Nyakati.
Tabia chafu inayoonyeshwa na baadhi ya wasichana wanaoenda kwenye mikutano ya Injili ya kuvaa nguo zinazobana kiasi cha kuonyesha maungo yao ya ndani ilikuwa kero kubwa kwa watu waliohudhuria mkutano wa Injili uliofanyika mjini Moshi wa makanisa ya kipentekoste Kilimanjaro na kuhubiriwa na mhubiri wa Kimataifa Peter Pretorius kutoka Africa ya Kusini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya waliohudhuria mkutano huo walionyesha kukasirishwa mno na tabia hiyo. Mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Faraja alisema inabidi waandaaji wa mikutano kama hiyo wawe na watu maalum wa kuzuia wanaoenda mkutanoni na nguo za ajabu kwani zinapunguza uchaji wa ibada na mafundisho. Mtu mwingine ambaye alijitambulsha kwa jina la Mama Hawa alisema kitendo cha mabinti kuingia uwanjani na nguo za kubana ni aibu na haimpendezi MUNGU.
Katibu wa maandalizi ya mkutano huo Bw: Unity R. Msami alisema wao kama viongozi wamepokea kauli hiyo kama changamoto kwani na kwamba katika mikutano ijayo wataangalia suala hilo kwa umakini sana. Alisema kama ilivyo makanisani wataangalia pia uwezekano wa kuzuia watu kuhudhuria mikutanoni wakiwa wamevaa kofia, pamoja na kufunga simu…….(Mwisho wa kunukuu).
Mambo muhimu yanayojitokeza
Mambo muhimu yanayojitokeza katika barua hii ni haya yafuatayo;
- Wapo watu wanaokerwa au wanaokwazwa na tabia ya uvaaji usiofaa.
- Wapo wakristo waliojisahau mno mpaka wanaona ni jambo la kawaida kwenda kwenye mikutano ya Injili huku wakiwa wamevalia mavazi ya aibu.
- Uvaaji usiofaa unapunguza uchaji wa Mungu na usikivu wa mafundisho au mahubiri.
- Wakristo wengine hawana hofu ya Mungu kiasi ambacho, licha ya kuvaa mavazi yasiyofaa, vile vile hawavui kofia, hawazimi simu na kadhalika, wakati wanapoingia katika nyumba za ibada.
UVAAJI NGUO HUU UNADHALILISHA KINA DADA (Msemakweli Toleo Na. 473 la Tarehe 24-30 Septemba 2006)
Mawazo mengine niliyoweza kukusanya kuhusiana na uvaaji usiofaa yaliandikwa na Marietta Julius, Jovita Marko na Husna Rashid katika Gazeti la Msemakweli. Hawa ni wanafunzi wa shule moja iliyoko mjini Arusha, na walikuwa na haya ya kusema;
Mhariri,Mambo muhimu ya kujifunza
Tunapenda kutoa shukrani zetu kwa Gazeti lako kwa kutoa nafasi kwa wasomaji wake kutoa maoni yao na hivyo kudumisha dhana ya uhuru wa kutoa mawazo. Sisi wanafunzi wa kidato cha kwanza mjini Arusha, ambao kwa uchungu mkubwa tunaandika barua hii tukitarajia viongozi wanaohusika watachukua hatua ya kukabiliana na Suala hili.
Suala kubwa ambalo tunataka kuzungumzia hapa ni juu ya dada zetu ambao wameamua kutembea wakiwa nusu uchi, bila ya wasiwasi, kwa kisingizio cha kwenda na wakati. Hivi sasa baadhi ya watu wanaona aibu kutembea na wazazi wao barabarani kwa kuhofia kukutana na wanawake hawa kwani utakapokutana nao hutaweza kumwangalia mzazi usoni. Ni aibu na fedheha kubwa.
Hawa kinadada wamekuwa wakivaa nguo laini sana zinazobana mwili, kiasi cha kuona maumbile ya ndani, nyingine zikiwa fupi mno ambapo mhusika mwenyewe hawezi hata kuinama. Lakini jambo moja linalotushangaza ni kwamba pamoja na ukweli kwamba hiki ni kipindi cha utandawazi, lakini hakuna kongozi hata mmoja anayekemea uvaaji huu. Wote wanaonekana kufurahia hali hii, ambayo inaharibu jamii yetu. Mfano baadhi ya kinadada wamewahi kumtembelea nyumbani kiongozi mmoja wa kitaifa, huku wakiwa wamevaa nguo ambazo kwa kweli hazistahili hata kidogo.
Ningeomba serikali itoe tamko la kupiga marufuku nguo za namna hii, kwani siyo tu kwamba zinatia aibu lakini zimekuwa chimbuko la kumomonyoka kwa maadili ya taifa letu. Aidha sambamba na nguo hizi, pia ningependa kuomba serikali ikemee majarida yanayohusiana na masuala ya ngono kwani kinachoonekana zaidi ni kwamba wenye majarida hayo wanajali zaidi fedha na biashara kuliko staha ya Watanzania. Tunaomba viongozi wetu waelewe sisi wanafunzi hatutaki haya mambo. Ni aibu kubwa kwa taifa letu na wengine wanasababishwa kubakwa kwa wingi na kujiletea madhara. (Mwisho wa kunukuu)
- Hawa wanafunzi walioandika barua hii wanatufundisha mambo yafuatayo;
- Wapo wakina dada wanaotembea nusu uchi kwa kisingizio cha kwenda na wakati.
- Hakuna viongozi wa Serikali wanaoonekana kukemea tabia ya kuvaa mavazi yasiyofaa. Wengi wanaonekana kufurahia hali hii.
- Uvaaji usifaa ni aibu sio kwa huyo mvaaji tu, bali hata kwa jamii inayomzunguka.
- Nguo zisizofaa ni chimbuko na matokeo ya mmomonyoko wa maadili.
- Sambamba na mavazi yasiyofaa, majarida ya ngono nayo ni tatizo lingine linaloikabili jamii ya Watanzania.
- Mvaaji wa nguo za aibu anaweza kujiletea madhara kama vile kubakwa.
WATUMISHI WA MUNGU MNALIJUA HILI? (Nyakati Toleo Na. 315-Desemba 24-30, 2006)
Na mwisho kabisa yafuatayo ni mawazo ya ndugu Ibrahim Xavery kama yalivyotokea katika Gazeti la Nyakati.
Kwanza napenda kutoa shukrani kwa MUNGU kwa ajili ya Gazeti letu la Nyakati ambalo limekuwa mstari wa mbele kuutetea mwili wa Kristo, ambao ulikwisha jengwa na Kristo mwenyewe (Mathayo 16:18). Baada ya kulipongeza gazeti hili, niingie kwenye kiini chenyewe.
Ninajisikia furaha sana, tena sana, hasa ninapoona mwili wa Kristo ukiongezeka kwa ukubwa na kuimarika kiimani. Lakini kuna tatizo ambalo linatia dosari, kama siyo kuleta kichefuchefu ndani ya kanisa. Watumishi wa MUNGU wenye waumini wengi, hili limeingia kwenye mikusanyiko yenu. Nasema hivyo ni kwanini? Ni kwa sababu imekuwa ni desturi kwa wakristo wa sasa, ambao hawana hofu ya MUNGU, kuwa wanafanya vituko huko mitaani. Sisi ndio tunaowaona, utadhani hawajaokoka.
Ukimshuhudia kwa habari ya kuokoka anakwambia nimeokoka naabudu (utakuta anataja makanisa yenye waumini wengi) mimi nasali pale. Unauliza umeokoka? Anakujibu ndiyo! Unauliza, hivi MUNGU anapenda kuona wewe dada umevaa suruali na hivyo vitop ulivyovaa? Au je, utaweza kwenda kanisani umevaa hivyo?
Majibu yanakuwa siyo mazuri, siyo ya kuridhisha. Atakuambia MUNGU haangalii mavazi. Hivi ni kweli MUNGU wetu haangalii mavazi? Utaweza kwenda kanisani uchi, eti kwa kigezo kwamba MUNGU haangalii mavazi? Soma 1Petro 1:14-15, 3:2-3. Akina dada jirekebisheni; mnaongoza kuvaa ovyo makanisani…. (Mwisho wa kunukuu).
Mambo ya kujifunza
- Katika barua hii tunajifunza mambo yafuatayo;
- Wapo wakristo wanaokiri wokovu, lakini mitaani wanaonekana wakiwa wamevaa mavazi ya aibu.
- Wanaovaa mavazi ya aibu wanajitetea kuwa Mungu hajishughulishi na mavazi bali anaangalia moyo tu.
- Wakina dada wanaongoza kwa kuvaa ovyo makanisani mwao.
- Watumishi au viongozi wa makanisa wanapaswa kukemea kwa nguvu zao zote tabia ya kuvaa mavazi yasiyofaa.
- Makanisa makubwa yanaweza kuwa ni vichaka vizuri sana vya kuwaficha wanawake wanaovaa mavazi ya aibu.
Tatizo lipo
Ninaamini mpaka sasa msomaji wangu utakubaliana nami kuwa tatizo lipo. Mimi sijui wewe una msimamo upi, lakini ninachoweza kusema kwa yakini ni kuwa lipo tatizo katika aina ya uvaaji wetu sisi tunaojiita wateule wa Bwana. Wapo waliopitiliza mipaka; wanaokaidi maagizo ya Mungu yanayohusu jinsi anavyotutaka tuvae. Na hiki ndicho kinachonisukuma kuandika makala haya.
Kama nilivyotangulia kutoa tahadhari mwanzoni kabisa mwa makala haya, ni kwamba ninatambua wazi kuwa mjadala wa mavazi, hasa siku za leo, ni mgumu na mara nyingi huwa hauna mshindi. Watu wengi, ikiwa ni pamoja na wakristo waliookoka, wanataka uhuru usio na mipaka katika maswala mbalimbali yanayohusu maisha yao. Hii ni pamoja na swala la mavazi.
Kwa sababu hiyo mimi na wewe msomaji tunaweza tusikubaliane ni aina gani ya mavazi tuvae na yepi tusiyavae. Katika jambo hili la mavazi, wengine huwa wanafikia hatua ya kuwa na misimamo yao, hata kama misimamo hiyo ipo kinyume kabisa na maagizo ya Mungu. Anayejua ni nani aliye sahihi ni Mungu mwenyewe. Na hilo hata mimi namwachia Yeye.
Lakini pamoja na sisi wanadamu kutofautiana, kuna jambo moja ambalo binafsi nina uhakika nalo. Nalo ni kwamba, hata kama tuna uhuru wa kuvaa tutakavyo, bado Mungu ametuwekea mipaka. Hakutuacha tuvae vyovyote vile tupendavyo. Hapana. Hakukaa kimya kuhusu eneo la mavazi. Ukweli ni kwamba, ametoa maagizo ni kwa namna gani wanadamu wavae. Ndio kusema ametuwekea mipaka katika jambo hili.
Hiki ndicho ninachotaka kuwakumbusha wakristo wenzangu. Na kama nilivyosema katika utangulizi wa makala haya, ninaamini wapo watakaonielewa. Kama tayari walikuwa wamepitiliza mipaka katika uvaaji wao, bila shaka watajirekebisha. Watapona sio wao tu, bali pamoja na watu wengine ambao tayari walishaanza kuathirika kutokana na kukithiri kwa tabia ya kuvaa mavazi yasiyofaa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 maoni:
Kilio cha mavazi ni kilio endelevu. Kibaya zaidi ni kwamba tunaowatarajia kukemea hawafanyi hivyo. Wengine kwa kupenda fedha zaidi wameyavumilia maovu kanisani. Si hilo la mavazi tu bali hata na dhambi zingine nyingi tu. Miaka ya themanini mtu alikuwa akitegwa kanisani kwa ajili ya zinaa kwa mfano kanisa liliangua kilio. Lakini siku hizi hata kutangazwa kwenyewe inakuwa siri, tena tangazo linatolewa wakati mahudhurio ni hafifu kanisani ndipo mkosaji anatengwa, ni kama kumsitiri vile. Kweli hizi nyakati za mwisho zitatugharimu sana.
Post a Comment
Tafadhali kuwa mstaarabu.
Jiheshimu kwa kutokuacha maneno yenye kauli ya kutusi ama kuudhi wengine.
Maoni yasiyofaa hayatachapishwa.